Dabi ya Midlands: Tuta la utata lawabeba Villa!!
Katika dabi ya Timu za eneo la Midlands huko England, Aston Villa leo wamefanikiwa kuwatungua jirani zao Birmingham kwa bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu kwa penalti yenye utata iliyotolewa na Refa Martin Atkinson huku kila mtu alimwona Beki Roger Johnson akiucheza mpira na sio Fowadi wa Villa Agbonlahor.
James Milner ndie aliefunga penalti hiyo katika dakika ya 83 na kuwafanya Villa wawe pointi 64 sawa na Timu ya 4 Tottenham ingawa Villa wamecheza mechi moja zaidi.
Birmingham ndio waliopata nafasi nyingi katika mechi hii na wangeweza kuibuka na ushindi kama si uhodari wa Kipa wa Villa Brad Friedel.
Torres : “Ligi Kuu ni hatari kwangu!”
Fernando Torres amedokeza kuwa afya yake iko mashakani kwa kuchezea Liverpool kwenye Ligi Kuu na ana wasiwasi wa kupata maumivi yatakayoathiri maisha yake ya baadae.
Torres amedokeza kuwa akiacha kucheza Liverpool ataondoka kabisa Uingereza hivyo kuondoa zile fikra kuwa huenda akachukuliwa na Manchester City ambao imedaiwa wametenga dau la Pauni Milioni 60 ili kumnasa Msimu utakapoisha.
Torres, ambae huu ni Msimu wake wa tatu tangu ahamie Liverpool kutoka Atletico Madrid, amesema Ligi Kuu ni ngumu na Wachezaji hutumia miguvu sana. Pia, amesema anashangazwa kuwaona Rooney, Lampard na Gerrard wakicheza miaka nenda rudi bila kuathirika.
Torres, ambae sasa anauguza goti, alisema: “Sijui ntakuwaje nikiendelea kucheza hapa kwa miaka mitano au sita ijayo! Nadhani itanisumbua baadaye nikistaafu kucheza kwa kuwa na maumivu!”
Wadau wanahisi matamshi ya Torres ni dalili yuko mbioni kuondoka.
Meneja wa Stoke adai Timu kubwa zinabebwa
Meneja wa Stoke City, Tony Pulis, amedai Timu kubwa zinapendelewa na kubebwa na Marefa.
Stoke leo wako Stamford Bridge kucheza na Chelsea kwenye mechi muhimu sana kwa Chelsea wanaotaka ushindi ili waing’oe Manchester United kileleni.
Pulis ametamka hayo akikumbushia mechi yao ya mwisho walipocheza na Chelsea kwenye Ligi Kuu mwezi Septemba na Chelsea walifunga bao mbili katika mbili za mwisho na kuibuka na ushindi.
Pulis alichukizwa na Refa wa mechi hiyo Mike Dean na akawapelekea FA mkanda wa DVD waone jinsi Refa huyo alivyochezesha mechi hiyo.
Stoke City wataumaliza Msimu wao huu kwa kucheza na Manchester United huko Old Trafford Mei 9.
Redknapp adai presha iko kwa Chelsea
Bosi wa Tottenham, Harry Redknapp, anaamini Chelsea ndio wenye mechi ngumu kuliko Manchester United katika vita kati yao ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu.
Man United wanaongoza Ligi kwa pointi mbili baada ya kuifunga Tottenham hapo jana lakini Chelsea wana mechi moja mkononi ambayo wanaicheza leo nyumbani kwao na Stoke City.
Lakini Redknapp amedai: “Naona Man United watapata pointi 6 katika mechi zao mbili za mwisho wakicheza na Sunderland na Stoke. Si rahisi kwa Chelsea kwani wanacheza na Stoke kisha Liverpool halafu Wigan!”
Redknapp amedai pia Stoke mara zote huwa wagumu kwa Chelsea na kukumbushia katika mechi mbili za mwisho ambazo Chelsea wamekuwa wakiifunga Stoke kwa mbinde dakika za majeruhi na kwa msaada wa utata wa Marefa.
No comments:
Post a Comment