Wednesday, 6 May 2009

UEFA: 'KADI YA FLETCHER HAIFUTWI!!!'
UEFA, Chama cha Soka Ulaya, kimethibitisha Kiungo wa Manchester United, Darren Fletcher, ataikosa Fainali ya Klabu Bingwa Ulaya itakayochezwa huko Rome, Italy Mei 27 kati ya Klabu yake Manchester United na mshindi wa leo kati ya Chelsea v Barcelona, kwa sababu ya kupewa Kadi Nyekundu katika mechi ya jana Man U walipoiua Arsenal 3-1.
Fletcher alipewa Kadi Nyekundu dakika ya 75 baada ya Refa Roberto Rosetti kumdhania amemchezea rafu Cesc Fabregas wa Arsenal ndani ya boksi. Kwa kosa hilo, Refa huyo pia aliwapa Arsenal penalti waliyofunga bao lao moja.
Marudio ya video ya tukio hilo yalionyesha dhahiri Fletcher alicheza mpira na hivyo kupewa Kadi Nyekundu ni kosa. Hata Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, alikubali Refa alichemsha kwa uamuzi ule.
Baada ya mechi kulikuwa na dhana kuwa endapo Refa Roberto Rosetti ataandika kwenye ripoti yake ya mechi kuwa, baada ya kuliona tena tukio hilo, amegundua alifanya kosa na asingetoa Kadi Nyekundu, basi Fletcher atasamehewa na UEFA na hivyo kucheza Fainali.
Leo, UEFA imetangaza hairuhusiwi kukata rufaa yeyote kuhusu Kadi Nyekundu hata kama Refa anakubali kosa.
Taarifa ya UEFA ilifafanua: 'Manchester United wana haki ya kuleta malalamiko yao ndani ya saa 24 baada ya mechi. Lakini malalamiko hayo yanakubalika pale tu Refa akikubali kuwa alitoa Kadi, iwe Njano au Nyekundu, kwa Mchezaji mwingine kimakosa badala ya yule ambae kweli katenda kosa. Hamna Rufaa yeyote inayosikilizwa kuhusu maamuzi yeyote ya Refa. Kuhusu Fletcher hamna ushahidi wowote unaoonyesha Refa alimpa Kadi Nyekundu kwa makosa wakati aliecheza Rafu ni Mchezaji mwingine.'
Akieleza masikitiko yake, Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, amesema: 'Namheshimu Refa yule lakini ni juu yake kusema alikosea. Fletcher ni Mchezaji mkweli kabisa na kukosa Fainali ni mkosi mkubwa sana kwake!!'

No comments:

Powered By Blogger