Tuesday, 18 May 2010

Chamakh atua London, yuko mezani na Ze Gunners
Marouane Chamakh yupo Jijini London kujadiliana na Arsenal kuhusu maslahi yake ili ajiunge nao kufuatia kumalizika kwa Mkataba wake na Klabu ya Ufaransa Bordeaux ambao unamfanya awe Mchezaji huru.
Mchezaji huyo wa Kimataifa toka Morocco, mwenye umri wa miaka 26, amekuwa akiripotiwa atajiunga na Arsenal tangu Msimu uliopita.
Chamakh, ambae ni Fowadi, ataacha majonzi huko Bordeaux kwani Klabu hiyo ilijaribu sana kuongeza Mkataba wake lakini walishindwa.
Rais wa Bordeaux Jean-Louis Triaud amelalamika: “Tulijaribu kuongeza Mkataba wake. Yeye amesema hajaongea na Wenger lakini ajabu anajiunga na Klabu bila kuongea na Wenger! Tangu niwe hapa nimepata matatizo kwenye uhamisho wa Wachezaji wawili, Wiltord na Chamakh, na wote wanahamia Arsenal!”
Hata hivyo Triaud amesema anamtakia kila la heri Chamakh kwani ni Kijana mzuri na Mpiganaji hodari.
Nyota AC Milan kucheza bureeeeee!!
Difenda wa AC Milan, anaechezea USA, Oguchi Onyewu, ameipa ofa Klabu yake AC Milan ya kucheza mwaka mmoja bure bila malipo ikiwa kama fidia ya kushindwa kucheza Msimu wote wa 2009/10 kwa sababu ya kuumia goti na ofa hiyo imekubaliwa.
Onyewu, miaka 28, alijiunga na AC Milan kutoka Standard Liege na akacheza mechi moja tu kisha akaumia goti katika mechi ya mchujo wa Kombe la Dunia kati ya Nchi yake USA na Costa Rica.
Mkataba wa Mchezaji huyo na Milan ulikuwa ni wa miaka mitatu na unatakiwa kumalizika 2012 lakini mwaka mmoja mzima kati ya hiyo mitatu alishindwa kucheza na hivyo kwa ridhaa yake mwenyewe ameomba nyongeza ya kuanzia Juni, 2012 hadi Juni, 2013 acheze bure.
Onyewu sasa amepona na yumo kwenye Kikosi cha USA cha Kombe la Dunia linaloanza Afrika Kusini Juni 11.
FIFA kumchunguza kibopa toka England
Kamati ya Maadili ya FIFA itachunguza kauli zinazodaiwa kutolewa na Lord Triesman aliekuwa Kiongozi wa Maombi ya England kuwa Mwenyeji Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 na pia wa FA ya England, nyadhifa ambazo zote amelazimika kujiuzulu kufuatia kuvuja kwa kauli hizo zinazodaiwa alizitoa kuhusu rushwa kwa Vyama vya Soka vya Spain na Urusi kuhusiana na uombaji wa kuwa Wenyeji wa Kombe la Dunia.
Jumapili iliyopita FA ilimbadili Lord Triesman na kumweka Geoff Thompson kama Mwenyekiti wa FA England.
Geoff Thompson ni Makamu wa Rais wa FIFA.
Inadaiwa Lord Triesman alimwambia Msaidizi wake mmoja wa zamani kuwa Spain inapanga kuwahonga Marefa kwenye Fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu na wataisaidia Urusi kushinda Uenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2022 ikiwa Urusi itaisaidia Spain kufanikisha wao kuwa Wenyeji mwaka 2018.
Kamati ya Maombi ya Uenyeji wa Kombe la Dunia ya England imeshapeleka kwa Vyama vya Soka vya Spain na Urusi taarifa za kuomba radhi kwa mkanganyiko uliotokea.

No comments:

Powered By Blogger