Saturday, 25 April 2009

LIGI KUU England WIKIENDI HII: [Saa ni za Bongo]

JUMAMOSI, 25 April 2009
[Saa 11 jioni]
Bolton v Aston Villa
Everton v Man City
Fulham v Stoke
Hull v Liverpool
West Brom v Sunderland
West Ham v Chelsea
[Saa 1 na nusu usiku]

Man U v Tottenham


JUMAPILI, 26 April 2009
[Saa 9 na nusu]
Arsenal v Middlesbrough
[Saa 12 jioni]
Blackburn v Wigan


JUMATATU, 27 April 2009
[Saa 4 usiku]
Newcastle v Portsmouth

Man U: Wanashughulikia Tevez kubakia hapo!
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amesema wanashughulikia suala la Carlos Tevez kuendelea kubaki Klabuni hapo huku kukiwa na tetesi nyingi kuwa Mchezaji huyo huenda akaondoka mwishoni mwa msimu mkataba wake wa kucheza hapo kwa mkopo utakapoisha.
Ferguson ametamka: 'Tunaifanyia kazi ishu hiyo. Muhimu ni kuwa Tevez mwenyewe anapenda kubaki hapa.'
Fabregas na Phil Brown, Meneja wa Hull, matatani na FA!!
FA, Chama cha Soka England, kimewafungulia mashtaka Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, na Meneja wa Hull City, Phil Brown, kufuatia tafrani zilizotokea kwenye mechi kati ya Arsenal na Hull ya Kombe la FA ambyo ilichezwa katikati ya Machi na Arsenal kushinda 2-1.
Fabregas anakabiliwa na mashtaka mawili, moja likiwa ni vitendo vyake baada ya kuingia uwanjani mechi ilipomalizika na la pili ni kumtemea mate Meneja Msaidizi wa Hull, Brian Horton.
Siku hiyo Fabregas alikuwa si Mchezaji kwani alikuwa majeruhi.
Nae Phil Brown anakabiliwa na mashtaka ya kuuingiza mchezo kwenye kashfa kufuatia kauli zake baada ya mechi za kumkashifu Refa Mike Riley.
Watuhumiwa wote wawili wamepewa mpaka Mei 12 ili kujibu mashtaka hayo.

Thursday, 23 April 2009

Scholes afikisha mechi 600 Man United!!

Kiungo wa Mabingwa Manchester United Paul Scholes, jana alipocheza katika mechi ya LIGI KUU England dhidi ya Portsmouth ambayo Man U walishinda mabao 2-0 na kupaa kileleni mwa ligi hiyo, amefikisha jumla ya mechi 600 kwenye Klabu hiyo na sasa yeye ni Mchezaji wa 4 katika safu ya Wachezaji wa Klabu hiyo waliocheza mechi nyingi katika historia yake. Ryan Giggs, ambae jana pia alicheza, ndie anaeongoza kwa mechi 799, Sir Bobby Charlton mechi 758 na Bill Foulkes mechi 658.
Scholes ni Mchezaji asie na makuu, mkimya sana na siku zote hapendi kutangazwa lakini watu humsifia kama alivofanya Mchezaji Bora wa zamani Duniani, Zinedine Zidane ambae aliwahi kusema: 'Ni Kiungo Bora Duniani katika Wachezaji wa rika lake!!'
Paul Scholes ambae sasa ana umri wa miaka 34 alianza kuichezea Man U tangu akiwa na miaka 19 na ameshafunga jumla ya mabao 142.
Rio Ferdinand anamwelezea: 'Tukiwa nae mazoezini huwa anafanya vitu vya ajabu ambavyo hakuna Mchezaji mwingine anaweza! Siku moja tukiwa mazoezini kwenye Kituo chetu Carrington, nadhani alikuwa Rooney, alikuwa anajisaidia pembeni mwa uwanja mita kama 80 toka tulipo. Scholes akachukua mpira na kutuonyesha alipo Rooney. Akafumua shuti umbali huo wa mita kama 80 na kumpiga Rooney na mpira!! Wote tukajaribu kulenga umbali ule na hakuna hata mmoja aliefanikiwa kupata shabaha!! Vitu kama hivyo anavifanya mara kwa mara tu!!!'
Kepteni wake wa zamani Roy Keane anasema: 'Ni mchezaji Staa anaeshangaza!! Hana makuu!!'
Nae Mfaransa Laurent Blanc aliekuwa Nahodha wa Ufaransa na aliewahi kuchezea Man U amesifia: 'Huwa namwambia kila mtu anaeniuliza- Scholes ndie bora Uingereza!!'
Sir Bobby Charlton, mwenyewe akiwa Mchezaji wa zamani alietukuka na kusifika, anatoa sifa za kipekee: 'Kuna Wachezaji niliowaabudu na wakapotea kwenye ajali ya ndege ya Timu ya Man U kule Munich, kuna Wachezaji kama Dennis Law na George Best ambao nilicheza nao, na sasa, kuna Wachezaji wa Sir Alex Ferguson ambao nawatizama lakini katika wote hakuna bora kama Paul Scholes!!'
Chelsea wabwaga manyanga!!! Wakiri kutwaa Ubingwa LIGI KUU ni ndoto!!
Meneja wa Chelsea, Guus Hiddink, baada ya Timu yake jana kutoka suluhu 0-0 na Everton na hivyo kujikuta wakiwa pointi 6 nyuma ya Man U ambao pia wana mechi moja mkononi huku Chelsea wakibakisha mechi 5 tu, amekiri Chelsea hawana matumaini tena ya kutwaa Ubingwa wa LIGI KUU.
Hiddink amekiri: 'Ingawa kimahesabu nafasi ipo lakini ukweli Man U wako mbali na ni bora tuwe wakweli na kukazania tu kwenye FA CUP ambako tuko Fainali na kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE ambako tuko Nusu Fainali. LIGI KUU itabidi tutegemea wengine watusaidie ili tuwe Bingwa!! Hiyo haipo mikononi mwetu!!!'
Chelsea kwenye Fainali ya FA CUP itakayochezwa Mei 30 watakumbana na Everton. Kwenye Nusu Fainali UEFA CHAMPIONS LEAGUE wanachuana na Barcelona.
ROY KEANE AUKWAA UMENEJA IPSWICH TOWN!!
Nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane, ameteuliwa kuwa Meneja mpya wa Timu ya Ipswich Town ambayo inachezea Daraja la chini ya LIGI KUU England liitwalo Coca Cola Championship.
Keane alikuwa Meneja wa Timu ya LIGI KUU Sunderland hadi alipong'atuka mwenyewe mwezi Desemba 2008 baada ya kutoelewana na Bodi ya timu hiyo.
Keane aliteuliwa kuwa Meneja wa Sunderland Agosti 2006 wakati huo Sunderland ikiwa ipo nafasi ya pili toka mwisho kwenye Ligi ya Coca Cola Champioship na msimu huohuo akamudu kuipandisha daraja na kuiingiza LIGI KUU.

Man U warudi kileleni sasa pointi 3 mbele, mechi moja mkononi!!!

Manchester United jana waliifunga Portsmouth mabao 2-0 uwanjani kwake Old Trafford na kurudia tena kushika uongozi wa LIGI KUU England safari hii wakiwa pointi 3 mbele ya Liverpool na huku wana mechi moja mkononi. Mabao ya Wayne Rooney na Michael Carrick yamewapa ushindi Mabingwa hao.
Sasa Man U wana pointi 74, Liverpool pointi 71, Chelsea pointi 68 na Arsenal pointi 62
Man Utd: Van der Sar, Neville, Vidic, Evans, Evra, Fletcher, Scholes, Anderson, Giggs, Ronaldo, Rooney.
Akiba: Kuszczak, Berbatov, Carrick, Nani, Rafael Da Silva, O'Shea, Tevez.
Portsmouth: James, Johnson, Campbell, Distin, Hreidarsson, Davis, Mullins, Hughes, Belhadj, Nugent, Crouch.
Akiba: Begovic, Pennant, Pamarot, Utaka, Cranie, Kanu, Basinas.
Refa: Peter Walton
Chelsea 0 Everton 0
Wakiwa nyumbani kwao Stamford Bridge, Chelsea jana walibanwa na Everton ambae ndie atakuwa mpinzani wake kwenye Fainali ya FA CUP itakayochezwa Mei 30.
Hadi mwisho wa mechi Chelsea 0 Everton 0.
Chelsea: Cech, Ivanovic, Alex, Terry, Ashley Cole, Ballack, Essien, Lampard, Drogba, Anelka, Malouda.
Akiba: Hilario, Di Santo, Mikel, Kalou, Belletti, Mancienne, Mellis.
Everton: Howard, Jacobsen, Lescott, Yobo, Baines, Osman, Castillo, Neville, Pienaar, Jo, Cahill.
Akiba: Nash, Hibbert, Jagielka, Saha, Vaughan, Rodwell, Gosling.
Refa: Mark Halsey

Wednesday, 22 April 2009

Scholes kufikisha mechi ya 600 leo?

Paul Scholes [34,] endapo atapangwa katika Kikosi cha Manchester United kinachoshuka Old Trafford leo usiku kupambana na Portsmouth katika mechi muhimi sana ya LIGI KUUambayo Man U wanataka washinde ili wawe pointi 3 juu ya Liverpool, basi atafikisha mechi 600 katika Klabu yake tangu aanze kuichezea mwaka 1994.
Ni Wachezaji watatu tu waliochezea mechi nyingi Manchester United kumzidi Paul Scholes katika historia ya Klabu hiyo nao ni Ryan Giggs, mechi 798, Sir Bobby Charlton, mechi 758 na Bill Foulkes, mechi 658.
Meneja wake, Sir Alex Ferguson, anamsifia: 'Katika wakati wangu hapa Old Trafford, bila shaka yeye yupo katika listi ya Wachezaji 6 au 7 bora.'
Ni Mchezaji ambae hapendi makuu na ni mkimya sana. Kila awezapo, yeye huwakimbia Waandishi wa Habari.
Inasemekana aliwahi kusema anapenda kucheza soka lakini hapendi kuwa Mwanasoka
.


MECHI ZA LEO LIGI KUU England:
[saa 4 usiku bongo taimu]
Man U v Portsmouth
Chelsea v Everton

VUTA NIKUVUTE LIVERPOOL, ARSENAL!!!!!

Andrey Arshavin ameifungia Arsenal mabao manne lakini hilo halikuweza kuwapa ushindi kwani mabao mawili kila mmoja kutoka kwa Fernando Torres na Yossi Benayoun yalifanya mechi hii iishe 4-4. Sasa Liverpool amechukua uongozi wa ligi ingawa yuko pointi sawa na Man U wote wakiwa na pointi 71 lakini Liverpool ana tofauti ya magoli bora. Hata hivyo Liverpool amecheza mechi 2 zaidi ya Man U.
Kesho Jumatano Manchester United anacheza kwake Old Trafford na Portsmouth.
Vikosi vilikuwa:
Liverpool:
Reina, Arbeloa, Carragher, Agger, Aurelio, Alonso, Mascherano, Benayoun, Kuyt, Riera, Torres. Akiba: Cavalieri, Dossena, Babel, Lucas, Ngog, El Zhar, Skrtel.
Arsenal: Fabianski, Sagna, Toure, Silvestre, Gibbs, Arshavin, Song Billong, Fabregas, Denilson, Nasri, Bendtner. Akiba: Mannone, Diaby, Eduardo, Vela, Walcott, Ramsey, Eboue.

Monday, 20 April 2009

Sir Alex Ferguson atetea kupanga 'Chekechea' Nusu Fainali ya FA CUP!!

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ametetea uamuzi wake wa kupanga Kikosi ambacho wengi wanaamini kilikuwa 'hafifu' kwenye mechi ya jana ya Nusu Fainali ya Kombe la FA walipocheza na Everton na kutolewa kwa mabao 4-2 ya matuta baada ya mechi kwisha sare 0-0 kwa dakika 120.

Kikosi kilichoanza kwa Man U jana kilikuwa: Foster, Rafael Da Silva, Ferdinand, Vidic, Fabio Da Silva, Welbeck, Gibson, Anderson, Park, Tevez, Macheda.

Ukiwatoa Ferdinand na Vidic, Wachezaji wengine wote waliobaki si Wachezaji wa kawaida wa Kikosi cha Kwanza na wengi ni Vijana wadogo sana ambao wameanza karibuni kuichezea Timu ya Akiba ya Man U.

Mjadala mkali umeibuka kuhusu umakini wa uamuzi wa kuwaacha nyota kutocheza mechi ya Nusu Fainali Kombe la FA Uwanjani Wembley ambayo wadau wengi huabudu kuwa ni 'bigi mechi'!!

Inastaajabisha Timu yenye Mchezaji Bora wa Dunia, Cristiano Ronaldo, Mchezaji Bora wa England, Wayne Rooney, Wachezaji mahiri kama Carrick, Giggs, Van der Sar, Evra, Berbatov na Scholes, inawatupa nje na kuchezesha 'vifaranga' vya miaka 17 na 18 dhidi ya mibavu na Michezaji iliyokubuhu mikikimikiki ya LIGI KUU wa Everton kama kina Lescott, Cahill, Jagielka wakiongozwa na vigogo wa zamani wa Man U kina Phillip Neville, Saha na Kipa Tim Howard!!!

Lakini, Sir Alex Ferguson hayumbishwi na mijadala hiyo na ametamka: 'Baada ya kushinda Ureno Jumatano tulipowatoa FC Porto, tuliamua kuchezesha Kikosi hicho hicho na kupumzisha Wachezaji wawili au watatu tu. Lakini, baada ya kuwaona Chelsea na Arsenal wakicheza Wembley na kuuona jinsi uwanja unavyoharibika huku nyasi ziking'oka na kuacha mashimo, tuliogopa kuchezesha kikosi chetu bora!! Tuna mechi ngumu na muhimu zinakuja!!'

Ferguson aliongeza; 'Tulifanya kitu sahihi kuchezesha chipukizi. Najua katika mechi yeyote ile mbele yetu Macheda, Welbeck na Rafael wanaweza kucheza bila wasiwasi!'

Ferguson alimaliza kwa kusema: 'Baada ya mechi ya jana tulifanya tathmini yake na leo tunaangalia mechi ya Jumatano na Portsmouth. Ni mechi kubwa kwetu kwani tuna mechi 7 za ligi zimebaki na tuna matumaini tutashinda zote.'


Kuhusu mechi ya kesho Jumanne kati ya Liverpool na Arsenal, Ferguson alisema wao hawana tatizo kwa Liverpool kutangulia kucheza kabla yao na akapuuza imani ya wengi kuwa Bosi wa Arsenal Arsene Wenger atapumzisha baadhi ya Wachezaji wake ili kuikabili Man U wiki ijayo kwenye Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.

'Arsene Wenger ni mshindi' Ferguson alitoboa. 'Sitegemei atacheza na Liverpool asitafute ushindi'

Baada ya kubwagwa Nusu Fainali FA CUP, Ferguson ana wasiwasi Refa alipata shinikizo asiwape Penalti!!!!!

Sir Alex Ferguson amesema matamshi ya Meneja wa Everton David Moyes kabla ya mechi yao ya Nusu Fainali ya Kombe la FA kuhusu uteuzi wa Refa Mike Riley kuchezesha pambano hilo huenda yalimpa shinikizo Refa huyo kuwanyima penalti ya wazi pale Danny Welbeck alipokuwa akienda kufunga kuangushwa ndani ya boksi na Mlinzi wa Everton Phil Jagielka.

Awali Refa Steve Bennet ndie alipangwa kuchezesha pambano hilo lakini akajitoa kwa kuwa alikuwa anaugua na FA ikamteua Mike Riley na hilo likalalamikiwa na Meneja wa Everton David Moyes ambae huko nyuma ashawahi kumlaumu Riley kwa kuipendelea Man U pale mwaka 2003 kwenye mechi ya mwisho kabisa ya LIGI KUU alipoipa Man U penalti iliyoiua Everton na kuwakosesha nafasi ya kucheza UEFA CUP msimu uliofuata.

Ferguson amesema: 'Sijui kama hilo lilimfanya Refa asite kutoa penalti lakini inawezekana. Inawezekani hilo lilikuwa kwenye ubongo wa Refa. Nimetazama video na ile ni penalti. Lakini siwezi kusema hiyo ndio sababu tumeshindwa Nusu Fainali!!'

Baada ya mechi, David Moyes amekubali Man U walikosa bahati kwa kunyimwa penalti ile. Moyes alisema: 'Nadhani ni penalti. Hata mie ningelalamika.'

Wachezaji wapewa VIAGRA ili wacheze vyema!!!!
Afisa wa Klabu moja huko Bolivia amekiri kuwa aliwapa baadhi ya Wachezaji wa Timu yake dawa ya Viagra, ambayo kawaida hutumika kuongeza nguvu za kufanya ngono, ili waweze kumudu na kucheza vyema huko mjini La Paz, mji ambao uko juu sana toka usawa wa bahari na hivyo kufanya Wachezaji kushindwa kupumua vyema na kuchoka haraka.
Mara nyingi Timu ambazo hazijazoea kucheza huko La Paz hupata vipigo kutokana na ugumu wa kucheza hapo kwa kuwa hewa ya Oksijeni ni nyepesi kutokana na mji huo kuwa juu sana toka usawa wa bahari na watu wasio na mazoea na mji huo hupumua kwa shida sana na huchoka haraka sana.
FIFA iliwahi kupiga marufuku mechi za Kimataifa kuchezwa hapo.
Wiki chache zilizopita Argentina, moja ya Timu bora duniani, ilipigwa bao 6-1 na Bolivia mjini hapo kwenye mechi ya mchujo wa kuwania kuingia Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.
Afisa wa Klabu hiyo iliyotumia Viagra inayotoka mji wa Santa Cruz ulio mita 400 juu toka usawa wa bahari alisema walienda kucheza La Paz mji ulio mita 3500 toka usawa wa bahari na aliwachanganyia Wachezaji Juisi na Viagra ili kuwaongezea uwezo wa damu zao kuchanganyika vizuri na oksijen na hivyo kuongeza nguvu na kupumua kirahisi.
Afisa huyo pia alisema Viagra haimo kwenye listi ya madawa yaliyopigwa marufuku na FIFA.

MECHI ZIJAZO LIGI KUU ENGLAND:
Jumanne, 21 Aprili 2009

[saa 4 usiku]
Liverpool v Arsenal
Jumatano, 22 Aprili 2009
[saa 4 usiku]
Chelsea v Everton
Man U v Portsmouth

Sunday, 19 April 2009

Ni Chelsea, Everton Fainali FA CUP!!!

Everton wamemudu kuingia Fainali ya FA CUP na sasa watakutana na Chelsea hapo Mei 30 baada ya kuwashinda Man U kwa penalti katika pambano lililoisha 0-0 na lililochezwa hadi muda wa nyongeza wa dakika 30 baada ya mechi kuwa sare. Ilikuwa mechi ambayo Sir Alex Ferguson aliwashangaza wengi kwa uteuzi wa timu 'chekechea' iliyokuwa na Wachezaji wengi wadogo na wa akiba na wawili tu ambao ndio 'vigogo', yaani Ferdinand na Vidic.
Hata hivyo, ingawa ilikuwa Man U 'hafifu', mechi ilkuwa nguvu sawa na pengine katika dakika 90 za kawaida hata Man U wangeweza kushinda kwa jinsi walivyopata nafasi na hata kunyimwa penalti ya dhahiri pale Welbeck alipoangushwa kwenye boksi.
Everton walishinda penalty 4-2 huku Cahill akikosa yao moja na waliofunga Man U ni Vidic na Anderson na wakosaji ni Berbatov na Ferdinand.
Man Utd:
Foster, Rafael Da Silva, Ferdinand, Vidic, Fabio Da Silva, Welbeck, Gibson, Anderson, Park, Tevez, Macheda.
Akiba: Kuszczak, Neville, Evra, Berbatov, Nani, Scholes, Evans.
Everton: Howard, Hibbert, Jagielka, Lescott, Baines, Osman, Neville, Fellaini, Pienaar, Cahill, Saha.
Akiba: Nash, Yobo, Castillo, Vaughan, Jacobsen, Rodwell, Gosling.
Refa: Mike Riley (Yorkshire)

MATOKEO LIGI KUU LEO:
Tottenham 1 Newcastle 0
Man City 4 West Brom 2


LEO VITA ya Ndugu wawili: Gary na Phillip Neville!!!!!

Gary Neville na Phillip Neville ni mtu na mdogo wake, baba mmoja na mama mmoja.
Gary ni mkubwa kwa Phillip kwa miaka miwili. Gary alizaliwa mwaka 1975 na Phillip mwaka 1977.
Ndugu hawa wote ni Wachezaji wa Timu ya Taifa ya England na wanae Dada yao, mdogo kwao aitwae Tracy, ambae yumo kwenye Timu ya Taifa ya Wanawake ya England.
Wote walianza kucheza soka tangu wako watoto wakiwa Manchester United lakini Phillipi Neville akauzwa kwenda Everton mwezi Agosti mwaka 2005 na Gary akabaki Man U.
Kwa sasa Najodha wa Manchester United ni Gary Neville na Nahodha wa Everton ni Phillip Neville.
Na leo, ndani ya Uwanja maarufu wa Wembley, Manchester United na Everton zinacheza kwenye Nusu Fainali ya FA CUP na mshindi atakutana na Chelsea hapo Mei 30.
Na ndugu hao wawili, wakiwa Manahodha wa Timu zao, wanatarajiwa kuziongoza Timu zao kuingia na kupambana katika jukwaa maarufu na la kihistoria huko Uingereza na Dunia nzima- Wembley Stadium.
Manchester United v Everton

Leo saa 12 jioni, saa za kibongo, Mabingwa wa England, Ulaya na Dunia, Manchester United, wanajimwaga Wembley Stadium, London, kuvaana na Timu nyingine ya LIGI KUU England, Everton kwenye Nusu Fainali ya Kombe la FA na mshindi atakutana na Chelsea iliyoifunga Arsenal hapo jana bao 2-1 kwenye Fainali itakayochezwa tarehe 30 Mei 2009. Mbali ya kuwakosa majeruhi wa muda mrefu, Owen Hargreaves, na Wes Brown [ingawa ameshaanza mazoezi], Man U wanategemewa kuwa na kikosi chao kamili wakiwemo Garry Neville na Rafael da Silva ambao wamepona hivi karibuni.
Leo, baada ya kukosa mechi iliyopita dhidi ya FC Porto iliyochezwa Jumatano, Paul Scholes, Park Ji-sung na Carlos Tevez wanategemewa sana kuanza hasa baada ya Meneja Sir Alex Ferguson kuahidi mabadiliko ili kupumzisha baadhi ya Wachezaji hasa ukitilia maanani Jumatano ijayo kuna mechi muhimu ya LIGI KUU dhidi ya Portsmouth.
Meneja wa Everton, David Moyes, inabidi aamue kama atamuanzisha Louis Saha ambae alikuwa anaugua tumbo kwani hatowezi kumchezesha Mshambuliaji Jo ambae haruhusiwi kucheza mashindano haya kwa vile alishacheza alipokuwa na Timu yake Manchester City. Jo yuko Everton kwa mkopo.
Majeruhi wa muda mrefu wa Everton ambao sasa wamepona na wanaweza kucheza ni pamoja na Mlinzi kutoka Nigeria Joseph Yobo na Mshambuliaji James Vaughan.
Vikosi vinategemewa kuwa
Man Utd: Van der Sar, Foster, Kuszczak, Neville, Evra, Ferdinand, Vidic, Rafael, Fabio, O'Shea, Evans, Ronaldo, Anderson, Scholes, Fletcher, Gibson, Carrick, Park, Nani, Giggs, Rooney, Tevez, Berbatov, Macheda.
Everton: Howard, Hibbert, Lescott, Jagielka, Baines, Osman, Pienaar, Neville, Rodwell, Fellaini, Cahill, Yobo, Saha, Vaughan, Nash, Gosling, Jacobsen, Van der Meyde, Castillo, Baxter.
Refa: Mike Riley


Wenger akiri wamefungwa kwa kuwa walishindwa kumdhibiti Drogba


Baada ya kipigo cha 2-1 cha jana, goli la ushindi likifungwa na Mshambuliaji Didier Drogba, Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amekiri: 'Drogba ni muuaji! Tulimrahisishia kazi lakini Drogba ni Mchezaji anaefunga magoli muhimu kwenye mechi kubwa! Huwa anajidondosha maksudi mara kwa mara lakini ni Mchezaji hatari!'

Ingawa amekiri Drogba ndie aliewaua, Wenger amesema Kipa wao Lucasz Fabianski haepuki lawama ingawa hakutaka kusisitiza hilo akiogopa kumvunja moyo hasa kwa kuwa Jumanne wana mechi ngumu watakapochuana na Liverpool kwenye LIGI KUU.

Na Meneja wa Chelsea, Guus Hiddink, akiwa na furaha kubwa, alimmiminia sifa nyingi Drogba na kusema huwezi kumtathmini Mshambuliaji kwa kufunga tu bali pia kwa kuhangaika kwake kuisaidia Timu kitu ambacho Drogba anakifanya kwa bidii sana.

Timu ya Ujerumani yaomba radhi kwa Mashabiki wake kwa kufungwa kwa kuwarudishia pesa zao za viingilio!!!!!

Baada ya kubandikwa mabao 4-0 ugenini kwenye mechi ya Bundesliga siku ya Ijumaa iliyopita huko Ujerumani walipokutana na Schalke, Timu ya Energie Cottbus imewataka radhi Mashabiki wake 600 waliosafiri umbali wa Kilomita 610 hadi Gelsenkirchen na kuambulia kuona Timu yao ikipata kipigo chake cha sita katika mechi 7. Cottbus ambao wako nafasi ya pili toka chini kwenye msimamo wa Bundesliga na wako hatari ya kuporomoka Daraja imetamka itarudisha pesa za viingilio kwa Mashabiki wake waliokwenda kuiona mechi hiyo ikiwa ni ishara ya kuomba msamaha.

MECHI ZA LEO: Jumapili, 19 Aprili 2009
LIGI KUU ENGLAND

[saa 9 na nusu mchana]Tottenham v Newcastle

[saa 11 jioni]Man City v West Brom

Powered By Blogger