Liverpool watwaa uongozi LIGI KUU: West Ham 0 Liverpool 3
Liverpool wakicheza nyumbani kwa West Ham Uwanja wa Upton Park wameweza kuwafunga wenyeji wao West Ham kwa mabao 3-0 kwa magoli mawili ya Nahodha wao Steven Gerrard na la tatu alilofunga Ryan Babel.
Bao la kwanza alifunga Gerrard, akicheza mechi yake ya kwanza baada ya kukosa mechi kadhaa kwa kuwa majeruhi, baada ya pande zuri la Fernando Torres kwenye dakika ya pili tu. Goli la pili lilifungwa baada ya Gerrard kupiga penalti ambayo Kipa wa West Ham Robert Green aliokoa lakini Gerrard akautokea tena mpira na kuukwamisha wavuni.
Hadi mapumziko West Ham 0 Liverpool 2.
Kipindi cha pili, Ryan Babel, alieingizwa kipindi hicho alifunga bao la 3.
Sasa Liverpool anaongoza LIGI KUU England akiwa na pointi 80 sawa na Manchester United lakini ana tofauti ya magoli bora ingawa amecheza mechi 2 zaidi ya Manchester United. Liverpool amecheza mechi 36 na Man U mechi 34.
Kesho Manchester United atacheza na Mtani wake wa Jadi Manchester City nyumbani kwake Old Trafford.
Jumatano Man U anacheza mechi yake ya kiporo ugenini kwa Wigan na Jumamosi ijayo tarehe 16 Mei Man U anamkaribisha Arsenal Old Trafford.
Liverpool mechi yake inayofuata ni Jumapili tarehe 17 Mei wakati atakapokuwa mgeni wa West Bromwich Timu inayopigana isishushwe Daraja.
Lakini Manchester United akishinda mechi yake ya kesho na Man City, na ile ya Jumatano na Wigan, na, pengine, kushinda au kutoka suluhu mechi ya Jumamosi ijayo na Arsenal, basi atakuwa Bingwa moja kwa moja hata kabla Liverpool hajacheza mechi yake inayokuja dhidi ya West Bromwich.
Vikosi ni:
West Ham: Green, Neill, Tomkins, Upson, Ilunga, Boa Morte, Noble, Kovac, Stanislas, Di Michele, Tristan.
Akiba: Lastuvka, Lopez, Nsereko, Spector, Collison, Sears, Payne.
Liverpool: Reina, Arbeloa, Skrtel, Carragher, Aurelio, Benayoun, Mascherano, Lucas, Gerrard, Kuyt, Torres.
Akiba: Cavalieri, Dossena, Hyypia, Babel, Insua, Ngog, Degen.
Refa: Alan Wiley
LIGI ITALIA SERIE A: KIBANO KWA CLAUDIO RANIERI WA JUVENTUS!!!!
Claudio Ranieri, Meneja wa zamani wa Chelsea ambae sasa yuko Juventus huko kwao Italy, kesho ana kitimtim kikubwa kwani kesho Timu yake Juventus inacheza na AC Milan na wakiwafunga tu AC Milan basi Bingwa Italia ni Inter Milan, inayoongozwa na pia Meneja wa zamani wa Chelsea Jose Mourinho, huku kukiwa na mechi 3 za LIGI YA SERIE A zimebaki.
Ikiwa Ubingwa watachukuwa Inter Milan kwa sababu tu Juventus kawafunga AC Milan Mashabiki wa Juventus watakasirika sana kwa sababu hawaipendi Inter Milan ambao wakichukua tena Ubingwa itakuwa ni mara ya 4 mfululizo.
Lakini kitimtim cha Claudio Ranieri si hicho tu!
Juventus wakifungwa na AC Milan vilevile Mashabiki watakasirika kwani AC Milan pia ni adui mkubwa wa Juventus.
Kwa kifupi, Claudio Ranieri, inategemewa hana kazi msimu ujao.
Juventus walikuwa bado kwenye kinyang'anyiro cha Ubingwa lakini wamepoteza mwelekeo kwa kutokushinda mechi 5 mfululizo hadi sasa.
Mpaka sasa Juventus wako nafasi ya 3 wakiwa na pointi 65 kwa mechi 33, AC Milan pointi 67 mechi 33 na vinara Inter Milan wana pointi 77 kwa mechi 34.
MECHI ZA KESHO JUMAPILI ZA ITALIA SERIE A: [saa za bongo]
AC Milan v Juventus, [saa 1 na nusu usiku]
Chievo v Inter Milan, [saa 10 jioni]
Kindumbwendumbwe cha kuingia LIGI KUU: Burnley 1 Reading 0
Katika mtoano maalum wa kutafuta Timu ya 3 itakayojumuika na Wolverhampton Wanderers na Birmingham kuingia LIGI KUU msimu ujao, leo Timu ya Burnley imeifunga Reading bao 1-0. Reading ilishushwa Daraja kutoka LIGI KUU England msimu uliokwisha.
Timu hizi zitaruadiana Mei 12 na mshindi atachuana na mshindi kati ya Preston na Sheffield United ambazo jana zilitoka suluhu 1-1 na ambazo zinarudiana tarehe 11 Mei.
Mchezaji wa Cameroun, Andre Bikey, anaechezea Reading alipewa Kadi Nyekundu na Refa baada ya kumkanyaga kwa makusudi Robbie Blake wa Burnley.
Bikey alipopewa Kadi hiyo alikasirika sana na kuvua jezi na kuichana.
Bikey atakumbukwa sana kwenye mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika alileta aibu kubwa alipompiga Mhudumu wa Kwanza alieingia uwanjani kumsaidia Mchezaji alieumia katika Nusu Fainali kati ya Cameroun na Ghana ambayo Cameroun walishinda 1-0.