Saturday 1 May 2010

LIGI KUU waisafisha Fulham
Ligi Kuu imeamua Fulham haikuvunja kanuni zozote baada ya West Ham kuwasilisha malamiko yao kwao kwamba Fulham walichezesha Kikosi dhaifu walipocheza na Hull City mwezi Machi na kufungwa 2-0.
West Ham, ambao walikuwa wakiandamwa mno na balaa la kushuka Daraja, walilalamika baada ya Fulham kupumzisha Wachezaji wao wa kawaida watano katika mechi hiyo na Hull City labda kwa sababu mechi iliyokuwa inafuata kwao ni ile ya EUROPA LIGI.
Ushindi wa Hull City wakati huo uliwafanya wafungane pointi na West Ham na ndio maana West Ham wakakasirishwa na kitendo hicho.
Ligi Kuu imetoa tamko kwamba wamepitia malamiko ya West Ham na maelezo ya Fulham na wameridhika Fulham haikuvunja kanuni yeyote.
Tayari Timu mbili, Portsmouth na Burnley, zimeshaporomoka Daraja na Hull City ambao wako pointi 6 nyuma ya West Ham ndio wenye nafasi kubwa ya kuungana nao labda washinde mechi zao mbili zilizobaki na West Ham wafungwe mbili zao zilizobaki na tofauti ya magoli iliyopo kati yao ya goli 23 ifutwe katika matokeo ya mechi hizo mbili zilizobaki.
Neville aongeza mkataba
Nahodha wa Manchester United Gary Neville, miaka 35, amesaini nyongeza ya mwaka mmoja ya mkataba wake na Klabu yake utakaomweka Old Trafford hadi mwishoni mwa Msimu wa 2010/11.
Baada ya kukosa Miezi 18 alipoumia vibaya enka hapo Machi 2007, Neville amerudi tena dimbani na ameshacheza mechi 27 za Man United na kumfanya akaribie kuichezea mechi 600 Klabu hiyo tangu aanze kuichezea mwaka 1992.
Neville sasa ameungana na Wakongwe wengine Paul Scholes na Ryan Giggs waliopata nyongeza ya mkataba ya mwaka mmoja kila mmoja.
Msimu huu, Neville amekuwa akipokezana nafasi ya Fulbeki na Kinda toka Brazil Rafael, miaka 19.
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ametamka: “Anastahili. Gary amekuwa nje kwa miezi 18 lakini, kwa mtu wa zaidi ya miaka 30 baada ya kuumia vibaya, kurudi tena uwanjani na kucheza kwa kiwango cha juu ni kitu cha kushangaza na kinastahili pongezi!”
Nyongeza hii ya mkataba inamfanya Gary Neville awepo Man United kwa Msimu wa 19 tokea alipotokea Timu ya Vijana na kina David Beckham, Nicky Butt na Scholes.
Ferguson pia alitambulisha kuwa Neville, Giggs na Scholes kwa sasa wanasomea Ukocha na wameanza kupata Beji mbalimbali za hatua tofauti za masomo ya Ukocha na Klabu itauzingatia uzoefu na utumishi wao.
Ferguson alisema: “Huwezi ukapuuza mchango wa maisha yao katika Klabu hii. Uzoefu wao unaweza ukawa lulu kwa maendeleo ya Wachezaji Chipukizi.”

No comments:

Powered By Blogger