Monday 20 April 2009

Baada ya kubwagwa Nusu Fainali FA CUP, Ferguson ana wasiwasi Refa alipata shinikizo asiwape Penalti!!!!!

Sir Alex Ferguson amesema matamshi ya Meneja wa Everton David Moyes kabla ya mechi yao ya Nusu Fainali ya Kombe la FA kuhusu uteuzi wa Refa Mike Riley kuchezesha pambano hilo huenda yalimpa shinikizo Refa huyo kuwanyima penalti ya wazi pale Danny Welbeck alipokuwa akienda kufunga kuangushwa ndani ya boksi na Mlinzi wa Everton Phil Jagielka.

Awali Refa Steve Bennet ndie alipangwa kuchezesha pambano hilo lakini akajitoa kwa kuwa alikuwa anaugua na FA ikamteua Mike Riley na hilo likalalamikiwa na Meneja wa Everton David Moyes ambae huko nyuma ashawahi kumlaumu Riley kwa kuipendelea Man U pale mwaka 2003 kwenye mechi ya mwisho kabisa ya LIGI KUU alipoipa Man U penalti iliyoiua Everton na kuwakosesha nafasi ya kucheza UEFA CUP msimu uliofuata.

Ferguson amesema: 'Sijui kama hilo lilimfanya Refa asite kutoa penalti lakini inawezekana. Inawezekani hilo lilikuwa kwenye ubongo wa Refa. Nimetazama video na ile ni penalti. Lakini siwezi kusema hiyo ndio sababu tumeshindwa Nusu Fainali!!'

Baada ya mechi, David Moyes amekubali Man U walikosa bahati kwa kunyimwa penalti ile. Moyes alisema: 'Nadhani ni penalti. Hata mie ningelalamika.'

Wachezaji wapewa VIAGRA ili wacheze vyema!!!!
Afisa wa Klabu moja huko Bolivia amekiri kuwa aliwapa baadhi ya Wachezaji wa Timu yake dawa ya Viagra, ambayo kawaida hutumika kuongeza nguvu za kufanya ngono, ili waweze kumudu na kucheza vyema huko mjini La Paz, mji ambao uko juu sana toka usawa wa bahari na hivyo kufanya Wachezaji kushindwa kupumua vyema na kuchoka haraka.
Mara nyingi Timu ambazo hazijazoea kucheza huko La Paz hupata vipigo kutokana na ugumu wa kucheza hapo kwa kuwa hewa ya Oksijeni ni nyepesi kutokana na mji huo kuwa juu sana toka usawa wa bahari na watu wasio na mazoea na mji huo hupumua kwa shida sana na huchoka haraka sana.
FIFA iliwahi kupiga marufuku mechi za Kimataifa kuchezwa hapo.
Wiki chache zilizopita Argentina, moja ya Timu bora duniani, ilipigwa bao 6-1 na Bolivia mjini hapo kwenye mechi ya mchujo wa kuwania kuingia Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.
Afisa wa Klabu hiyo iliyotumia Viagra inayotoka mji wa Santa Cruz ulio mita 400 juu toka usawa wa bahari alisema walienda kucheza La Paz mji ulio mita 3500 toka usawa wa bahari na aliwachanganyia Wachezaji Juisi na Viagra ili kuwaongezea uwezo wa damu zao kuchanganyika vizuri na oksijen na hivyo kuongeza nguvu na kupumua kirahisi.
Afisa huyo pia alisema Viagra haimo kwenye listi ya madawa yaliyopigwa marufuku na FIFA.

MECHI ZIJAZO LIGI KUU ENGLAND:
Jumanne, 21 Aprili 2009

[saa 4 usiku]
Liverpool v Arsenal
Jumatano, 22 Aprili 2009
[saa 4 usiku]
Chelsea v Everton
Man U v Portsmouth

No comments:

Powered By Blogger