Tuesday 27 April 2010

UEFA CHAMPIONS LIGI: Bayern watinga Fainali!!!
Ndani ya Stade Gerland, Bayern Munich walitawala mechi ya marudiano na Wenyeji wao Lyon na kuwachakaza kwa bao 3-0 na hivyo kutinga Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI ambako watakutana na Mshindi kati ya Barcelona na Inter Milan.
Bayern, walioshinda mechi ya kwanza bao 1-0 huko Allianz Arena wiki iliyopita, walipata bao zote 3 kupitia Straika kutoka Croatia Ivica Olic.
Ushindi huu kwa namna nyingine ulichangiwa na kupewa Kadi Nyekundu kwa Nahodha wa Lyon Cris ambae alipata Kadi za Njano mbili ndani ya dakika moja na hivyo kutolewa.
Olic alipachika bao la kwanza dakika ya 26.
Lyon walipata pigo lao kubwa dakika ya 60 Cris alipotolewa nje na mechi kwao ikaharibika kwani wakati huo walikuwa wanahitaji bao 3 kusonga mbele.
Wakionyesha kutokuwa na pengo kwa kucheza bila ya Staa Franck Ribery, Olic aliongeza bao la pili dakika ya 67 na dakika ya 78 Olic alifunga bao la 3 kwa kichwa kufuatia krosi ya Fulbeki Philipp Lahm.
Mchecheto Liverpool v Chelsea Jumapili
-Gerrard aahidi ushindi!
-Rooney adai Liverpool haitaitupa mechi hiyo!
Mechi ya Ligi Kuu kati ya Liverpool na Chelsea itakayochezwa Jumapili hii huko Anfield ni mechi ambayo tayari imeshaanza kuzua mijadala toka kila kona.
Liverpool bado wana imani wa kuikwaa nafasi ya 4 na hivyo kucheza Ulaya Msimu ujao ingawa ukweli ni kuwa nafasi ya kuipata ni finyu kwa vile Tottenham na Man City, na hata Aston Villa, wanaiwania na wana nafasi kubwa kupita wao.
Lakini, ni ukweli pia, kimahesabu Liverpool wanaweza kuipata nafasi hiyo ya 4 ikiwa wataifunga Chelsea na pia kushinda mechi yao ya mwisho huku wakiombea matokeo mabovu kwa wengine wanaowania nafasi hiyo.
Endapo Liverpool atamsimamisha Chelsea kwa ama kumfunga au kutoka sare na Manchester United kushinda mechi yake na Sunderland ambayo pia inachezwa Jumapili, Man United atautwaa uongozi wa Ligi Kuu na akiifunga Stoke City katika mechi ya mwisho Mei 9 Uwanjani Old Trafford wao watauchukua Ubingwa kwa mara ya 4 mfululizo, hiyo ikiwa ni rekodi, na pia itakuwa ni mara ya 19 kuwa Bingwa na hivyo kuwapita Liverpool waliochukua mara 18.
Sasa swali ni, Liverpool, ambao ni Mahasimu wakubwa wa Man United, watakubali “kuisaidia” ichukue Ubingwa na kuweka rekodi hizo mbili?
Staa wa Man United, Wayne Rooney, ametamka: “Sidhani Liverpool watapoteza mechi hiyo kwa makusudi! Sihitaji kuongea na Gerrard ili kuhakikisha Liverpool wanashinda. Yeye ni Mchezaji wa Kulipwa na siku zote ni mshindani asiekubali kufungwa hata mechi ya kirafiki!”
Na kweli, Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, amesema wao wanataka kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao na akaongeza: “Tukishinda mechi zetu mbili na Timu zilizo juu yetu zikiteleza lolote linaweza kutokea. Lazima tuweke presha na ni lazima tushinde mechi zetu!”
Baada ya kutwangwa 7, Wachezaji watwangana!!!
Taarifa toka ndani ya Klabu ya Stoke City zimetoboa kuwa Wachezaji wao wawili walitwangana mara baada ya kutandikwa bao 7-0 na Chelsea huko Stamford Bridge siku ya Jumapili.
Wachezaji hao ni Abdoulaye Faye kutoka Senegal na Glenn Whelan anaetoka Ireland na bifu lao inasemekana lilianza kabla ya mchezo wakati Whelan alipomtaka Faye kutopasha moto kwenye Vyumba vya Kudalisha jezi huku amevaa makubadhi kwani hilo linaonyesha hana nidhamu.
Inasemekana bifu hilo liliendelea hadi wakati wa mapumziko na lilichochewa zaidi ilipotokea Faye kushindwa kuendelea na mechi na kubadilishwa dakika ya 9 tu ya mchezo na ndipo Whelan alipodai kushindwa kwa Faye kuendelea kucheza kumechangiwa na utovu wake wa nidhamu kuhusu maandalizi bora kwa mechi.
Faye akakasirishwa na kauli za Whelan na wakaanza kufarakana lakini Whelan akamwambia Faye waongee baada ya mechi.
Mechi ilipokwisha kwa Stoke kubondwa bao 7, Faye kweli akamfuata Whelan na maneno yao yakafuatiwa na konde la Faye lililotua usoni kwa Whelan na kusababisha Wachezaji kadhaa kuingilia kati na kuamua.
Kwa Stoke City hii ni skandali ya pili kuibuka toka Vyumba vyao vya Kubadilisha Jezi baada ya ile inayosemekana kutokea miezi minne iliyopita ambapo ilidaiwa Meneja Toni Pulis alimtwanga kichwa Straika wake James Beattie.

No comments:

Powered By Blogger