Tuesday, 20 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Vuvuzela marufuku Emirates & White Hart Lane
Klabu za Arsenal na Tottenham zimekuwa za kwanza toka kwenye Ligi Kuu England kutangaza kuwa Vuvuzela ni marufuku kwenye Viwanja vyao.
Vuvuzela zilishamiri huko Afrika Kusini wakati wa Kombe la Dunia na kufanya baadhi ya Timu na Wanahabari, hasa wa TV, kulalamikia matumizi yake yaliyozima kabisa sauti za Washabiki.
Tottenham imekuwa Klabu ya kwanza kuzipiga marufuku Uwanjani kwao White Hart Lane na wamedai zitavuruga ushangiliaji wa Washabiki wao na pia kuwa tishio kwenye usalama wa Washabiki hao kwani zikiwa zinapulizwa zinaweza kuwafanya wasisikie matangazo ya usalama wakati wa dharura.
Mara baada ya Tottenham kutoa taarifa hizo wakafuata jirani zao Arsenal ambao wametoa sababu hizo hizo katika kuzikataza Vuvuzela.
Gerrad hang’oki Liverpool
Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, amedokeza kuwa hana mpango wa kuhama wakati alipozungumzia kuhusu kusajiliwa Joe Cole.
Gerrard amesema: “Nilitaka mazungumzo na Meneja Roy Hodgson. Baada ya kuongea nae nimeridhika na plani zake. Ndio kwanza nimeanza mazoezi na nangojea kwa hamu Msimu mpya uanze.”
Gerrard, Miaka 30, amekuwa akivumishwa kuhamia kwa Jose Mourinho huko Real Madrid lakini kurudi kwake mazoezini hapo jana Jumatatu pamoja na wenzake Jamie Carragher na Glen Johnson ambao wote kwa pamoja walikuwa kwenye Kikosi cha England cha Kombe la Dunia huko Afrika Kusini, kumetuliza Mashabiki wa Liverpool.
Kuhusu kusainiwa Joe Cole Liverpool, Gerrard ametamka: “Ni usajili mzuri kwetu. Ni Mchezaji mzuri sana.”
Loew kubaki Kocha wa Germany
Kocha wa Timu ya Taifa ya Germany Joachim Loew amesaini Mkataba mpya na atakuwa na Timu hiyo hadi 2012.
Mkataba wa Loew ulimalizika mara baada ya Kombe la Dunia kuisha na aliiwezesha Timu hiyo kufika Nusu Fainali ya Mashindano hayo na kutolewa na Spain.
Wasaidizi wa Loew kwenye Timu hiyo, Oliver Bierhoff, aliekuwa Timu Meneja, Kocha Msaidizi, Hans Dieter Flick na Kocha wa Makipa, Andreas Kopke, wote kwa pamoja, wamekubali kuendelea kubaki kuwa na Loew.
Kazi iliyo mbele ya Loew ni kuhakikisha Germany inafuzu na kuingia Fainali za EURO 2012 zitakazochezwa huko Poland na Ukraine kwa pamoja.
Eduardo anaelekea Shakhtar
Klabu ya Ukraine, Shakhtar Donetsk, iko mbioni kumsaini Fowadi wa Arsenal Eduardo da Silva na inadaiwa tayari washafikia makubaliano na Arsenal kuhusu ada watakayotakiwa kulipa kumchukua Mchezaji huyo.
Eduardo, Miaka 27, Mchezaji wa Kimataifa wa Croatia mwenye asili ya Brazil, amekuwa na wakati mgumu huko Arsenal tangu avunjike vibaya mguu walipocheza na Birmingham Februari 2008 kwani fomu yake ilikuwa haijarudi sawa na kumfanya asicheze mechi mara kwa mara.
Arsenal tayari wameimarisha Fowadi kwa kumsajili Marouane Chamakh.
Kocha wa Shakhtar Donetsk, Mircea Lucescu, amesema Eduardo ni mzuri licha ya kutopata namba mara kwa mara na hilo limeungwa mkono na Kocha wa Croatia, Bilic, ambae amesema kuhamia kwa Eduardo huko Ukraine kutampa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

No comments:

Powered By Blogger