Saturday, 9 May 2009

Ferguson, Arshavin ndio BORA Aprili!!!

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ameshinda Tuzo ya Meneja Bora wa LIGI KUU kwa mwezi Aprili na Mchezaji wa Arsenal, Andrey Arshavin, ametunukiwa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Aprili kwa ligi hiyo.
Sir Alex Ferguson ameshashinda Tuzo ya Meneja Bora jumla ya mara 23 na kwa msimu huu hii ni mara yake ya pili baada ya kushinda mwezi Januari. Ferguson amepata Tuzo hii baada ya kuiongoza vizuri Manchester United kushinda mechi 4 za ligi kati ya 4 walizocheza mwezi Aprili na kuwafanya wajizatiti kileleni mwa LIGI KUU. Nazo ni ile waliyoifunga 3-2 Aston Villa, Sunderland wakafungwa 2-1, Portsmouth 2-0 na kile kipigo cha 5-2 walichowashushia Totenham.
Andrey Arshavin amepewa Tuzo ya Mchezaji Bora baada ya kufunga goli 5 katika mechi 4 alizochezea Arsenal mwezi Aprili.
Mrusi Arshavin atakumbukwa aliifungia Arsenal mabao yao yote manne katika sare ya 4-4 na Liverpool katika mwezi huo.
Kindumbwendumbwe cha kuingia LIGI KUU: Preston 1 Sheffield United 1
Katika mtoano maalum wa kutafuta Timu ya 3 itakayojumuika na Wolverhampton Wanderers na Birmingham kuingia LIGI KUU msimu ujao, Timu za Preston na Sheffiled United zimetoka sare ya bao 1-1.
Timu hizi zitaruadiana Mei 11 na mshindi atachuana na mshindi kati ya Burnley na Reading ili kupata Timu moja itakayopanda Daraja.
Jumamosi Mei 9, Burnley watawakaribisha Reading katika mechi ya kwanza na marudiano ni Mei 12 huko nyumbani kwa Reading.
UEFA KUTOA UAMUZI HATMA YA CHELSEA NA WACHEZAJI WAKE WIKI IJAYO!!!
UEFA, Chama cha Soka Ulaya, kimetoa tamko kuwa watatoa uamuzi wa hatua zitakazochukuliwa wa ama kuwaadhibu Chelsea na baadhi ya Wachezaji wake au la wiki ijayo kufuatia vitendo vyao vya kumzonga na kumkashifu Refa kutoka Norway Tom Henning Ovrebo baada ya mechi ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Barcelona kwa madai kuwa aliwanyima takriban penalti 4 za wazi.
Pambano hilo liliisha bao 1-1 baada ya Andres Iniesta kuisawazishia Barcelona dakika za majeruhi na hivyo kuipa Barcelona ushindi kwa bao la ugenini.
Mara baada ya kipyenga cha mwisho, Wachezaji wa Chelsea hasa John Terry, Michael Ballack na Didier Drogba walimzonga Refa na Drogba akasikika akifoka na kutoa kashfa huku akizuiwa na Walinzi. Pia, Mchezaji mwingine, Jose Bosingwa, alikaririwa na vyombo vya habari akimwita Refa huyo 'mwizi'.
Hata hivyo Klabu ya Chelsea pamoja na Drogba na Bosingwa wameomba radhi kwa vitendo vyao.
Vilevile, UEFA imethibitisha haikupokea Rufaa yeyote kutoka kwa Barcelona ndani ya Masaa 24 kama kanuni zinavyotaka kuhusu Kadi Nyekundu ya Mchezaji wa Barcelona Eric Abidal na hivyo hawezi kucheza Fainali ambayo Barcelona watakutana na Mabingwa Watetezi Manchester United huko Rome Mei 27.
Thierry Henry huenda asicheze Fainali na Manchester United!!!
Klabu ya Barcelona imetangaza kuwa kuna wasiwasi mkubwa wa Mchezaji wao Thierry Henry, miaka 31, kutocheza Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE huko Rome Mei 27 watakapokutana na Mabingwa Watetezi Manchester United baada ya kuumia goti.
Henry hakucheza mechi ya Nusu Fainali huko Stamford Bridge walipotoka sare 1-1 na Chelsea na imethibitika hatocheza mechi ya Fainali ya Kombe la Spain ambayo Barcelona watakutana na Athletic Bilbao Jumatano ijayo. Vilevile atazikosa mechi 3 za La Liga ambazo Barcelona wamebakisha.
Thierry Henry aliumia Jumamosi iliyopita kwenye mechi Barcelona waliyoikung'uta Real Madrid mabao 6-2 huku Henry akipachika bao 2 na alitolewa kwenye dakika ya 60 baada ya kuumia.

No comments:

Powered By Blogger