Tuesday 18 May 2010

Neville ahoji uteuzi wa Capello
Gary Neville ameutia walakin uteuzi wa Kocha wa England Fabio Capello hasa kwa kumchukua Beki mmoja tu wa kulia Glen Johnson wa Liverpool katika Kikosi chake kwa ajili ya Kombe la Dunia.
Neville amesema: “Nashangaa kuona Beki mmoja tu wa kulia!”
Kwa mtazamo wa Neville, yeye alitaka achukuliwe Mchezaji mwenzake wa Manchester United Wes Brown ambae pia hucheza kama Beki wa Kulia lakini Capello amemchukua Sentahafu wa Liverpool, Jamie Carragher, ambae pia huweza kucheza kama Beki wa Kulia.
Carragher alikuwa ameshaamua kustaafu kucheza mechi za Kimataifa lakini Capello akamshawishi kurudi kilingeni.
Hata hivyo, Capello alishindwa kumshawishi Kiungo wa Man United, Paul Scholes, aliestaafu arudi kuchezea England tena.
Neville aliongeza: “Binafsi sijuti kukosa kuitwa ingawa nilidhani kuna nafasi ya hilo lakini nadhani kutochukuliwa Wes Brown kunashangaza!”
Neville ameshaichezea England mara 85.
Boateng amtaka radhi Ballack kumkosesha Kombe la Dunia
Kiungo wa Portsmouth Kevin-Prince Boateng amemwomba radhi Nahodha wa Ujerumani kwa kumuumiza na hata kumsababisha akose Kombe la Dunia.
Boateng alimuumiza Ballack katika Fainali ya Kombe la FA kati ya Chelsea na Portsmouth Jumamosi iliyopita.
Boateng ametamka: “Sina cha kufanya ila kumwomba radhi tu. Niliuchelewa mpira na nikamvaa. Nilimwomba radhi mara mbili Uwanjani!”
Ingawa amezaliwa na kuwahi kuzichezea Timu za Taifa za Vijana za Ujerumani, Boateng ameamua kuchezea Ghana ambako Baba yake anatoka lakini mdogo wake, Jerome Boateng, ni Mchezaji wa Ujerumani.
Kwenye Fainali za Kombe la Dunia, Ujerumani na Ghana, zimo Kundi moja.
Mwenyewe Ballack amekaririwa akisema: “Nimechukizwa na kuvunjika moyo. Sitaki kusema chochote. Inaumiza roho kwa vile Kombe la Dunia lipo karibu lakini hii ni Soka na maisha yanaendelea!”

No comments:

Powered By Blogger