Friday 30 April 2010

Rooney aopoa Tuzo ya Pili!!
Wayne Rooney amefanikiwa kupata Tuzo nyingine siku chache baada ya kupewa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka na PFA, Chama cha Wachezaji Soka wa Kulipwa, na sasa ameikwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka toka kwa Waandishi Habari wa Soka na Tuzo hii inaheshimika sana.
Tuzo hii ya Waandishi hutolewa kwa Mchezaji kufuatia kura inayoendeshwa kati ya Waandishi wa Soka na Rooney alipata kura asilimia 81 na kuwabwaga Didier Drogba na Carlos Tevez.
Rooney, Straika wa Manchester United na tegemezi kubwa kwa matumaini ya England huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia, amefunga jumla ya magoli 34 Msimu huu.
Rooney, aliefurahishwa na Tuzo hii, amenena: “Nina furaha kubwa kushinda Tuzo kubwa yenye historia ndefu na asili ya muda mrefu ambayo Wachezaji bora wamewahi kuitwaa tangu mwaka 1948!"
Rooney atakabidhiwa Tuzo yake hapo Mei 13 kwenye chakula maalum cha usiku huko Lancaster London Hotel.
Rooney pia alitoa shukrani kwa Meneja wake, Sir Alex Ferguson na Wasaidizi wake, Wachezaji wenzake wa Man United, Familia na Marafiki zake kwa kumwezesha kupata Tuzo hiyo.
Wenger kusajili wawili au watatu wapya
Bosi wa Arsenal Arsene Wenger ametamka kuwa atasajili Wachezaji kadhaa kwa ajili ya Msimu ujao na inasemekana mara baada ya Msimu kwisha katikati ya Mei na kabla ya Fainali za Kombe la Dunia kuanza hapo Juni 11, Wenger atamtambulisha rasmi Straika kutoka Bordeaux Marouane Chamakh kama Mchezaji mpya wa Arsenal.
Arsenal inategemewa sana kununua Madifenda hasa kwa vile Madifenda wa sasa William Gallas, Sol Campbell na Mikael Silvestre wote mikataba yao inaisha mwezi Juni.
Wenger ametamka: “Nakiamini Kikosi cha sasa lakini ikiwa upo uwezekano wa kupata Wachezaji wawili mwisho watatu, tutanunua Wachezaji. Lakini yote inategemea nani ataondoka kwenye Kikosi cha sasa.”
Wenger aliongeza kwa kusema hakuna anaejua soko la Ulaya lilivyo kwa sasa hadi usajili wa kwanza utakapofanyika.
Vilevile, Wenger alisikitishwa na kauli zinazodaiwa kutoka kwa Mchezaji wake Andriy Arshavin aliekaririwa kusema anaihusudu Barcelona.
Arshavin, aliechukuliwa na Arsenal Januari 2009 kutoka Zenit St Petersburg ya Urusi, alikaririwa akisema kuichezea Barcelon, ambayo ndiyo iliitupa nje Arsenal toka kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu huu, kutakuwa ni kilele cha maisha yake kimpira.
Wenger alisema: “Nasikitika. Anaonyesha tabia tofauti wakati anataka kuboresha mkataba wake na sisi. Yeye ana furaha hapa hebu muulizeni kelele za nini?”
Listi ya Mameneja Tajiri
Gazeti kubwa Nchini Uingereza, Sunday Times, limechapisha Listi ya Wanamichezo Matajiri kwa Mwaka 2010 na katika Mameneja wa Soka, Meneja wa England, Fabio Capello, ndie ameibuka mwenye ‘vijisenti’ vingi kupita wengine.
Capello, miaka 63, anasadikiwa kuwa ndie Meneja wa England anaelipwa pesa nyingi kupita wengine kwenye historia ya Mameneja wa England na sasa anapata Pauni Milioni 6.5 kwa mwaka.
Hata hivyo, utajiri wa Capello umepatikana kabla ya kwenda England kwani alikuwa na vipindi vya mafanikio makubwa kwake huko Klabu za AC Milan, Roma, Juventus na Real Madrid ambako aliwahi kuwa Meneja.
Alieshika nafasi ya pili ni Nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane, ambae sasa ni Meneja wa Ipswich na utajiri wake unasemekana ni kuwa na kitita cha Pauni Milioni 30.
Bosi wa zamani wa Roy Keane, Sir Alex Ferguson wa Manchester United, ni wa tatu kwa kuwa na Pauni Milioni 24.
Katika Listi hiyo na kwenye 10 Bora wamesheheni Mameneja wenye asili ya Italia ambao ni Carlo Ancelotti wa Chesea na yuko nafasi ya 4 akiwa na Pauni Milioni 21, anafuata Meneja wa Republic of Ireland Giovanni Trapattoni mwenye Pauni Milioni18.
Roberto Mancini, Meneja wa Manchester City, yupo nafasi ya 8 akiwa na Paui Milioni 13 na Bosi wa West Ham Gianfranco Zola ni wa 10 na ana Pauni Milioni 10.

No comments:

Powered By Blogger