Saturday, 12 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Nigeria yalala!
Leo, Argentina imewafunga Nigeria bao 1-0 katika mechi ya pili ya pili Kundi B iliyochezwa Uwanja wa Ellis Park huko Johannesburg.
Awali leo katika mechi nyingine ya Kundi B, Korea Kusini iliwapiga Ugiriki bao 2-0.
Ni bao la Mkongwe na Mchezaji wa zamani wa Manchester United, Beki Gabriel Heinz, alilofunga kwa kichwa baada ya kona ya Mkongwe mwingine ambae pia aliwahi kuichezea Manchester United, Juan Sebastian Veron, la dakika ya 6 ndilo lililowaua Nigeria.
Ingawa Argentina walionekana ni hatari sana, lakini Nigeria walipata nafasi nyingi za wazi za kusawazisha lakini wakazipoteza.
Kwa upande wa Nigeria Shujaa mkubwa ni Kipa wao Enyeama alieokoa bao nyingi za wazi na hasa kumzuia Lionel Messi kupata bao wakati alipata nafasi nyingi.
Mechi zinazofuata kwa Timu hizi ni Juni 17 Nigeria v Ugiriki na Argentina v Korea Kusini.
Timu:
Argentina: Romero; Gutierrez, Demichelis, Samuel, Heinze; Mascherano, Veron, Di Maria; Messi, Higuain, Tevez.
Nigeria: Enyeama; Odiah, Shittu, Yobo, Taiwo; Etuhu, Haruna, Kaita; Ogbuke Obasi, Yakubu, Obinna.
Refa Wolfgang Stark (Germany)
CHEKI: www.sokainbongo.com

NINI WALISEMA:
-“Sichezi peke yangu na siwezi kuleta miujiza” Cristiano Ronaldo akikiri yeye ni binadamu kama wengine.

-“Hukuona ng’ombe wakizunguka nje ya Hoteli huko Ujerumani!” Kiungo wa USA DarMarcus Beasley akibainisha tofauti ya Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka huu 2010 na zile za Mwaka 2006 huko Ujerumani.

-“Lazima wawe werevu na kuusahau Usupastaa wao na kutambua kitu pekee muhimu ni Timu na si wao. Kama hawaelewi hilo nitahitaji bunduki!” Kocha wa Ufaransa Raymond Domenech akihidhihirisha Timu ina mpasuko wa Masupastaa.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Ugiriki 0 Korea Kusini 2
Korea Kusini leo imeanza vyema kampeni yao kwenye Fainali za Kombe la Dunia walipoidunda Ugirki kwa bao 2-0 katika mechi ya Kundi B iliyochezwa Uwanja wa Nelson Mandela huko Port Elizabeth.
Korea Kusini walifunga bao la kwanza kwenye dakika ya 7 baada ya frikiki ya Ki karibu na kibendera cha kona kuingizwa ndani ya boksi na kumfanya Katsouranis kumchanganya Kipa Tzorvas na mpira kumkuta Lee Jung-soo alieupachika wavuni.
Hadi mapumziko Korea walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha Pili, Nahodha wa Korea Kusini, ambae pia ni Mchezaji wa Manchester United, Park Ji-Sung aliinasa pasi mbovu ya Vyntra katikati ya upande wa Ugiriki na kuchanja mbuga huku akiwatambuka Mabeki kadhaa wa Ugiriki na kumchambua Kipa Tzorvas na kupiatia Korea bao la pili, hiyo ikiwa dakika ya 52.
Korea ingeweza kupata bao zaidi ya mbili kama wangetuliza bongo kwani waliizidi kila kitu Ugiriki.
Mechi zinazofuata kwa Timu hizi ni Juni 17 Korea Kusini v Argentina na Ugiriki v Nigeria.
Timu:
Greece: Tzorvas, Torosidis, Papadopoulos, Vyntra, Seitaridis, Samaras, Tziolis, Katsouranis, Karagounis, Charisteas, Gekas.
Akiba: Chalkias, Patsatzoglou, Spyropoulos, Moras, Salpingidis, Kyrgiakos, Ninis, Papastathopoulos, Kapetanos, Malezas, Prittas, Sifakis.
South Korea: Jung, Cha, Cho, Jung-Soo Lee, Young-Pyo Lee, Chung-Yong Lee, Ki, Jung-Woo Kim, Ji-Sung Park, Chu-Young Park, Yeom.
Akiba: Woon-Jae Lee, Oh, Hyung-il Kim, Nam-Il Kim, Bo-Kyung Kim, Ahn, Seung-Youl Lee, Jae-Sung Kim, Dong-Jin Kim, Dong-Gook Lee, Kang, Young-Kwang Kim.
Refa: Michael Hester (New Zealand)
CHEKI: www.sokainbongo.com
Kanu amshambulia Maradona, Kocha asema hawamjali Messi!!
Nahodha wa Nigeria, Nwankwo Kanu, amemshambulia Kocha wa Argentina, Diego Maradona, kwa kauli yake kuwa Super Eagles watatumia mabavu na kuwaumiza Argentina ili kuwadhibiti.
Maradona pia alidai Nigeria itawaandama Wachezaji wake Mastaa kama Lionel Messi ili kuwachezea vibaya na kuwaumiza.
Leo Jumamosi Juni 12, saa 11 jioni saa za bongo, Argentina na Nigeria zinakumbana kwenye mechi ya Kundi B Uwanja wa Ellis Park, Johannesburg.
Kanu, akionyesha kukasirishwa na kauli za Maradona, ametamka: “Tuko hapa kucheza Soka. Haitakuwa tofauti na mechi nyingine. Sisi ni wapiganaji lakini tunacheza Soka.”
Nae Kocha wa Nigeria, Lars Lagerbach, amesema Timu yake haina plani yeyote ya kumdhibiti au kumchezea vibaya Lionel Messi.
Lagerbach amesema: “Sisi tunacheza na Argentina na sio Messi. Hakuna Mchezaji wetu atakaepewa kazi maalum ya kumchunga Messi.”
Kocha huyo akaongeza kwa kusema kuwa ukicheza na Timu nzuri kama Argentina ambao ina Wachezaji wengi wenye vipaji ni muhimu kucheza vizuri Kitimu.
Lagerback amesema: “Tukiwa na mpira, tutashambulia kwa akili. Tukiwa hatuna mpira, tutajihami. Na kama Wapinzani wetu ni bora kupita sisi, itabidi tujihami sana kuliko kushambulia!”
CHEKI: www.sokainbongo.com

Les Bleus yakabwa!
France 0 Uruguay 0
Uwanjani Green Point, Cape Town, Ufaransa na Uruguay zimetoka sare 0-0 katika mechi ya pili ya Kundi A.
Awali, South Afrika na Mexico zilitoka droo ya 1-1.
Mechi hii ya Ufarans v Uruguay ilikosa msisimko ukiondoa mara chache zilizoleta kizaazaa golini hasa shuti la Diego Forlan Uruguay kupanguliwa na Kipa Kipindi cha Kwanza.
Uruguay walimaliza mchezo wakiwa Mtu 10 kufuatia Nicolas Lodeiro kupewa Kadi mbili za Njano na hivyo kupata Nyekundu.
Uruguay: Muslera, Lugano, Godin, Victorino, Pereira, Perez (Eguren, 87), Arevalo Rios, Gonzalez, Lodeiro, Suarez (Abreu, 73) Forlan
France: Lloris, Sagna, Abidal, Gallas, Evra, Gourcuff (Malouda, 75), Toulalan, Diaby, Ribery, Govou (Gignac, 85), Anelka (Henry, 71)
CHEKI: www.sokainbongo.com


KOMBE LA DUNIA: Mechi Jumamosi Juni 12
England v USA
KIWANJA: Royal Bafokeng, Rustenburg
TAREHE: 12 JUNI 2010
SAA: 3 na nusu usiku [Bongo]
HABARI ZA TIMU:
Timu ya England inabeba matumaini makubwa ya Nchi yao ambayo wengi wanategemea makubwa toka kwao na zigo hilo kubwa na zito liko mabegani mwa Straika Wayne Rooney.
England, chini ya Meneja kutoka Italia, Fabio Capello, itawavaa ‘wapwa zao’ USA.
Capello hajakitaja Kikosi chake cha Kwanza na kitakachocheza na USA lakini mwenyewe ameshasema anajua nani watacheza.
Ingawa Wadau wanaweza kuotea Timu itakuwa ipi lakini nafasi ya Kipa ndio haina uhakika kabisa na yeyote kati ya Makipa watatu, David James, Rob Green na Joe Hart, anaweza kupangwa.
Katika Difensi, Capello itabidi amtafute nani atakuwa patna wa John Terry baada ya Nahodha wao, Rio Ferdinand, kuumia na kutolewa kwenye Fainali hizi.
Hivyo, Capello itabidi amchague mmoja kati ya Ledley King, Matthew Upson, Jamie Carragher au Michael Dawson awe patna wa John Terry.
Kwenye Kiungo, bado Gareth Barry hayuko fiti hivyo huenda Michael Carrick, Steven Gerrard na Frank Lampard wakacheza kwa pamoja.
Mbele, Rooney tayari namba yake ipo na swali lililobaki ni nani atakuwa patna wake kwenye mashambulizi. Patna huyo atatoka kati ya Peter Crouch, Emile Heskey au Jermain Defoe.
USA, iliyo chini ya Kocha Bob Bradley, si Timu mchekechea ni Timu ngumu mno na yenye Wachezaji wapiganaji wazuri.
USA, Mwaka jana, waliitoa Spain na kutinga Fainali ya Kombe la Mabara na kufungwa na Brazil kwa bao 1-0.
USA ina Wachezaji kadhaa wanaocheza Ligi Kuu Engand nao ni Kipa Tim Howard wa Everton, Jonathan Spector alieanzia kucheza Manchester United na sasa yupo West Ham, Landon Donovan, Mchezaji wa Timu ya David Beckham LA Galaxy ya Marekani ambae alichezea Everton kwa mkopo, Clint Dempsey wa Fulham na Jozy Altidore wa Hull City.
Argentina v Nigeria
KIWANJA: Ellis Park, Port Elizabeth
TAREHE: 12 JUNI 2010
SAA: 11 jioni [Bongo]
HABARI ZA TIMU:
Inaaminika Diego Maradona ataibadilisha Fomesheni ya Argentina ili awe na Mastraika Watatu ili kumruhusu Carlos Tevez acheze pamoja na Gonzalo Higuiain wa Real Madrid na Lionel Messi wa FC Barcelona.
Hii ni mechi ya kwanza ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Kocha wa Argentina, Diego Maradona, ambae alikuwa Mchezaji Gwiji wa Argentina ambae mara ya mwisho kuichezea Nchi hiyo ilikuwa Mwaka 1994 dhidi ya Nigeria.
Nigeria, walio chini ya Kocha toka Sweden Lars Lagerback, watamkosa Kiungo wa Chelsea John Mikel Obi ambae amejitoa Kikosini baada ya kutopona goti lake na nafasi yake itachukuliwa na Chipukizi Lukman Haruna anaecheza Ufaransa na Klabu ya Monaco.
Argentina wameshaifunga Nigeria mara 3 katika mechi zao za mwisho kati yao ikiwa pamoja na mechi za Makundi kwenye Kombe la Dunia Mwaka 1994 na 2202 ambako walishinda 2-1 na 1-0.
South Korea v Greece
KIWANJA: Nelson Mandela, Port Elizabeth
TAREHE: 12 JUNI 2010
SAA: 8 na nusu mchana [Bongo]
HABARI ZA TIMU:
Mwaka 2002, Korea Kusini walitinga Nusu Fainali za Kombe la Dunia zilipochezwa huko kwao wakishirikiana na Japan lakini Mwaka 2006 walishindwa kuvuka hatua ya Makundi hivyo safari hii watataka kujitutumua kufanya vizuri zaidi.
Mpinzani wa kwanza wa Korea Kusini ni Ugiriki ambao kawaida ni Timu isiyotabirika.
Hii ni mara ya pili kwa Ugiriki kucheza Fainali hizi, mara ya kwanza ilikuwa ni Mwaka 1994 huko Marekani na walifungwa mechi zote 3 za Kundi lao.
Ugiriki walitwaa Ubingwa wa Ulaya Mwaka 2004.
Korea Kusini hawana majeruhi baada ya kupona kwa Nahodha wao Park Ji-sung, Mchezaji wa Manchester United pamoja na mwenziwe Lee Dong-gook.
Ugiriki itamkosa Difenda Vangelis Moras ambae ameumia enka lakini Kiungo Kostantinos Katsouranis anaweza kushika nafasi yake.

Friday, 11 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Bafana, El Tri ngoma ngumu!
Afrika Kusini 1 Mexico 1
Mechi ya ufunguzi ya Fainali za Kombe la Dunia kati ya Wenyeji Afrika Kusini na Mexico iliyochezwa Soka City, Soweto ilimalizika kwa sare ya 1-1.
Matokeo haya hayakuwafurahisha Afrika Kusini lakini ukweli ni kwamba ni matokeo bora kwao kwa vile Mexico walitawala muda mwingi na hasa Kipindi cha Kwanza walikosa mabao ya wazi kadhaa.
Hadi mapumziko mabao yalikuwa 0-0.
Kipindi cha Pili, dakika ya 55, Siphiwe Tshabalala aliachia mzinga uliokwenda juu na kutikisa nyavu na kufanya Soweto yote itetemeke kwa Vuvuzela na shangwe zilizotoka ndani ya Uwanja wa Soka City.
Mexico walisawazisha kwenye dakika ya 79 baada ya pasi ndefu kumkuta Beki Rafael Marquez, aliepanda, akiwa peke yake na kumchambua Kipa Khune.
Hata hivyo, Bafana Bafana wangeweza kushinda mechi hii kama Mphela angetuliza akili pale alipopewa bonge la pande na kujikuta yuko yeye na Kipa Perez lakini kutaka kufunga kifundi kulisababisha mpira huo ugonge mwamba na kutoka.
Mechi inayofuata kwa Bafana ni Juni 16 watakapocheza na Uruguay Uwanja wa Loftus Versfed, Pretoria.
Mexico watacheza Juni 17 na Ufaransa huko Uwanja wa Peter Mokaba, Polokwane.
Timu:
South Africa: Khune, Gaxa, Mokoena, Khumalo, Thwala,
Tshabalala, Dikgacoi, Letsholonyane, Modise, Pienaar, Mphela.
Akiba: Josephs, Masilela, Ngcongca, Sibaya, Davids, Booth, Parker, Nomvethe, Moriri, Sangweni, Walters, Khuboni.
Mexico: Perez, Aguilar, Rodriguez, Osorio, Salcido, Torrado, Marquez, Juarez, Giovani, Franco, Vela.
Akiba: Ochoa, Barrera, Castro, Blanco, Hernandez, Moreno, Guardado, Magallon, Torres, Bautista, Medina, Michel.
Refa: Ravshan Irmatov (Uzbekistan
CHEKI: http://www.sokainbongo.com/


Bafana Bafana ya kuikwaa Mexico yatajwa
Afrika Kusini imekitangaza Kikosi chake cha Wachezaji 11 wataocheza na Mexico leo saa 11 katika mechi ya ufunguzi ya Fainali za Kombe la Dunia mechi ambao itachezwa Uwanja wa Soccer City, Soweto, Johannesburg.
Wachezaji hao 11 ni: Itumeleng Khune; Siboniso Gaxa, Lucas Thwala, Bongani Khumalo, Aaron Mokoena; Reneilwe Letsholonyane, Kagisho Dikgacoi, Steven Pienaar, Teko Modise, Siphiwe Tshabalala; Katlego Mphela.
Afrika Kusini wako Kundi A na timu nyingine kwenye Kundi hili ni Uruguay na Ufaransa ambazo zitacheza leo saa 3 na nusu usiku, saa za bongo huko Uwanja wa Green Point, Cape Town.
CHEKI: www.sokainbongo.com

PATI ya KOMBE LA DUNIA J’BURG!!!
Maelfu ya Watu walifurika na kuselebuka Uwanja wa Orlando, Soweto Jijini Johannesburg, Afrika Kusini huku wakiimba kwa furaha kusheherekea kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia ambazo kwa mara ya kwanza kabisa zitachezwa Barani Afrika kuanzia leo hadi Julai 11.
Watu waliimba, kupiga makofi, kucheza na kufurahia huku kibaridi kikali kikizizima.
Konseti hiyo ilipeperushwa Duniani kote huku Mastaa kina Alicia Keys, Angelique Kidjo na Vusi Mahlasela wakinguruma stejini.
Shakira ndie aliehitimisha sherehe hizo kwa Wimbo ‘Waka Waka This Time for Afrika’ alioimba na Kikundi cha Soweto Freshly Ground.
Watoto kwa Wakongwe wa Afrika Kusini walijumuika kuimba ‘Shosholoza’, Wimbo maarufu wa huko Afrika Kusini.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, na Rais wa FIFA, Sepp Blatter, walikuwa miongoni mwa kadamnasi hiyo.
Makusanyo toka mapato ya Konseti hiyo yatatumiwa kujenga Vituo 20 vya Afya, Elimu na Kufundisha Soka sehemu mbalimbali Afrika.
Askofu Desmond Tutu alipopanda jukwaani umati ulilipuka kwa kelele za : “Tutu, Tutu!”
Askofu Tutu akawaambia: “Ni kama niko ndotoni- niamsheni!”

Thursday, 10 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com


Ni Bondeni Taimu....KOMBE LA DUNIA 2010!!!
Hii ni mara ya kwanza kwa Afrika kuwa Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia na Afrika Kusini ndio Wenyeji wa kihistoria wa Mashindano haya makubwa kabisa Duniani na ambayo ni Fainali za 19 za Kombe la Dunia.
Ijumaa Juni 11, Soccer City, Uwanja uliopo Kitongoji cha Soweto, Johannesburg unaoingiza Watu 94,000, ndio utakaofanyiwa sherehe za ufunguzi na pia Mechi ya ufunguzi kufanyika kati ya Wenyeji Bafana Bafana na El Tri, yaani Mexico.
Inaaminika Madiba, Mzee Nelson Mandela, Miaka 91, atakuwepo japo kwa muda mdogo tu wakati wa ufunguzi huo.
Mechi hii itaanza saa 11 jioni saa za bongo.
Sherehe hizo za ufunguzi zinategemewa kudumu kwa dakika 40 na zitaanza saa 9 mchana, bongo taimu, huku Mmarekani R&B Staa R Kelly, akiwa mmoja wa Watumbuizaji 1581 wakiwemo Wacheza densi, Waimbaji na wengineo.
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, ambae atakuwepo Uwanjani hapo, ametamka: “Afrika Kusini imefufuka na haitabaki nyuma baada ya Kombe la Dunia!”
Aliongeza: “Nelson Mandela amefanya kazi kubwa ya kutuwezesha sisi kuwa Wenyeji wa Mashindano haya. Tunamtunukia Kombe la Dunia yeye! “
Alhamisi, Juni 10, kuna konseti huko Soweto ikitumbuizwa na kina Shakira na wimbo spesheli kwa Kombe la Dunia ‘Waka Waka Time for Africa’, Black Eyed Peas, Alicia Keys, Hugh Masekela, Kidjo na wengineo.
Mashindano haya yanajumuisha Nchi 32 na Mwandaaji Mkuu toka Afrika Kusini, Danny Jordaan, amezungumza: “Watu walisema hakuna Nchi ya Afrika inaweza hili! Huu ni wakati bora katika Miaka 80 ya historia ya Kombe hili! Hii ni ndoto iliyotimia kwangu! Wale waliokuwa hawaamini sasa wamekuwa ndio waaminifu wakubwa!”
Mechi za Fainali za Kombe la Dunia zitachezwa katika Miji ya Johannesburg, yenye Viwanja viwili, Soccer City na Ellis Park, na Miji mingine ni Cape Town, Pretoria, Polokwane, Rustenburg, Bloemfontein, Port Elizabeth, Durban na Nelspruit.
Fainali ya Kombe la Dunia ni Julai 11.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Benitez rasmi Inter!!
Meneja wa zamani wa Liverpool Rafael Benitez amethibitishwa rasmi kama Meneja mpya wa Inter Milan baada ya kusaini Mkataba wa Miaka miwili na Mabingwa hao wa Italia na Ulaya.
Klabu ya Inter Milan ilitoa matangazo: “Inter inamkaribisha Rafael Benitez,”
Pia Inter imesema Benitez atatambulishwa rasmi Juni 22 kwenye Mkutano na Wanahabari.
Benitez aliondoka Liverpool wiki iliyopita baada ya kudumu huko kwa Miaka 6.
Pele atoa utabiri Kombe la Dunia 2010….
Mkongwe, aliepachikwa cheo cha Mfalme wa Soka, Pele, kutoka Brazil, kwa mara nyingine tena amejikita kutabiri kwenye Kombe la Dunia ingawa katika Miaka 20 iliyopita utabiri wake umekuwa hautimii na hata kumfanya Straika na Staa wa zamani wa Brazil, Romaria, kutoa kauli: “Pele asiposema kitu ni Mshairi mzuri mno lakini akifungua mdomo hutoa utumbo mtupu!”
Safari hii kwenye Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza kesho Ijumaa Juni 11 huko Afrika Kusini, Pele ameeleza imani yake kuwa ni Spain na Brazil ndio wenye nafasi kubwa kutwaa Kombe la Dunia ingawa ametoa pia matumaini yake kuwa huenda Timu moja ya Afrika ikafika Fainali.
Pele ametamka: “Spain na Brazil ni Timu Bora lakini ni ngumu kusema nani bora zaidi! Ningependa kuiona Brazil ikicheza Fainali na Timu moja toka Afrika! Fainali hizi zitakuwa nzuri kwani maandalizi ni mazuri na zinaendeshwa vizuri!”
Kuhusu Brazil, Pele amesema ni lazima Brazil wajikaze ikiwa watataka kuwa Mabingwa wa Dunia ingawa uwezo wanao.
Pia ameitaja England kuwa ni moja ya Timu ngumu na kumsema Kocha wake Fabio Capello kama ni mzuri huku Kikosi chake kikiwa na Wachezaji wazuri na Wayne Rooney ndio tishio kubwa.
Ballack adai Abramovich ndie aliamua ang’oke Ze Bluzi!!
Michael Ballack amesema uamuzi wa kutokumwongezea Mkataba Chelsea umefanywa na Mmiliki wake Roman Abramovich.
Ballack, Miaka 33, ambae pia amezikosa Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuumia kwenye Fainali ya FA Cup Chelsea ilipoifunga Portsmouth 2-0, ataondoka Chelsea mwisho wa Mwezi huu baada ya Mkataba wake kumalizika.
Ballack amekuwepo Stamford Bridge toka 2006 na amesema: “Siku zote Chelsea ni chaguo langu la kwanza lakini huu si uamuzi wangu ni wa mwenye mali Abramovich.”
Ballack aliongeza kuwa alitambua kitambo kuwa mwisho wake umefika baada ya mazungumzo yake na Chelsea kuhusu kuongeza Mkataba kusimama.
Ballack amesema hayuko tayari kustaafu au kwenda kucheza Marekani au Dubai hivyo atatafuta Klabu yoyote Ulaya na hata kurudi kwao Ujerumani ambako alikuwa Mchezaji wa Bayern Munich kabla kwenda Chelsea.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Fergie: ‘Hamna mabadiliko makubwa Man United!”
Sir Alex Ferguson amerudia tena kauli yake kwamba hakutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye Kikosi chake kwa ajili ya Msimu ujao na amesisitiza kuwa Kikosi kilichopo ni kizuri na kina uwezo wa kugombea Vikombe vikubwa.
Tangu auzwe Cristiano Ronaldo kwa Pauni Milioni 80 Mwaka jana ni Antonio Valencia, Chris Smalling na Javier Hernandez aka Chicharito ndio Wachezaji wapya walionunuliwa kwa thamani ndogo mno ambayo pengine haifiki robo ya thamani ya Ronaldo.
Mkurugenzi Mtendaji David Gill amekuwa akisisitiza na kuwapoza Washabiki kila mara kuwa fedha za kununua Wachezaji zipo ila ni juu ya Ferguson kuamua ni nani anamtaka.
Lakini Ferguson amekuwa na msimamo na mtizamo tofauti na amesema: “Kwa miaka mingi tumefanya juhudi kubwa kuwakuza Wachezaji Vijana na kuwaendeleza. Inabidi tutathmini hilo na labda tutaongeza Wachezaji wawili au mmoja.”
Fergusona akaongeza: “Soko la Wachezaji siku hizi ni gumu na hata hivyo Kikosi chetu ni kizuri. Msimu ujao tutapigana kurudisha Ubingwa nyumbani kwake na mahala bora Duniani.Tutarudi tena mwakani, siku zote Manchester United hufanya hivyo!”
Man City wambakisha Vieira
Manchester City wametangaza Kiungo Patrick Vieira atabakia hapo baada ya kumuongezea Mkataba wa Mwaka mmoja.
Viera, Miaka 33, alijiunga kutoka Inter Milan Mwezi Januari kwa Mkataba wa Miezi 6 na sasa atabaki Man City hadi mwishoni mwa Msimu ujao wa Mwaka 2010/11.
Msimu uliopita aliichezea Man City mechi 14.
Viera alishawahi kucheza Ligi Kuu akiwa na Arsenal aliokaa nao Miaka 9 hadi alipohama Mwaka 2005 kwenda Juventus.
Wachezaji Afrika Kusini wakiri mchecheto!!
Wachezaji wa Timu ya Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia, Afrika Kusini, wamekiri kuwa wanapatwa na wasiwasi kadri Ijumaa inapozidi kukaribia kwa ajili ya mechi yao ya ufunguzi na Mexico itakayochezwa Uwanja wa Soccer City huko Kitongoji cha Soweto Jijini Johannesburg.
Mshambuliaji wa Bafana Bafana, Bernard Parker, amesema: “Kadri ijumaa inavyokaribia tunapatwa na mchecheto! Fikra zetu zote hatutaki kuwaangusha Watu wetu!”
Hali hiyo imeungwa mkono na Winga Siphiwe Tshabalala lakini amesema kwa vile Taifa lote liko nyuma yao wanapata moyo mkubwa.
Afrika Kusini haijafungwa katika mechi 12 za majaribio walizocheza wakiwa chini ya Kocha toka Brazil Carlos Alberto Pereira.
Nae Kipa wa Bafana Bafana, Itumeleng Khune, amesisitiza: “Tunajua umuhimu wa kushinda mechi ya kwanza! Tupo nyumbani mbele ya Mashabiki wetu na hilo litatupa nguvu zaidi!”
Mitaa ya Johannesburg imetapakaa uzalendo wa kila aina kiasi cha kumfanya Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kuielezea hali hiyo ni nzuri kwani inaunganisha Taifa na ni manufaa makubwa kwa kuleta mshikamano kwa Watu wa rangi na asili tofauti Nchini humo na ametabiri hilo litadumu na kutawala muda mrefu.
Wengi wanategemea mengi toka kwa Bafana Bafana na wengi hawatachoka kupuliza Vuvuzela.

Wednesday, 9 June 2010

CHEKI www.sokainbongo.com

Robinho ng’o kurudi Man City!!
Mawakala wa Robinho wanategemewa kuruka hadi Manchester wiki ijayo ili kwenda kuwajulisha Manchester City kuwa Mteja wao hana nia
ya kurudi huko baada ya Mkataba wake wa mkopo kuchezea Santos ya Brazil kumalizika.
Robinho, aliesajiliwa kwa dau la rekodi huko Uingereza la Pauni Milioni 32.5 Septemba 2005 kutoka Real Madrid, alikuwa hapendezewi na maisha ya Manchester na pia kutoridhika na Meneja wa Man City, Roberto Mancini, ambae Robinho amemwelezea kama Mtu anaekosa uwezo wa kuongoza Timu.
Msimamo wa Man City ni kuwa wanamtaka Robinho arudi Klabuni hapo Agosti 3 tayari kwa Msimu mpya wa Ligi Kuu lakini kuna kila dalili Man City wanajua Robinho harudi tena hapo.
Kuna mipango ya chinichimi ya kumpeleka Robinho FC Barcelona ingawa Mawakala wake hawajathibitisha hilo mbali ya kugusa tu kijuujuu kuwa Mchezaji yeyote Yule atafurahi kuchezea Barca.
Ballack, Cole na Belletti kwa heri Ze Bluzi!!
Chelsea imethibitisha Wachezaji wake watatu, Joe Cole, Michael Ballack na Juliano Belletti, wataondoka Klabu hiyo baada ya Mikataba yao kumalizika mwishoni mwa Mwezi huu.
Wakati Belletti, mwenye umri wa miaka 33, hakupewa ofa yeyote ya kuongezewa Mkataba, Cole na Ballack walipewa ofa mpya ya nyongeza ya Mikataba yao lakini hawakuridhika nayo na hivyo mazungumzo yakavunjika.
Belletti, Raia wa Brazil, alijiunga na Chelsea Mwaka 2007 akitokea Barcelona na amechezea Chelsea mechi 54 na kufunga bao 5.
Cole, Miaka 28, alijiunga na Chelsea Mwaka 2003 akitokea West Ham na hivi sasa yuko huko Afrika Kusini na Kikosi cha England kinachosubiri kucheza Fainali za Kombe la Dunia.
Ballack, Miaka 33, alijiunga na Chelsea Mwaka 2006 na alitegemewa kuiongoza Nchi yake Ujerumani kama Nahodha huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia lakini akaumizwa kwenye Fainali ya FA Cup Chelsea ilipocheza na Portsmouth na kushinda 2-0 hapo Mei 15 na hivyo kuikosa michuano hiyo ya Dunia.
Fulham wamsaini Senderos
Fulham imekamilisha taratibu za kumsaini Difenda wa Arsenal Philippe Senderos kwa Mkataba wa Miaka mitatu.
Senderos amejiunga na Fulham kama Mchezaji huru baada ya Mkataba wake huko Arsenal kumalizika.
Mchezaji huyo ambae yuko Afrika Kusini na Uswisi kwenye Kombe la Dunia aliichezea Everton kwa mkopo nusu ya mwisho ya Msimu wa Ligi Kuu wa 2009/10 uliomalizika Mei 9 na Msimu wa nyuma yake alikaa Mwaka mzima huko AC Milan akicheza kwa mkopo.
Sendoros, Miaka 25, alijiunga na Arsenal Mwaka 2003 akitokea Servette ya Uswisi lakini amekuwa hana namba ya kudumu.

Tuesday, 8 June 2010

CHEKI www.sokainbongo.com

Padri aadhibiwa kwa uhuni kwenye Soka
Thessaloniki, Ugiriki
Padri wa Kigiriki ambae ni Shabiki lililokubuhu la Soka ameadhibiwa na Kanisa la Orthodox huko Mji wa Thessaloniki, Ugiriki kwa kufanya uhuni wakati akishabikia Klabu anayoisapoti.
Padri Christos ni Shabiki wa kutupwa wa Klabu kubwa na maarufu ya PAOK FC inayosifika kwa kuwa na Mashabiki wenye fujo huko Ugiriki na kawaida Padri huyo huenda kutazama Mechi zake akiwa na Majoho ya Upadre huku amejitanda skafu ya PAOK FC.
Mashabiki wenzake wa PAOK wamembatiza jina la ‘Papa PAOK’.
Padre Christos, mwenye umri wa miaka 60 na kitu, alijijengea sifa mbaya pale aliponaswa kwenye mikanda ya Video iliyozagaa mtandaoni kwenye tovuti ya You Tube ikimwonyesha yuko katikati ya Mashabiki waliokuwa wakiwatukana Wapinzani wao na nyingine zilionyesha genge la PAOK FC wakiimba: “Padre ndie Mungu.”
Kanisa lake likachoshwa na vitimbwi vya Papa PAOK na wakaamua kumwadhibu kwa kumshusha wadhifa wake na pia kumpiga marufuku kushiriki Magenge ya Washabiki.
Hatua ya Kanisa hilo imewaudhi Washabiki wa PAOK ambao wameanzisha Kampeni kwenye mtandao wa Facebook inayoitwa “Mfungulieni Papa PAOK”.
Rio: ‘Heskey hana kosa!’
Rio Ferdinand amesisitiza Emile Heskey sio wa kulaumiwa kwa kuumia kwake kulikomfanya alikose Kombe la Dunia.
Beki huyo wa Manchester United na Nahodha wa England aliumia goti Ijumaa iliyopita mazoezini alipovaana na Heskey walipokuwa wanagombea mpira na maumivu hayp yamemfanya awe nje ya uwanja kwa wiki 6 hivyo kuzikosa Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 11.
Ingawa hawezi kucheza, Ferdinand ameamua kubaki na Kikosi cha England huko Rusternburg, Afrika Kusini hadi baada ya Mechi ya Kwanza ya England Jumamosi ijayo Juni 12 England itakapocheza na USA.
Rio ametamka: “Ni bahati mbaya! Ni eksidenti tu!”
Rio aliongeza kuwa alitambua palepale alipoumia kuwa ndoto yake ya kuiongoza England kama Nahodha imekwisha.
Rio amesema: “Inavunja moyo lakini nimeshakubali ukweli. Usiku wa kwanza ulikuwa mgumu kila kitu nilikifikiria sana. Kuiongoza Nchi yako katika Mashindano makubwa ni ndoto kubwa. Inasikitisha!”
Kombe la Dunia: Utabiri wa Pele
Straika wa zamani wa Brazil na Mtu anaesifiwa kuwa ndie Mchezaji Bora wa Soka katika Historia aliepewa cheo cha ‘Mfalme wa Soka’ ni Pele lakini siku zote utabiri wake kwenye Soka umekuwa si sahihi na haupewi uzito mkubwa na Wadau.
Hali hiyo imemfanya hata Staa wa zamani wa Brazil, Straika ambae alipata sifa kubwa, Romario, kutamka: “Pele akikaa kimya ni Mshairi mzuri lakini akifungua mdomo tu hubwabwaja utumbo tu!”
Ufuatao ni utabiri wa Pele kuhusu Kombe la Dunia katika Miaka 20 iliyopita:
1990
UTABIRI: "Italy ndio washindi"
MATOKEO: Italy walifungwa na Argentina kwenye Nusu Fainali na Ujerumani Magharibi wakawa Mabingwa wa Dunia.
1994
UTABIRI: "Kwangu mimi Colombia ndio Timu Bora. Haimaanishi watashinda Kombe la Dunia lakini watakuwa moja ya Timu 4 kwenye Nusu Fainali. Brazil wana Wachezaji wazuri lakini Kitimu si wazuri. Ujerumani ni wazuri Kitimu.”
MATOKEO: Colombia wanatolewa mapema na Beki alejifunga mwenyewe Andres Escobar anapigwa risasi na kuuliwa waliporudi kwao huko Colombia.
Ujerumani wanatolewa Robo Fainali.
Brazil wanachukua Ubingwa wa Dunia.
1998
UTABIRI: "Spain ndio Washindi na siku zote naamini Brazil watafika Fainali. Ufaransa ina Wachezaji wazuri wanaocheza Kitimu na wako nyumbani. Wana nafasi nzuri kufika Fainali. England wana Meneja mzuri, staili nzuri na Timu ngumu.”
MATOKEO: Spain wanatolewa kwenye Makundi na Ufaransa inaifunga Brazil kwenye Fainali.
2002
UTABIRI: "Brazil wamekuwa hawachezi vizuri, hawachezi Kitimu. Kuna msululu wa Timu Bora hivi sasa zikiwemo Argentina, Ufaransa, Italia na Ureno lakini hamna moja bora kupita wenzake. Chini yao zipo Ujerumani, England na Spain.”
MATOKEO: Argentina, Ufaransa na Ureno zinabwagwa kwenye Makundi.
Italia wanatolewa Raundi ya Pili na Korea Kusini.
Brazil wanachukua Ubingwa wa Dunia.
2006
UTABIRI: "Timu 4 za Nusu Fainali ni Brazil, Argentina, England na France"
MATOKEO: England, Argentina na Brazil zote zinatolewa Robo Fainali.
Italy anamfunga Ufaransa Fainali na kuwa Bingwa.
UTABIRI WA PELE MKUBWA: “Nchi ya Afrika itashinda Kombe la Dunia kabla Mwaka 2000.”
MATOKEO: Hadi leo hamna hata Nchi moja ya Afrika iliyovuka Robo Fainali ya Kombe la Dunia
CHEKI www.sokainbongo.com

Refa adai Rooney ana matusi
Refa aliechezesha pambano la kirafiki hapo jana kati ya England na Platinum Stars, Timu ya huko Rusternburg, Afrika Kusini, Jeff Selogilwe, amedai Wayne Rooney angepewa Kadi Nyekundu kama mechi hiyo ingekuwa ya Kombe la Dunia kwa kumtukana Refa.
Refa huyo alimpa Rooney Kadi ya Njano kwa lugha chafu katika mechi hiyo ambayo England walishinda bao 3-0.
Tangu Rooney apewe Kadi Nyekundu katika Mechi ya Robo Fainali ya Kombe la Dunia Mwaka 2006 England walipocheza na Ureno baada ya kumkanyaga Beki wa Ureno Ricardo Carvalho, Rooney hajawahi kutolewa nje tena.
Lakini Refa Selogilwe amedai: “Ni aibu. Ni Mchezaji mzuri na nampenda lakini tatizo anatukana Marefa. Hilo limenisikitisha.”
Hata hivyo, Refa huyo amesema baada ya Mechi hiyo Rooney alimfuata na kumwomba radhi na kisha kumpa Jezi yake kama zawadi.
Nani nje Kombe la Dunia
Ureno imepata pigo baada ya Winga wa Manchester United, Nani, kujitoa kushiriki Fainali za Kombe la Dunia kufuatia kuumia bega.
Habari hizo za kuumia kwa Nani zimethibitishwa na Kocha wa Ureno Carlos Queiroz ambae tayari ameshamwita Mchezaji wa Benfica, Ruben Amorim, kuchukua nafasi ya Nani.
Nani aliumia bega mazoezini wiki iliyopita na awali ilidhaniwa si maumivu makubwa lakini uchunguzi wa kina umedhihirisha hawezi kupona mapema na kucheza Kombe la Dunia ambalo Ureno wanacheza Mechi yao ya kwanza Juni 15 na Ivory Coast.
Man City kuwaondoa wachezaji watatu.
Wachezaji watatu wa Manchester City, Martin Petrov, Sylvinho na Benjani wataondolewa Klabu hiyo kabla Msimu ujao kuanza hapo Agost 14.
Petrov, mwenye Miaka 31 na ni Raia wa Bulgaria, alisainiwa Mwaka 2007 wakati huo Timu ikiwa chini ya Meneja Sven-Goran Eriksson lakini amemudu kucheza Mechi 57 tu na kufunga bao 15 kwa vile amekuwa akiumia mara kwa mara.
Nae Beki toka Brazil, Sylvinho, Miaka 35, alisaini Mkataba wa Mwaka mmoja Agosti mwaka jana lakini amemudu kuanza Mechi 9 tu tangu wakati huo.
Mchezaji mwingine atakaeondolewa ni kutoka Zimbabwe, Benjani, Miaka 31, alietua Man City Mwaka 2008 lakini ameshindwa kupata namba na nusu ya pili ya Msimu wa Ligi Kuu wa 2009/10 alipelekwa Sunderland kwa mkopo.

Monday, 7 June 2010

Cheki www.sokainbongo.com

SAMBA PATI Bongo:
Taifa Stars 1 Brazil 5
Brazil wameifunga Tanzana mabao 5-1 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete pamoja na maelfu ya Watu wengine.
Brazil, ambao wako Afrika Kusini kwa ajili ya Kombe la Dunia, walipanga Kikosi chao chote kamili wakiwemo Masupastaa Kaka, Robinho, Fabiano, Maikon, Lucio na wengine ambao Bongo wamezoeleka kuonekana kwenye luninga tu.
Ingawa Tanzania walifungwa lakini mabao hayo, hasa ya kipindi cha kwanza, yametokana na uzembe wa Mabeki na si kwa sababu ya ufundi mkubwa wa Brazil ingawa walionyesha ni wepesi mno kutumia makosa ya Mabeki.
Kipindi cha kwanza Tanzania walijitahidi mno kushambulia na mara kadhaa walimpa misukosuko Kipa wa Brazil anaedakia Tottenham, Gomez, alielazimika kuokoa mipira kadhaa hasa toka kwa Mrisho Ngassa ambae hakika kiwango chake ni cha juu.
Mabao mawili ya kwanza ya Brazil yalifungwa na Robinho dakika ya 13 na 33.
Hadi mapumziko Tanzania 0 Brazil 2.
Kipindi cha pili, Brazil walionyesha kuongeza kasi, kutulia na kutumia utaalam wa juu kidogo na kwenye dakika ya 53, Ramirez alieingizwa kipindi hicho kuchukua nafasi ya Mkongwe Gilberto aliachia fataki iliyomshinda Kipa Mohamed.
Dakika ya 75 krosi ya Fulbeki Maikon aliepanda ilikoswa na Kipa Mohamed na Kaka akamalizia na kuipatia Brazil bao la 4.
Lakini Tanzania ikafanya kitu ambacho Nchi nyingi zimeshindwa kukifanya tangu Oktoba Mwaka jana pale walipoitoboa ngome ya Brazil kwa mara ya kwanza kupitia Jabir Aziz alieingia Kipindi cha Pili alipofunga bao kwa kichwa kwenye dakika ya 86.
Brazil wakafunga kitabu cha mabao dakika za majeruhi kwa Ramirez kupachika bao lake la pili na la 5 kwa Brazil.
Vikosi vilikuwa:
Tanzania: Mohamed, Yondani, Cannavaro, Kigi, Mgosi, Ngassa, Shadrak, Nizar Khalfan, Makasi [Aziz], Mwasiga, Nyoni [Nurdin Bakari]
Brazil: Gomez, Maikon, Lucio [Luisao], Juan, Bastos [Gilberto], Elano [Dani Alves], Gilberto [Ramirez], Felipe Melo [Josue], Robinho, Kaka, Fabiano Nilmar]
PATA MAMBO MOTO: www.sokainbongo.com

BONGO LEO NI SAMBA PATI!!!!
Leo Jiji la Dar es Salaam litawaka moto baada ya Magwiji wa Soka Duniani Brazil kutua Bongo wakitokea Afrika Kusini hapo jana usiku na leo kuanzia saa 12 jioni saa za Bongo watashuka Uwanja wa Taifa kuchuana na Tanzania kwenye mechi ya kirafiki.
Brazil, ambao wako kambini Afrika Kusini, wakisubiri kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia, walicheza Harare, Zimbabwe Jumatano iliyopita na wakaifunga Zimbabwe bao 3-0 kwa bao za Bastos, Robinho na Elano.
Pichani ni Staa Kaka akiwa na Meneja wake Dunga ambae ndie alikuwa Nahodha wa Brazil waliochukua Ubingwa wa Dunia huko USA Mwaka 1994.
Timu ya Taifa ya Tanzania jana ilikuwa Kigali, Rwanda na ilifungwa na Nchi hiyo bao 1-0 na kutupwa nje ya Fainali za CHAN, Mashindano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani.
Timu hiyo ilitegemewa kurudi Dar es Salaam leo asubuhi.
Mechi hii ya leo ya Tanzania v Brazil itarushwa moja kwa moja kwenye TV na kushuhudiwa kwenye zaidi ya Nchi 160 Duniani [ikiwemo Qatar alipo Mdau wa Blogu hii na itaonyeshwa na Al Jazeera Sports +1].
Kwa bahati mbaya, Wabongo watakaoshindwa kwenda huko Uwanja wa Taifa hawataiona mechi hii moja kwa moja kupitia TV kwa madai kuwa haki ya kurushwa kwa matangazo wanayo Globo TV ya Brazil na hakuna Kituo chochote cha Tanzania kilichopewa haki ya kurusha laivu ila wataruhusiwa kuionyesha mechi hiyo baadae kwa kuirekodi.

Sunday, 6 June 2010

PATA MAMBO MAPYA MOTO: http://www.sokainbongo.com/

Nigeria 3 Korea Kaskazini 1
• Washabiki wavamia milango, wengi waumia!
Washabiki 13 pamoja na Polisi mmoja walikimbizwa Hospitali baada ya kuvamia milango ya Uwanja wa Makhulong huko Johannesburg, Afrika Kusini, wengi wao wakiwa Mashabiki wa Nigeria, ili kuona pambano la kirafiki kati ya Korea Kaskazini na Nigeria lililofanyika leo Jumapili Juni 6.
Ingawa hakuna aliefariki, Watu kadhaa walijeruhiwa katika harakati za kutaka kuingia Uwanjani katika mechi hiyo ambayo ilikuwa haina kiingilio ila zilitolewa Tiketi za mwaliko za bure wa kuingia Uwanja wa Makhulong unaoweza kuchukua Watu 10,000 tu.
Uwanja huo wa Makhulong si mmoja wa Viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia.
Hata hivyo mechi hiyo ya kirafiki iliendelea na Nigeria waliifunga Korea Kaskazini bao 3-1.
Mabao yalifungwa na Yakubu Aiyegbeni, dakika ya 17, Victor Obinna, dakika ya 62 kwa penalti na Obafemi Martins kwa upande wa Nigeria.
Bao la Korea Kaskazini lilifungwa na Jong Tea-Se dakika ya 61.
PATA MAMBO MAPYA MOTO: http://www.sokainbongo.com/



Taifa Stars nje……. Twiga Stars yatinga Fainali!!!
Leo Timu ya Taifa ya Tanzania imebwagwa nje na Rwanda baada ya kupigwa bao 1-0 huko Kigali, Rwanda na hivyo Rwanda itacheza Fainali za CHAN, Mashindano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani yatakayochezwa huko Sudan Mwakani.
Taarifa kamili za mechi hii tutaleta baadae.
Hapo jana, Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, imefuzu kuingia Fainali za Kombe la Afrika kwa Wanawake zitakazochezwa huko Afrika Kusini Mwezi Oktoba baada ya kutoka sare na Eritrea kwa bao 3-3 katika mechi iliyochezwa Mjini Asmara, Eritrea na hivyo kufuzu kwa jumla ya goli 11-4.
Twiga Stars walishinda mechi ya kwanza Jijini Dar es Salaam kwa bao 8-1.
Katika mechi ya jana, Twiga Stars, wakiwa chini ya Kocha Charles Boniface Mkwasa, walijikuta wako nyuma kwa bao 3-0 lakini Shujaa alikuwa Asha Rashid aka Mwalala aliepachika bao zote 3 na kuifanya mechi imalizike 3-3.
PATA MAMBO MAPYA MOTO: http://www.sokainbongo.com/

Benitez kutua Inter?
Bosi wa zamani wa Liverpool Rafael Benitez yupo mbioni kufanya mazungumzo na Inter Milan ili kuziba pengo la Umeneja lililoachwa wazi na Jose Mourinho aliehamia Real Madrid.
Benitez aliacha kazi Liverpool kwa makubaliano na uongozi wa Klabu hiyo Alhamisi iliyopita baada ya kudumu hapo kwa Miaka 6.
Rais wa Inter Milan, Massimo Moratti, ametamka: “Lengo letu ni kuongea nae. Halafu tutajua na kuamua.”
Hata hivyo Benitez atakumbana na mzigo mkubwa huko Inter kwa vile Klabu hiyo chini ya Mourinho ilinyakua Trebo, yaani Vikombe vitatu kwa mpigo pale iliposhinda Serie A, Coppa Italia na UEFA Champions Ligi, na kurudia mafanikio hayo ni kazi ngumu.
Drogba apasuliwa!!
Nahodha wa Ivory Coast, Didier Drogba, amefanyiwa operesheni yenye mafanikio ili kuunga mfupa karibu na kiwiko chake cha mkono wa kulia aliovunjika Ijumaa kwenye mechi ya kirafiki ambayo Ivory Coast iliifunga Japan 2-0.
Drogba aliumia baada ya kuvaana na Sentahafu wa Japan mzaliwa wa Brazil, Marcus Tulio Tanaka.
Lakini hadi sasa haijasemwa kama atapona baada ya muda gani ili aweze kuiwakilisha Nchi yake kwenye Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 11 na mechi ya kwanza kwa Ivory Coast ni Juni 15 watakapoivaa Ureno.
Timu nyingine kwenye Kundi la Ivory Coast ni Brazil na Korea Kaskazini.
Rio kubaki na Timu ya England Afrika Kusini
Rio Ferdinand atabaki huko Afrika Kusini na Timu ya England hadi itakapocheza mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia Jumamosi ijayo dhidi ya USA licha ya kuwa yeye yupo nje ya Mashindano hayo baada ya kuumia goti mazoezini.
Madaktari wamesema atachukua Wiki 4 hadi 6 kupona na hivyo ikabidi aondolewe kwenye Kikosi hicho cha Kombe la Dunia na nafasi yake kujazwa na Beki wa Tottenham Michael Dawson aliesafirishwa haraka toka England na tayari yuko kambini huko Rustenburg, Afrika Kusini.
Nafasi ya Unahodha ya Rio amepewa Naibu wake Steven Gerrard.
MATOKEO:
Jumamosi, Juni 5
Holland 6 v Hungary 1
South Africa 1 v Denmark 0
Australia 1 v USA 3
Ghana 1 v Latvia 0
Slovakia 3 v Costa Rica 0
Algeria 1 v UAE 0
Romania 3 v Honduras 0
Serbia 4 v Cameroon 3
Switzerland 1 v Italy 1
MECHI YA LEO:
Jumapili, Juni 6
Nigeria v Korea Kaskazini
Powered By Blogger