Wednesday, 6 May 2009

Mchezaji Mikosi: Joey Barton!!!!!!

Jumapili iliyopita, Joey Barton, Kiungo wa Newcastle alichapwa Kadi Nyekundu baada ya kumrukia miguu miwili Xabi Alonso wa Liverpool katika mechi Liverpool waliyoshinda mabao 3-0 na kuzidi kuitosa Newcastle kwenye hatari ya kushushwa Daraja.
Kwa kosa la kupewa Kadi Nyekundu, Joey Barton atakosa mechi 3 lakini kwa vile Newcastle imabakiza mechi 3 kumaliza ligi msimu huu ina maana msimu wa Joey Barton umeshakwisha mapema.
Sakata la Joey Barton halikuisha hapo kwani baada ya mechi hiyo kwisha yeye na Meneja wake Alan Shearer nusura wapigane ngumi ndani ya vyumba vya kubadilishia jezi na sasa Klabu yake ya Newcastle imeamua kumsimamisha kwa muda usiojulikana.
Kwa Joey Barton hili si tukio la kwanza kwani Joey Barton ana mlolongo wa mikasa ambayo inaweza kutungiwa muvi na ikashinda kila tuzo.
Joey Barton, ambae ameichezea Timu ya Taifa ya England mara moja, alinunuliwa na Newcastle kutoka Manchester City ambao walilazimika kumuuza baada ya yeye kumpiga na kumuumiza vibaya Mchezaji mwenzake Ousmane Dabo mazoezini.
Wakati kesi ya Ousmane Dabo iko Mhakamani, Joey Barton akakamatwa uraiani kwa kumpiga na kumjeruhi mtu na kuhukumiwa kwenda jela miezi 6.
Akiwa kifungoni, hukumu ya kesi yake ya kumjeruhi Ousmane Dabo ikatoka na akabahatika kupata kifungo cha nje cha miezi minne.
Lakini kwa tukio la Ousmane Dabo, Joey Barton akapewa adhabu na FA, Chama cha Soka England, ya kufungiwa mechi 12 [alipunguziwa ikawa mechi 6 na 6 zikawekwa kiporo kuangaliwa mwenendo wake] na kupigwa faini Pauni Elfu 25.
Huko nyuma Joey Barton ashapatwa na mikasa kibao na baadhi ni:
-Msimu wa 2004/5 kwenye Pati ya Chrismas ya Klabu ya Manchester City, Joey Barton alimchoma jichoni na moto wa sigara Mchezaji wa Vijana wa Timu hiyo. Alinusurika kufukuzwa.
-2005, kwenye ziara ya kabla ya msimu kuanza ya Manchester City huko Thailand, Joey Barton alimkung'uta shabiki wa Everton kwenye baa ya hoteli waliyofikia. Joey Barton akapandishwa ndege kurudishwa England na Klabu ikampa adhabu nyingine.
Tangu ajiunge na Newcastle kutokea Manchester City mwaka 2007, Joey Barton amecheza mechi 26 tu na amekosa mechi nyingi ama kwa kuwa jela au kufungiwa na FA au kuwa majeruhi.
Msimu huu ameichezea Newcastle mechi 9 tu na hiyo mechi ya Jumapili waliyocheza na Liverpool na kupewa Kadi Nyekundu ilikuwa ni mechi yake ya kwanza tangu auumie Januari 28 mwaka huu.
Wadau wengi wanadhani huu ndio mwisho wake Joey kuichezea Newcastle na wengi wanahisi hakuna Klabu huko England inayoweza kumpokea. Gordon Taylor, Bosi wa PFA [Professional Footballers Association] yaani Chama Cha Wachezaji Soka wa Kulipwa, amewasiliana na Mchezaji huyo na amesema Joey Barton anatambua madhara ya sakata lake hili la mwisho. Gordon Taylor amesema: 'Joey anajua ile ilikuwa rafu mbaya na ameomba radhi kwa Alonso, Refa na Meneja wake. Muda unazidi kuyoyoma kwa Joey lakini watu hawana budi kumvumilia na kumsaidia. Maisha yetu yamejaa watu ambao siku zote unajiuliza kama watajifunza. Na hii ni kwa Joey pia lakini tunachoomba asaidiwe hadi maisha yake kimpira yatakapoisha.'

No comments:

Powered By Blogger