Saturday 9 May 2009

Wababe Scotland wapambana leo: Rangers 1 Celtic 0

Huku kukiwa kumebakiwa mechi 3 tu kwa LIGI KUU Scotland kumalizika leo Rangers wamewafunga watani zao wa jadi Celtic bao 1-0 Uwanjani Ibrox, Glasgow na kuchukua uongozi wa ligi hiyo wakiwa na pointi 79 na Celtic wakifuatia wakiwa na pointi 77. Bao lililoinyuka Celtic lilifungwa na Davis dakika ya 37 na Davis huyo huyo akawa tena shujaa wa Rangers pale alipookoa mpira kwa kichwa kwenye mstari wa goli wakati Kipa wake keshapitwa.
Kabla ya mechi yao ya kesho, Wenger aikandya Chelsea!!!
Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal, ameiponda Chelsea kwa kuwaambia pesa hazinunui mafanikio na kauli hii imekuja huku Timu hizo zinategemewa kupambana hapo kesho jioni kwenye LIGI KUU England katika mechi inayozikutanisha Chelsea iliyo nafasi ya 3 na Arsenal nafasi ya 4 kwenye msimamo wa ligi.
Pia mechi ya kesho inazikutanisha Timu mbili zilizotolewa wiki hii kwenye Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE wakati Arsenal ilitupwa nje na Manchester United kwa jumla ya magoli 4-1, Chelsea ilibwagwa kwa goli la ugenini baada ya kutoka sare 1-1 na Barcelona.
Wenger ameiponda Chelsea kwa kusema: 'Chelsea wametumia mamilioni ya pesa lakini mpaka sasa hajashinda Kombe la Ulaya!! Si kutumia pesa tu bali ni lazima kuendeleza msimamo wa kukuza vipaji!! Sisi tunaweza kuendelea zaidi kwani tuna Wachezaji chipukizi lakini wao Wachezaji wao wanashuka mlima na sisi ndio kwanza tunapanda kilima!! Tumeingia nne bora huko Ulaya, hatujafungwa mechi yeyote ya LIGI KUU tangu Novemba!! Ndio tumefungwa kwenye Nusu Fainali ya Ulaya na si kitu cha kuona haya kwani tumefungwa na Timu bora!! Manchester United ni Mabingwa wa Ulaya na Dunia!!!'
Ovrebo, Refa wa Chelsea v Barcelona, asema hakujificha!!!

Refa Tom Henning Ovrebo, raia wa Norway, aliechezesha Nusu Fainali ya Chelsea na Barcelona ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE amekanusha taarifa zilizozagaa kuwa amejificha kwa kuwa anawindwa kuuliwa na Mashabiki wa Chelsea.
Refa huyo alizua mzozo mkubwa kuhusu maamuzi yake ya utata na mara baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo Wachezaji wa Chelsea walimzonga na kumkashifu kwa madai amewanyima penalti kadhaa.
Katika mechi hiyo Barcelona walisawazisha bao dakika za majeruhi na kuwatupa nje Chelsea kwa bao la ugenini.
Ovrebo amesema: 'Wikiendi ijayo nachezesha mechi huku Norway.'
Chelsea haimwadhibu Drogba!!

Meneja wa Chelsea, Guus Hiddink, ametamka kuwa Klabu yao haina nia ya kumpa adhabu yeyote Didier Drogba kwa utovu wa nidhamu alioufanya mara baada ya mechi ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE kati yao na Barcelona iliyomalizika 1-1 lakini Barcelona wakaingia Fainali kwa goli la ugenini.
Hiddink ametamka: 'Ndio ni makosa lakini hatumpi adhabu kwani ameshaomba radhi waziwazi. Tukimpiga faini haiwezi kumponya adhabu ya UEFA.'
Inasemekana Mwakilishi wa UEFA kwenye mechi hiyo, Janis Mezeckis kutoka Nchi ya Latvia ameandika kwenye ripoti yake kuhusu vitendo vyote vya Wachezaji wa Chelsea baada ya mechi hasa Drogba.
UEFA imeahidi kutoa tamko lao wiki ijayo.
ARSENAL NAO MATATANI NA UEFA!!!!

Kuna habari kwamba UEFA huenda ikaipiga faini Arsenal kufuatia vitendo vya baadhi ya Watazamaji uwanjani kwao Emirates kuonekana wakirusha chupa za plastiki za maji wakati Manchester United wakisherehekea bao la pili la Ronaldo katika pambano la Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE Jumanne iliyopita mechi ambayo Man U waliifunga Arsenal 3-1.
Inasemekana Refa wa pambano hilo Roberto Rosetti ameandika kwenye ripoti yake ya mechi hiyo kuhusu tukio hilo na sasa UEFA inategemewa kutoa tamko hapo Julai 23.
HOMA YA MAFUA YA KITIMOTO YAZITOA TIMU ZA MEXICO KWENYE COPA LIBERTADORES!!!

Klabu mbili za Mexico, Chivas Guadalajara na San Luis, zimelazimika kujitoa kwenye Kombe la Klabu Bingwa za Nchi za Marekani ya Kusini maarufu kwa jina la Copa Libertadores baada ya kukosa viwanja vya kuchezea mechi hizo kufuatia mlipuko wa gonjwa la ‘homa ya mafua ya kitimoto’ nchini Mexico ambako mpasa sasa watu 42 wamefariki.
Chivas Guadalajara walikuwa wawakaribishe Sao Paulo ya Brazil na San Luis walikuwa wawe wenyeji wa Nacional ya Uruguay.
Juhudi za mechi hizo kuchezwa nje ya Mexico ziligonga mwamba baada ya Serikali za Colombia na Chile kuvigomea Vyama vya Soka vyao kuwa wenyeji wa mapambano hayo kuogopa kuambukizwa gonjwa hilo.
Hivyo, Chama cha Soka cha Mexico kikawajulisha Shirikisho la Soka za Nchi za Marekani ya Kusini kujitoa kwa Timu zao.

No comments:

Powered By Blogger