Wenger alia: 'Ni usiku mbaya maishani mwangu!!'
Mabingwa Watetezi wa Klabu Bingwa Ulaya, Manchester United, jana wamefanikiwa kuingia Fainali ya Kombe hilo kwa msimu huu baada ya kuwashindilia Arsenal mabao 3-1 uwanjani kwao Emirates katika mechi ya marudiano ya Nusu Fainali.Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Old Trafford, Manchester United walishinda kwa bao 1-0.
Mechi hii ya marudiano ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu sana hasa baada ya Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, kuwapa matumaini makubwa wapenzi wao kwamba watashinda mechi hii. Lakini, baada ya dakika 11 za kwanza tu za mechi, matumaini hayo yalizikwa pale Man U walipobandika bao mbili za haraka haraka ndani ya kipindi cha dakika tatu.
Bao la kwanza lilifungwa na Ji-Sung Park dakika ya 7 baada ya krosi ya Ronaldo kumfikia huku kila mtu akitegemea Beki Chipukizi wa Arsenal, Kieran Gibbs, angeunasa mpira huo lakini akateleza na mpira kumfikia Park aliemhadaa vizuri Kipa Almunia kwa shuti lake.
Bao la pili lilifungwa dakika ya 11 na Ronaldo alipofumua frikiki ya umbali wa mita kama 30 na kumbabaisha Kipa Almunia. Hadi mapumziko Man U walikuwa mbele kwa bao 2-0.Kipindi cha pili, kwenye dakika ya 60, Arsenal walipata kona na ilipopigwa Vidic akaokoa kwa kichwa na mpira kumkuta Ronaldo aliempasia Park kwa kisigo na haraka Park akampa Rooney ambae alimwona vizuri Ronaldo ameshachomoka kwa kasi kubwa kuelekea golini kwa Arsenal, na Rooney hakuchelewasha, akatoa pasi murua kwa Ronaldo aliepachika bao la 3. Hilo lilikuwa shambulio la haraka na kustukiza ambalo Wataalam huliita 'counter attack!!'.
Dakika ya 75, Manchester United wakapata mkosi pale Darren Fletcher alipotwangwa Kadi Nyekundu baada ya Refa toka Italia Roberto Rosetti kuuamua amemchezea madhambi Cesc Fabregas ndani ya boksi na pia kutoa penalti iliyofungwa na Robin van Persie. Lakini marudio ya tukio hilo yameonyesha dhahiri Fletcher aliucheza mpira. Kwa Kadi hiyo Fletcher haruhusiwi kucheza Fainali.
Baada ya mechi, Arsene Wenger, aliekuwa na majonzi makubwa alikiri walizidiwa na hasa mabao mawili ya mapema yaliwatia kiwewe. Wenger vilevile alikiri usiku wa jana ulikuwa mbaya sana katika historia yake ya Soka ya zaidi ya miaka 25.
Kwa kufungwa jana Arsenal wanaendeleza wimbi la kutokushinda Kikombe chochote tangu mwaka 2005 walipotwaa Kombe la FA baada ya kuifunga Man U kwa matuta.
Vikosi vilikuwa:
Arsenal: Almunia, Sagna, Toure, Djourou, Gibbs (Eboue 45), Walcott (Bendtner 63), Fabregas, Song Billong, Nasri, Van Persie (Vela 79), Adebayor. Akiba hawakucheza: Fabianski, Silvestre, Diaby, Denilson.
Kadi: Nasri, Adebayor, Eboue.
Goals: Van Persie 76 pen.
Man Utd: Van der Sar, O'Shea, Ferdinand, Vidic, Evra (Rafael Da Silva 65), Fletcher, Carrick, Anderson (Giggs 63), Park, Ronaldo, Rooney (Berbatov 66). Akiba hawakucheza: Kuszczak, Evans, Scholes, Tevez.
Kadi Nyekundu: Fletcher (75).
Watazamaji: 59,867
Refa: Roberto Rosetti (Italy).
No comments:
Post a Comment