Wednesday 6 May 2009

Chelsea v Barcelona

Leo tena London inawaka moto na dunia nzima 'itakuwa huko jijini London' kushuhudia mechi ya marudiano ya Nusu Fainali Kombe la Klabu Bingwa Ulaya, UEFA CHAMPIONS LEAGUE, kati ya Chelsea na Barcelona huko Stamford Bridge nyumbani kwa Chelsea. Mechi hii itaanza saa 3 dakika 45 bongo taimu.
Mechi ya kwanza kati ya timu hizi iliyochezwa huko Nou Camp nyumbani kwa Barcelona iliisha 0-0 na leo lazima Chelsea ashinde ili kuingia Fainali kupambana na Mabingwa Watetezi wa Kombe hili, Manchester United, ambao jana waliwakung'uta Arsenal 3-1 huko Emirates Stadium, nyumbani kwa Arsenal.
Suluhu ya magoli ya aina yeyote ile itawapa mwanya Barcelona kuingia Fainali kwa vile wanacheza ugenini na mabao ya ugenini huhesabika mawili endapo timu zipo suluhu.
Chelsea leo watamkaribisha tena Beki wao wa pembeni kushoto Ashley Cole ambae aliikosa mechi ya kwanza kwa kuwa alikuwa na Kadi.
Lakini Barcelona ndio wenye pengo kubwa kwenye defense yao kwa kuwakosa Mabeki wao wawili wa kati, yaani sentahafu, kina Carles Puyol, mwenye Kadi, na Rafael Marques alie majeruhi. Inategemewa Gerrard Pique, Mchezaji Chipukizi wa zamani wa Manchester United, na Martin Caceres, toka Uruguay, wanaweza kuziba pengo hilo.
Hata hivyo, Barcelona wana wasiwasi mkubwa kuhusu kucheza kwa Mshambuliaji wao nyota Thierry Henry ambae aliumia goti siku ya Jumamosi Barcelona walipoibamiza Real Madrid 6-2. Henry jana alishindwa kufanya mazoezi na Barcelona wamesema leo atachekiwa ili kutoa uamuzi achezeshwe au la.
Meneja wa Chelsea, Guus Hiddink, akielezea kuhusu pambano la leo, alisema: 'Ushindi wao wa 6-2 kwa Real Madrid ni ubora wao. Sisi hatutishiki kwani kila mechi ni tofauti. Sisi tutacheza mpira wetu wa kawaida tu.'
Nae Meneja wa Barcelona, Pep Guardiola, amesema: 'Hatuwezi kushindana na Chelsea kwa mibavu kwani hio ndio staili yao. Itabidi tucheze staili yetu na staili yetu ni kumiliki mpira na kufunga magoli tu.'
Hii ni mechi ngumu isiyotabirika na iitakayokuwa na soka tofauti kwa kila Timu.
Kwa Chelsea, ni mechi muhimu sana hasa ukitilia maanani hawajawahi kuchukua Kombe hili na katika misimu 6 iliyopita wamefika Nusu Fainali mara 5 na msimu uliopita waliingia Fainali na kubwagwa na Manchester United waliotwaa Ubingwa.
Vikosi vitatokana:
Chelsea: Cech, Hilario, Belletti, Bosingwa, A Cole, Terry, Alex, Ivanovic, Lampard, Obi, Ballack, Essien, Kalou, Malouda, Drogba, Anelka, Stoch, Di Santo, Mancienne.
Barcelona: Victor Valdes, Pinto, Jorquera, Victor Sanchez, Caceres, Pique, Daniel Alves, Abidal, Sylvinho, Busquets, Iniesta, Hleb, Keita, Toure, Xavi, Eto'o, Messi, Henry, Gudjohnsen, Krkic, Pedro.

No comments:

Powered By Blogger