Thursday 20 May 2010

Webb kuchezesha Fainali ya UEFA
Refa wa Ligi Kuu Howard Webb ndie atakaechezesha Fainali ya Jumamosi ya UEFA CHAMPIONS LIGI huko Stadio Santiago Bernabeau kati ya Inter Milan na Bayern Munich.
Refa huyu mwenye miaka 38 pia yumo kwenye Kundi la Marefa watakaochezesha Fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Juni 11 huko Afrika Kusini.
Msimu huu, Webb amechezesha mechi 6 za UEFA CHAMPIONS LIGI ikiwemo ile ya Robo Fainali ya kwanza kati ya Inter Milan na CSKA Moscow.
Webb atasaidiwa na Waingereza wenzake Michael Mullarkey na Darren Cann na Refa wa 4 [wa Akiba] Martin Atkinson.
Villa wakataa Pauni Milioni 20 kwa Milner
Aston Villa wameikataa ofa ya Pauni Milioni 20 ya Manchester City ya kumnunua Mchezaji wao James Milner ambae sasa yupo Kikosi cha England kilichopiga Kambi huko Austria kwa ajili ya Kombe la Dunia
Klabu ya Aston Villa imesema imekataa ofa hiyo kwa vile wanataka kukaa chini na Milner mara baada ya Kombe la Dunia kumalizika ili kuuboresha na kuurefusha Mkataba wa Milner.
Hivi karibuni, Milner, mwenye miaka 24, ndie alieshinda Tuzo ya PFA ya Mchezaji Bora Kijana kwa Msimu wa 2009/10 na alinunuliwa na Villa toka Newcastle mwaka 2008 kwa Pauni Milioni 12 kwa Mkataba wa Miaka minne.
Bifu la Boateng na Ballack
Kiungo wa Portsmouth Kevin-Prince Boateng amedai Michael Ballack alimzaba kibao na hilo ni jambo baya kupita rafu aliyocheza yeye na kumuumiza na kumkosesha Fainali za Kombe la Dunia.
Ballack ameripotiwa kumlaumu sana Boateng ambae alizaliwa Ujerumani na kuichezea Nchi hiyo Timu zake za Vijana lakini kwenye Kombe la Dunia ameamua kuchezea Ghana ambako Baba yake ndiko anakotoka.
Boateng amedai Ballack analalamika sana lakini amesahau kuwa yeye Ballack aliwahi kupigwa kibao na Mchezaji mwenzake wa Ujerumani Lukas Podolski na akaligeuza tukio hilo nongwa kwa kulalamika kwa wiki kadhaa.
Boateng amesema inashangaza kumwona Ballack akilalamikia kitu ambacho yeye mwenyewe ni kawaida kufanya.
Boateng vilevile amemponda Kocha wa Ujerumani Joachim Low kwa kusema rafu ya Boateng kwa Ballack ilistahili Kadi Nyekundu.
Boateng amehoji: “Nikisikia hilo naona wao ni ndumilakuwili! Je Nahodha wake anaweza kumzaba mtu amtakae kibao na asichukuliwe hatua? Ningefanya mimi hilo ningefungiwa kwa miaka! Ndio maana nimegoma kuchezea Ujerumani na kuichagua Ghana!”
Ghana na Ujerumani zipo Kundi D kwenye Fainali za Kombe la Dunia na zitacheza Juni 23 Mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Kingine chenye mvuto kwenye sakata la Boateng na Ujerumani ni kuwa mdogo wake, Beki Jerome Boateng, yupo kwenye Kikosi cha Ujerumani.

No comments:

Powered By Blogger