Monday, 20 April 2009

Sir Alex Ferguson atetea kupanga 'Chekechea' Nusu Fainali ya FA CUP!!

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ametetea uamuzi wake wa kupanga Kikosi ambacho wengi wanaamini kilikuwa 'hafifu' kwenye mechi ya jana ya Nusu Fainali ya Kombe la FA walipocheza na Everton na kutolewa kwa mabao 4-2 ya matuta baada ya mechi kwisha sare 0-0 kwa dakika 120.

Kikosi kilichoanza kwa Man U jana kilikuwa: Foster, Rafael Da Silva, Ferdinand, Vidic, Fabio Da Silva, Welbeck, Gibson, Anderson, Park, Tevez, Macheda.

Ukiwatoa Ferdinand na Vidic, Wachezaji wengine wote waliobaki si Wachezaji wa kawaida wa Kikosi cha Kwanza na wengi ni Vijana wadogo sana ambao wameanza karibuni kuichezea Timu ya Akiba ya Man U.

Mjadala mkali umeibuka kuhusu umakini wa uamuzi wa kuwaacha nyota kutocheza mechi ya Nusu Fainali Kombe la FA Uwanjani Wembley ambayo wadau wengi huabudu kuwa ni 'bigi mechi'!!

Inastaajabisha Timu yenye Mchezaji Bora wa Dunia, Cristiano Ronaldo, Mchezaji Bora wa England, Wayne Rooney, Wachezaji mahiri kama Carrick, Giggs, Van der Sar, Evra, Berbatov na Scholes, inawatupa nje na kuchezesha 'vifaranga' vya miaka 17 na 18 dhidi ya mibavu na Michezaji iliyokubuhu mikikimikiki ya LIGI KUU wa Everton kama kina Lescott, Cahill, Jagielka wakiongozwa na vigogo wa zamani wa Man U kina Phillip Neville, Saha na Kipa Tim Howard!!!

Lakini, Sir Alex Ferguson hayumbishwi na mijadala hiyo na ametamka: 'Baada ya kushinda Ureno Jumatano tulipowatoa FC Porto, tuliamua kuchezesha Kikosi hicho hicho na kupumzisha Wachezaji wawili au watatu tu. Lakini, baada ya kuwaona Chelsea na Arsenal wakicheza Wembley na kuuona jinsi uwanja unavyoharibika huku nyasi ziking'oka na kuacha mashimo, tuliogopa kuchezesha kikosi chetu bora!! Tuna mechi ngumu na muhimu zinakuja!!'

Ferguson aliongeza; 'Tulifanya kitu sahihi kuchezesha chipukizi. Najua katika mechi yeyote ile mbele yetu Macheda, Welbeck na Rafael wanaweza kucheza bila wasiwasi!'

Ferguson alimaliza kwa kusema: 'Baada ya mechi ya jana tulifanya tathmini yake na leo tunaangalia mechi ya Jumatano na Portsmouth. Ni mechi kubwa kwetu kwani tuna mechi 7 za ligi zimebaki na tuna matumaini tutashinda zote.'


Kuhusu mechi ya kesho Jumanne kati ya Liverpool na Arsenal, Ferguson alisema wao hawana tatizo kwa Liverpool kutangulia kucheza kabla yao na akapuuza imani ya wengi kuwa Bosi wa Arsenal Arsene Wenger atapumzisha baadhi ya Wachezaji wake ili kuikabili Man U wiki ijayo kwenye Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.

'Arsene Wenger ni mshindi' Ferguson alitoboa. 'Sitegemei atacheza na Liverpool asitafute ushindi'

No comments:

Powered By Blogger