Tuesday, 5 January 2010

Malipo ya TV kulipia deni la Pompey
Uongozi wa Ligi Kuu England umeamua kuwa malipo yote toka Makampuni ya TV yatakayolipwa mwezi huu Januari ambayo ni mgao wa Klabu ya Portsmouth yaende katika kulipia madeni ya Klabu hiyo kwa Klabu nyingine zinazoidai pesa za uhamisho za Wachezaji wao kwa Klabu hiyo.
Mgao huo unaosadikiwa kuwa ni Pauni Milioni 7 utagawanywa kwa Chelsea, Tottenham na Watford ambazo ni miongoni mwa Klabu inazozidia Portsmouth na uamuzi huo wa Uongozi wa Ligi Kuu umechukuliwa kulingana na Sheria za Ligi Kuu.
Portsmouth wapo kwenye matatizo makubwa ya kifedha na hata Mamlaka ya Kodi ya Mapato imetaka Klabu hiyo ifilisiwe kwa sababu ya kutokulipa deni la Kodi la Pauni Milioni 60.
Vilevile, Pompey mpaka sasa haijawalipa Wachezaji wake Mishahara ya mwezi Desemba na hii ikiwa ni mara ya 3 kwa Mishahara kucheleweshwa.
Kwa sasa Pomey imefungiwa na Ligi Kuu kutosajili Mchezaji yeyote hadi watakapolipa madeni yao ya uhamisho wa Wachezaji.
Kifungo hicho huenda kikaathiri kuwepo kwa Mchezaji wa Tottenham, Jamie O’Hara ambae yuko Portsmouth kwa mkopo wa miezi 6 na mkataba wake utaisha hivi karibuni lakini mpaka sasa Ligi Kuu hawajabariki kuongezwa kwake.
Rosicky asaini Mkataba mpya Arsenal
Kiungo kutoka Czech Republic Tomas Rosicky, miaka 29, amesaini Mkataba mpya na Arsenal.
Rosicky alijiunga na Arsenal Mei 2006 akitokea Borussia Dortmund na ameshaichezea Arsenal mechi 76 na kufunga goli 14 lakini Msimu uliokwisha hakucheza baada ya kuwa nje ya uwanja kwa miezi 18 alipoumia misuli na goti.
Rosicky ni Mchezaji wa 15 wa Arsenal kusaini Mikataba mipya tangu Mei 2009 wengineo wakiwa ni pamoja na Abou Diaby, Robin van Persie, Theo Walcott na Eduardo.

No comments:

Powered By Blogger