Baada ya kuporomoshwa toka LIGI KUU England msimu wa 2007/8 na kukaa COCA COLA CHAMPIONSHIP kwa msimu mmoja tu, jana Birmingham wakicheza ugenini Madejski Stadium waliwafunga wenyeji wao Reading mabao 2-1 na kumudu kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, hivyo kupandishwa kwenda LIGI KUU, wakiwa nyuma ya Mabingwa wa Ligi hiyo Woverhampton Wanderers, maarufu kama Wolves, ambao nao wamepanda Daraja kwenda LIGI KUU. Timu nyingine iliyokuwa inawania kuipuka Birmingham ili kupanda Daraja hapo jana ilikuwa Sheffield United lakini ikakwaa kisiki pale ilipotoka sare 0-0 na Crystal Palace. Hata hivyo, ingawa Reading na Sheffield United zimekosa nafasi ya kupanda Daraja moja kwa moja, kwa kumaliza Ligi nafasi za 3 na ya 4, zitaingia kwenye kapu pamoja na Burnley iliyomaliza ya 5 na Preston ya 6, katika mtoano maalum wa kutafuta Timu moja kuungana na Wolves na Birmigham kupanda Daraja. Timu 3 za mwisho toka LIGI KUU England zitashushwa Daraja kwenda COCA COLA CHAMPIONSHIP kuchukua nafasi ya hizo 3 zilizopanda.
Newcastle na Sunderland zafungwa, hali ni ya hatari kwao!!!! Liverpool ashinda na kujipa matumaini ya Ubingwa endapo Man U atateleza!!
Jana, Timu ya Liverpool, ikiwa Anfield, iliibamiza bila huruma Newcastle mabao 3-0 na kujiongeza matumaini ya kutwaa Ubingwa endapo Man U atateleza lakini ushindi huo umezidi kuididimiza Newcastle katika balaa la kushushwa Daraja.
Wakati Liverpool ikijichimbia nafasi ya 2 wakiwa na pointi 77 kwa mechi 35 huku Man U akiendelea kuongoza kwa pointi 80 mechi 34, Newcastle wamechimbiwa nafasi ya 18 wakiwa na pointi 31 sawa na Middlesbrough walio nafasi ya 19. West Brom wako nafasi ya 20 na ya mwisho wakiwa na pointi 28.
Timu hizi tatu, Newcastle, Middlebrough na West Brom, ndizo zimekalia kuti kavu kwani zipo kwenye nafasi za timu zitakazoporomoka Daraja.
Juu yao kwenye nafasi ya 17 yuko Hull City mwenye pointi 34 lakini amecheza mechi moja pungufu mechi ambayo anaicheza leo usiku na Aston Villa.
Liverpool, wakicheza bila ya shujaa wao Fernando Torres lakini wakimkaribisha shujaa mwingine, Nahodha Steven Gerrard aliekosa mechi kadhaa kwa kuwa majeruhi, walipata ushindi huo wa mabao 3-0 kupitia kwa Yossi Benayoun, dakika ya 22, Kuyt [28] na Lucas[87].
Sunderland, wakicheza nyumbani, walipigwa mabao 2-0 na Everton na hivyo kubakizwa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 35 kwa mechi 35 [pointi moja tu juu ya Hull City waliocheza mechi moja pungufu] na wako pointi 4 tu juu ya Timu zilizo eneo la kushushwa Daraja huku kukiwa kumesaliwa mechi 3 Ligi kumalizika.
RATIBA LIGI KUU England:[saa za bongo]
Jumatatu, 4 Mei 2009
[saa 4 usiku] Aston Villa v Hull City
Jumamosi, 9 Mei 2009
[saa 11 jioni]
Blackburn v Portsmouth
Bolton v Sunderland
Everton v Tottenham
Fulham v Aston Villa
Hull City v Stoke City
West Brom v Wigan
[saa 1 na nusu usiku]
West Ham v Liverpool
Jumapili. 10 Mei 2009
[saa 9 na nusu mchana]
Man U v Man City
[saa 12 jioni]
Arsenal v Chelsea
Jumatatu, 11 Mei 2009 [saa 4 usiku]
Newcastle v Middlesbrough
Jumatano, 13 Mei 2009
[saa 4 usiku]
Wigan v Man U [HII NDIO ILE MECHI YA KIPORO YA MAN U YA MUDA MREFU]
No comments:
Post a Comment