Wednesday 6 January 2010

LIGI KUU England: Leo ni Arsenal v Bolton
Leo usiku saa 4 dakika 45 saa za bongo, Arsenal watajimwaga Uwanjani kwao Emirates kucheza na Bolton katika mechi yao ya kiporo na ushindi kwao utawafanya wawakaribie mno vinara wa Ligi Kuu Chelsea na pia kuwapita Manchester United wanaoshika nafasi ya pili.
Chelsea wanaongoza Ligi wakiwa na pointi 45 kwa mechi 20, Man U pointi 43 mechi 20 na Arsenal pointi 41 mechi 19.
Bolton wanasuasua kwenye Ligi Kuu wakiwa nafasi ya 18 kwenye Ligi ikiwa ni wa tatu toka mwisho na wiki iliyopita walimtimua Meneja wao Gary Megson.
Mpaka sasa mechi ya leo iko kwenye hatihati kama itachezwa kufuatia hali mbaya ya hewa iliyoambatana na baridi kali na kuanguka kwa barafu hali ambayo imeikumba Uingereza.
Ingawa Kiwanja cha Emirates kinachezeka kwa vile chini ya nyasi ardhini kuna vipasha moto [under-soil heaters] vinavyozuia barafu kuganda Mamlaka za Usalama huenda zikaamua mechi kuahirishwa kwa sababu ya usalama wa Mashabiki kwa vile barabara na njia zimefunikwa na barafu.
Hali hiyo na sababu hiyo hiyo ilifanya mechi za jana na leo za Nusu Fainali za Carling Cup ziahirishwe.
Endapo mechi itachezwa kama ilivyopangwa, Arsenal wanategemewa kumkosa Nahodha wao Cesc Fabregas ambae bado ana maumivu ya musuli lakini huenda wakamchezesha Denilson ambae amepona maumivu ya mgongo.
VIKOSI VINATEGEMEWA KUWA:
ARSENAL: Almunia, Sagna, Vermaelen, Gallas, Traore, Nasri, Denilson, Ramsey, Diaby, Rosicky, Arshavin.
BOLTON: Laaskelainen, Steinsson, Cahill, Knight, Robinson, Taylor, Muamba, Cohen, Lee, Davies, Klasnic.
Mwana wa Ferguson kuwa Bosi Preston

Darren Ferguson, miaka 37, ambae ni mtoto wa Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, yuko njiani kutangazwa kuwa Meneja mpya wa Preston North End Timu inayocheza Daraja chini tu ya Ligi Kuu liitwalo Championship.
Ferguson alikuwa Meneja wa Klabu nyingine ya Championship iitwayo Peterborough lakini alijiengua mwenyewe Mwezi Novemba mwaka jana na sasa atachukua nafasi ya Alan Irvine ambae ameondolewa na Preston.

No comments:

Powered By Blogger