Saturday 9 January 2010

Birmingham 1 Man U 1
Leo, Man U wameweza kulazimisha sare ya 1-1 ugenini kwa goli walilojifunga wenyewe Birmingham na hivyo kuikaribia Chelsea kileleni sasa wakiwa pointi moja tu nyuma yao ingawa wamecheza mechi moja zaidi.
Birmingham ndio walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 38 mfungaji akiwa Jerome.
Man U wakasawazisha dakika ya 64 baada ya Beki wa Birmingham Dann kujifunga mwenyewe.
Zikiwa zimesalia dakika 5 mpira kwisha Refa Clattenburg alimpa Kadi ya Njano ya pili Fletcher wa Man U na hivyo kumtoa nje kwa Kadi Nyekundu.
VIKOSI:
Birmingham: Hart, Carr, Roger Johnson, Dann, Ridgewell, Larsson, Ferguson, Bowyer, McFadden, Jerome, Benitez.
AKIBA: Maik Taylor, Martin Taylor, Phillips, Fahey, McSheffrey, Queudrue, Parnaby.
Man Utd: Kuszczak, Rafael Da Silva, Brown, J Evans, Evra, Valencia, Carrick, Scholes, Fletcher, Park, Rooney.
AKIBA: Amos, Neville, Owen, Anderson, Giggs, Fabio Da Silva, Diouf.
Arsenal yashindwa kuipiku Man U kuchukua nafasi ya pili!!
Wakiwa Uwanjani kwao Emirates huku barafu ikidondoka mfululizo, Arsenal ilibidi wajitutumue na kusawazisha mara mbili na kulazimisha sare ya 2-2 na Everton kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Katika mzunguko wa kwanza wa Ligi, Arsenal iliisulubu Everton 6-1 Uwanjani Goodison Park nyumbani kwa Everton.
Kwa sare hiyo, Arsenal wamebaki nafasi ya 3 wakiwa na pointi 42 kwa mechi 20, Man U wa pili wakiwa na pointi 43 kwa mechi 20 na Chelsea bado vinara wakiwa wamecheza mechi 20 na wana pointi 45.
Everton walitangulia kufunga dakika ya 12 kupitia Leon Osman na Denilson akaisawazishia Arsenal dakika ya 28 baada ya shuti lake kumbabatiza Osman na kumhadaa Kipa Howard.
Dakika ya 81 Steven Pienaar aliipa Everton bao la pili lakini Arsenal walisawazisha dakika za majeruhi, dakika ya 92, kwa shuti la Rosicky kumbabatiza Beki wa Everton Lucas Neill na kumhadaa Kipa Howard.
VIKOSI:
Arsenal: Almunia, Sagna, Gallas, Vermaelen, Traore, Denilson, Diaby, Ramsey, Nasri, Eduardo, Arshavin.
AKIBA: Fabianski, Rosicky, Vela, Silvestre, Merida, Eastmond, Emmanuel-Thomas.
Everton: Howard, Neville, Neill, Heitinga, Baines, Osman, Cahill, Fellaini, Pienaar, Donovan, Saha.
AKIBA: Nash, Bilyaletdinov, Vaughan, Coleman, Duffy, Baxter, Mustafi.
LIGI KUU England: Mechi 7 zaganda na barafu!!!
Mechi 7 kati ya 10 zilizokuwa zichezwe wikiendi hii, yaani Jumamosi na Jumapili, hazitachezwa kufuatia barafu na baridi kali iliyoikumba Uingereza na ni mechi 2 tu za leo, Arsenal v Everton na Birmigham v Manchester United, ndizo ambazo zimebaki kwenye Ratiba.
Mechi ya Jumatatu usiku kati ya Manchester City na Blackburn bado haijazungumziwa lolote.
Mechi ambazo hazitochezwa ni:
-Hull v Chelsea
-Burnley v Stoke
-Fulham v Portsmouth
-Sunderland v Bolton
-Wigan v Aston Villa
-West Ham v Wolves
-Liverpool v Tottenham
Tevez na McLeish ni Bora Desemba Ligi Kuu!!
Meneja wa Birmingham, Alex McLeish, na Mchezaji wa Manchester City, Carlos Tevez, ndio Washindi wa Tuzo ya Mdhamini wa Ligi Kuu Barclays kwa Mwezi Desemba ya Meneja Bora na Mchezaji Bora.
Washindi hao wawili ni mara yao ya kwanza kutwaa Tuzo hizo ambazo uamuzi wa kuzizawadia hutolewa na Jopo la Wadhamini hao Barclays ambalo huwa na wawakilishi kutoka Ligi Kuu, FA, Vyombo vya Habari na Mashabiki.
Alex McLeish ametunukiwa Tuzo hiyo, akiwa Meneja wa kwanza wa Birmingham kuipata, baada ya kuiongoza Timu yake kushinda mechi 4 na kutoka sare 2 kwa Mwezi Desemba kwenye Ligi na hivyo kuendeleza wimbi la kutofungwa kufikia mechi 11 mfululizo na kuifikia rekodi ambayo Klabu hiyo ilijiwekea miaka 100 iliyopita.
Nae Tevez ameikwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Desemba baada ya kufunga mabao 7 katika mechi 6 za Ligi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Tevez kupata Tuzo hii tangu aanze kucheza Ligi Kuu mwaka 2006 akiwa na West Ham.
KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA: Togo yajitoa!!!
Kufuatia kushambuliwa kwa risasi basi lao walilokuwa wakisafiri nalo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hadi Cabinda, Angola na kuuawa kwa Dereva wa basi hilo na kujeruhiwa kwa Wachezaji wao wawili pamoja na wengine kadhaa kwenye Kikosi chao, Togo imetangaza kujitoa kwenye Mashindano hayo.
Kuna taarifa zisizothibitishwa kuwa mbali ya Dereva wa basi hilo alietangazwa kufariki mara tu baada ya taarifa za shambulio hilo kuzagaa, pia watu wengine wawili ambao hawakutajwa nao wamefariki dunia.
Togo wamepangwa Kundi B pamoja na Ghana, Ivory Coast na Burkina Faso na mechi zao zimepangiwa Mjini Cabinda.
Mpaka sasa CAF imesema Mashindano hayo yataendelea huku ikiitaka Serikali ya Angola iongeze ulinzi.
Waasi wanaotaka uhuru wa Jimbo la Cabinda ambalo ni tajiri kwa mafuta wametangaza kuhusika na shambulio hilo.
RATIBA LIGI KUU England: [saa za bongo]
Jumamosi, 9 Januari 2010
Hull v Chelsea [IMEAHIRISHWA]
[saa 12 jioni]
Arsenal v Everton
Burnley v Stoke [IMEAHIRISHWA]
Fulham v Portsmouth [IMEAHIRISHWA]
Sunderland v Bolton [IMEAHIRISHWA]
Wigan vAston Villa [IMEAHIRISHWA]
[saa 2 na nusu usiku]
Birmingham v Man U
Jumapili, 10 Januari 2010
[saa 10 na nusu jioni]
West Ham v Wolves [IMEAHIRISHWA] 
Liverpool v Tottenham [IMAEHIRISHWA]
Jumatatu, 11 Januari 2010
[saa 5 usiku]
Man City v Blackburn
Adebayor asimulia shambulio!!
Nahodha wa Togo, Emmanuel Adebayor, amesema Timu yao Togo itakutana leo ili kuamua kama waendelee kubaki Angola au waondoke kufuatia kupigwa risasi jana kwa Basi lao lililowabeba wakati likitokea Jamhuri ya Congo na kuelekea Cabinda huko Angola kilipo kituo cha Togo kwenye Kundi B la Kombe la Mataifa ya Afrika ambalo wako pamoja na Ghana, Ivory Coast na Burkina Faso.
Katika shambulio hilo Dereva wa basi aliuawa na Wachezaji wawili wa Togo, Serge Akakpo na Kodjovi Obilale pamoja na watu kadhaa, walijeruhiwa kwa risasi.
Adebayor alisema walivuka mpaka wa Congo na Angola salama na kuona Askari wengi wamevalia kivita lakini hilo halikuwastua kwani walidhani ni kwa sababu ya ulinzi mkali kwa ajili ya Mashindano makubwa na wao wakaendelea na safari na walipofika kama kilomita 5 hivi toka mpakani risasi zikaanza kunguruma.
Adebayor akasikitika: “Kuna vitu tunasema na kuvirudia, Afrika lazima tubadilike ili tuheshimiwe lakini hili halitokei!!! Inasikitisha!!! Tuna nafasi ya Mashindano makubwa Duniani, Kombe la Dunia, na unaona kinachotokea? Ni aibu kubwa na si haki!!”
Adebayor akaongeza: “Lakini tunawashkuru askari Walinzi kwani bila wao tungekuwa maiti!! Zilikuwa dakika 30 za mauti!!”
Kufuatia tukio hilo, FIFA imetamka, kupitia Rais wao Sepp Blatter, kusikitishwa na kutoa rambirambi na pole kwa wote waliothirika na vilevile imeahidi kushirikiana na CAF kuchunguza tukio hilo.
CAF imetangaza Mashindano hayo yataendelea Angola kama yalivyopangwa.
Straika wa zamani arudi kama Meneja
Bolton Wanderers wamethibitisha Owen Coyle ambae ni Meneja wa Burnley ndie ameteuliwa kuwa Meneja wao mpya kuchuku nafasi ya Gary Megson aliefukuzwa hivi karibuni.
Oweni Coyle, Raia wa Scotland, amepewa Mkataba wa miaka miwili na nusu na Bolton, Timu ambayo aliwahi kuwa Mchezaji wake hapo zamani.
Uteuzi wa Coyle kuwa Meneja wa Bolton umefikiwa baada ya Klabu za Burnley na Bolton kufikia uamuzi kuhusu kuhama kwake.
Kimsimamo, Bolton wako nafasi ya 18 kwenye Ligi Kuu England na wamemudu kushinda mechi moja tu katika mechi zao 9 za mwisho kwenye Ligi hiyo.
KOMBE LA AFRIKA ANGOLA: Basi la Timu ya Togo lashambuliwa kwa risasi!
Waasi wa huko Jimbo la Cabinda Nchini Angola wamelishambulia kwa risasi basi lililobeba Wachezaji wa Timu ya Togo na kumuua Dereva wa basi hilo na kuwajeruhi Wachezaji wa Togo.
Washambuliaji hao walilipiga risasi basi hilo kwa kutumia bunduki aina ya “Mashine Gani” wakati likivuka mpaka kutoka Jamhuri ya Congo na kuingia Cabinda ambalo ni Jimbo la Angola lenye utajiri mkubwa wa mafuta.
Wachezaji wa Togo waliojeruhiwa ni Mlinzi Serge Akakpo, miaka 22, anaechezea Klabu ya Romania FC Vaslui na Kipa Kodjovi Obilale lakini hali zao zinasemekana sio mbaya.
Straika wa Manchester City Emmanuel Adebayor alikuwemo ndani ya basi hilo lakini alinusurika.
Togo wanategemewa kuanza kampeni yao Kombe la Afrika Jumatatu Januari 11 kwa kucheza na Ghana. Timu nyingine kwenye KUNDI lao B ni Ivory Coast na Burkina Faso.
Viongozi wa Angola wamesema mechi za Cabinda zitaendelea na walionyesha kushangazwa na hatua ya Togo kutumia usafiri wa ardhini badala ya kuruka na Ndege hadi Mji Mkuu Luanda halafu kuunganisha Ndege nyingine hadi Cabinda.
Waasi hao wa Cabinda, waliotangaza kusitisha vita mwaka 2006, wamedai ni wao waliofanya shambulio hilo na hatua yao ya kuanza mashambulizi jana imeishtua Angola.
Mechi za Hull v Chelsea na Liverpool v Tottenham nazo zaganda!!!!
Mechi ya Hull City v Chelsea ya Ligi Kuu iliyokuwa ichezwe leo Jumamosi Januari 9 imeahirishwa shauri ya hali ya hewa mbaya yenye baridi kali a kutanda kwa barafu na hivyo kuungana na mechi nyingine 3 za Ligi Kuu za leo zilizoahirishwa.
Mechi nyingine za leo ambazo hazitachezwa ni za Fulham v Portsmouth, Burnley v Stoke na Sunderland v Bolton.
Mechi ya Liverpool v Tottenham iliyokuwa ichezwe Jumapili tayari nayo imeahirishwa baada ya Liverpool kuviomba vyombo husika kuiahirisha mapema kutokana na kutokuwa na uhakika wa usalama wa Washabiki.
Giggs apewa “Uhuru wa Mji wa Salford”!!
Nyota wa Manchester United Ryan Giggs ametunukiwa Tuzo ya ‘Uhuru wa Mji wa Salford’ hapo juzi.
Mji wa Salford ndiko makazi ya Giggs.
Giggs, miaka 33, sasa anajumuika na watu maarufu kina Nelson Mandela na wengineo, waliowahi kupewa Tuzo hiyo.
Ingawa Giggs alizaliwa Cardiff lakini tangu utoto wake amekuwa akiishi Salford na kujiunga na Manchester United wakati bado akiwa shule.
Aliempendekeza Giggs kupewa Tuzo hiyo ni Diwani John Warmisham ambae amesema ni ‘furaha na sifa kubwa’ kumpendekeza Giggs kwa sababu Giggs si Mcheza Mpira tu bali ni mtu wa kuigwa na ni Balozi mzuri wa Salford.
Warmisham amesema: “Yeye ni Balozi wa Unicef na siku zote anaisaidia Salford!”
Siku hizi ukipewa ‘Uhuru wa Mji” unapata Shahada na utambuzi tu lakini enzi za kale ulimaanisha wewe ni Mtu Huru na si Mtumwa wa Mtajiri hivyo uko huru kufanya kazi na kupata pesa na pia kumiliki ardhi.

Friday 8 January 2010

Baadhi ya mechi za Ligi Kuu zaahirishwa!!
• Wenger ataka mechi zote zisichezwe!!!
Hali ya hewa ya baridi kali na barafu mtindo mmoja zimesababisha mechi kadhaa za Ligi Kuu England za hapo kesho ziahirishwe hasa kwa sababu ya usalama wa Washabiki ikizingatiwa barabara kuwa za hatari kwa ajili ya barafu.
Mpaka saa Mechi ambazo hazitachezwa kesho ni:
-Fulham v Portsmouth
-Burnley v Stoke
-Sunderland v Bolton
Mechi kati ya Liverpool v Tottenham ipo kwenye hatihati kubwa hasa baada ya Liverpool kuitaka Ligi Kuu kuiahirisha kutokana na hali ya hewa.
Wakati huo huo, Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ameitaka LigI kuu kuahirisha mechi zote za Ligi Kuu za wikiendi hii ili kuwe na usawa kwa Timu zote na amedai kuwa ikiwa baadhi tu ya mechi hazitachezwa baadhi ya Timu zitanufaika kwa mechi hizo kuchezwa baadae kwa vile watakuwa washajijua wako nafasi gani katika msimamo wa Ligi.
Pichani juu ni mitutu ya Arsenal nje ya Uwanja wa Emirates ilivyoganda barafu.
Viera ni rasmi Man City
Manchester City wamekamilisha usajili wa mkopo wa Patrick Viera kutoka Inter Milan na atakuwa hapo awali kwa miezi 6 na kuna kipengele cha kuongezewa miezi 12 mingine hapo baadae.
Viera, miaka 33, ni Mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Meneja mpya wa Man City Roberto Mancini na wawili hao wanajumuika tena baada ya kuwa pamoja Inter Milan ambako walitwaa Ubingwa wa Italia wa Serie a mwaka 2007 na 2008.
Viera amekuwa akitaka kuihama Inter Milan ambako hakuwa akipata namba ili afanikishe kuchukuliwa Timu ya Taifa ya Ufaransa kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwezi Juni.
Viera ameshachezea Ligi Kuu England alipokuwa Nahodha wa Arsenal na kuihama mwaka 2005 kwenda Juventus alikokaa msimu mmoja tu na kisha kuhamia Inter milan
Gary Neville hastaafu!!
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amepuuza taarifa za Magazeti kuwa Nahodha wake Gary Neville atastaafu soka Msimu huu ukimalizika.
Taarifa hizo zimezagaa hasa baada ya Maveterani wenzake Ryan Giggs na Paul Scholes kuongezewa Mikataba na yeye Neville kutopewa kitu.
Neville, miaka 35, amekuwa akiandamwa na kuumia mara kwa mara katika Misimu ya hivi karibuni lakini Ferguson amesisitiza: “Hamna kilichoamuliwa kuhusu Neville. Kwa nini tuamue hatma yake ya baadae wakati hatuhitajiki kufanya hivyo? Hufanyi maamuzi katikati ya Msimu! Huo ni upuuzi mkubwa!!!”
Dossena wa Liverpool ahamia Napoli
Mlinzi wa Liverpool Andrea Dossena, miaka 28, amehamia Klabu ya Italia ya Serie A Napoli kwa Mkataba wa Miaka minne.
Dossena alijunga na Liverpool mwaka 2008 kutoka Udinese ya Italia kwa Pauni Milioni 7 lakini ameichezea Liverpool mechi 30 tu na kufunga bao 2.
Liverpool pia wapo katika hatua za mwisho za mauzo ya Straika Andriy Voronin ambae atajiunga na Dynamo Moscow kwa Pauni Milioni 2.
Voronin alijiunga na Liverpool mwaka 2007 kutoka Bayer Leverkusen lakini Msimu uliokwisha alikuwa akicheza huko Ujerumani kwa mkopo kwenye Timu ya Hertha Berlin.
Barafu yagandisha Mechi Uingereza!!!!
Barafu na baridi kali iliyoshuka hadi viwango chini ya sifuri imesababisha mechi nyingi za Soka na mashindano ya Michezo ya aina mbalimbali Nchini Uingereza kuahirishwa ama kwa vile Viwanja vimeganda barafu au kwa usalama wa Raia kufuatia barabara kufungwa, usafiri kusimamishwa na njia za watu wa miguu kutopitika.
Hadi sasa hakuna mechi za Ligi Kuu England za wikiendi hii zilizotangazwa kuahirishwa lakini mechi kadhaa za Ligi chini ya Ligi Kuu, yaani Daraja liitwalo Championship, zimeahirishwa.
Pia baadhi ya mechi za Madaraja chini ya Championship, yaani Ligi 1 na Ligi 2, zimeahirishwa.
Mechi zilizoahirishwa:
Jumamosi:
Championship: Sheffield Wednesday v Peterborough, Preston v Doncaster, Reading v Newcastle, Watford v Sheff Utd
Tembo wawaua Amavubi
Timu ya Taifa ya Ivory Coast iliyopo maandalizini Bongo kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika yanayoanza Jumapili huko Angola jana waliifunga Rwanda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Mabao yote ya Tembo yalifungwa dakika 4 za mwisho za mchezo la kwanza likipachikwa na Bamba Souleymane dakika ya 86 kufuatia kona ya Emmanuel Eboue na la pili na Angoua Brou katika dakika za majeruhi.
Katika mechi hiyo Didier Drogba alikosa mabao mengi.
Juzi Tembo waliifunga Bongo 1-0 kwa bao la Drogba.
Ivory Coast wataanza kampeni yao huko Angola kwa kucheza na Burkina Faso Jumatatu.
Hatimaye Wachezaji Pompey wapata Mishahara!!
Baada ya kuchelewa wiki kulipwa Mishahara yao ya Desemba, hii ikiwa ni mara ya 3 kwao kucheleweshewa Mishahara, hatimaye jana Portsmouth iliwalipa Wachezaji wake.
Portsmouth, Timu ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ipo kwenye balaa kubwa la matatizo ya kifedha na inakabiliwa na kesi ya kutaka kufilisiwa na Mamlaka ya Kodi ya Mapato kwa kushindwa kulipa kodi.
Vilevile, imefungiwa kutonunua Wachezaji kwa kushindwa kulipa madeni ya ununuzi wa Wachezaji toka Klabu nyingine.

Thursday 7 January 2010

Straika toka Senegal amkuna Fergie, apewa Jezi ya Tevez!!

Mame Biram Diouf huenda akapata namba muda si mrefu Klabuni Manchester United baada ya Bosi Sir Alex Ferguson kuthibitisha Mshambuliaji huyo Raia wa Senegal anafanya vizuri sana mazoezini.
Diouf, miaka 22, ameshapata kibali cha kazi na tayari Manchester United imeshamkabidhi Jezi Namba 23 iliyokuwa ikivaliwa na Carlos Tevez.
Diouf amesainiwa na Man U kutoka Klabu ya Norway Molde FK Julai 2009 lakini akabakishwa huko huko kwa mkopo kwa vile kulikuwa na utata kuhusu kibali chake cha kazi England.
Ferguson amesema: “Amemudu mazoezi yetu vizuri sana na ametufurahisha! Ni mwepesi, hodari kwa mipira ya juu na mpiga vigongo kweli! Kwa ujumla, ni Senta Fowadi mzuri na atacheza Msimu huu!”
Straika alieiua Man U ataka kuhama Leeds
Mshambuliaji wa Leeds Jermaine Beckford aliefunga bao moja na la ushindi lililoitupa Manchester United nje ya FA Cup ameiandikia klabu yake ili kuonyesha dhamira yake ya kutaka kuhama huku Klabu kedekede zikimkodolea macho kwa umaarufu alioupata baada ya kuiua Man U.
Beckford Msimu huu ameifungia Leeds mabao 16 katika mechi 21 alizoanza na mwanzoni mwa Msimu aligoma kusaini Mkataba mpya na Leeds.
Kwa vile Mkataba wa Beckford unaisha Mwezi Juni Leeds inabidi wamuuze sasa ili wapate pesa na wakishindwa kufanya hivyo Mwezi Juni ataondoka bure bila Leeds kulipwa chochote.
Inasemekana Newcastle imeshatoa ofa ya Pauni Milioni 1 na nusu kumnunua.
Klabu yenye madeni Pompey italazimika kuuza Wachezaji
Mkurugenzi Mtendaji wa Portsmouth Peter Storrie amesema watalazimika kuwauza baadhi ya Wachezaji wao muhimu ili kuinusuru Klabu hiyo kutangazwa mufilisi.
Habari hizi za kuuzwa Wachezaji zimekuja huku Klabu ikishindwa kulipa Mishahara ya Wachezaji ya Mwezi Desemba ingawa Mkuu huyo ameahidi leo Mishahara italipwa.
Hii ni mara ya tatu kwa Mishahara kucheleweshwa.
Neville: “Tunamtegemea Rooney!”
Nahodha wa Manchester United Garry Neville amekiri Timu yao inamtegemea sana Wayne Rooney katika ufungaji na kuleta ushindi hasa baada ya kuondoka Cristiano Ronaldo.
Rooney Msimu huu amefunga mabao 15 katika mechi 23 alizoanza.
Neville amesema: “Tunamtegemea Rooney. Wayne anatuletea ushindi. Ni Mfungaji Bora Ligi Kuu! Ni mpiganaji na anajituma sana kwenye mechi!”
Man U wako nafasi ya pili kwenye Ligi wakiwa pointi 2 nyuma ya vinara Chelsea na bado wamo kwenye vinyang’anyiro vya Makombe ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Carling lakini wamebwagwa nje ya Kombe la FA.
Neville ameongeza: “Msimu huu Ligi imekuwa ya ajabu! Vigogo wote wamepoteza pointi nyingi! Nadhani ikifika Machi ndio itajionyesha nani ni mgombea Ubingwa wa kweli! Inashangaza tumepoteza mechi 5 lakini tupo pointi 2 tu nyuma ya anaeongoza!”
RATIBA LIGI KUU England WIKIENDI HII:
[saa za bongo]
Jumamosi, 9 Januari 2010
[saa 9 dak 45 mchana]
Hull v Chelsea
[saa 12 jioni]
Arsenal v Everton
Birmingham v Man U
Burnley v Stoke
Fulham v Portsmouth
Sunderland v Bolton
Wigan vAston Villa
[saa 2 na nusu usiku]
Birmingham v Man U
Jumapili, 10 Januari 2010
[saa 10 na nusu jioni]
West Ham v Wolves
[saa 1 usiku]
Liverpool v Tottenham
Jumatatu, 11 Januari 2010
[saa 5 usiku]
Man City v Blackburn
Beckham aanza AC Milan kwa ushindi!!!
Hapo jana, David Beckham alianza kuchezea AC Milan kwa mkopo kwa ushindi wa 5-2 dhidi ya Genoa Uwanjani San Siro kwenye mechi ya Ligi Serie A.
Huku Kocha wa England Fabio Capello akiwa miongoni mwa Watazamaji, Beckham alicheza vizuri sana huku akishangiliwa na Washabiki na pengine kumfanya Capello aikubali kauli yake kuwa Beckham alie fiti lazima atakuwa na namba Kikosi cha England kitakachotua Afrika Kusini mwezi Juni kwa Fainali za Kombe la Dunia.
Hata Kocha wa AC Milan, Leonardo, alimsifia: “Ni Mchezaji anaeweza kucheza kokote! Ana kipaji na akili kubwa ya kimbinu mpirani!”
Katika mechi hiyo Ronaldinho alikosa kufunga penalti na Genoa wakapata bao la utangulizi lakini AC Milan wakasawazisha na kuwa mbele 2-1 hadi mapumziko.
Inter Milan ndio vinara wa Ligi Serie A na wako mbele ya AC Milan kwa pointi 8 lakini AC Milan wana mechi moja mkononi.
Inter Milan pia walishinda mechi yao ya Ligi jana walipoifunga Chievo 1-0 kwa goli la Mario Balotelli lakini katika mechi hiyo walipata pigo kubwa baada ya Defenda wao toka Romania Cristian Chivu kuvunjika fuvu kichwani baada ya kugongana vichwa na kulazimika kufanyiwa operesheni ya dharura kichwani.
Madaktari wamesema opersheni hiyo ilienda salama na wana matumaini makubwa Chivu atapona na kuwa salama.

Wednesday 6 January 2010

Barafu balaaa!!!! Arsenal v Bolton imegandishwa!!!
Mechi ya Ligi Kuu iliyokuwa ichezwe leo usiku Uwanja wa Emirates kati ya Arsenal na Bolton imeahirishwa kwa sababu ya baridi na barafu zilizotanda na kuzidi kuanguka Jijini London.
Ingawa Uwanja wa Emirates unachezeka lakini kwa sababu za kiusalama hasa barabara kuwa na barafu nyingi hivyo kuhatarisha usafiri wa Washabiki Mamlaka za Usalama wa Raia zimeshauri mechi hiyo isichezwe leo.
Mechi hiyo sasa itapangiwa tarehe ya baadae.
Pompey Mishahara ni fumbo!!!
Desemba ni mara ya tatu kwa Wachezaji wa Portsmouth kukosa Mishahara na waliahidiwa kulipwa leo lakini hata hii leo imeshindikana na Wawakilishi wa Mmiliki wa Klabu hiyo, Ali al-Faraj, wamekuwa wakihaha kutafuta mkopo wa muda mfupi wa Pauni Milioni 3 ili wawalipe Wachezaji wao.
Klabu hiyo ipo kwenye mashaka makubwa huku ikikabiliwa na kesi Mahakama Kuu baada ya Mamlaka ya Kodi ya Mapato kuwashitaki kwa kutokulipa kodi ya Pauni Milioni 3 na imetaka Klabu hiyo ifilisiwe.
Kesi hiyo itaanza kusikilizwa mwezi ujao.
Nao Ligi Kuu wanashikilia mgao wa Pauni Milioni 7 na nusu zikiwa ni sehemu ya fungu la malipo kwa Portsmouth kutoka kwa Vituo vya TV vinavyorusha matangazo ya moja kwa moja ya mechi za Ligi ili kulipa deni la Klabu hiyo kwa Klabu nyingine baada ya kushindwa kuzilipa ada za uhamisho za Wachezaji waliowanunua.
Kushindwa huko kulipa madeni hayo ya uhamisho pia kumeifanya Ligi Kuu kuifungia Portsmouth kutokununua Wachezaji.
Inakisiwa Portsmouth inadaiwa jumla ya Pauni Milioni 60 na inasemekana kama Ali al-Faraj asingetoa Pauni Milioni 20 katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, Klabu hiyo ingekuwa mufilisi.
Wakati huo huo, Ligi Kuu imewaambia Portsmouth kuwa hawawezi kuongeza mkataba wa mkopo wa Mchezaji Jamie O’Hara waliemkopa kutoka Tottenham mpaka wafunguliwe kifungo cha kutokusajili Mchezaji.
Mkataba wa O’Hara unakwisha Januari 15 na Klabu yake Tottenham ilikuwa tayari imekubali kuongeza mkataba wa mkopo wa O’Hara hapo Portsmouth.
Liverpool ina Pauni Milioni 1.5 tu kununua Wachezaji hii Januari!!!!
Uongozi wa Liverpool umemzuia Meneja wao Rafa Benitez kutonunua Mchezaji yeyote kwenye dirisha hili la uhamisho la Januari mbali ya Kiungo wa Argentina Maxi Rodriguez kutoka Atletico Madrid atakaegharimu Pauni Milioni 1.5 tu kwa vile mkataba wake utakuwa wa Miezi 18 tu.
Ingawa Liverpool inategemewa kuvuna zaidi ya Pauni Milioni 16 Januari hii kutokana na kuuzwa kwa Wachezaji Andriy Voronin kwa Dynamo Moscow, Andrea Dossena kwa Napoli na Philipp Degen anaetegemewa kwenda Klabu za Bundesliga huko Ujerumani, Liverpool inataka pesa hizo ziwekwe hadi Msimu ukiisha na ndipo watafutwe Wachezaji kwani wanadhani Januari Wachezaji huuzwa bei mbaya.
Wakati huo huo, Liverpool imegoma kumuuza Winga Ryan Babel kwa Birmingham waliotoa ofa ya Pauni Milioni 8.
Babel mwenyewe amekuwa akitaka kuhama ili aende Klabu nyingine ambako atapata namba ya kudumu ili ajiongezee matumaini ya kuitwa kwenye Kikosi cha Holland kitakachokwenda Afrika Kusini mwezi Juni kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
LIGI KUU England: Leo ni Arsenal v Bolton
Leo usiku saa 4 dakika 45 saa za bongo, Arsenal watajimwaga Uwanjani kwao Emirates kucheza na Bolton katika mechi yao ya kiporo na ushindi kwao utawafanya wawakaribie mno vinara wa Ligi Kuu Chelsea na pia kuwapita Manchester United wanaoshika nafasi ya pili.
Chelsea wanaongoza Ligi wakiwa na pointi 45 kwa mechi 20, Man U pointi 43 mechi 20 na Arsenal pointi 41 mechi 19.
Bolton wanasuasua kwenye Ligi Kuu wakiwa nafasi ya 18 kwenye Ligi ikiwa ni wa tatu toka mwisho na wiki iliyopita walimtimua Meneja wao Gary Megson.
Mpaka sasa mechi ya leo iko kwenye hatihati kama itachezwa kufuatia hali mbaya ya hewa iliyoambatana na baridi kali na kuanguka kwa barafu hali ambayo imeikumba Uingereza.
Ingawa Kiwanja cha Emirates kinachezeka kwa vile chini ya nyasi ardhini kuna vipasha moto [under-soil heaters] vinavyozuia barafu kuganda Mamlaka za Usalama huenda zikaamua mechi kuahirishwa kwa sababu ya usalama wa Mashabiki kwa vile barabara na njia zimefunikwa na barafu.
Hali hiyo na sababu hiyo hiyo ilifanya mechi za jana na leo za Nusu Fainali za Carling Cup ziahirishwe.
Endapo mechi itachezwa kama ilivyopangwa, Arsenal wanategemewa kumkosa Nahodha wao Cesc Fabregas ambae bado ana maumivu ya musuli lakini huenda wakamchezesha Denilson ambae amepona maumivu ya mgongo.
VIKOSI VINATEGEMEWA KUWA:
ARSENAL: Almunia, Sagna, Vermaelen, Gallas, Traore, Nasri, Denilson, Ramsey, Diaby, Rosicky, Arshavin.
BOLTON: Laaskelainen, Steinsson, Cahill, Knight, Robinson, Taylor, Muamba, Cohen, Lee, Davies, Klasnic.
Mwana wa Ferguson kuwa Bosi Preston

Darren Ferguson, miaka 37, ambae ni mtoto wa Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, yuko njiani kutangazwa kuwa Meneja mpya wa Preston North End Timu inayocheza Daraja chini tu ya Ligi Kuu liitwalo Championship.
Ferguson alikuwa Meneja wa Klabu nyingine ya Championship iitwayo Peterborough lakini alijiengua mwenyewe Mwezi Novemba mwaka jana na sasa atachukua nafasi ya Alan Irvine ambae ameondolewa na Preston.
LIGI KUU England: Stoke 3 Fulham 2
Katika mechi pekee ya Ligi Kuu iliyochezwa jana usiku huku ikitaliwa na barafu, Stoke City iliibwaga Fulham kwa mabao 3-2 na kutinga nafasi ya 10 ikiwa sasa imecheza mechi 20 na ina pointi 24.
Fulham wako nafasi ya 9 na wamecheza mechi 20 na wana pointi 27.
Mabao yote ys Stoke yalifungwa Kipindi cha Kwanza na Tuncay Sanli, dakika ya 12, Abdoulaye Faye dakika ya 34 na Mamady Sidibe dakika ya 37.
Fulham walicharuka Kipindi cha Pili na kupata bao zao mbili kupitia Damien Duff dakika ya 61 na Clint Dempsey dakika ya 85.
Mancini amtaka Viera
Roberto Mancini anataka ajumuike tena na Patrick Viera na yumo mbioni kumleta Mchezaji huyo Manchester City kutokea Inter Milan ambako kwa sasa hana namba.
Viera, miaka 33, alicheza England akiwa na Arsenal ambako alikuwa Nahodha na kuondoka kuhamia Juventus mwaka 2005 na huko alicheza Msimu mmoja tu na kuhamia Inter Milan wakati huo ikiwa chini ya Roberto Mancini na waliweza kutwaa Ubingwa wa Serie A mwaka 2007 na 2008.
Viera ameichezea Arsenal mechi 400 na kushinda Ligi Kuu mara 3 na Vikombe vya FA mara 4.

Tuesday 5 January 2010

CARLING CUP: NUSU FAINALI ZOTE MBILI ZAGANDA BARAFU!!
Mechi za kwanza za Nusu Fainali za Kombe la Carling zilizokuwa zichezwe leo kati ya Blackburn na Aston Villa na nyingine kesho kati ya Manchester City na Manchester United zimeahirishwa kutokana na hali ya hewa mbaya kufuatia baridi kali na barafu.
Ingawa Viwanja vya Ewood Park, Kiwanja cha Blackburn, na City of Manchester cha Man City vinaweza kuchezeka lakini Viongozi wa Maeneo hayo wameamua ni hatari kwa Watazamaji kusafiri na kwenda kushuhudia mechi hizo hasa baada ya raia wote kutangaziwa kupunguza safari zisizokuwa za lazima kutokana na kutanda kwa barafu.
Huko Manchester, Kiwanja cha Ndege kilifungwa leo kutokana na barafu kufunika sehemu zote za kuruka na kutua ndege.
Mpaka sasa mechi kati ya Blackburn v Aston Villa haijapangwa lini itachezwa lakini mechi kati ya Manchester City na Manchester United itachezwa Januari 19 Uwanjani City of Manchester na marudio ni Old Trafford Januari 27.
Boateng si ruksa kuhamia Blackburn!!!
Ligi Kuu England imethibitisha kuwa Mchezaji wa Portsmouth Kevin-Prince Boateng haruhusiwi kuchezea Klabu nyingine yeyote Msimu huu kwa mujibu wa Sheria za FIFA kwa sababu tayari ameshachezea Klabu mbili kwa msimu mmoja na haruhusiwi kujiunga Timu ya tatu Msimu huohuo mmoja.
Boateng, ambae ashaichezea Timu ya Taifa ya Ujerumani ya Vijana Chini ya Miaka 21 lakini asili yake ni Ghana, msimu huu ameshazichezea Tottenham na Portsmouth.
Boateng amekuwa akihusishwa na kuhamia Blackburn.
Malipo ya TV kulipia deni la Pompey
Uongozi wa Ligi Kuu England umeamua kuwa malipo yote toka Makampuni ya TV yatakayolipwa mwezi huu Januari ambayo ni mgao wa Klabu ya Portsmouth yaende katika kulipia madeni ya Klabu hiyo kwa Klabu nyingine zinazoidai pesa za uhamisho za Wachezaji wao kwa Klabu hiyo.
Mgao huo unaosadikiwa kuwa ni Pauni Milioni 7 utagawanywa kwa Chelsea, Tottenham na Watford ambazo ni miongoni mwa Klabu inazozidia Portsmouth na uamuzi huo wa Uongozi wa Ligi Kuu umechukuliwa kulingana na Sheria za Ligi Kuu.
Portsmouth wapo kwenye matatizo makubwa ya kifedha na hata Mamlaka ya Kodi ya Mapato imetaka Klabu hiyo ifilisiwe kwa sababu ya kutokulipa deni la Kodi la Pauni Milioni 60.
Vilevile, Pompey mpaka sasa haijawalipa Wachezaji wake Mishahara ya mwezi Desemba na hii ikiwa ni mara ya 3 kwa Mishahara kucheleweshwa.
Kwa sasa Pomey imefungiwa na Ligi Kuu kutosajili Mchezaji yeyote hadi watakapolipa madeni yao ya uhamisho wa Wachezaji.
Kifungo hicho huenda kikaathiri kuwepo kwa Mchezaji wa Tottenham, Jamie O’Hara ambae yuko Portsmouth kwa mkopo wa miezi 6 na mkataba wake utaisha hivi karibuni lakini mpaka sasa Ligi Kuu hawajabariki kuongezwa kwake.
Rosicky asaini Mkataba mpya Arsenal
Kiungo kutoka Czech Republic Tomas Rosicky, miaka 29, amesaini Mkataba mpya na Arsenal.
Rosicky alijiunga na Arsenal Mei 2006 akitokea Borussia Dortmund na ameshaichezea Arsenal mechi 76 na kufunga goli 14 lakini Msimu uliokwisha hakucheza baada ya kuwa nje ya uwanja kwa miezi 18 alipoumia misuli na goti.
Rosicky ni Mchezaji wa 15 wa Arsenal kusaini Mikataba mipya tangu Mei 2009 wengineo wakiwa ni pamoja na Abou Diaby, Robin van Persie, Theo Walcott na Eduardo.
Drogba aiua Bongo: Taifa Stars 0 Tembo 1!!
Jana kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam mbele ya maelfu ya Wabongo wakiongozwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Ivory Coast iliifunga Tanzania bao 1-0 kwa bao lililofungwa na Didier Drogba kwa kichwa baada ya krosi ya Emmanuel Eboue dakika ya 37 ya mchezo.
Ingawa Taifa Stars walifungwa lakini waliweza kumudu kucheza soka la heshima na kuwafanya Tembo hao watumie misuli zaidi ili kuimudu Bongo iliyokuwa ikicheza kitimu na kiakili zaidi.
Ivory Coast wako Dar kwa maandalizi na mazoezi ya kwenda Angola kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazoanza Nchini humo Januari 10.
Kwenye michuano hiyo, Ivory Coast wamepangwa Kundi B pamoja na Ghana, Burkina Faso na Togo.
Ivory Coast wataanza kucheza mechi yao ya kwanza kwenye Kombe hilo Januari 11 kwa kuvaana na Burkina Faso.

Monday 4 January 2010

Meneja wa Burnley azungumza na Bolton ili achukue ofisi!!
Burnley imethibitisha kuwa Meneja wao Owen Coyle yuko kwenye mazungumzo na Bolton Wanderers ili achukue nafasi ya Umeneja iliyo wazi huko baada ya kufukuzwa kazi Garry Megson wiki iliyokwisha.
Coyle, miaka 43, ni Raia wa Scotland aliewahi kuichezea Bolton kati ya 1993 na 1995.
Endapo Coyle atakubaliana na Bolton kuhusu ajira hiyo basi Bolton itabidi wailipe Burnley Pauni Milioni 3 ili wamruhusu ahamie Bolton kwa vile mkataba wake una kipengele cha aina hiyo.
Taarifa zaidi za mazungumzo hayo zitatolewa baadae.
MECHI ZA WIKI HII England:
Jumanne, 5 Januari 2010
KOMBE LA CARLING, NUSU FAINALI
Blackburn v Aston Villa [Marudio Januari 20]
LIGI KUU England
Stoke v Fulham
Jumatano, 6 Januari 2010
KOMBE LA CARLING, NUSU FAINALI
Man City v Man U [Marudio Januari 19]
LIGI KUU England
Arsenal v Bolton
Jumamosi, 9 Januari 2010
LIGI KUU England
Arsenal v Everton
Birmingham v Man U
Burnley v Stoke
Fulham v Portsmouth
Hull v Chelsea
Sunderland v Bolton
Wigan vAston Villa
Jumapili, 10 Januari 2010
LIGI KUU England
Liverpool v Tottenham
West Ham v Wolves
Jumatatu, 11 Januari 2010
LIGI KUU England
Man City v Blackburn
KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA: Kunguruma Angola kuanzia Jumapili ijayo!!
Huko Nchini Angola, Nchi 16 za Afrika, wakiwemo Wenyeji Angola na Mabingwa Watetezi Egypt, wataanza kumenyana kuanzia Jumapili ijayo Januari 10 ili kumpata Bingwa wa Afrika.
Nchi hizo 16 zimegawanywa Makundi Manne na zitacheza kwa mtindo wa ligi na Timu mbili za juu toka kila Kundi zitasonga mbele kuingia Robo Fainali.
Mashindano ya kugombea Kombe la Mataifa ya Afrika yalianza rasmi mwaka 1957 na kuchezwa huko Sudan na kushirikisha Nchi 4, Egypt, Sudan, Ethiopia na Afrika Kusini.
Lakini Afrika Kusini wakatolewa hata kabla ya kushirika kwa sababu ya siasa yake ya ubaguzi wa rangi.
Egypt walinyakua Kombe hilo la kwanza walipoifunga Sudan mabao 4-0.
Kuanzia mwaka 1968 Kombe hili limekuwa likishindaniwa kila baada ya miaka miwili.
Katika historia ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Egypt ndio wanaongoza kwa kulitwaa mara nyingi na wamelichukua mara 6.
Ghana na Cameroun wamelitwaa mara 4 kila mmoja.
Congo DR na Nigeria mara 2 kila mmoja.
Nchi zilizolichukua mara moja kila mmoja ni Algeria, Congo, Ivory Coast, Ethiopia, Morocco, Afrika Kusini, Sudan na Tunisia.
RATIBA: KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA ANGOLA 2010
Januari 10:
[KUNDI A]
Angola v Mali
Januari 11:
[KUNDI A]
Malawi v Algeria
[KUNDI B]
Ivory Coast v Burkina Faso
Ghana v Togo
Januari 12:
[KUNDI C]
Egypt v Nigeria
Mozambique v Benini [
Januari 13:
[KUNDI D]
Cameroun v Gabon
Zambia v Tunisia
Januari 14:
[KUNDI A]
Mali v Algeria
Angola v Malawi
Januari 15:
[KUNDI B]
Burkina Faso v Togo
Ivory Coast v Ghana
Januari 16:
[KUNDI C]
Nigeria v Benin
Egypt v Mozambique
Januari 17:
[KUNDI D]
Gabon v Tunisia
Cameroun v Zambia
Januari 18:
[KUNDI A]
Angola v Algeria
Mali v Malawi
Januari 19:
[KUNDI B]
Burkina Faso v Ghana
Ivory Coast v Togo
Januari 20:
[KUNDI C]
Egypt v Benin
Nigeria v Mozambique
Januari 21:
[KUNDI D]
Gabon v Zambia
Cameroun v Tunisia
ROBO FAINALI
Januari 24:
1A v 2B
1B v 2A
Januari 25:
1C v 2D
1D v 2C
NUSU FAINALI
Januari 28:
W25 V w28
W26 V w27
FAINALI
Januari 30
Fergie alia, akasirishwa na Timu yake kuanza mwaka vibaya na kutupwa nje ya FA Cup!!!
• Aahidi Fulu Nondo Jumatano na Man City!!
Sir Alex Ferguson amebainisha kuwa aliikemea Timu yake hapo jana mara baada ya kipigo cha 1-0 na Leeds United walichokipata Uwanjani kwao Old Trafford na kutupwa nje ya FA Cup.
Ferguson alipanga Kikosi ‘dhaifu’ mchanganyiko hapo jana kikiwa na Chipukizi Jonny Evans, Fabio, Gibson, Anderson, Obertan na Wellbeck pamoja na Maveterani Garry Neville, Wes Brown na Mastaa Rooney na Berbatov huku Kipa akiwa Kuszczak. Na mwishoni mwa mechi, huku jahazi tayari liko mrama, akawaingiza Owen, Giggs na Valencia.
Jumatano, Man U inakumbana na Mahasimu wao wakubwa Manchester City Uwanjani City of Manchester katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling na awali Ferguson alitangaza Chipukizi ndio watacheza mechi hiyo lakini baada ya kipigo kikubwa cha jana, Ferguson ametamka: “Tuna Nusu Fainali Jumatano na Wachezaji wengi waliocheza jana hawatacheza!’
Wadau wanachukulia kauli ya Ferguson, hasa baada ya kuudhiwa na mpira mbovu wa Timu yake hapo jana, ataacha mpango wake wa kuwapanga Makinda na badala yake kuweka Fulu Nondo kama vile Man City wanavyotegemewa kufanya.
Marudiano ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling yatakuwa Old Trafford Januari 19.
KOMBE LA FA: Raundi ya 4 yapangwa, Mechi kuchezwa Januari 23 na 24
Baada ya hekaheka za Raundi ya 3 kupita Jumamosi na Jumapili huku baadhi ya Timu  kushinda na kuingia Raundi ya 4, nyingine kutoka sare na hivyo kulazimika kurudiana na mechi kadhaa kuahirishwa kwa ajili ya kutanda kwa barafu, hatimaye Ratiba ya Raundi ya 4 imetolewa na mechi hizo zinatakiwa zichezwe Wikiendi ya Januari 23 na 24.
Katika Ratiba ifuatayo, zikitajwa Timu 2 ni kwamba Mshindi kati yao hajapatikana na mechi inarudiwa na pia Timu inayotajwa kwanza ndio iko nyumbani.
RATIBA:
Southampton v Ipswich
Reading/Liverpool v Burnley
Millwall/Derby v Brentford/Doncaster
Bristol City/Cardiff v Leicester
Stoke v Arsenal
Notts County/Forest Green v Wigan
Scunthorpe v Man City
West Brom v Plymouth/Newcastle
Everton v Nottm Forest/Birmingham
Accrington/Gillingham v Fulham
Bolton v Sheff Utd/QPR
Portsmouth/Coventry v Sunderland
Preston v Chelsea
Aston Villa v Brighton
Wolves v Crystal Palace
Tottenham v Leeds

Sunday 3 January 2010

KOMBE LA FA: Arsenal yapeta!!!
Magoli mawili ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Ramsey na Eduardo yameipeleka Arsenal Raundi ya 4 ya Kombe la FA baada ya kuifunga West Ham 2-1 Uwanjani Upton Park.
Hadi mapumziko, Goli la Mtaliana Diamanti dakika za mwisho za kipindi cha kwanza ziliifanya West Ham iwe mbele kwa bao 1-0.
Huku West Ham wakishambulia na kutishia kupata bao la pili, Arsenal wakazinduka na kupachika bao mbili za haraka zilizoikata maini West Ham.
VIKOSI:
West Ham: Green, Faubert, Tomkins, Upson, Daprela, Behrami, Jimenez, Kovac, Diamanti, Stanislas, Nouble.
AKIBA: Stech, Sears, Da Costa, Payne, Lee, Edgar, N'Gala.
Arsenal: Fabianski, Sagna, Vermaelen, Gallas, Silvestre, Song Billong, Ramsey, Merida, Wilshere, Vela, Eduardo.
AKIBA: Mannone, Diaby, Nasri, Traore, Eastmond, Emmanuel-Thomas, Gilbert.
REFA: Mark Clattenburg
Ngoma droo kwa Wababe wa Glasgow!!!
Leo, Uwanjani Parkhead, nyumbani kwa Celtic, Wababe na Mahasimu wa Jijini Glasgow, Scotland, Celtic na Rangers walipambana kwenye mechi ya Ligi Kuu Scotland lakini hakupatikana mbabe na mechi ikaisha 1-1.
Hadi mapumziko, Timu zilikuwa 0-0 na Celtic wakafunga bao lao dakika ya 79 kupitia Scott McDonald lakini dakika mbili baadae Rangers wakarudisha Mfungaji akiwa Lee McCulloch.
Rangers ndio wanaongoza Ligi hiyo kwa kuwa na pointi 44 na Celtic ni wa pili wakiwa na pointi 37 lakini wamecheza mechi moja pungufu.
KOMBE LA FA: Chelsea yaua 5-0!!!
Chelsea wamesonga mbele Raundi ya 4 ya Kombe la FA baada ya kuibamiza Watford mabao 5-0 Uwanjani Stamford Bridge.
Hadi mapuziko Chelsea walikuwa mbele kwa bao 3-0 zilizofungwa na Daniel Sturridge, John Eustace wa Watford aliejifunga mwenyewe na Yuri Zhirkov.
Kipindi cha pili Sturridge alifunga tena na Frank Lampard akapiga la mwisho.
VIKOSI:
Chelsea: Hilario, Ivanovic, Alex, Terry, Ashley Cole, Lampard, Belletti, Zhirkov, Joe Cole, Malouda, Sturridge.
AKIBA: Turnbull, Carvalho, Ballack, Paulo Ferreira, Matic, Kakuta, Borini.
Watford: Loach, Hodson, Mariappa, DeMerit, Doyley, Eustace, Cowie, Lansbury, Severin, Cleverley, Graham.
AKIBA: Lee, Jenkins, Harley, Bennett, Hoskins, Henderson, Kiernan.
REFA: Kevin Friend
MATOKEO MECHI ZA Jumapili, 3 JanuarI 2010
Chelsea 5 v Watford 0
Man U 0 v Leeds United 1
Notts County v Forest Green [IMEAHIRISHWA=HALI YA HEWA MBAYA]
Sheffield United 1 v QPR 1
Tranmere v Wolves [ITAANZA saa 3 na robo usiku saa za bongo]
West Ham 1 v Arsenal 0 ****MATOKEO MPAKA HAFUTAIMU [MECHI INAENDELEA ILIANZA saa 1 na robo usiku saa za bongo]
Meneja Msaidizi wa Man U akiri kipigo ni kikubwa!!!
• Wadau walamikia Fergie kubadili Timu kila kukicha, wengine wahoji siku hizi Man U haina Festi Ilevuni!!!
Baada ya kubwagwa nje ya Kombe la FA leo kwa kipigo cha bao 1-0 na Leeds United ambayo iko Madaraja mawili chini ya Manchester United tena Uwanjani kwao Old Trafford mbele ya Mashabiki 74,000, Meneja Msaidizi wa Man U Mike Phelan amekiri kuwa kipigo hicho ni kikubwa kwao na kukubali kuwa Wachezaji wao hawakujituma kama walivyopaswa na kuwa Leeds United ndio waliocheza kwa kujituma kupita wao.
Phelan pia aliilaumu defensi yao kwa kuruhusu bao laini lilofungwa na Jermaine Beckford dakika ya 19.
Hata hivyo, baadhi ya Wadau wa Manchester United wameulalamikia mtindo wa siku hizi wa Meneja Sir Alex Ferguson wa kubadili Kikosi chake kila kukicha.
Baadhi ya Wadau hao wamesema kwa sasa festi ilevuni ya Man U haijulikana na huwezi hata siku moja ukaotea Wachezaji gani watacheza kwenye mechi.
Hilo, Wadau hao wamesistiza, ndio linafanya Timu siku hizi icheze bila maelewano na mwelekeo.
Mmoja wa Wadau hao alihoji iweje Ferguson kwenye mechi ya leo na Leeds United ambao wana uhasama wa enzi na Man U awapange Chipukizi na wageni wasio na uzoefu wa mechi za mikikimikiki kwa pamoja kama alivyofanya leo kwa kuwaweka kina Fabio, Anderson, Gibson, Obertan na Wellbeck ambao walipwaya mno.
Kwa hilo, Wadau sasa wameanza kuiogopa mechi ijayo ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling itakayochezwa huko City of Manchester Stadium Jumatano tarehe 6 Januari dhidi ya Mahasimu wao Manchester City na woga huo mkubwa unakuja kufuatia kauli ya Sir Alex Ferguson kuwa atachezesha Chipukizi wake kwenye mechi hiyo wakati kila mtu anajua Man City watashuka fulu nondo.
KOMBE LA FA: Man U nje, wapigwa 1-0 Old Trafford!!
Goli la dakika ya 19 alilofunga Jermaine Beckford limewabwaga nje ya Kombe la FA Manchester United wakiwa Uwanjani kwao Old Trafford mbele ya Mashabiki zaidi ya 74000.
Ingawa Man U walikuwa na nafasi nyingi za kufunga mabao walishindwa kuzitumia na Leeds United inayocheza Daraja la Ligi 1 sasa imesonga kuingia Raundi ya 4.
VIKOSI:
Man Utd: Kuszczak, Neville, Brown, Jonathan Evans, Fabio Da Silva, Welbeck, Gibson, Anderson, Obertan, Berbatov, Rooney.
AKIBA: Amos, Owen, Vidic, Giggs, Tosic, Carrick, Rafael Da Silva.
Leeds: Ankergren, Crowe, Naylor, Kisnorbo, Hughes, Howson, Kilkenny, Doyle, Johnson, Beckford, Becchio.
AKIBA: David Martin, Prutton, Grella, Michalik, Snodgrass, Capaldi, White.
REFA: Chris Foy
KOMBE LA FA MECHI ZA LEO Jumapili, 3 JanuarI 2010
Chelsea v Watford
Man U v Leeds United
Notts County v Forest Green [IMEAHIRISHWA=HALI YA HEWA MBAYA ]
Sheffield United v QPR
Tranmere v Wolves
West Ham v Arsenal
Meneja aliepigwa shoka Bolton aishambulia Klabu hiyo
Garry Megson alietimuliwa kazi ya Umeneja Bolton Wanderers wiki iliyopita ameishutumu vikali Bolton kwa kudai alifukuzwa kinyama.
Megson alidai Mwenyekiti Phil Gartside hakutumia uungwana kwani alimfukuza kwa njia ya simu Jumatano iliyopita.
Bolton wako nafasi ya 18 kwenye Ligi Kuu, hiyo ikiwa ni nafasi ya 3 toka chini, lakini wamecheza mechi chache kuliko Timu nyingine zinazowazunguka.
Megson amesema: “Kwenye Ligi tumecheza mechi chache na tuna mechi mbili mkononi na kama Bolton ikipata pointi mbili kwenye mechi hizo tutakuwa nafasi ya 14! Na, ikishinda mechi moja kati ya hizo mbili, itakuwa nafasi ya 12 nafasi ambayo Bolton hawajahi kufikia kwa miaka mitatu sasa!”
Megson akaongeza na kudai Klabu hiyo kwa sasa ipo kwenye hali bora kuliko alipoingia.
Megson amesema: “Wengi hawajui Klabu hiyo ilikuwa taabani! Wengi wanafikiri ukiingia hapo ni kama kuirithi Real Madrid na mambo yakipinda uko lawamani!”
KOMBE LA FA: Liverpool afueni kwa sare, mechi kurudiwa!!
Jana Liverpool walinusurika kubwagwa nje ya Kombe la FA na Reading baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na mechi hii sasa itarudiwa huko Anfield tarehe itakayotajwa baadae.
Reading, ambao wako Daraja la chini ya Ligi Kuu, waliitawala mechi hii na walifunga bao la kuongoza lakini Steven Gerrard akaisawazishia Liverpool.
Powered By Blogger