Saturday, 22 May 2010

LEO NDIO LEO NDIO FAINALI!!!!
Mabaki ya Real yatua Real: Robben v Sneijder
Leo ni Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI inayochezwa Stadio Santiago Bernabeau, Uwanja maarufu wa Real Madrid, ambao walikuwa na ndoto kubwa yakucheza Fainali hii nyumbani kwao pale walipovunja Benki zote za Spain na kutumia zaidi ya Euro Milioni 200 kuwanunua Masupastaa Cristiano Ronaldo, Kaka, Xabi Alonso na Karim Benzema na kuwabwaga Wachezaji, miongoni mwa wengine, Arjen Robben na Wesley Sneijder.
Lakini leo si Real Madrid na Masupastaa wake ndio wako Fainali, leo ni Timu ya Bayern Munich ya Arjen Robben na Inter Milan ya Wesley Sneijder ndio wako Fainali nyumbani kwa Real Madrid.
Walipotimuliwa Real Madrid mwanzoni mwa Msimu uliokwisha juzi hakuna alieota ‘Takataka’ hizo za Real Madrid ndizo zitaongoza Timu zao kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI ndani ya Stadio Santiago Bernabeau.
Kwa namna moja au nyingine Sneijder na Robben, ambao wote ni Wadachi, ndio walioziongoza Timu zao na kuzifikisha Fainali.
Robben ndie aliefunga magoli muhimu katika mechi dhidi ya Fiorentina na Manchester United na kuhakikisha Bayern Munich inasonga mbele.
Sneijder ndie ‘akili’ ya Inter Milan kwa pasi zake na frikiki zake.
Robben amesema: “Mie na Sneijder tulitaka kubakia Real! Lakini ilibidi tuondoke. Ndoto ya Real ilikuwa kucheza Fainali hii Uwanjani kwao! Sisi tuliondoka, tumepata Klabu mpya na sasa tumerudi hapa tuko Fainali!”
Mshindi leo kuziiga Barca na Man United!!!
Katika Fainali ya leo ya UEFA CHAMPIONS LIGI, Mshindi kati ya Bayern Munich na Inter Milan atakuwa ameingia kwenye historia iliyowekwa na Klabu za Manchester United na FC Barcelona ya kutwaa Mataji Matatu kwa mpigo katika Msimu mmoja.
Mwaka 1999, Manchester United ilitwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England, FA CUP na UEFA CHAMPIONS LIGI na Msimu uliokwisha FC Barcelona ilifanya hivyo kwa kushinda La Liga, Copa del Rey na UEFA CHAMPIONS LIGI.
Msimu huu, huko kwao, tayari Inter Milan na Bayern Munich zimeshatwaa Ubingwa wa Nchi zao na pia Vikombe vya Nchi zao na Timu yoyote ikishinda leo itakuwa inatwaa Taji la 3.
Makocha Mourinho na Van Gaal kuweka Historia!!!
Msisimko mwingine kwenye Fainali ya leo ni ule ukweli kuwa Makocha wote wa Inter Milan, Jose Mourinho, na wa Bayern Munich, Louis van Gaal, wameshawahi kushinda Kombe hili la UEFA CHAMPIONS LIGI wakiwa na Klabu nyingine.
Mourinho alitwaa Kombe hili Mwaka 2004 akiwa na FC Porto na Van Gaal alishinda Mwaka 1995 akiwa na Ajax.
Kocha atakaeshinda leo ataingia kwenye ile Orodha iliyotukuka ya Makocha walioshinda Kombe hili wakiwa na Vilabu tofauti ambayo kwa sasa wamo Ottmar Hitzfield [Akiwa na Borrussia Dortmund Mwaka 1997 na Bayern Munich Mwaka 2001] na Ernst Happel [Feyenoord Mwaka 1970 na Hamburg Mwaka 1983].
Chamakh rasmi Ze Gunners
Arsenal wamethibitisha kumsaini Mchezaji wa Kimataifa kutoka Morocco, Marouane Chamakh, ambae ni Mchezaji huru baada ya Mkataba wake na Klabu ya Bordeaux ya Ufaransa kumalizika.
Wenger amesema: “Tuna furaha kumchukua. Ni Mchezaji tuliekuwa tukimtaka kwa muda mrefu.”
Mwenyewe Chamakh, miaka 26, amesema: “Hii ni ndoto yangu. Lengo langu lilikuwa kucheza Ligi Kuu na Arsenal ni chaguo langu!”

No comments:

Powered By Blogger