Tevez abatukiwa afunge domo au aondoke Man City
Roberto Mancini amemwambia Mchezaji wake Carlos Tevez aache kulalamika kuhusu mazoezi Klabuni Manchester City au atafute Klabu nyingine.
Meneja huyo wa Manchester City alichukizwa na kauli za Tevez aliedai kuwa mazoezi ya asubuhi na jioni yanawaumiza Wachezaji na pia alipohoji kufukuzwa kwa Meneja aliepita Mark Hughes katikati ya Msimu.
Wachunguzi wanahisi Tevez ametoa kauli hizo ili afanikishe mpango wake wa kuhamia Spain Ligi ikimalizika na huenda akafanikiwa aada ya Mancini kumtaka anyamaze au ahame.
Msimu mbovu kwa Liverpool lakini Rafa ajipa matumaini
Alipohojiwa kuhusu Msimu huu na nini hatma yake na Liverpool mara baada ya kufyekwa nje ya EUROPA LIGI na Atletico Madrid hapo juzi, Meneja Rafa Benitez alijibu: “Hatima yetu ni Jumapili kwenye mechi na Chelsea.”
Na alipoulizwa nini kitafuta baada ya hapo, Benitez alijibu Hull City akimaanisha mechi yao ya mwisho ya Ligi.
Wengi walitegemea mengi toka kwa Liverpool Msimu huu baada ya msimu uliopita kumaliza Timu ya pili nyuma ya Mabingwa Manchester United lakini mambo yakaenda shaghalabaghala baada ya kutupwa nje katika kila mashindano na sasa wamebakiwa na nafasi finyu sana ya kuweza kumaliza nafasi ya 4 na hivyo kucheza Ulaya Msimu ujao.
Juu ya yote, Benitez ambae anavumishwa yuko njiani kuhamia Juventus, amenena kwa matumaini: “Juu ya yote, Wachezaji wameonyesha kupigana siku zote, lazima tuwasifie kwa hilo. Lazima tujariu tena Msimu ujao kwani Msimu huu tulikuwa na matatizo mengi!”
AC Milan kuishabikia Inter Milan Fainali ya UEFA
Pengine Washabiki wa AC Milan wamestushwa sana na kauli ya Makamu wa Rais wao, Adriano Galliani, kuwa ataisapoti Inter Milan ambao ni Mahasimu wao wakubwa siku ya Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI watakapocheza na Bayern Munich hapo Mei 22 huko Santiago Bernabeau.
Lakini hilo si kwa sababu ni Mzalendo bali tu ni kwa sababu Italia ipo hatarini kunyang’anywa nafasi ya 4 ya kuingiza Timu 4 kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI ikiwa Bayern Munich watashinda Fainali hiyo na Ujerumani ndio watapewa nafasi nne za kuingiza Timu.
UEFA huipa Nchi pointi na hizo ndizo huamua Nchi inaingiza Timu ngapi kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI.
AC Milan bado wanahaha kuitafuta nafasi ya 3 au ya 4 ili wafuzu kuingia UEFA na wapo kwenye ushindani mkubwa toka kwa Sampdoria, Palermo, Juventus na Napoli.
Ubingwa huko Italia unagombewa na Inter Milan na AS Roma.
No comments:
Post a Comment