Sir Alex Ferguson amedai Roy Hodgson wa Fulham ndie anastahili kuwa Meneja Bora wa Mwaka kwa kuiletea Fulham mafanikio ya ajabu pale alipoiwezesha Klabu hiyo kutinga Fainali ya EUROPA LIGI na hilo ni jambo kubwa sana kwa Klabu ya Uingereza.
Jana, Fulham, walitoka nyuma kwa bao 1-0 na kuichapa Hamburg 2-1 na kutinga Fainali ambako watakutana na Atletico Madrid walioitoa Liverpool pia hapo jana.
Ferguson ametamka: “Roy ni lazima awe Meneja wa Mwaka! Ni miujiza! Naomba ashinde Kombe hilo na haya ni mafanikio makubwa kupita yote kwa Klabu ya Uingereza!”
Ferguson alibainisha alimtumia Hodgson ujumbe wa kumtakia heri kabla ya mechi na hata Wachezaji wa Timu yake, akiwemo Kipa Edwin van der Sar aliesajiliwa na Man United kutoka Fulham, walikuwa wakitaka Fulham ishinde.
Nae Meneja wa Wolves Mick McCarthy pia aliunga mkono uteuzi wa Hodgson kuwa Meneja wa Mwaka kwa kuiwezesha Fulham kupata mafanikio makubwa licha ya kuwa Klabu ndogo na uwezo duni kiuchumi.
Ferguson awategemea Liverpool kuwa kidete!
Sir Alex Ferguson amesisitiza Mahasimu wao wakubwa Liverpool hawawezi ‘kutupa mkono historia’ na kuwapa ushindi wa chee Chelsea ili mradi tu Manchester United wasipate nafasi ya kuwa Bingwa.
Chelsea, wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi moja tu mbele ya Manchester United huku kuna mechi mbili zimebaki, Jumapili wanasafiri hadi Anfield kucheza na Liverpool ambao bado wana matumaini finyu ya kunyakua nafasi ya 4 na hivyo kucheza Ulaya Msimu ujao.Takriban nusu saa tu baada ya mechi ya Liverpool na Chelsea, Man United watajimwaga Uwanjani Stadium of Light kucheza na wenyeji wao Sunderland na ikiwa Chelsea atafungwa au kutoka sare na Liverpool na Man United kuifunga Sunderland, Man United watatwaa uongozi wa Ligi na washindani hao watakuwa wamebakiwa na mechi moja tu.
Ikiwa Manchester United watatwaa Ubingwa Msimu huu watawapita Liverpool kwa kutwaa Ubingwa mara nyingi kwani Klabu hizi mbili zimefungana kwa kuutwaa mara 18 kila mmoja.
Ferguson amedai: “Klabu kubwa haziwezi kutupa asili yao ya jadi kwa ajili ya gemu moja tu. Mashabiki wanajua hilo. Hivi unafikiri Mashabiki wanataka kurudi nyumbani huku wakilaumu Wachezaji wao kuitupa mechi kwa kusudi na huku wakijua hilo linaweza kutokea tena?”
Baadhi ya Wadau wanaukumbuka Msimu wa Mwaka 1995 ambao siku ya mwisho ya Ligi Manchester United walisafiri hadi Upton Park kucheza na West Ham wakitaka ushindi na pia kuomba Liverpool waifunge Blackburn Uwanjani Anfield ili wawe Mabingwa.
Siku hiyo Liverpool waliifunga Blackburn lakini Man United walitoka sare na West Ham na Ubingwa ukabebwa na Blackburn.
Ferguson alikumbushia hilo: “Tuliwategemea Liverpool! Walitusaidia lakini tulishindwa wenyewe!”
Nae Kipa wa Liverpool, Pepe Reina, amedai: “Sichezi Timu yao! Mie nacheza Liverpool na sijali Man United watafanya nini. Jumapili ntacheza tushinde kwa sababu tunataka pointi 3 na bado tuna nafasi ya kuitwaa nafasi ya 4! Tunacheza nyumbani na hapa hatuchezi kutoka sare au kufungwa! Tunataka kuleta ushindi wa mwisho wa Msimu hapa nyumbani!”
No comments:
Post a Comment