Saturday 1 May 2010

LIGI KUU: Matokeo mechi za Leo
Birmingham 2 v Burnley 1
Man City 3 v Aston Villa 1
Portsmouth 3 v Wolves 1
Stoke 0 v Everton 0
Tottenham 1 v Bolton 0
Vita ya Nafasi ya 4
Tottenham imezidi kujichimbia nafasi ya 4 ya Ligi Kuu na hivyo kuweza kucheza Ulaya Msimu ujao baada ya kuwafunga Bolton bao 1-0, bao lililofungwa na Kiungo Tom Huddlestone Uwanjani White Hart Lane.
Huko City of Manchester Stadium, Man City walitanguliwa bao moja la John Carew wa Aston Villa dakika ya 16 na Carlos Tevez akasawazisha kwa penalti dakika ya 41 na dakika mbili baadae Adebayor akaipatia City bao la kuongoza.
Craig Bellamy alihakikishia ushindi Man City alipofunga dakika ya 89.
Ushindi huu wa Tottenham na ushindi wa Manchester City unaifanya mechi ya Jumatano Uwanjani City of Manchester kati ya Man City na Tottenham iwe kama Fainali ya kuamua nani Bingwa wa nafasi ya 4.
Ukweli ni kuwa Liverpool wana nafasi finyu na Aston Villa tayari washabwagwa kwenye kugombea nafasi ya 4 kwa vile wamebakisha mechi moja tu na hata wakishinda mechi hiyo watafikisha pointi 67 ambazo tayari Tottenham anazo na tatizo nyingine kwa Villa ni kuwa wana tofauti ya magoli machache mno ukilinganisha na Tottenham.
Msimamo kwa wagombea nafasi ya 4 baada ya mechi za leo:
-Tottenham mechi 36 pointi 67
-Man City mechi 36 pointi 66
-Aston Villa mechi 37 pointi 64
-Liverpool mechi 36 pointi 62
Birmingham 2-1 Burnley
Katika mechi ya Ligi Kuu iliyoanza mapema leo, Birmingham walitawala na kuifunga Burnley, Timu ambayo tayari imeshaporomoshwa kwenda kucheza Daraja la chini Msimu ujao, kwa bao 2-1 Uwanjani Mtakatifu Andrew.
Mabao ya Birmingham yalifungwa na Cameron Jerome na Christian Benitez.
Bao la Burnley lilifungwa na Steven Thompson.
Tevez abatukiwa afunge domo au aondoke Man City
Roberto Mancini amemwambia Mchezaji wake Carlos Tevez aache kulalamika kuhusu mazoezi Klabuni Manchester City au atafute Klabu nyingine.
Meneja huyo wa Manchester City alichukizwa na kauli za Tevez aliedai kuwa mazoezi ya asubuhi na jioni yanawaumiza Wachezaji na pia alipohoji kufukuzwa kwa Meneja aliepita Mark Hughes katikati ya Msimu.
Wachunguzi wanahisi Tevez ametoa kauli hizo ili afanikishe mpango wake wa kuhamia Spain Ligi ikimalizika na huenda akafanikiwa aada ya Mancini kumtaka anyamaze au ahame.
Msimu mbovu kwa Liverpool lakini Rafa ajipa matumaini
Alipohojiwa kuhusu Msimu huu na nini hatma yake na Liverpool mara baada ya kufyekwa nje ya EUROPA LIGI na Atletico Madrid hapo juzi, Meneja Rafa Benitez alijibu: “Hatima yetu ni Jumapili kwenye mechi na Chelsea.”
Na alipoulizwa nini kitafuta baada ya hapo, Benitez alijibu Hull City akimaanisha mechi yao ya mwisho ya Ligi.
Wengi walitegemea mengi toka kwa Liverpool Msimu huu baada ya msimu uliopita kumaliza Timu ya pili nyuma ya Mabingwa Manchester United lakini mambo yakaenda shaghalabaghala baada ya kutupwa nje katika kila mashindano na sasa wamebakiwa na nafasi finyu sana ya kuweza kumaliza nafasi ya 4 na hivyo kucheza Ulaya Msimu ujao.
Juu ya yote, Benitez ambae anavumishwa yuko njiani kuhamia Juventus, amenena kwa matumaini: “Juu ya yote, Wachezaji wameonyesha kupigana siku zote, lazima tuwasifie kwa hilo. Lazima tujariu tena Msimu ujao kwani Msimu huu tulikuwa na matatizo mengi!”
AC Milan kuishabikia Inter Milan Fainali ya UEFA
Pengine Washabiki wa AC Milan wamestushwa sana na kauli ya Makamu wa Rais wao, Adriano Galliani, kuwa ataisapoti Inter Milan ambao ni Mahasimu wao wakubwa siku ya Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI watakapocheza na Bayern Munich hapo Mei 22 huko Santiago Bernabeau.
Lakini hilo si kwa sababu ni Mzalendo bali tu ni kwa sababu Italia ipo hatarini kunyang’anywa nafasi ya 4 ya kuingiza Timu 4 kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI ikiwa Bayern Munich watashinda Fainali hiyo na Ujerumani ndio watapewa nafasi nne za kuingiza Timu.
UEFA huipa Nchi pointi na hizo ndizo huamua Nchi inaingiza Timu ngapi kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI.
AC Milan bado wanahaha kuitafuta nafasi ya 3 au ya 4 ili wafuzu kuingia UEFA na wapo kwenye ushindani mkubwa toka kwa Sampdoria, Palermo, Juventus na Napoli.
Ubingwa huko Italia unagombewa na Inter Milan na AS Roma.
LIGI KUU WIKIENDI: Bigi Mechi ni Jumapili Liverpool v Chelsea!!!!
Ingawa leo Jumamosi kuna mechi kadhaa na muhimu kwa Timu zinazogombea nafasi ile ya 4 ili wacheze Ulaya Msimu ujao, macho na masikio yetu sote yapo Jumapili hasa kwa ile BIGI MECHI kati ya Liverpool na Chelsea huko Anfield na itafuatiwa na Sunderland v Manchester United huko Stadium of Light.
Huku zikiwa zimebaki mechi mbili Ligi kwisha, Chelsea yupo kileleni kwa pointi moja dhidi ya Man United.
Ikiwa Chelsea atateleza kwa Liverpool kwa ama kutoka sare au kufungwa na Man United kumfunga Sunderland, uongozi utatwaliwa na Man United na Timu zote zitabakiza mechi moja tu.
Liverpool bado ana nafasi finyu ya kuipata nafasi ya 4 na hivyo kucheza Ulaya Msimu ujao.
Arsenal wao tayari wamefuzu kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI na Ubingwa washawapisha Chelsea na Man United kuugombea.
Nafasi ya 4 bado inagombewa na Tottenham, Man City, Aston Villa na Liverpool.
Everton wao wapo kwenye vita ya kuipata nafasi ya 7 ili wacheze EUROPA LIGI Msimu ujao.
Huko mkiani tayari Timu mbili kati ya 3 zinazoporomoka Daraja zishapatikana na nazo ni Portsmouth na Burnley.
Timu ya mwisho kuungana na Portsmouth na Burnley, bila shaka, ni Hull City ambao wako pointi 6 nyuma ya West Ham na ndio wenye nafasi kubwa ya kuungana na Portsmouth na Burnley labda washinde mechi zao mbili zilizobaki na West Ham wafungwe mbili zao zilizobaki na tofauti ya magoli iliyopo kati yao ya goli 23 ifutwe katika matokeo ya mechi hizo mbili zilizobaki.
RATIBA:
Jumamosi, 1 Mei 2010
[saa 8 dak 45 mchana]
Birmingham v Burnley
[saa 11 jioni]
Man City v Aston Villa
Portsmouth v Wolves
Stoke v Everton
Tottenham v Bolton
Jumapili, Mei 2
[saa 9 na nusu mchana]
Liverpool v Chelsea
[saa 11 jioni]
Fulham v West Ham
[saa 12 jioni]
Sunderland v Man United
Jumatatu, Mei 3
[saa 9 na nusu mchana]
Wigan v Hull
[saa 1 usiku]
Blackburn v Arsenal
MSIMAMO LIGI KUU England:
[KILA TIMU IMECHEZA MECHI 36 ISIPOKUWA INAPOTAJWA]
1. Chelsea pointi 80====KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
2. Man United 79======KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
3. Arsenal 72========KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
4. Tottenham mechi 35 pointi 64
-------------------------------------------
5. Aston Villa 64
6. Man City mechi 35 pointi 63
7. Liverpool 62
8. Everton 57
9. Birmingham 47
10. Sunderland 44
11. Blackburn 44
12. Fulham mechi 35 pointi 43
13. Stoke mechi 35 pointi 43
14. Bolton 36
15. Wolves 35
16. Wigan 35
17. West Ham 34
--------------------------------------
18. Hull City 28
19. Burnley 27==========IMESHUSHWA
20. Portsmouth 16=======IMESHUSHWA
--------------------------------------------------------------
MECHI SPESHELI za Jumamosi:
Man City v Aston Villa
Hii ni vita ya kugombea ile lulu ya nafasi ya 4 ili kucheza Ulaya Msimu ujao na vita hii ipo ndani ya City of Manchester Stadium.
Nafasi hiyo ya 4 imeshikwa na Tottenham waliocheza mechi 35 na wana pointi 64 sawa na Aston Villa waliocheza mechi moja zaidi.
Man City wao wamecheza mechi 35 na wana pointi 63.
Villa hawajafungwa katika mechi 5 zilizopita na wameshinda 3 kati ya hizo na Man City walitoka sare na Arsenal ya 0-0 wikiendi iliyopita.
Baada ya mechi hii, City watacheza na Tottenham Jumatano katika vita nyingine ya nafasi ya 4.
Man City, waliopata hofu ya kukosa Kipa baada ya Makipa wao wote kuumia, tayari washamchukua kwa mkopo wa dharura Kipa wa Akiba wa Sunderland, Martin Fulop, ili awadakie mechi zao tatu zilizobaki.
Tottenham v Bolton
Tottenham, wanaokalia Taji linalotafutwa kwa udi na uvumba la nafasi ya 4 kwenye Ligi, wapo nyumbani White Hart Lane kuwakaribisha Bolton Wanderers.
Baada ya kuzichapa mfululizo Chelsea na Arsenal, Tottenham walikung’utwa mechi yao iliyofuatia wikiendi iliyokwisha na Mabingwa Watetezi Manchester United kwa bao 3-1 huko Old Trafford na leo watataka kufuta machungu hayo na kujikita nafasi ya 4 kwa kuifunga Timu inayoelea kwenye bahari ya Ligi Kuu, Bolton, bila misukosuko ya kushuka Daraja au kucheza Ulaya.
LIGI KUU waisafisha Fulham
Ligi Kuu imeamua Fulham haikuvunja kanuni zozote baada ya West Ham kuwasilisha malamiko yao kwao kwamba Fulham walichezesha Kikosi dhaifu walipocheza na Hull City mwezi Machi na kufungwa 2-0.
West Ham, ambao walikuwa wakiandamwa mno na balaa la kushuka Daraja, walilalamika baada ya Fulham kupumzisha Wachezaji wao wa kawaida watano katika mechi hiyo na Hull City labda kwa sababu mechi iliyokuwa inafuata kwao ni ile ya EUROPA LIGI.
Ushindi wa Hull City wakati huo uliwafanya wafungane pointi na West Ham na ndio maana West Ham wakakasirishwa na kitendo hicho.
Ligi Kuu imetoa tamko kwamba wamepitia malamiko ya West Ham na maelezo ya Fulham na wameridhika Fulham haikuvunja kanuni yeyote.
Tayari Timu mbili, Portsmouth na Burnley, zimeshaporomoka Daraja na Hull City ambao wako pointi 6 nyuma ya West Ham ndio wenye nafasi kubwa ya kuungana nao labda washinde mechi zao mbili zilizobaki na West Ham wafungwe mbili zao zilizobaki na tofauti ya magoli iliyopo kati yao ya goli 23 ifutwe katika matokeo ya mechi hizo mbili zilizobaki.
Neville aongeza mkataba
Nahodha wa Manchester United Gary Neville, miaka 35, amesaini nyongeza ya mwaka mmoja ya mkataba wake na Klabu yake utakaomweka Old Trafford hadi mwishoni mwa Msimu wa 2010/11.
Baada ya kukosa Miezi 18 alipoumia vibaya enka hapo Machi 2007, Neville amerudi tena dimbani na ameshacheza mechi 27 za Man United na kumfanya akaribie kuichezea mechi 600 Klabu hiyo tangu aanze kuichezea mwaka 1992.
Neville sasa ameungana na Wakongwe wengine Paul Scholes na Ryan Giggs waliopata nyongeza ya mkataba ya mwaka mmoja kila mmoja.
Msimu huu, Neville amekuwa akipokezana nafasi ya Fulbeki na Kinda toka Brazil Rafael, miaka 19.
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ametamka: “Anastahili. Gary amekuwa nje kwa miezi 18 lakini, kwa mtu wa zaidi ya miaka 30 baada ya kuumia vibaya, kurudi tena uwanjani na kucheza kwa kiwango cha juu ni kitu cha kushangaza na kinastahili pongezi!”
Nyongeza hii ya mkataba inamfanya Gary Neville awepo Man United kwa Msimu wa 19 tokea alipotokea Timu ya Vijana na kina David Beckham, Nicky Butt na Scholes.
Ferguson pia alitambulisha kuwa Neville, Giggs na Scholes kwa sasa wanasomea Ukocha na wameanza kupata Beji mbalimbali za hatua tofauti za masomo ya Ukocha na Klabu itauzingatia uzoefu na utumishi wao.
Ferguson alisema: “Huwezi ukapuuza mchango wa maisha yao katika Klabu hii. Uzoefu wao unaweza ukawa lulu kwa maendeleo ya Wachezaji Chipukizi.”

Friday 30 April 2010

Fergie na Wenzake wataka Hodgson awe Meneja wa Mwaka
Sir Alex Ferguson amedai Roy Hodgson wa Fulham ndie anastahili kuwa Meneja Bora wa Mwaka kwa kuiletea Fulham mafanikio ya ajabu pale alipoiwezesha Klabu hiyo kutinga Fainali ya EUROPA LIGI na hilo ni jambo kubwa sana kwa Klabu ya Uingereza.
Jana, Fulham, walitoka nyuma kwa bao 1-0 na kuichapa Hamburg 2-1 na kutinga Fainali ambako watakutana na Atletico Madrid walioitoa Liverpool pia hapo jana.
Ferguson ametamka: “Roy ni lazima awe Meneja wa Mwaka! Ni miujiza! Naomba ashinde Kombe hilo na haya ni mafanikio makubwa kupita yote kwa Klabu ya Uingereza!”
Ferguson alibainisha alimtumia Hodgson ujumbe wa kumtakia heri kabla ya mechi na hata Wachezaji wa Timu yake, akiwemo Kipa Edwin van der Sar aliesajiliwa na Man United kutoka Fulham, walikuwa wakitaka Fulham ishinde.
Nae Meneja wa Wolves Mick McCarthy pia aliunga mkono uteuzi wa Hodgson kuwa Meneja wa Mwaka kwa kuiwezesha Fulham kupata mafanikio makubwa licha ya kuwa Klabu ndogo na uwezo duni kiuchumi.
Ferguson awategemea Liverpool kuwa kidete!
Sir Alex Ferguson amesisitiza Mahasimu wao wakubwa Liverpool hawawezi ‘kutupa mkono historia’ na kuwapa ushindi wa chee Chelsea ili mradi tu Manchester United wasipate nafasi ya kuwa Bingwa.
Chelsea, wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi moja tu mbele ya Manchester United huku kuna mechi mbili zimebaki, Jumapili wanasafiri hadi Anfield kucheza na Liverpool ambao bado wana matumaini finyu ya kunyakua nafasi ya 4 na hivyo kucheza Ulaya Msimu ujao.
Takriban nusu saa tu baada ya mechi ya Liverpool na Chelsea, Man United watajimwaga Uwanjani Stadium of Light kucheza na wenyeji wao Sunderland na ikiwa Chelsea atafungwa au kutoka sare na Liverpool na Man United kuifunga Sunderland, Man United watatwaa uongozi wa Ligi na washindani hao watakuwa wamebakiwa na mechi moja tu.
Ikiwa Manchester United watatwaa Ubingwa Msimu huu watawapita Liverpool kwa kutwaa Ubingwa mara nyingi kwani Klabu hizi mbili zimefungana kwa kuutwaa mara 18 kila mmoja.
Ferguson amedai: “Klabu kubwa haziwezi kutupa asili yao ya jadi kwa ajili ya gemu moja tu. Mashabiki wanajua hilo. Hivi unafikiri Mashabiki wanataka kurudi nyumbani huku wakilaumu Wachezaji wao kuitupa mechi kwa kusudi na huku wakijua hilo linaweza kutokea tena?”
Baadhi ya Wadau wanaukumbuka Msimu wa Mwaka 1995 ambao siku ya mwisho ya Ligi Manchester United walisafiri hadi Upton Park kucheza na West Ham wakitaka ushindi na pia kuomba Liverpool waifunge Blackburn Uwanjani Anfield ili wawe Mabingwa.
Siku hiyo Liverpool waliifunga Blackburn lakini Man United walitoka sare na West Ham na Ubingwa ukabebwa na Blackburn.
Ferguson alikumbushia hilo: “Tuliwategemea Liverpool! Walitusaidia lakini tulishindwa wenyewe!”
Nae Kipa wa Liverpool, Pepe Reina, amedai: “Sichezi Timu yao! Mie nacheza Liverpool na sijali Man United watafanya nini. Jumapili ntacheza tushinde kwa sababu tunataka pointi 3 na bado tuna nafasi ya kuitwaa nafasi ya 4! Tunacheza nyumbani na hapa hatuchezi kutoka sare au kufungwa! Tunataka kuleta ushindi wa mwisho wa Msimu hapa nyumbani!”
Rooney aopoa Tuzo ya Pili!!
Wayne Rooney amefanikiwa kupata Tuzo nyingine siku chache baada ya kupewa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka na PFA, Chama cha Wachezaji Soka wa Kulipwa, na sasa ameikwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka toka kwa Waandishi Habari wa Soka na Tuzo hii inaheshimika sana.
Tuzo hii ya Waandishi hutolewa kwa Mchezaji kufuatia kura inayoendeshwa kati ya Waandishi wa Soka na Rooney alipata kura asilimia 81 na kuwabwaga Didier Drogba na Carlos Tevez.
Rooney, Straika wa Manchester United na tegemezi kubwa kwa matumaini ya England huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia, amefunga jumla ya magoli 34 Msimu huu.
Rooney, aliefurahishwa na Tuzo hii, amenena: “Nina furaha kubwa kushinda Tuzo kubwa yenye historia ndefu na asili ya muda mrefu ambayo Wachezaji bora wamewahi kuitwaa tangu mwaka 1948!"
Rooney atakabidhiwa Tuzo yake hapo Mei 13 kwenye chakula maalum cha usiku huko Lancaster London Hotel.
Rooney pia alitoa shukrani kwa Meneja wake, Sir Alex Ferguson na Wasaidizi wake, Wachezaji wenzake wa Man United, Familia na Marafiki zake kwa kumwezesha kupata Tuzo hiyo.
Wenger kusajili wawili au watatu wapya
Bosi wa Arsenal Arsene Wenger ametamka kuwa atasajili Wachezaji kadhaa kwa ajili ya Msimu ujao na inasemekana mara baada ya Msimu kwisha katikati ya Mei na kabla ya Fainali za Kombe la Dunia kuanza hapo Juni 11, Wenger atamtambulisha rasmi Straika kutoka Bordeaux Marouane Chamakh kama Mchezaji mpya wa Arsenal.
Arsenal inategemewa sana kununua Madifenda hasa kwa vile Madifenda wa sasa William Gallas, Sol Campbell na Mikael Silvestre wote mikataba yao inaisha mwezi Juni.
Wenger ametamka: “Nakiamini Kikosi cha sasa lakini ikiwa upo uwezekano wa kupata Wachezaji wawili mwisho watatu, tutanunua Wachezaji. Lakini yote inategemea nani ataondoka kwenye Kikosi cha sasa.”
Wenger aliongeza kwa kusema hakuna anaejua soko la Ulaya lilivyo kwa sasa hadi usajili wa kwanza utakapofanyika.
Vilevile, Wenger alisikitishwa na kauli zinazodaiwa kutoka kwa Mchezaji wake Andriy Arshavin aliekaririwa kusema anaihusudu Barcelona.
Arshavin, aliechukuliwa na Arsenal Januari 2009 kutoka Zenit St Petersburg ya Urusi, alikaririwa akisema kuichezea Barcelon, ambayo ndiyo iliitupa nje Arsenal toka kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu huu, kutakuwa ni kilele cha maisha yake kimpira.
Wenger alisema: “Nasikitika. Anaonyesha tabia tofauti wakati anataka kuboresha mkataba wake na sisi. Yeye ana furaha hapa hebu muulizeni kelele za nini?”
Listi ya Mameneja Tajiri
Gazeti kubwa Nchini Uingereza, Sunday Times, limechapisha Listi ya Wanamichezo Matajiri kwa Mwaka 2010 na katika Mameneja wa Soka, Meneja wa England, Fabio Capello, ndie ameibuka mwenye ‘vijisenti’ vingi kupita wengine.
Capello, miaka 63, anasadikiwa kuwa ndie Meneja wa England anaelipwa pesa nyingi kupita wengine kwenye historia ya Mameneja wa England na sasa anapata Pauni Milioni 6.5 kwa mwaka.
Hata hivyo, utajiri wa Capello umepatikana kabla ya kwenda England kwani alikuwa na vipindi vya mafanikio makubwa kwake huko Klabu za AC Milan, Roma, Juventus na Real Madrid ambako aliwahi kuwa Meneja.
Alieshika nafasi ya pili ni Nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane, ambae sasa ni Meneja wa Ipswich na utajiri wake unasemekana ni kuwa na kitita cha Pauni Milioni 30.
Bosi wa zamani wa Roy Keane, Sir Alex Ferguson wa Manchester United, ni wa tatu kwa kuwa na Pauni Milioni 24.
Katika Listi hiyo na kwenye 10 Bora wamesheheni Mameneja wenye asili ya Italia ambao ni Carlo Ancelotti wa Chesea na yuko nafasi ya 4 akiwa na Pauni Milioni 21, anafuata Meneja wa Republic of Ireland Giovanni Trapattoni mwenye Pauni Milioni18.
Roberto Mancini, Meneja wa Manchester City, yupo nafasi ya 8 akiwa na Paui Milioni 13 na Bosi wa West Ham Gianfranco Zola ni wa 10 na ana Pauni Milioni 10.
Liverpool washinda lakini nje EUROPA!!!
FAINALI: Fulham v Atletico Madrid Mei 12
Licha ya kushinda bao 2-1 dhidi ya Atletico Madrid, Liverpool walijikuta wakitupwa nje kwa goli la ugenini baada ya jumla ya magoli katika mechi mbili kuwa 2-2 na hivyo Atletico Madrid kutinga Fainali kucheza na Fulham hapo Mei 12 huko Uwanja Nordbank Arena, Hamburg.
Atletico Madrid waliifunga Liverpool bao 1-0 katika mechi ya kwanza kwa bao la Diego Forlan, aliekuwa Mchezaji wa zamani wa Manchester United, na ni Diego Forlan tena aliepachika bao la leo muhimu la ugenini la Atletico.
Hadi dakika 90 za mchezo kumalizika Liverpool walikuwa mbele kwa bao 1-0 kwa bao la dakika ya 44 la Alberto Aquilani lakini matokeo yalikuwa ni 1-1 kwa vile Atletico walishinda mechi ya kwanza bao 1-0 na ndipo dakika 30 za nyongeza zikaanza kutumika.
Liverpool wakapata bao la pili dakika ya 95 kupitia Yossi Benayoun na kuwafanya wawe wanaongoza 2-0 na kama matokeo yangebaki hivi basi ni wao ndio wangetinga Fainali.
Lakini kwenye dakika ya 102, krosi ya Mchezaji wa zamani wa Arsenal, Antonio Reyes, ilimkuta Diego Forlan yuko peke yake na akapachika bao na kuwapa Atletico bao lao la ugenini lililowapa ushindi baada dakika 120 kumalizika huku Liverpool wakiwa bao 2-1 mbele katika mechi hii.
Vikosi vilikuwa:
Liverpool: Reina, Mascherano, Carragher, Agger, Johnson, Gerrard, Lucas, Benayoun, Aquilani, Babel, Kuyt.
Akiba: Cavalieri, Kyrgiakos, Ngog, Degen, El Zhar, Ayala, Pacheco.
Atletico Madrid: De Gea, Valera, Dominguez, Perea, Antonio Lopez, Reyes, Paulo Assuncao, Raul Garcia, Simao, Aguero, Forlan.
Akiba: Sergio Asenjo, Camacho, Jurado, Salvio, Juanito, Ujfalusi, Cabrera.
Refa: Terje Hauge (Norway)
Fulham Fainali EUROPA
Wakiwa nyuma kwa bao 1-0 hadi mapumziko, kwa bao la frikiki ya mita 30 iliyopigwa na Petric na kutinga moja kwa moja wavuni, Fulham wakiwa nyumbani kwao Craven Cottage walijikakamua na kufunga bao mbili kipindi cha pili na kutinga Fainali ya Kombe la EUROPA mahsusi kwa jina la EUROPA LIGI, hii ikiwa ni Fainali yao ya kwanza katika Ulaya.
Timu hizi zilitoka sare 0-0 katika mechi ya kwanza huko Hamburg, Ujerumani wiki iliyokwisha.
Mfungaji mkuu wa Fulham Bobby Zamora, aliekuwa na hatihati kucheza mechi hii kwa kuwa majeruhi, alianza mechi hii na nusura aipatie Timu yake bao lakini Kipa wa Hamburg Frank Rost aliokoa.
Ndipo Hamburg wakafunga bao kutokana na frikiki ya Mladen Petric ya mita 30 iliyoenda moja kwa moja juu wavuni.
Hiyo ilikuwa dakika ya 22.
Dakika ya 69 ya mchezo pasi ndefu toka Defensi ilimkuta Simon Davies aliemgeuza Beki Guy Durnel na kuachia kigongo kufanya bao ziwe 1-1.
Kona ya Simon Davies kwenye dakika ya 76 ilimkuta Zoltan Gera aliemalizia na kufunga bao la pili na la ushindi ni lililowapeleka Fulham Fainali ya EUROPA LIGI itakayochezwa Uwanja wa Timu waliyoifunga, Hamburg, uitwao Nordbank Arena hapo Mei 12.
Vikosi vilikuwa:
Fulham: Schwarzer, Pantsil, Hangeland, Hughes, Konchesky, Davies, Murphy, Etuhu, Duff, Gera, Zamora.
Akiba: Zuberbuhler, Nevland, Riise, Dempsey, Smalling, Greening, Dikgacoi.
Hamburg: Rost, Aogo, Mathijsen, Boateng, Demel, Pitroipa, Ze Roberto, Jarolim, Tesche, Petric, van Nistelrooy.
Akiba: Hesl, Rozehnal, Guerrero, Berg, Arslan, Rincon, Schulz.
Refa: Cuneyt Cakir (Turkey)

Thursday 29 April 2010

Ni Usiku wa EUROPA!!!
Liverpool v Atletico Madrid
Liverpool wako nyumbani Anfield wakijaribu kuambulia kitu Msimu huu baada ya kupoteza mwelekeo katika Mashindano yote lakini inabidi waupindue ushindi wa bao 1-0 walioupata Atletico Madrid kwenye mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ili watinge Fainali.
Hii ni mara ya tatu kwa Liverpool kufungwa mechi za kwanza katika EUROPA LIGI na kisha kuibuka kidedea mechi za marudiano dhidi ya Lille na Benfica.
Hata hivyo Liverpool wana kazi kubwa kulifuta goli la Mchezaji wa zamani wa Manchester United Diego Forlan hasa kwa vile wana matatizo kwenye safu ya mashambulizi kwa kukosekana Fernando Torres ambae ni majeruhi na pia kuna hati hati kuhusu kucheza kwa Dirk Kuyt na David Ngog kwani nao pia wana maumivu.
Pia Maxi Rodriguez haruhusiwi kucheza leo baada ya kuwahi kuichezea Atletico awali kwenye Mashindano haya.
Atletico wataongezeka nguvu baada ya Straika wao kutoka Argentina Sergio Aguero kumaliza kifungo cha mechi moja na hivyo atashirikiana na Diego Forlan mbele na pembeni watakuwepo Mawinga Antonio Reyes, Mchezaji wa Arsenal zamani, na Simao Sabrosa.
Fulham v Hamburg
Baada ya sare 0-0 ugenini huko Ujerumani, Fulham watajihisi wana nafasi nzuri sana kuwashinda Hamburg leo na kuingia Fainali hasa ukizingatia Hamburg ni goigoi na wikiendi iliyopita waliwashwa bao 5-1 na Hoffenheim kwenye Bundesliga na ikabidi Kocha wao Bruno Labbadia atimuliwe kufuatia matokeo hayo pamoja na kushinda mechi 3 tu kati ya 14 za nyuma yake.
Hata hivyo motisha pekee kwa Hamburg ni kutambua kwao kuwa Fainali ya EUROPA LIGI Msimu huu itafanyika Uwanjani kwao Nordbank Arena hapo Mei 12.
Fulham wana wasiwasi mkubwa kuhusu Mfungaji wao mkuu Bobby Zamora ambae ana maumivu ya mguu.
Pia watamkosa Chris Baird ambae amefungiwa mechi hii lakini nafasi yake itazibwa kirahisi na Beki toka Ghana John Pantsil ambae amepona.
Man City yapata Kipa
Uhaba wa Kipa ulioikumba Manchester City sasa umekwisha baada ya kumsajili kwa dharura Kipa wa Akiba kutoka Sunderland, Marton Fulop, ili awadakie mechi 3 za Ligi Kuu zilizobaki.
Man City walikumbwa na upungufu huo baada ya Makipa wao wote kuumia na hao ni Kipa Nambari Wani Shay Givens, alieumia kwenye droo ya 0-0 na Arsenal wikiendi iliyopita, Stuart Taylor na David Gonzalez.
Kipa mwingine wao wa kutumainiwa, Joe Hart, yupo Birmingham kwa mkopo na mkataba wake umemzuia kurudi Klabuni kwake Man City hadi Msimu huu unapokwisha.
Furlop alizungumza: “Nilipata simu Jumanne. Na nilifurahi kuja kuisaidia Man City. Itanipa chansi kucheza!”
Nae Meneja wa Sunderland, Steve Bruce, amesema ni nafasi nzuri kwa Kipa wao huyo wa Akiba kucheza kwani Klabuni hapo Kipa Nambari wani ni Craig Gordon, ambae ni Kipa wa Taifa wa Scotland, na ndie amemfanya Furlop kukosa namba.
"MTU SPESHELI”: Misifa Mourinho achekelea, asifiwa!!
Kocha mpenda sifa, mwenye kauli za kejeli na machachari, aliebatizwa “Mtu Spesheli”, Jose Mourinho, ameisifia Timu yake Inter Milan kwa kuibwaga Barcelona waliokuwa Mabingwa Watetezi wa Ulaya na wao kuingia Fainali na watakutana na Bayern Munich hapo Mei 22 kupata Bingwa mpya wa Ulaya.
Ingawa Barca walishinda 1-0 hapo jana wametupwa nje kwa jumla ya bao 3-2 baada ya kufungwa mechi ya kwanza 3-1.
Inter walicheza mechi ya jana kwa zaidi ya saa moja huku wakiwa Mtu mmoja pungufu Mchezaji wao Thiago Motta alipopewa Kadi Nyekundu.
Mourinho alinena: “Hii ni bora kuliko kushinda CHAMPIONS LIGI! Barca walitegemea kushinda! Huwa na maajabu Nou Camp lakini tuligundua wanatuogopa!”
Huku akiwa na furaha Mourinho ameihakikishia Inter kuwa atabaki nao Msimu ujao licha ya kuwa na tetesi nyingi kuwa yuko njiani kuondoka.
Mwenyewe alisema: “Naiheshimu Soka ya Italia lakini sina mapenzi na Soka ya Italia! Ntabaki Msimu ujao!”
Kuhusu Refa, Mourinho alizungumza: “Sitaki kumhukumu. Nilisema kabla ya mchezo kama Wachezaji watamsaidia Refa mechi ni nzuri lakini wakiwa wakorofi, kuna matatizo. Na usiku huu, Wachezaji walijaribu kuleta utata na ugumu!”
Nae Rais wa Inter Milan, Massimo Moratti, alimsifia Mourinho na kumwita Bora.
Moratti alisema: “Mourinho ni shujaa! Sasa tupo Fainali 3! Tupo Ulaya, tupo Coppa Italia na kwenye Serie A tuko karibu! Shukrani zote kwa Mourinho! Ni Meneja bora yeye!!”
Leo ni Marudiano NUSU FAINALI: Liverpool v Atletico Madrid na Fulham v Hamburg
Liverpool leo wako kwao Anfield wakitaka kuupinndua ushindi wa bao 1-0 wa Atletico Madrid katika mechi ya kwanza ili wasonge na kuingia Fainali ya EUROPA LIGI.
Nako huko Craven Cottage kwenye marudio ya Nusu Fainali nyingine, wenzao Fulham watawakaribisha Hamburg waliotoka nao sare 0-0 kwenye mechi ya kwanza huko Ujerumani.
Timu zote, Liverpool na Fulham, zilipata taabu mno kwenda kucheza mechi zao za kwanza za ugenini za huko Spain na Ujerumani pale walipolazimika kutumia usafiri wa ardhini wa Treni, Meli na Mabasi kwa vile wiki iliyopita Ulaya ilikumbwa na balaa la Majivu ya Volcano kutoka Iceland iliyosababisha safari za anga kusimama.
Balaa hilo leo halipo na Atletico Madrid na Hamburg zimesafiri raha mustarehe kwenda kwnye vituo vyao vya Miji ya London na Liverpool kwa ndege.

Inter Fainali!!!! Barca washinda lakini njeee!!!!
Barcelona, mbele ya Mashabiki wao 98,000, walishindwa kuingia Fainali itayochezwa kwenye Uwanja wa Mahasimu zao wakubwa Real Madrid, Uwanja wa Santiago Bernabeau hapo Mei 22, licha ya kuifunga Inter Milan bao 1-0 na hivyo kutolewa nje kwa jumla ya mabao 3-2 kwa vile Inter Milan walishinda mechi ya kwanza 3-1.
Inter Milan walijihami vizuri mno licha ya kucheza Mtu 10 kwa zaidi ya saa moja baada ya Thiago Motta kutolewa kwa Kadi Nyekundu na Refa kutoka Ubelgiji Frank de Bleeckere kwa kumpiga Sergio Busquets.
Bao lililowapa matumaini Barca lilifungwa na Gerrard Pique dakika 6 kabla mpira kwisha na Barca walifunga tena dakika za majeruhi kwa bao la Bojan lakini Refa alilikataa kwa kufanyika madhambi kabla ya kufungwa.
Inter Milan watakutana na Bayern Munich kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI na hii ni Fainali ya kwanza ya Ulaya kwa Inter tangu 1972.

Wednesday 28 April 2010

Ribery kuikosa Fainali UEFA
-Kifungo Mechi 3!!!
Nyota wa Bayern Munich Franck Ribery ataikosa Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI baada ya UEFA kumfungia mechi tatu.
Ribery alipewa Kadi Nyekundu katika mechi ya kwanza kati ya Bayern Munich na Lyon baada ya kumkanyaga Fowadi wa Lyon Lisandro Lopez na jana hakucheza mechi ya marudiano ambayo Bayern walishinda 3-0 na kufuzu kuingia Fainali.
Lakini sasa UEFA imeamua kumfungia mechi 3 baada ya kupitia upya tukio hilo na hivyo Fainali itakuwa mechi yake ya pili ya kifungo chake cha mechi 3.
Bayern Munich imepewa siku tatu kukata Rufaa lakini kwa kawaida kwa UEFA Rufaa huwa zinapiga chini.
Mkongwe amtaka Scholes arudishwe England
Mkongwe Sir Geoff Hurst ambae aliisaidia England kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1966 ametaka Mchezaji wa Manchester United Paul Scholes arudishwe tena Kikosi cha England na amemwomba Meneja wa England Fabio Capello amwite Mchezaji huyo.
Scholes, miaka 35, alieichezea England mara 66, alistaafu kucheza Timu hiyo mwaka 2004.
Lakini Sir Geoff Hurst, aliefunga goli 3 mguuni kwake na kuiua Ujerumani 4-2 katika Fainali ya Kombe la Dunia iliyochezwa Wembley mwaka 1966 na kuifanya England iwe Bingwa wa Dunia, amemtaka Capello amwite Scholes kwenye Kikosi chake na amedai hilo litaongeza uwezo wa England kunyakua Kombe la Dunia huko Afrika Kusini.
LISTI YA UBORA FIFA: Brazil Nambari Wani, Spain mbili, England 8 na Bongo yapanda nafasi moja……..ni wa 108!!!!
Brazil wameipiku Spain na kuchukua uongozi na kuwa Timu Bora Duniani kwa mara ya kwanza baada ya Miezi mitano kufuatana na Listi ya FIFA.
Spain wako nafasi ya pili.
Ureno imepanda hadi nafasi ya 3 na hii ikiwa nafasi ya juu kwa wao kuifikia.
Argentina wamepanda nafasi mbili na kushika nafasi ya 7 na hivyo England kushuka hadi nafasi ya 8.
Holland wako nafasi ya 4, Italy ya 5, Ujerumani ya 6 na Croatia nafasi ya 9.
Timu kutoka Afrika ambayo iko nafasi ya juu kabisa ni Misri iliyo nafasi ya 13 baada ya kupanda nafasi moja.
Katika Nchi za afrika ambazo ziko Fainali ya Kombe la Dunia, Cameroun ndio wako juu na wapo nafasi ya 19 baada ya kupanda nafasi moja.
Tanzania nayo imepanda nafasi moja na kushika namba ya 108.
Barcelona v Inter Milan
Leo, Barcelona wako nyumbani Nou Camp huku wakiwa nyuma kwa bao 3-1 walizofungwa na Inter Milan katika mechi ya kwanza huko San Siro.
Ili waingie Fainali, Mabingwa hao watetezi wa Ulaya wanahitaji ushindi wa bao 2-0.
Lengo hilo limewafanya Wachezaji wa Barca, wakiongozwa na Mfungaji Bora mpaka sasa wa UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu huu, Lionel Messi, kuitaka Timu yao itafute mabao mengi kiasi wawezacho.
Barca watamkosa Beki wao mahiri Puyol ambae amefungiwa na Inter wana wasiwasi huenda wakamkosa Goran Pandev na Nyota wao Wesley Sneijder ambao wana maumivu.
Kocha wa Barca, Pep Guardiola, akizungumzia mechi hii, amesema: “Lazima tuukontroli mpira na kushambulia vyema kupita mechi ya kwanza. Lazima tuwe kama kawaida yetu tusiwajali wao. Huu si uchawi ni soka tu!”
Nae Kocha machachari wa Inter Milan, Jose Mourinho, amesema: “Tuna ndoto ya kucheza Fainali. Kwa Barca si ndoto ni wazimu! Wao walitimiza ndoto yao waliposhinda Fainali mwaka jana! Kwao, safari hii, si ndoto ni wazimu kutaka kucheza Fainali Madrid Uwanjani Santiago Bernabeau!”
Hii ni mara ya 4 kwa Timu hizi kukutana kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu huu.
Walikuwa Kundi moja na mechi ya kwanza huko San Siro ilikuwa 0-0 na marudiano Nou Camp, Barca waliinyuka Inter 2-0.
Solano abambwa!!
Mchezaji wa Leicester City ambae zamani alikuwa Newcastle United, Norberto Solano, amekamatwa na Polisi wa Mjini Newacastle kwa tuhuma za kubaka.
Solano, miaka 35, alikamatwa jana asubuhi baada ya Mwanamke mmoja wa miaka 22 kushitaki na Polisi walithibitisha kumkamata Solano na kumuhoji kisha kumuachia kwa dhamana.
Solano, Raia wa Peru, alikaa Newcastle kwa miaka minane kwa vipindi viwili na pia amewahi kuchezea Aston Villa na West Ham.
Alijiunga na Leicester City Januari mwaka huu.
Beki Sunderland apunguziwa adhabu ya kufungiwa
Beki wa Sunderland, Alan Hutton, amepunguziwa adhabu ya kufungiwa mechi 3 na sasa atatumikia kifungo cha mechi moja tu.
Hutton na Fowadi wa Hull City, Jozy Altidore, wote wawili walitolewa kwa Kadi Nyekundu na Refa Lee Probert walipofarakana katika mechi ya Ligi Kuu Jumamosi ambayo Sunderland waliishinda Hull bao 1-0 Uwanjani KC.
Altidore alimpiga kichwa Hutton na Hutton akarudishia kwa kumpiga Altidore kwa mpira lakini Sunderland wakata Rufaa kwa Kamati Huru ya Sheria ya FA na Kamati hiyo imeafiki Rufaa na kupunguza adhabu.
Hutton sasa ataikosa mechi ya Jumapili Sunderland watakapoikaribisha Man United Stadium of Light lakini yuko ruksa kucheza mechi inayofuata na ambayo ndio ya mwisho ya Ligi watakapocheza na Wolves Uwanjani Molineux.

Tuesday 27 April 2010

UEFA CHAMPIONS LIGI: Bayern watinga Fainali!!!
Ndani ya Stade Gerland, Bayern Munich walitawala mechi ya marudiano na Wenyeji wao Lyon na kuwachakaza kwa bao 3-0 na hivyo kutinga Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI ambako watakutana na Mshindi kati ya Barcelona na Inter Milan.
Bayern, walioshinda mechi ya kwanza bao 1-0 huko Allianz Arena wiki iliyopita, walipata bao zote 3 kupitia Straika kutoka Croatia Ivica Olic.
Ushindi huu kwa namna nyingine ulichangiwa na kupewa Kadi Nyekundu kwa Nahodha wa Lyon Cris ambae alipata Kadi za Njano mbili ndani ya dakika moja na hivyo kutolewa.
Olic alipachika bao la kwanza dakika ya 26.
Lyon walipata pigo lao kubwa dakika ya 60 Cris alipotolewa nje na mechi kwao ikaharibika kwani wakati huo walikuwa wanahitaji bao 3 kusonga mbele.
Wakionyesha kutokuwa na pengo kwa kucheza bila ya Staa Franck Ribery, Olic aliongeza bao la pili dakika ya 67 na dakika ya 78 Olic alifunga bao la 3 kwa kichwa kufuatia krosi ya Fulbeki Philipp Lahm.
Mchecheto Liverpool v Chelsea Jumapili
-Gerrard aahidi ushindi!
-Rooney adai Liverpool haitaitupa mechi hiyo!
Mechi ya Ligi Kuu kati ya Liverpool na Chelsea itakayochezwa Jumapili hii huko Anfield ni mechi ambayo tayari imeshaanza kuzua mijadala toka kila kona.
Liverpool bado wana imani wa kuikwaa nafasi ya 4 na hivyo kucheza Ulaya Msimu ujao ingawa ukweli ni kuwa nafasi ya kuipata ni finyu kwa vile Tottenham na Man City, na hata Aston Villa, wanaiwania na wana nafasi kubwa kupita wao.
Lakini, ni ukweli pia, kimahesabu Liverpool wanaweza kuipata nafasi hiyo ya 4 ikiwa wataifunga Chelsea na pia kushinda mechi yao ya mwisho huku wakiombea matokeo mabovu kwa wengine wanaowania nafasi hiyo.
Endapo Liverpool atamsimamisha Chelsea kwa ama kumfunga au kutoka sare na Manchester United kushinda mechi yake na Sunderland ambayo pia inachezwa Jumapili, Man United atautwaa uongozi wa Ligi Kuu na akiifunga Stoke City katika mechi ya mwisho Mei 9 Uwanjani Old Trafford wao watauchukua Ubingwa kwa mara ya 4 mfululizo, hiyo ikiwa ni rekodi, na pia itakuwa ni mara ya 19 kuwa Bingwa na hivyo kuwapita Liverpool waliochukua mara 18.
Sasa swali ni, Liverpool, ambao ni Mahasimu wakubwa wa Man United, watakubali “kuisaidia” ichukue Ubingwa na kuweka rekodi hizo mbili?
Staa wa Man United, Wayne Rooney, ametamka: “Sidhani Liverpool watapoteza mechi hiyo kwa makusudi! Sihitaji kuongea na Gerrard ili kuhakikisha Liverpool wanashinda. Yeye ni Mchezaji wa Kulipwa na siku zote ni mshindani asiekubali kufungwa hata mechi ya kirafiki!”
Na kweli, Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, amesema wao wanataka kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao na akaongeza: “Tukishinda mechi zetu mbili na Timu zilizo juu yetu zikiteleza lolote linaweza kutokea. Lazima tuweke presha na ni lazima tushinde mechi zetu!”
Baada ya kutwangwa 7, Wachezaji watwangana!!!
Taarifa toka ndani ya Klabu ya Stoke City zimetoboa kuwa Wachezaji wao wawili walitwangana mara baada ya kutandikwa bao 7-0 na Chelsea huko Stamford Bridge siku ya Jumapili.
Wachezaji hao ni Abdoulaye Faye kutoka Senegal na Glenn Whelan anaetoka Ireland na bifu lao inasemekana lilianza kabla ya mchezo wakati Whelan alipomtaka Faye kutopasha moto kwenye Vyumba vya Kudalisha jezi huku amevaa makubadhi kwani hilo linaonyesha hana nidhamu.
Inasemekana bifu hilo liliendelea hadi wakati wa mapumziko na lilichochewa zaidi ilipotokea Faye kushindwa kuendelea na mechi na kubadilishwa dakika ya 9 tu ya mchezo na ndipo Whelan alipodai kushindwa kwa Faye kuendelea kucheza kumechangiwa na utovu wake wa nidhamu kuhusu maandalizi bora kwa mechi.
Faye akakasirishwa na kauli za Whelan na wakaanza kufarakana lakini Whelan akamwambia Faye waongee baada ya mechi.
Mechi ilipokwisha kwa Stoke kubondwa bao 7, Faye kweli akamfuata Whelan na maneno yao yakafuatiwa na konde la Faye lililotua usoni kwa Whelan na kusababisha Wachezaji kadhaa kuingilia kati na kuamua.
Kwa Stoke City hii ni skandali ya pili kuibuka toka Vyumba vyao vya Kubadilisha Jezi baada ya ile inayosemekana kutokea miezi minne iliyopita ambapo ilidaiwa Meneja Toni Pulis alimtwanga kichwa Straika wake James Beattie.
Nusu Fainali: Leo Lyon v Bayern, kesho Barca v Inter
Bayern Munich na Inter Milan zimeshika mpini katika Nusu Fainali za UEFA CHAMPIONS LIGI baada ya kushinda mechi zao za kwanza na leo na kesho ni marudiano lakini hakuna anaeweza kusema basi Bayern na Inter tayari zipo Fainali.
Lyon alipigwa na Bayern bao 1-0 huko Ujerumani na leo yuko nyumbani Stade Gerland akiwania kuupindua ushindi wa Bayern Munich.
Kesho ndio kindumbwendumbwe huko Nou Camp wakati Wenyeji Barcelona watawania kuifunga Inter Milan kwa bao 2-0 ili waipiku Inter kwa goli la ugenini baada ya kufungwa mechi ya kwanza 3-1 huko San Siro.
Kocha wa Lyon, Claude Puel, amedai wao hucheza vizuri zaidi wakitaka ushindi kuliko wanapokuwa wanajilinda tu na hilo limeungwa mkono na Mfungaji wao mkuu kutoka Argentina, Lisandro Lopez, ambae ametaka mashambulizi mfululizo.
Katika mechi hiyo ya leo Bayern watamkosa Nyota Franck Ribery na Lyon hawatakuwa na Jeremy Toulalan baada ya Wachezaji hao kutolewa kwa Kadi Nyekundu katika mechi ya kwanza.
Vile vile, Bayern huenda wakawakosa Masentahafu wao, Daniel van Buyten na Martin Demichelis, ambao wameumia.

Monday 26 April 2010

Man City hawana Kipa!!!
Manchester City wamepeleka ombi la dharura kwa Wasimamizi wa Ligi Kuu ili waruhusiwe kusajili Kipa kwa mkopo wa dharura ili waweze kumaliza mechi zao 3 za Ligi Kuu zilizobaki na kuweza kufanikisha azma yao kuinyaka nafasi ya 4 kwenye Ligi na hivyo kucheza Ulaya Msimu ujao.
Ghafla majeruhi kwa Makipa wao imeifanya Man City ikose Kipa wa kutegemewa hata mmoja.
Kipa wao nambari moja Shay Givens aliteguka bega Jumamosi Uwanjani Emirates walipotoka droo na Arsenal.
Kipa wao nambari mbili, Stuart Taylor, alifanyiwa operesheni ya goti na hajapona na Kipa wao mwingine wa kutumainiwa, Joe Hart, ambae ndie ametajwa kuwa ndio Kipa wa Timu Bora ya Msimu, yuko kwa mkopo kwa Msimu wote huu huko Birmingham na mkataba wake haumruhusu kurudi Klabuni kwake Man City hadi Msimu huu uishe.
Kipa nambari nne, David Gonzalez nae pia majeruhi baada ya kuumia nyonga.
Baada ya kuumia Shay Givens Jumamosi akaingizwa Kipa kutoka Faroe Islands Gunnar Nielsen ambae haaminiki kabisa.
Kipa pekee mwingine Man City wanaweza kumchukua ni Bwana Mdogo Loris Karius anaechezea Timu ya Watoto kwenye Chuo chao cha Mafunzo.
Ancelotti avimba bichwa!!
Baada ya kupata lundo la magoli jana walipoibamiza Stoke City bao 7-0 na kutwaa tena uongozi wa Ligi Kuu wakiwa mbele ya Manchester United kwa pointi moja, Meneja wa Ancelotti amedai hawana presha yeyote na wanajua wakishinda mechi zao mbili zilizobaki wao ni Mabingwa.
Ancelotti amedai: “Tulikuwa na presha kabla ya mechi na Stoke. Lakini sasa hatuna na tunajua tukishinda mechi mbili ni Mabingwa.”
Chelsea Jumapili watakuwa Anfield kuikwaa Liverpool ambao bado wana matumaini ya kuitwaa nafasi ya 4 ya Ligi na hivyo kucheza Ulaya Msimu ujao.
Mechi yao ya mwisho ni Stamford Bridge na Wigan.
Rooney ni Mchezaji wa Mwaka
-Milner aopoa kwa Vijana
-Radebe apewa Tuzo ya Kutukuka
Wayne Rooney amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka huko England katika uchaguzi uliofanywa na Wachezaji wa Kulipwa kupitia Chama chao PFA [Professional Footballers Association].
Straika huyo wa Manchester United aliwabwaga Didier Drogba, Carlos Tevez na Cesc Fabregas katika uchaguzi huo.
Rooney, miaka 24, alisema: “Najiskia furaha sana kushinda Tuzo hii kwa sababu nimechaguliwa na Wachezaji wenzangu. Ni heshima kubwa na nasikia fahari mno!”
Msimu huu, Rooney amefunga mabao 34 na ameng’ara sana hasa kwa vile amesogezwa mbele zaidi katika pozisheni ya uchezaji na hilo limemfanya afunge bao nyingi.
Pia kuondoka kwa Ronaldo na Tevez Man United kulimtwisha mzigo mkubwa lakini ameweza kuleta mafanikio makubwa Klabuni kwake.
Katika Tuzo kama hiyo kwa upande wa Wachezaji Vijana, James Milner wa Aston Villa ndie Mshindi.
Nae Mchezaji wa zamani wa Leeds na Bafana Bafana, Lucas Radebe, miaka 41, ametunukiwa Tuzo ya Kutukuka ya PFA kwa kutambua mchango wake mkubwa kwa jamii.
Radebe amezungumza: “Michezo hubadilisha Dunia. Soka imetoa mchango mkubwa kuinua jamii yangu. Nasikia fahari mno kushinda Tuzo hii!”
-TIMU BORA YA LIGI KUU YA MWAKA:
Sambamba na Wachezaji Bora, pia ilichaguliwa Timu Bora na ni kama ifuatavyo huku Klabu za Wachezaji kwenye mabano:
-Kipa: Joe Hart [Man City, yuko kwa mkopo Birmingham]
-Branislav Ivanovic [Chelsea], Thomas Vermaelen [Arsenal], Richard Dunne [Aston Villa], Patrice Evra [Man United], Cesc Fabregas [Arsenal], James Milner [Aston Villa], Darren Fletcher [Man United], Antonio Valencia [Man United], Wayne Rooney [Man United], Didier Drogba [Chelsea].
Deco kung’atuka Chelsea
Mchezaji wa Kimataifa wa Ureno mwenye asili ya Brazil, Deco, miaka 32, ameamua kuondoka Chelsea Msimu huu ukiisha na kurudi kwao Brazil ili kuendesha Shule aliyoianzisha Nchini humo.
Deco alijiunga na Chelsea mwaka 2008 akitokea Barcelona.
Deco alizaliwa Mji wa Sao Bernardo do Campo huko Brazil na kuhamia Ureno akiwa na miaka 19 na akapata uraia wa Ureno mwaka 2002.
Hata hivyo mwenyewe Deco hajasema kama akiwa huko Brazil ataendelea kucheza mpira au la.
Deco amesema: “Nina rafiki yangu huko Brazil ambae ni Daktari na huniambia ipo siku nitakuwa Mchezaji mpira wa zamani lakini yeye hawezi kuwa Daktari wa zamani! Kuna taaluma nyingi huwezi kuziacha lakini soka lazima unaiacha!”

Sunday 25 April 2010

Chelsea 7 Stoke 0
-Chelsea yarudi kileleni kwa kishindo!!
Wakiwa nyumbani Stamford Bridge, Chelsea leo wameishindilia Stoke City bao 7 na kuipiku Manchester United kileleni.
Zikiwa zimebaki mechi mbili, Chelsea wanaongoza wakiwa na pointi 80 na Manchester United wana pointi 79.
Mechi inayofuata kwa Chelsea ni safari ya Anfield kuivaa Liverpool wakati Manchester United watakuwa Stadium of Light kucheza na Sunderland.
Mechi zote hizo zitakuwa Jumapili Mei mbili.
Mpaka mapumziko Chelsea walikuwa mbele kwa 3-0.
Mabao ya Chelsea yalifungwa na Kalou, bao 3, Lampard bao 2, Sturridge moja na Malouda moja.
Rangers Mabingwa Scotland
Leo Rangers wamefanikiwa kutetea Taji la Ubingwa wa Scotland walipowalaza Hibernian kwa bao 1-0 Mfungaji akiwa Kyle Lafferty.
Rangers wangeweza kuutwaa Ubingwa mapema leo kama Celtic wangeteleza lakini hao Mahasimu wao wakubwa waliibuka washindi walipowafunga Dundee United bao 2-0 katika mechi iliyoanza mapema kabla ya Rangers.
Burnley waporomoka!
Burnley imekuwa Timu ya pili Msimu huu kushuka Daraja na kuifuata Portsmouth walipotandikwa bao 4-0 na Liverpool Uwanjani Turf Moor.
Burnley walivimba hadi mapumziko bao zikiwa 0-0 lakini kisago chao kikaanza kipindi cha pili Steven Gerrard alipofunga bao mbili dakika ya 52 na 59.
Kisha Maxi Rodriguez akapachika bao la 3 dakika ya 74 na Babel amaliza kwenye dakika za majeruhi.
Liverpool wapo nafasi ya 7 wakiwa pointi mbili tu nyuma ya Tottenham walio nafasi ya 4.
Everton 2 Fulham 1
Penalti ya dakika za majeruhi iliyofungwa na Mikel Arteta imewapa Everton ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Fulham Uwanjani Goodison Park kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Fulham walitangulia kupata bao baada ya makosa ya Beki Leighton Baines kutaka kumrudishia Kipa Tim Howard na Erik Nevland akaunasa na kufunga.
Hiyo ilikuwa dakika ya 36.
Kipindi cha pili dakika ya 49, kichwa cha Victor Anichebe kilimgonga Beki Chris Smalling, ambae Msimu ujao atachezea Man United, na kuisawazishia Everton.
Ndipo ngoma ikielekea kulala Chris Baird akamchezea madhambi Tim Cahill na ikaamuliwa penalti.
Dabi ya Midlands: Tuta la utata lawabeba Villa!!
Katika dabi ya Timu za eneo la Midlands huko England, Aston Villa leo wamefanikiwa kuwatungua jirani zao Birmingham kwa bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu kwa penalti yenye utata iliyotolewa na Refa Martin Atkinson huku kila mtu alimwona Beki Roger Johnson akiucheza mpira na sio Fowadi wa Villa Agbonlahor.
James Milner ndie aliefunga penalti hiyo katika dakika ya 83 na kuwafanya Villa wawe pointi 64 sawa na Timu ya 4 Tottenham ingawa Villa wamecheza mechi moja zaidi.
Birmingham ndio waliopata nafasi nyingi katika mechi hii na wangeweza kuibuka na ushindi kama si uhodari wa Kipa wa Villa Brad Friedel.
Torres : “Ligi Kuu ni hatari kwangu!”
Fernando Torres amedokeza kuwa afya yake iko mashakani kwa kuchezea Liverpool kwenye Ligi Kuu na ana wasiwasi wa kupata maumivi yatakayoathiri maisha yake ya baadae.
Torres amedokeza kuwa akiacha kucheza Liverpool ataondoka kabisa Uingereza hivyo kuondoa zile fikra kuwa huenda akachukuliwa na Manchester City ambao imedaiwa wametenga dau la Pauni Milioni 60 ili kumnasa Msimu utakapoisha.
Torres, ambae huu ni Msimu wake wa tatu tangu ahamie Liverpool kutoka Atletico Madrid, amesema Ligi Kuu ni ngumu na Wachezaji hutumia miguvu sana. Pia, amesema anashangazwa kuwaona Rooney, Lampard na Gerrard wakicheza miaka nenda rudi bila kuathirika.
Torres, ambae sasa anauguza goti, alisema: “Sijui ntakuwaje nikiendelea kucheza hapa kwa miaka mitano au sita ijayo! Nadhani itanisumbua baadaye nikistaafu kucheza kwa kuwa na maumivu!”
Wadau wanahisi matamshi ya Torres ni dalili yuko mbioni kuondoka.
Meneja wa Stoke adai Timu kubwa zinabebwa
Meneja wa Stoke City, Tony Pulis, amedai Timu kubwa zinapendelewa na kubebwa na Marefa.
Stoke leo wako Stamford Bridge kucheza na Chelsea kwenye mechi muhimu sana kwa Chelsea wanaotaka ushindi ili waing’oe Manchester United kileleni.
Pulis ametamka hayo akikumbushia mechi yao ya mwisho walipocheza na Chelsea kwenye Ligi Kuu mwezi Septemba na Chelsea walifunga bao mbili katika mbili za mwisho na kuibuka na ushindi.
Pulis alichukizwa na Refa wa mechi hiyo Mike Dean na akawapelekea FA mkanda wa DVD waone jinsi Refa huyo alivyochezesha mechi hiyo.
Stoke City wataumaliza Msimu wao huu kwa kucheza na Manchester United huko Old Trafford Mei 9.
Redknapp adai presha iko kwa Chelsea
Bosi wa Tottenham, Harry Redknapp, anaamini Chelsea ndio wenye mechi ngumu kuliko Manchester United katika vita kati yao ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu.
Man United wanaongoza Ligi kwa pointi mbili baada ya kuifunga Tottenham hapo jana lakini Chelsea wana mechi moja mkononi ambayo wanaicheza leo nyumbani kwao na Stoke City.
Lakini Redknapp amedai: “Naona Man United watapata pointi 6 katika mechi zao mbili za mwisho wakicheza na Sunderland na Stoke. Si rahisi kwa Chelsea kwani wanacheza na Stoke kisha Liverpool halafu Wigan!”
Redknapp amedai pia Stoke mara zote huwa wagumu kwa Chelsea na kukumbushia katika mechi mbili za mwisho ambazo Chelsea wamekuwa wakiifunga Stoke kwa mbinde dakika za majeruhi na kwa msaada wa utata wa Marefa.
Blatter aiponda Afrika kutimua Makocha kila kukicha!
Rais wa FIFA, Sepp Blatter, ambae husaidia sana Afrika kisoka, amelaumu vikali tabia ya Nchi za Afrika kubadilisha Makocha kila mara.
Blatter amesema Afrika ina vipaji sawa au zaidi ya Brazil na Nchi za Marekani ya Kusini lakini mbinu hamna na hilo haliwezi kupatikana ikiwa Makocha wanabadilika mara kwa mara na tena hufanyika karibu na Mashindano makubwa.
Afrika ina Nchi 5 kwenye Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 11 huko Afrika Kusini na tatu kati ya hizo zimebadilisha Makocha hivi karibuni.
Mwishoni mwa mwezi uliokwisha Ivory Coast ilimteua Kocha wa zamani wa England Sven-Goran Eriksson baada ya kumtimua Vahid Halilhodzic kutoka Bosnia.
Nigeria ilimteua Lars Lagerback kutoka Sweden kumbadili Shaibo Amodu mwezi Februari.
Afrika Kusini nao walimteua Mbrazil Carlos Alberto Parreira mwezi Oktoba mwaka jana baada ya kumfukuza Mbrazil mwingine Joel Santana.
Santana alikuwa kachukua nafasi ya Parreira Aprili 2008 alielazimika kuondoka baada ya kuuguliwa na Mkewe.
Powered By Blogger