Saturday 24 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Drogba kuukosa mwanzo Msimu Mpya
Straika wa Chelsea, Didier Drogba, ataukosa mwanzo wa Msimu mpya huko England baada ya kufanyiwa Operesheni ya nyonga yake iliyokuwa ikimsumbua toka mwishoni mwa Msimu uliokwisha.
Drogba, Miaka 32, alichelewesha kufanya operesheni hiyo ili aiwakilishe Nchi yake Ivory Coast Fainali za Kombe la Dunia lakini akakumbwa na kuvunjika kiwiko cha mkono wa kulia kabla ya Fainali hizo na ilibidi acheze huko Afrika Kusini huku amevaa gamba gumu kuulinda mkono huo alipopewa kibali maalum na FIFA kulivaa gamba hilo.
Inakadiriwa Drogba atakuwa nje ya uwanja kwa Wiki 3 na ataikosa mechi ya fungua pazia kugombea Ngao ya Hisani hapo Agosti 8 Uwanjani Wembley Chelsea watakapoivaa Manchester United.
Licha ya Drogba, Chelsea pia itawakosa kwa Wiki kadhaa mwanzo wa Msimu mpya Kipa Petr Cech, Difenda Alex na Mchezaji mpya Benayoun kwani wote ni majeruhi.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Ramalho agomewa na Fluminence, Brazil wampa ofa Menezes
Fluminense imekataa Kocha wao Muricy Ramalho aende kuifundisha Brazil na badala yake CBF, Shirikisho la Soka la Brazil, limempa ofa Kocha wa Corinthians, Mano Menezes, kuwa Kocha mpya wa Brazil kuchukua nafasi ya Dunga alietimuliwa.
Menezes, Miaka 48, amesema atatoa uamuzi wake baadae leo.
Inaaminika listi ya CBF ya Makocha ambao wanafaa kuwa Kocha wa Brazil wako Luiz Felipe Scolari, aliewahi kuifundisha Brazil, Ureno na Chelsea, Wanderley Luxemburgo, aliewahi kuwa Kocha wa Brazil, na Leonardo, aliekuwa Kocha wa AC Milan.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Arsene na Arsenal yake
Arsene Wenger amesema Nahodha wake Cesc Fabregas atarudi kiwango chake cha kawaida ikifika Septemba mwaka huu kufuatia kuumia muda mrefu na kushiriki Kombe la Dunia huko Afrika Kusini ambako Nchi yake Spain ilitwaa Ubingwa wa Dunia.
Wenger ametamka: “Kimwili, ni bora kama hukucheza Kombe la Dunia kwani unapumzika lakini kiakili, ukicheza Kombe la Dunia, ni vigumu kupumzika na kurudi uko fiti Msimu mpya unapoanza.”
Cesc Fabregas na Robin van Persie wote walicheza Fainali ya Kombe la Dunia Julai 11 huko Afrika Kusini Nchi zao Spain na Holland zilipokutana na wote bado wako likizo hadi mwishomi mwa Julai.
Hata hivyo, Van Persie alikosa Miezi mitano ya Msimu uliokwisha kwa vile alikuwa majeruhi.
Huenda Fabregas na Van Persie wakacheza mechi yao ya kwanza kwa Arsenal hapo Agosti 7 huko Poland watakapocheza mechi ya kirafiki na Legia Warsaw, mechi ambayo ni ya wajibu kufuatia Mkataba wa Kipa wao Lukasz Fabianski kuwa na kipengele Arsenal icheze na Timu hiyo ya zamani ya Kipa huyo.
Kuhusu Theo Walcott na Samir Nasri, ambao wote hawakuchukuliwa na Timu zao za Taifa kwenda Kombe la Dunia Afrika Kusini, Wenger ametamka: “Sasa wapo na morali kubwa baada ya kuhuzunishwa kutocheza Kombe la Dunia. Siku zote Wachezaji kama hawa baada ya kuvunjika moyo hurudi uwanjani na ari mpya. Nasri yuko fiti mno!”
Juzi Samir Nasri aliifungia Arsenal bao 2 katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Sturm Graz.
Arsene Wenger pia alitaja kuwa majeruhi wake, Denilson na Nicklas Bendtner, hawako katika hali mbaya sana.
CHEKI: www.sokainbongo.com

MATOKEO Mechi za Kirafiki Julai 23:
Ajax Amsterdam 3 v Chelsea 1
Deportivo la Coruna 1 v FC Twente 1 [FC Twente yashinda penalti 5-4]
Freiburg 1 v Werder Bremen 2
Panathinaikos 0 v West Ham 1
Manchester City 0 v Sporting Lisbon 2
Kocha adai amepewa ofa kuifundisha Brazil
Meneja wa Fluminense, Muricy Ramalho, amedai kuwa amepewa ofa ya kuchukua nafasi ya Dunga, alietimuliwa, kuifundisha Brazil lakini bado hajaikubali ofa hiyo.
Ramalho aliweza kutwaa Ubingwa wa Brazil mara 3 mfululizo kati ya 2006 na 2008 akiwa na Fluminense.
Ramalho amedai bado hajaongea na Viongozi wa Fluminense ili kuamua hatma yake.
Brazil ndio watakuwa Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014.
Chelsea watwangwa
Jana huko Amsterdam Arena, Uholanzi, Chelsea walichapwa bao 3-1 na Ajax Amsterdam.
Chelsea wako kwenye ziara ya Uholanzi na Ujerumani kwa ajili ya matayarisho ya Msimu mpya.
Huku wakichezesha Wachezaji Vijana wengi, Chelsea walijikuta wako nyuma dakika ya 6 tu baada ya Beki wao Jeffrey Bruma kujifunga mwenyewe.
Lakini dakika ya 25 Straika Daniel Sturridge alisawazisha.
Dakika mbili baadae Kipa wa Chelsea Turnbull alifanya kosa kubwa mpira ulipomponyoka na kumfikia Siem de Jong aliefunga kirahisi.
Dakika za mwishoni, Mchezaji toka Korea, Suk Hyunpjun aliifungia Ajax bao la 3 baada ya pasi ya Daley Blind.
Fulham wamlenga Eriksson na Hitzfeld
Baada ya Ajax Amsterdam kuwawekea ngumu kumchukua Kocha Martin Jol ambae tayari walishakubaliana maslahi binafsi, taarifa za toka ndani ya Klabu zinasema Fulham sasa inawataka ama Sven-Goran Eriksson, aliekuwa Kocha wa Ivory Coast huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia, au Ottmar Hitzfeld, Kocha wa Uswisi.
Eriksson, ambae Mkataba wake na Ivory Coast ulikuwa wa muda mfupi na ulikwisha tu mara baada ya Kombe la Dunia,  mwenyewe anataka kuifundisha Fulham licha ya Ivory Coast kutaka aendelee nao.
Mkataba wa Hitzfeld kwa Timu ya Taifa ya Uswisi unamalizika 2012.
Kwa sasa Fulham iko chini ya usimamizi wa Kocha Msaidizi Ray Lewington.
Vidic aukubali Mkataba mpya
Mkurugenzi Mkuu wa Manchester United, David Gill, ametangaza kuwa wamefikia makubaliano na Nemanja Vidic kuhusu Mkataba mpya na hivyo kuufuta utata wa kubaki kwake Manchester United.
Kumekuwa na habari kuwa Vidic yuko njiani kwenda Real Madrid lakini Gill ameziua habari hizo kwa kutamka: “Mwishoni mwa Msimu uliokwisha tulikaa pamoja na Vidic lakini hatukumaliza na Vidic akaenda kwenye Kombe la Dunia. Lakini baada ya Serbia kumaliza Kombe la Dunia tuliendelea tena kujadiliana na tumeshakubaliana. Atasaini akirudi toka likizo.”
Vidic alijiunga Man United kutoka Spartak Moscow Mwaka 2006 kwa Pauni Milioni 7 na Mkataba wake wa sasa kwa Man United utakwisha 2012.
Inasadikiwa Mkataba mpya una nyongeza ya Miaka miwili na pia Mshahara kupanda toka Pauni 70,000 kwa Wiki hadi 90,000.

Friday 23 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Wachezaji 23 wa Kombe la Dunia Ufaransa watemwa!
Kocha mpya wa Timu ya Ufaransa, Laurent Blanc, amekijulisha Chama cha Soka cha Ufaransa kuwa hatamwita hata Mchezaji mmoja kwa ajili ya mechi ijayo kati ya wale 23 walioiwakilisha Nchi hiyo kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na kukumbwa na kashfa ya ugomvi, kufukuzwa kwa Nicolas Anelka, kogomea mazoezi na hatimae kubwagwa nje ya Mashindano hayo Raundi ya Kwanza tu huku wakiwa mkiani kwenye Kundi lao.
Ufaransa itacheza mechi ya kirafiki na Norway Mjini Oslo hapo Agosti 11 na hiyo itakuwa mechi ya kwanza chini ya Kocha Laurent Blanc.
Bramble ahamia Sunderland
Beki wa Wigan Titus Bramble amehamia Sunderland kwa Mkataba wa Miaka mitatu na kwa dau ambalo halikuanikwa.
Habari hizo zimethibitishwa na Kocha wa Sunderland, Steve Bruce, ambae alikuwa pamoja na Bramble huko Wigan alipokuwa Meneja wa Klabu hiyo.
Bruce ametamka: “Titus, nlipokuwa Wigan alikomaa na kuwa Mchezaji mzuri sana na sikusita katika kumleta Sunderland.”
CHEKI: www.sokainbongo.com

Fabianski Kipa Nambari Wani Ze Gunners?
Baada ya kutamka Kipa wake Manuel Almunia hukumbwa na mchecheto kwenye mechi kubwa na pia kumuwinda Kipa wa Fulham Mark Schwarzer, inaelekea Bosi wa Arsenal Arsene Wenger tayari ashambwaga Almunia na kumteua Lukasz Fabianski kuwa ndie Kipa Nambari Wani.
Kwenye mechi ya kujipima juzi Jumatano ambayo Arsenal walishinda 3-0 dhidi ya Sturm Graz, Fabianski ndie alieanza golini na Kipindi cha Pili akaingizwa mwenzake kutoka Poland Woiciech Szczesny.
Almunia, Miaka 33, aliidakia Arsenal mara 44 Msimu uliopita na aliwahi kuwa Nahodha wakati Cesc Fabregas alipokuwa majeruhi.
Henry afunga bao mechi ya kwanza na Red Bulls
Akicheza mechi yake ya kwanza tangu ajiunge na New York Red Bulls inayocheza MLS huko Marekani akitokea Real Madrid, Thierry Henry alifunga bao dakika ya 25 lakini hilo halikuweza kuiokoa Timu yake mpya kwani ilipigwa bao 2-1 na Tottenham Hotspur.
Mabao ya Tottenham yalifungwa dakika ya 62 na Robbie Keane na la pili na Gareth Bale dakika ya 72.
Mechi hii ilichezwa leo alfajiri Uwanja wa Red Bull huko New York, Marekani.
Mechi za Kirafiki Leo Julai 23:
Ajax Amsterdam v Chelsea
Deportivo la Coruna v FC Twente
Freiburg v Werder Bremen
Panathinaikos v West Ham
Manchester City v Sporting Lisbon
CHEKI: www.sokainbongo.com

Liverpool wapata Mpinzani EUROPA LIGI
Liverpool watakutana na Ranotnicki ya Macedonia kwenye Raundi ya 3 ya Mtoano ya EUROPA LIGI baada ya Timu hiyo ya Macedonia kutoka sare 0-0 na Mirka ya Armenia.
Rabotnicki iliifunga Mirka 1-0 mechi ya kwanza.
Liverpool watacheza mechi ya kwanza na rabotnicki Julai 29 Uwanja wa Anfield na marudio ni Agosti 5 huko Macedonia.
Wakati huohuo, UEFA imeitoa Klabu ya Spain, Mallorca, kwenye Mashindano ya EUROPA LIGI baada ya Klabu hiyo kukumbwa na madeni.
Mallorca imepewa siku 3 kukata rufaa.
Riera kuhamia Olympiakos
Mchezaji wa Liverpool, Riera, amekwenda Ugiriki kukamilisha taratibu za kuhamia Olympiakos.
Riera, Miaka 28, alijiunga Liverpool Mwaka 2008 akitokea Espanyol ya Spain na anategemewa kusaini Mkataba wa Miaka mitatu na Olympiakos.
Vidic kuongezewa Mkataba Man United
Manchester United inategemewa kuuboresha na kuongeza Mkataba wa Beki wao Nemanja Vidic licha ya kuandamwa na uvumi kuwa yuko mbioni kwenda Real Madrid.
Hivi juzi Sir Alex Ferguson alishindwa kuwahakikishia Wanahabari hatma ya Vidic alipokuwa anahojiwa.
Inategemewa Vidic, Miaka 28, ataongezewa Miaka miwili kwenye Mkataba wake unaoisha 2012 na pia Mshahara kupanda kutoka Pauni 70,000 hadi 90,000 kwa wiki.
Vile vile, Sir Alex Ferguson amethibitisha Chipukizi Danny Welbeck na Tom Cleverly, wenye Miaka 20 na 19, watakopeshwa kwa Timu nyingine za Ligi Kuu kwa Msimu ujao ili kuwapa nafasi ya kucheza mechi nyingi na kupata uzoefu zaidi.
Sunderland imeshaonyesha nia ya kumchukua Welbeck.
Milner kuhama Villa
Aston Villa imenyoosha mikono kwa Mchezaji wao James Milner ambae ametaka kuihama Klabu hiyo huku Manchester City ikiwa ndio safari yake.
Martin O’Neill, Meneja wa Villa, meungama kuwa Milner ataondoka lakini kwa dau wanalotaka wao ambalo linakadiriwa kuwa ni Pauni Milioni 30.
Aston Villa walikuwa tayari kuuboresha Mkataba wa Milner na kumfanya awe Mchezaji anaelipwa bora kupita wote hapo lakini mwenyewe ameng’ang’ania kuhama.

Thursday 22 July 2010

PITIA: www.sokainbongo.com

Mvutano kufanya Afrika Kusini isiitwe Bafana Bafana
Wakati kila Mtu anatambua jina Bafana Bafana ni jina maarufu ambalo kila Mtu amelizoea kuwa ni jina la Timu ya Taifa ya Soka ya Afrika Kusini, huenda jina hilo lisitumike tena kuitambua Timu ya Afrika Kusini baada ya kuzuka mzozo mkubwa uliotinga hadi Mahakama Kuu ya Rufaa ya Afrika Kusini na sasa kuelekea Bungeni mwa Nchi hiyo.
Zozo hilo limelipuka baada ya Mfanyabiashara mmoja kupata hatimiliki za jina Bafana Bafana Mwaka 1994.
Ingawa Chama cha Soka cha Afrika Kusini, SAFA, kiliendelea kuiita Timu yao ya Taifa Bafana Bafana lakini hawakuruhusiwa kutumia jina hilo kwenye biashara ya aina yeyote na ndipo gomvi hilo likaangukia Mahakamani Mwaka 1997 na hatimae kuishia Mahakama Kuu ya Rufaa ambako SAFA kilishindwa.
Inasadikiwa Mfanyabiashara mwenye kumiliki jina hilo la Bafana Bafana alivuna kiubwete, bila jasho, faida ya Pauni Milioni 6.5 wakati wa Fainali za Kombe la Dunia zilizoisha hivi karibuni, kwa matumizi ya jina hilo.
Jina la Bafana Bafana, likimaanisha ‘Vidume Vidume’, lilibuniwa na Wanahabari wa Soweto Miaka ya 1990 mara tu baada ya Afrika Kusini kuruhusiwa tena kushiriki Mashindano ya Kimataifa baada ya sera dhalimu za ubaguzi kuuliwa.
Rais wa SAFA, Kirsten Nematandani, amelalama: “Sipendi kusema tuna hasira kuhusu hilo! Tuna wasiwasi kwamba ingawa jina la Bafana Bafana ni rasilimali ya Taifa lakini huenda likabadilika!”
SOMA: www.sokainbongo.com

Fergie hajui kama Vidic anabaki
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amekiri kuwa hana uhakika kama Beki wake Nemanja Vidic atakuwepo Man United Msimu ujao kwa vile kuna tetesi kubwa anaelekea Real Madrid.
Alipohojiwa, Ferguson alikataa kutoa ufafanuzi wowote licha ya kusema anaamini Beki huyo atabaki.
Kwa sasa Vidic na Wachezaji wenzake wengine waliokuwa kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini wamepewa likizo hadi Julai 28.
Hadi sasa hamna tamko lolote rasmi lililotolewa na upande wowote.
Fulham wamkosa Jol
Ajax Amsterdam imemtilia ngumu Meneja wake Martin Jol kuhamia Fulham licha ya Meneja huyo kutaka mwenyewe kuhama na pia kufikia makubaliano na Fulham kuhusu maslahi yake binafsi.
Fulham imekiri kumkosa Jol na imesema ipo mbioni kumsaka Mtu mwingine.
Kwa sasa Fulham haina Meneja baada ya Meneja wao Roy Hodgson kuhamia Liverpool.
Fulham pia imesema Kocha Msaidizi Ray Lewington ataendelea kuiendesha Timu hadi apatikane Meneja mpya.

Wednesday 21 July 2010

SOMA TOVUTI: www.sokainbongo.com

UEFA CHAMPIONS LIGI kuwa na Marefa Watano 2011/12
IFAB [The International Football Association Board], ambao ndio wasimamizi wa kurekebisha sheria za Soka, wamesema UEFA CHAMPIONS LIGI mwakani itakuwa na Waamuzi watano Uwanjani, yaani Refa Mkuu, Washika Vibendera wawili na Wasaidizi wengine wawili ambao kila mmoja atakuwa nyuma ya goli moja.
Mtindo huo uklitumika kwenye mechi za EUROPA LIGI Msimu uliokwisha na pia utaendelea tena kwenye Mashindano hayo Msimu mpya wa 2010/11.
FIFA imesema majaribio ya Marefa hao watano katika mechi moja kwenye Mashindano makubwa kama ya UEFA CHAMPIONS LIGI na EUROPA LIGI yatawasaidia kufikia uamuzi Mwaka 2012 kama mtindo huo uwe wa kudumu.
Majaribio ya mtindo huo yanategemewa kuzagaa kwenye Mashindano makubwa katika Mabara ya Asia na Marekani Kusini.
Matukio ya utata na kusikitisha kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini hasa yale ya England kunyimwa goli la wazi kwa mpira kudunda Mita moja ndani ya goli na Refa kuwa kipofu katika mechi na Germany na lile la Ghana kufunga goli lilionekana kudakwa mstarini na Suarez wa Chile ndiyo yameiamsha FIFA kufikiria kubadili mitindo yake.
Mwezi Oktoba FIFA na IFAB zinategemewa kujadili kutumia teknolojia ya kisasa kwenye mstari wa goli ili kuwasaidia Marefa kutoa uamuzi wa uhakika na haraka kama mpira umevuka mstari au la.
SOMA PIA: www.sokainbongo.com

Kipa Cech aumia, nje Wiki 4
Kipa Nambari Wani wa Mabingwa wa Ligi Kuu England, Petr Cech, ataukosa mwanzo wa Msimu mpya baada ya kuumia mguu mazoezini hapo jana Jumanne na atakuwa nje kwa Mwezi mmoja.
Uchunguzi wa kina umethibitisha kuwa amechanika musuli za mguu wake wa kulia.
Chelsea wana Makipa wengine wawili, Ross Turnbull na Henrique Hilario.
Mechi ya kwanza kwa Msimu mpya kwa Chelsea ni ile mechi ya kugombea Ngao ya Hisani hapo Agosti 8 watakapocheza na Manchester United Uwanja wa Wembley na wataanza kampeni yao ya kutetea Ubingwa wa Ligi Kuu hapo Agosti 14 watakapocheza na West Bromwich Albion, Timu ambayo imepanda Daraja Msimu huu.
Degen ruksa kuondoka Liverpool
Meneja mpya wa Liverpool Roy Hodgson amemwambia Beki Philipp Degen yuko huru kuhama Klabi hiyo ikiwa atapenda.
Degen, Beki wa Kimataifa wa Uswisi mwenye Miaka 27, alitua Liverpool Julai 2008 akitokea Borussia Dortmund, ameanza mechi 8 tu na kuingizwa toka benchi mechi 5 tu katika muda wote akiwa Liverpool.
Hodgson ametamka: “Tumekuwa nae kwenye mazungumzo mazuri na tumekubaliana yuko huru kutafuta Klabu nyingine.”
Hodgson yuko mbioni kuisuka upya Liverpool na tayari ameshawanasa Wachezaji wapya wawili, Fowadi wa England Joe Cole na yule wa Serbia Milan Jovanovic, na pia wameshakubaliana na Rangers ya Scotland kumsaini Beki Chipukizi Danny Wilson.
Vilevile, Hodgson amepata uhakika wa Nahodha Steven Gerrard kubakia Liverpool baada ya kufanya nae mazungumzo kufuatia uvumi kuwa anataka kuondoka.
Sasa Hodgson atakuwa akiomba Mastaa wake wawili, Fernando Torres na Javier Mascherano, watafuata nyayo za Gerrard.

Tuesday 20 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Man City yampuuza Drogba
Manchester City imezipuuza taarifa za kutaka kumchukua Didier Drogba ambazo Wakala wa Mchezaji huyo wa Chelsea amezitangaza.
Wakala huyo, Thierno Seydi, alidokeza kwenye mahojiano na Kituo kimoja cha Radio kuwa Drogba anaweza kuhama kutoka Chelsea kabla dirisha la uhamisho halijafungwa kwa vile yapo mazungumzo baina yao.
Lakini Man City, ambao tayari wameshatumia Pauni Milioni 60 kuwanunua Jerome Boateng, David Silva na Yaya Toure kwa ajili ya Msimu mpya, wamekanusha madai hayo na kusema hayana ukweli.
Drogba, Miaka 32, ndie alikuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Msimu uliokwisha kwa kupachika mabao 29 na amekuwapo Chelsea kwa Miaka 6 tangu ahamie hapo kutoka Marseille ya Ufaransa.
Seydi, akiongea na Radio RMC ya Ufaransa, alitamka: “Leo yupo Chelsea. Pengine kutakuwa na maajabu kabla ya Agosti 31. Sijaongea na Mtu yeyote ila ni Man City tu! Sisi tunamsikiliza kila Mtu”
Skandali zaiandama Ufaransa!!!
Baada ya kubwagwa nje ya Kombe la Dunia huko Afrika Kusini Raundi ya Kwanza tu na kushika mkia Kundi lao, Ufaransa, iliyogubikwa na kashfa ya ugomvi uliomfanya Mchezaji Nicolas Anelka afukuzwe huko Afrika Kusini na Wachezaji kugomea mazoezi, imetumbukizwa tena kwenye kashfa nzito baada ya uchunguzi wa Polisi uliokuwa ukizizima chini kwa chini kuibuka ghafla na kusababisha leo Wachezaji Mastaa, Franck Ribery na Karim Benzema, kuitwa Polisi na kuhojiwa kuhusu madai ya kutoa malipo ili kufanya ngono na Kahaba alie na umri mdogo ambao kisheria ulikuwa ukimtambua kama mtoto.
Uchunguzi wa Polisi ulianza tangu Aprili baada ya kuivamia Baa ya usiku huko Paris, Ufaransa na madai ya Kahaba huyo, Zahia Dehar, kwamba alitembea na Wachezaji wawili wakati umri wake ukiwa mdogo.
Hata hivyo, kitu kizuri kwa Benzema na Ribery, ni kuwa Zahia, mwenye Miaka 16, akiwa Miaka miwili chini ya umri unaoruhusiwa kwa Wafanyakazi halali wa ngono huko Ufaransa, amedai hakuwaambia Wachezaji hao kuwa alikuwa chini ya umri halali kwa Wafanyakazi wa fani hiyo.
Kisheria huko Ufaransa, kauli ya Zahia itawanusuru Mastaa hao.
Wote, Ribery, anaecheza Bayern Munich, na Benzema wa Real Madrid, wamekanusha kufanya kosa lolote.
Wakati Benzema amesema hahusiki na Binti huyo, Ribery amekiri kutembea nae lakini amesisitiza hakujua kama alikuwa ni chini ya umri halali.
Wakili wa Ribery, Sophie Bottai, amezungumza kuwa Mteja wake hastahili kuwa Kituo cha Polisi bali Uwanja wa Mpira.
Bottai amedai: “Uhalifu huu anaotuhumiwa, kisheria, lazima uwe na kusudio: inabidi awe anajua umri wa huyo Binti, na hilo hakujua! Inabidi huyo Binti awe anaonekana kama ni mdogo, hilo halikuwepo! Na inabidi Binti huyo adai alimwambia kuwa yeye ni mtoto, na hilo, pia, halikuwepo!”
Huko Ufaransa, ukipatikana na hatia ya kudai au kufanya ngono na Kahaba alie chini ya umri halali adhabu yake ni kifungo cha mpaka Miaka mitatu na faini ya Pauni 38,000.
Lakini ni jukumu la Upande wa Mashitaka kuthibitisha kuwa Mtuhumiwa aliujua umri wa Kahaba.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Vuvuzela marufuku Emirates & White Hart Lane
Klabu za Arsenal na Tottenham zimekuwa za kwanza toka kwenye Ligi Kuu England kutangaza kuwa Vuvuzela ni marufuku kwenye Viwanja vyao.
Vuvuzela zilishamiri huko Afrika Kusini wakati wa Kombe la Dunia na kufanya baadhi ya Timu na Wanahabari, hasa wa TV, kulalamikia matumizi yake yaliyozima kabisa sauti za Washabiki.
Tottenham imekuwa Klabu ya kwanza kuzipiga marufuku Uwanjani kwao White Hart Lane na wamedai zitavuruga ushangiliaji wa Washabiki wao na pia kuwa tishio kwenye usalama wa Washabiki hao kwani zikiwa zinapulizwa zinaweza kuwafanya wasisikie matangazo ya usalama wakati wa dharura.
Mara baada ya Tottenham kutoa taarifa hizo wakafuata jirani zao Arsenal ambao wametoa sababu hizo hizo katika kuzikataza Vuvuzela.
Gerrad hang’oki Liverpool
Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, amedokeza kuwa hana mpango wa kuhama wakati alipozungumzia kuhusu kusajiliwa Joe Cole.
Gerrard amesema: “Nilitaka mazungumzo na Meneja Roy Hodgson. Baada ya kuongea nae nimeridhika na plani zake. Ndio kwanza nimeanza mazoezi na nangojea kwa hamu Msimu mpya uanze.”
Gerrard, Miaka 30, amekuwa akivumishwa kuhamia kwa Jose Mourinho huko Real Madrid lakini kurudi kwake mazoezini hapo jana Jumatatu pamoja na wenzake Jamie Carragher na Glen Johnson ambao wote kwa pamoja walikuwa kwenye Kikosi cha England cha Kombe la Dunia huko Afrika Kusini, kumetuliza Mashabiki wa Liverpool.
Kuhusu kusainiwa Joe Cole Liverpool, Gerrard ametamka: “Ni usajili mzuri kwetu. Ni Mchezaji mzuri sana.”
Loew kubaki Kocha wa Germany
Kocha wa Timu ya Taifa ya Germany Joachim Loew amesaini Mkataba mpya na atakuwa na Timu hiyo hadi 2012.
Mkataba wa Loew ulimalizika mara baada ya Kombe la Dunia kuisha na aliiwezesha Timu hiyo kufika Nusu Fainali ya Mashindano hayo na kutolewa na Spain.
Wasaidizi wa Loew kwenye Timu hiyo, Oliver Bierhoff, aliekuwa Timu Meneja, Kocha Msaidizi, Hans Dieter Flick na Kocha wa Makipa, Andreas Kopke, wote kwa pamoja, wamekubali kuendelea kubaki kuwa na Loew.
Kazi iliyo mbele ya Loew ni kuhakikisha Germany inafuzu na kuingia Fainali za EURO 2012 zitakazochezwa huko Poland na Ukraine kwa pamoja.
Eduardo anaelekea Shakhtar
Klabu ya Ukraine, Shakhtar Donetsk, iko mbioni kumsaini Fowadi wa Arsenal Eduardo da Silva na inadaiwa tayari washafikia makubaliano na Arsenal kuhusu ada watakayotakiwa kulipa kumchukua Mchezaji huyo.
Eduardo, Miaka 27, Mchezaji wa Kimataifa wa Croatia mwenye asili ya Brazil, amekuwa na wakati mgumu huko Arsenal tangu avunjike vibaya mguu walipocheza na Birmingham Februari 2008 kwani fomu yake ilikuwa haijarudi sawa na kumfanya asicheze mechi mara kwa mara.
Arsenal tayari wameimarisha Fowadi kwa kumsajili Marouane Chamakh.
Kocha wa Shakhtar Donetsk, Mircea Lucescu, amesema Eduardo ni mzuri licha ya kutopata namba mara kwa mara na hilo limeungwa mkono na Kocha wa Croatia, Bilic, ambae amesema kuhamia kwa Eduardo huko Ukraine kutampa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Monday 19 July 2010

PITIA: www.sokainbongo.com

FIFA yaanza ukaguzi wagombea Uenyeji 2018 & 2022
Wakaguzi wa FIFA leo wanaanza ziara yao itakayodumu Miezi miwili kuzikagua Nchi zilizoomba kuwa Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 2018 na 2022.
Fainali za Kombe la Dunia Mwaka huu zilifanyika huko Afrika Kusini na kumalizika Julai 11 na zile zinazofuata za Mwaka 2014 zitakuwa Brazil.
Wakaguzi hao watakuwa kila Nchi ya muombaji kwa Siku 3.
Ziara hiyo itaanzia Japan, Korea Kusini, Australia na kisha kwa waombaji wa pamoja Uholanzi na Ubelgiji, baadae England, na kwa waombaji wengine wa pamoja Spain na Ureno, kisha USA na halafu Qatar.
Timu hiyo ya Wakaguzi inaongozwa na Rais wa Shirikisho la Soka la huko Chile, Harold Mayne-Nicholls.
FIFA itatoa uamuzi nani watakuwa Wenyeji Mwaka 2018 na 2022 kufuatia mkutano wao huko Zurich, Uswisi Desemba 2, Mwaka huu.
RATIBA YA UKAGUZI:
-Julai 19-22: Japan [Wameomba 2022]
-Julai 22-25: Korea Kusini [Wameomba 2022]
-Agosti 9-12: Uholanzi & Ubelgiji [Waombaji wa pamoja]
-Agosti 16-19: Urusi
-Agosti 23-26: England
-Agosti 30-Septemba 2: Spain & Ureno [Waombaji wa pamoja]
-Septemba 6-9: USA
-Septemba 13-17: Qatar [Wameomba 2022]
CHEKI: www.sokainbongo.com

Giggs akiri Man United ni ya Vijana!
Mkongwe Ryan Giggs amekiri Manchester United ya Msimu wa 2010/11 uanzao Agosti 8 kwa mechi ya fungua pazia kugombea Ngao ya Hisani kati ya Mabingwa wa Ligi Kuu Chelsea na Manchester United Uwanjani Wembley Jijini London ni ya Chipukizi.
Giggs amesema Wachezaji wapya Chipukizi, Chris Smalling na Javier Hernandez, pamoja na Chipukizi waliojitokeza na kung’ara Msimu uliopita kama Nani, Antonio Valencia, Jonny Evans na Mapacha wa Brazil, Rafael na Fabio, ndio nafasi yao kuibeba Man United kwenye ushindi.
Giggs ametamka: “Msimu uliokwisha Wachezaji wengi Vijana walicheza Timu ya Kwanza. Nani alikuwa na Msimu mzuri, Valencia ulikuwa Msimu wake wa kwanza mzuri tu, Macheda alipata mbaya ya kuumia na sasa tumewapata Smalling na Hernandez!”
Giggs, ambae ameshashinda Mataji 11 ya Ligi Kuu akiwa na Man United, amedai kila Mchezaji hapo Old Trafford ana usongo wa kulirudisha Taji lao Klabuni hapo toka Chelsea.
Nae, Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amefurahishwa na mchezo wa Difenda mpya Chipukizi Chris Smalling aliecheza mechi yake ya kwanza akiwa na Jezi ya Man United walipoifunga Celtic bao 3-1 huko Toronto, Canada hapo juzi.
Fergie ametamka: “Nimefurahishwa na uchezaji wake. Ni mwepesi na mtoaji pasi nzuri.”
Katika mechi hiyo ya kujipima nguvu, Smalling alicheza Sentahafu pamoya na Jonny Evans ikiwa ni mara yao ya kwanza kucheza pamoja.
CAF CHAMPIONS LIGI:
MATOKEO MECHI ZA MAKUNDI:
Julai 16: ES Setif [Algeria] 0 Esperance [Tunisia] 1
Julai 17: Dynamo [Zimbabwe] 0 TP Mazembe [Congo] 2
Julai 18:
Heartland [Nigeria] 1 El Ahly [Egypt] 1
El Ismaily [Egypt] 0 JS Kabylie [Algeria] 1
CHEKI: www.sokainbongo.com

Cole ni Liverpool!!!
Joe Cole atakuwa Mchezaji mpya rasmi wa Liverpool kwa Mkataba wa Miaka minne endapo atapita upimwaji wa afya yake unaotegemewa kufanyika katika Masaa 48 yajayo baada ya pande zote mbili kufikia makubaliano.
Cole amekuwa Mchezaji huru tangu mwanzoni mwa Mwezi huu baada ya Mkataba wake huko Chelsea, ambako alidumu Miaka 7, kumalizika bila ya maelewano ya kuundeleza.
Mchezaji huyo mwenye umri wa Miaka 28 alitua Chelsea akitokea West Ham Mwaka 2003.
Habari za Joe Cole kujiunga na Anfield zimethibitishwa na tovuti ya Liverpool.
Jol kutinga Fulham
Martin Jol anategemewa kutajwa kuwa ndie Meneja mpya wa Fulham kuchukua nafasi ya Roy Hodgson ambae amehamia Liverpool.
Jol, Miaka 54, ni Kocha wa Ajax ya Uholanzi kwa sasa na aliwahi kuifundisha Tottenham kati ya Mwaka 2004 na 2007.
Fulham imekuwa ikihusishwa na kuwachukua Kocha wa Ivory Coast Sven-Goran Eriksson, Kocha wa USA Bob Bradley na hata Kocha wa Uswisi Ottmar Hitzfield lakini kuna kila dalili nafasi hiyo imetwaliwa na Martin Jol ambae leo anategemewa kujiunga na Msafara wa Timu ya Fulham kwenda kwenye ziara ya Siku 10 huko Sweden kwa ajili ya maandalizi ya Msimu mpya.

Sunday 18 July 2010

PITIA: www.sokainbongo.com

Pique aonya: “Rooney ni Mbogo aliejeruhiwa!”
Mchezaji wa Mabingwa wa Kombe la Dunia Spain, Gerard Pique, anaechezea FC Barcelona, amewaonya wapinzani wa Manchester United kwenye Ligi Kuu kuwa Wayne Rooney atarudi Msimu mpya kama Mbogo aliejeruhiwa.
Pique, aliewahi kucheza na Rooney Man United kuanzia Mwaka 2004 hadi 2008 aliporudi tena Barcelona, amesema hajawahi kumwona Mchezaji akikasirika na kuumia moyo wakifungwa kama Rooney.
Pique ametamka: “Matokeo ya England huko Afrika Kusini na uchezaji wake utakuwa umemuumiza roho sana! Watu wanaweza kufikiri Wachezaji siku hizi wanalipwa pesa nyingi na haiwaumi wakifungwa lakini hebu wamtazame Rooney tu baada ya kufungwa kwenye chumba cha kubadilisha Jezi! Huwezi kuongea nae kwani ni kama Mtu anaeweza kulipuka dakika yeyote tu! Na Wachezaji wengi hupoa wikiendi baada ya mechi lakini Rooney hurudi Jumatatu akiwa na moto wa kulipiza kisasi! Hilo litawasaidia sana Man United!”
Kuhusu taarifa za Real Madrid na Klabu yake Barcelona kumtaka Rooney, Gerard Pique amesema hadhani kama Rooney atahama Man United kwa jinsi alivyokuwa na uhusiano mzuri na Meneja wake Sir Alex Ferguson.
Pique ametamka: “Rooney na Sir Alex ni kama Baba na Mwana! Sidhani kama Rooney atataka kuhama! Sir Alex ni Meneja mzuri mno na ni muungwana na mwema kwa kila Mchezaji! Lakini kwa Rooney, huyo ni kama Mtoto wake kipenzi!”
CHEKI: www.sokainbongo.com

Liverpool kumuuza Insua
Liverpool wamekubaliana na Klabu ya Italia Fiorentina ili kumuuza Fulbeki wao Emiliano Insua na tayari Beki huyo ameshaondoka kambi ya mazoezi huko Uswisi walikokuwa wakijitayarisha kwa Msimu mpya kwenda Italia kujadiliana na Fiorentina kuhusu maslahi yake binafsi.
Insua, Miaka 21, alijunga Januari 2007 akitokea Klabu ya kwao huko Argentina Boca Juniors na ameichezea Liverpool mechi 62 na kufunga bao moja.
Liverpool watalazimika kutafuta Beki wa kushoto baada ya Fabio Aurelio nae kuhama Mwezi Juni.
Wenger ataka wamkome Fabregas!
Arsene Wenger anategemea uvumi na maneno kwamba Nahodha wake hapo Arsenal, Cesc Fabregas, anahamia FC Barcelona sasa utakoma baada ya yeye na Fabregas kukutana na kufanya mazungumzo.
Arsenal tayari wameshaikataa ofa ya Barca na hivi juzi Rais wa Barca, Sandro Rosell, alionekana kukiri kushindwa kwao kumtoa Fabregas Arsenal.
Ingawa Wenger amegoma kutoboa nini alizungumza na Fabregas lakini amesema: “Kumekuwa na mengi yamesemwa! Siku zote nimekuwa nikisema Fabregas ni Nahodha wetu na ni Mtu muhimu kwetu! Tunataka abaki na ndio maana hatutaki kusikiliza ofa yeyote.”
Terry kulikwaa shoka la Capello
Nahodha wa zamani wa Italia, Fabio Cannavaro, ambae anamjua vyema Kocha wa England, Fabio Capello, ambae ni Mtaliana mwenzake, amedai John Terry hataendelea tena kuchezea England chini ya Capello.
Terry alikwaruzana na Capello huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia wakati alipodai Wachezaji wa England wako tayari kumhoji Capello kuhusu mbinu na uteuzi wa Timu na Capello akajibu kwa kudai Terry anafanya ‘kosa kubwa’ lakini hakumtema na England wakatupwa nje ya Kombe la Dunia walipopigwa 4-1 na Germany.
Cannavaro, aliewahi kufundishwa na Capello huko Real Madrid, amesema: “Mawazo yangu ni kuwa Terry hawezi kuwamo tena kwenye England ya Capello!”
Cannavaro akaongeza: “Huwezi kumkosa Fabio na akakutazama tu!”
Pia, Cannavaro amedai kuwa katika Kikosi cha England kilichocheza na kufungwa na Germany huko Afrika Kusini hadhani kama zaidi ya Wachezaji watano watabakia kwenye Timu ya baadae ya Capello na amesema ni Wachezaji wawili tu ndio wenye uhakika wa kuwemo kwenye Kikosi cha England na hao akawataja ni Ashley Cole na Wayne Rooney.
Powered By Blogger