Wednesday 6 January 2010

Barafu balaaa!!!! Arsenal v Bolton imegandishwa!!!
Mechi ya Ligi Kuu iliyokuwa ichezwe leo usiku Uwanja wa Emirates kati ya Arsenal na Bolton imeahirishwa kwa sababu ya baridi na barafu zilizotanda na kuzidi kuanguka Jijini London.
Ingawa Uwanja wa Emirates unachezeka lakini kwa sababu za kiusalama hasa barabara kuwa na barafu nyingi hivyo kuhatarisha usafiri wa Washabiki Mamlaka za Usalama wa Raia zimeshauri mechi hiyo isichezwe leo.
Mechi hiyo sasa itapangiwa tarehe ya baadae.
Pompey Mishahara ni fumbo!!!
Desemba ni mara ya tatu kwa Wachezaji wa Portsmouth kukosa Mishahara na waliahidiwa kulipwa leo lakini hata hii leo imeshindikana na Wawakilishi wa Mmiliki wa Klabu hiyo, Ali al-Faraj, wamekuwa wakihaha kutafuta mkopo wa muda mfupi wa Pauni Milioni 3 ili wawalipe Wachezaji wao.
Klabu hiyo ipo kwenye mashaka makubwa huku ikikabiliwa na kesi Mahakama Kuu baada ya Mamlaka ya Kodi ya Mapato kuwashitaki kwa kutokulipa kodi ya Pauni Milioni 3 na imetaka Klabu hiyo ifilisiwe.
Kesi hiyo itaanza kusikilizwa mwezi ujao.
Nao Ligi Kuu wanashikilia mgao wa Pauni Milioni 7 na nusu zikiwa ni sehemu ya fungu la malipo kwa Portsmouth kutoka kwa Vituo vya TV vinavyorusha matangazo ya moja kwa moja ya mechi za Ligi ili kulipa deni la Klabu hiyo kwa Klabu nyingine baada ya kushindwa kuzilipa ada za uhamisho za Wachezaji waliowanunua.
Kushindwa huko kulipa madeni hayo ya uhamisho pia kumeifanya Ligi Kuu kuifungia Portsmouth kutokununua Wachezaji.
Inakisiwa Portsmouth inadaiwa jumla ya Pauni Milioni 60 na inasemekana kama Ali al-Faraj asingetoa Pauni Milioni 20 katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, Klabu hiyo ingekuwa mufilisi.
Wakati huo huo, Ligi Kuu imewaambia Portsmouth kuwa hawawezi kuongeza mkataba wa mkopo wa Mchezaji Jamie O’Hara waliemkopa kutoka Tottenham mpaka wafunguliwe kifungo cha kutokusajili Mchezaji.
Mkataba wa O’Hara unakwisha Januari 15 na Klabu yake Tottenham ilikuwa tayari imekubali kuongeza mkataba wa mkopo wa O’Hara hapo Portsmouth.
Liverpool ina Pauni Milioni 1.5 tu kununua Wachezaji hii Januari!!!!
Uongozi wa Liverpool umemzuia Meneja wao Rafa Benitez kutonunua Mchezaji yeyote kwenye dirisha hili la uhamisho la Januari mbali ya Kiungo wa Argentina Maxi Rodriguez kutoka Atletico Madrid atakaegharimu Pauni Milioni 1.5 tu kwa vile mkataba wake utakuwa wa Miezi 18 tu.
Ingawa Liverpool inategemewa kuvuna zaidi ya Pauni Milioni 16 Januari hii kutokana na kuuzwa kwa Wachezaji Andriy Voronin kwa Dynamo Moscow, Andrea Dossena kwa Napoli na Philipp Degen anaetegemewa kwenda Klabu za Bundesliga huko Ujerumani, Liverpool inataka pesa hizo ziwekwe hadi Msimu ukiisha na ndipo watafutwe Wachezaji kwani wanadhani Januari Wachezaji huuzwa bei mbaya.
Wakati huo huo, Liverpool imegoma kumuuza Winga Ryan Babel kwa Birmingham waliotoa ofa ya Pauni Milioni 8.
Babel mwenyewe amekuwa akitaka kuhama ili aende Klabu nyingine ambako atapata namba ya kudumu ili ajiongezee matumaini ya kuitwa kwenye Kikosi cha Holland kitakachokwenda Afrika Kusini mwezi Juni kwenye Fainali za Kombe la Dunia.

No comments:

Powered By Blogger