Saturday 10 April 2010

FA Cup: Chelsea wako Fainali!!
• Chelsea 3 Villa 0
Chelsea leo wametinga Fainali ya Kombe la FA walipoichapa Aston Villa bao 3-0 na bao zote zilifungwa kipindi cha pili.
Fainali hiyo itafanyika Uwanja wa Wembley Mei 15 na Chelsea watakutana na Mshindi wa mechi ya kesho kati ya Tottenham na Portsmouth.
Villa walitawala mechi hii kipindi cha kwanza na ilionekana wazi Refa Webb amewanyima penalti ya wazi kwenye dakika ya 17 pale Mikel Obi alipomwangusha Agbonlahor ndani ya boksi.
Kipindi cha pili Chelsea walibadilika na kutawala na kona yao ya dakika ya 67 iliokolewa kizembe na Villa na kumkuta John Terry alieupiga mpira golini na kumfikia Didier Drogba aliefunga.
Dakika ya 89, krosi nzuri toka wingi ya kulia ya Michael Ballack ilimpata Malouda aliemalizia na kufunga.
Chelsea walipata bao la 3 dakika za majeruhi Mfungaji akiwa Frank Lampard kufuatia kaunta ataki iliyowahusisha Malouda na Anelka aliemsogezea Lampard.
Vikosi vilivyoanza:
Aston Villa: Friedel, Cuellar, Dunne, Collins, Warnock, Ashley Young, Milner, Petrov, Downing, Agbonlahor, Carew.
Akiba: Guzan, Luke Young, Sidwell, Delfouneso, Delph, Heskey, Beye.
Chelsea: Cech, Paulo Ferreira, Terry, Alex, Zhirkov, Deco, Mikel, Lampard, Joe Cole, Drogba, Malouda.
Akiba: Hilario, Ivanovic, Ballack, Kalou, Sturridge, Belletti, Anelka.
Refa: Howard Webb
LIGI KUU LEO: Pompey washuka Daraja!!!
West Ham 1 Sunderland 0
Bila ya kucheza mechi ya Ligi Kuu na kesho wakiwa Wembley kucheza Nusu Fainali ya FA Cup kwa kuivaa Tottenham, Portsmouth leo imekuwa Klabu ya kwanza Msimu huu kuporomoka Daraja kutoka Ligi Kuu baada ya West Ham kuifunga Sunderland bao 1-0.
Bao la dakika ya 51 la Mbrazil Ilan ndilo lililowapa ushindi West Ham wakiwa nyumbani Upton Park na kuwapa pointi 3 muhimu zinazowafanya washika nafasi ya 16 wakiwa na pointi 31 kwa mechi 34.
Chini yao wapo Wigan wamecheza mechi 33 wana pointi 31 na zile Timu 3 za mkiani zilizo eneo la kushushwa Daraja ni Burnley mechi 34 pointi 27, Hull mechi 33 pointi 27 na Pompey mechi 33 pointi 14.
Vikosi vilivyoanza:
West Ham: Green, Faubert, da Costa, Upson, Spector, Stanislas, Kovac, Behrami, Noble, Cole, Ilan.
Akiba: Kurucz, Gabbidon, Franco, McCarthy, Diamanti, Daprela, Spence.
Sunderland: Gordon, Ferdinand, Da Silva, Turner, Richardson, Henderson, Meyler, Cattermole, Malbranque, Bent, Campbell.
Akiba: Carson, Bardsley, Hutton, Zenden, Jones, Kilgallon, Mwaruwari.
Refa: Michael Jones
Hull City 1 Burnley 4
Bao la kipindi cha kwanza la Martin Paterson, bao mbili za penalti za Graham Alexander na frikiki ya Wade Elliott imewafanya Burnley waibuke na ushindi wa bao 4-1 ugenini baada ya kutanguliwa kufungwa bao na Hull City alilofunga Kevin Kilbane baada ya dakika mbili tu za mchezo.
Ushindi huu umeifanya Burnley waipite Hull kimsimamo kwa tofauti ya magoli zote zikiwa na pointi sawa lakini Hull wamecheza mechi moja pungufu lakini Timu zote hizo mbili badi zipo kwenye zile Timu 3 za mwisho.
Vikosi vilivyoanza:
Hull: Myhill, McShane, Sonko, Mouyokolo, Dawson, Mendy, Boateng, Bullard, Kilbane, Fagan, Altidore.
Akiba: Duke, Barmby, Geovanni, Folan, Marney, Vennegoor of Hesselink, Cairney.
Burnley: Jensen, Mears, Duff, Cort, Fox, Alexander, Paterson, Cork, Elliott, Nugent, Steven Fletcher.
Akiba: Weaver, Carlisle, Caldwell, Blake, Bikey, Thompson, Eagles.
Refa: Martin Atkinson
WBA yarudi tena Ligi Kuu!!!
  • Waungana na Newcastle Ligi Kuu
Baada ya kuporomoshwa Daraja Msimu uliokwisha, West Bromwich Albion leo imeungana na Newcastle kupanda na kurudi Ligi Kuu baada ya kuifunga Doncaster bao 3-2 kwenye mechi ya Ligi ya Coca Cola Championship huku Ligi hiyo ikiwa bado imebakisha mechi kadhaa kumalizika.
Newcastle ndio inayoongoza Ligi hiyo ya Coca Cola Championship na ilijihakikishia kurudi Ligi Kuu wiki iliyopita na leo imekuwa zamu ya WBA ambao wanashikilia nafasi ya pili kwenye Ligi hiyo.
Timu mbili za juu za Ligi ya Coca Cola Championship ndizo zinapandishwa moja kwa moja Daraja kwenda Ligi Kuu na Timu zilizo nafasi ya 3 hadi ya 6 zinapangiwa Michuano maalum kuipata Timu moja inayoungana na Timu hizo mbili za kwanza kupanda Daraja.
Fergie atoboa kuhusu Chicharita
Bosi wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amezungumzia jinsi walivyomtambua Mchezaji kutoka Mexico, Javier Hernandez aka Chicharita, miaka 21, na kuamua kumsajili.
Ferguson amesema: “Oktoba mwaka jana tulipata ripoti zake na Skauti wetu mmoja akaenda Mexico mwezi Desemba na kutazama mechi kadhaa. Ripoti yake ilikuwa nzuri. Wakati ule tulifikiria bado ni mdogo na tusubiri lakini akachaguliwa Timu ya Taifa. Sasa tatizo likaja, je akienda Kombe la Dunia na kufanya vizuri tunaweza kumpoteza!”
Ferguson akaelezea kuwa wakaamua kumpeleka Skauti wao Mkuu, Jim Lawlor, huko Mexico na akakaa wiki 3 kumchunguza Chicharita.
Katika wiki hizo tatu, Jim Lawlor, alimshuhudia Chicharita akiichezea Timu ya Taifa ya Mexico mara mbili na Klabu yake Chivas mara moja na katika mechi zote hizo alikuwa akifunga magoli.
Ingawa Chicharita si jina linalojulikana, Ferguson amesema: “Huwa tunapenda kufanya dili kama hizi. Huwa tunavitambua vipaji na kuviendeleza. Tuna uzoefu na hilo. Na tunapenda kusajili Wachezaji wa namna hiyo!”
FIFA yakamatia Watu kununua Tiketi Bondeni
FIFA imeanzisha kampeni kamambe huko Afrika Kusini ili Mashabiki wa Nchi hiyo wanunue Tiketi 500,000 ambazo hazijauzwa za mechi za Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 11 na kwisha Julai 11.
Ni mechi ya Fainali tu ya hapo Julai 11 ambayo ndio Tiketi zote zimeuzwa.
Waandaaji wa Mashindano hayo wamekiri kuwa limefanyika kosa kutegemea mauzo kwa njia ya Mtandao katika Nchi ambayo desturi yake ni kununua Tiketi kwenye siku ya pambano.
Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valckle, amesema: “Tunataka kuionyesha Dunia kuwa Viwanja vinajaa.”
Msimamizi Mkuu wa Mashindano hayo, Danny Jordaan kutoka Afrika Kusini, amesema vituo 11 katika Miji 9 itakayokuwa na mechi vimeanzishwa ili kuuza Tiketi kwenye kaunta.
Tiketi 100,000 zitauzwa kwa Watu wa Afrika Kusini kwa bei ya ‘chee’ ya Dola 20 kwa Tiketi moja kiwango ambacho ni cha chini mno kwa Viwango vya Kombe la Dunia.
Takwimu zimeonyesha USA ndio inaongoza kwa ununuzi wa Tiketi ikiwa imenunua Tiketi 118,945, Uingereza imenunua Tiketi 67,000 na Ujerumani Tiketi 32,269.
FA CUP: Pompey wapo Wembley licha ya mabalaa kibao!!
Jumapili, Portsmouth wanaingia Uwanja wa Wembley kucheza Nusu Fainali ya Kombe la FA na Tottenham wakiwa Klabu tofauti kabisa na ile ya mwaka 2008 iliyoingia Wembley na kutwaa Kombe hilo kwa kuifunga Cardiff City bao 1-0, bao alilofunga Nwankwo Kanu huku Meneja wa Timu akiwa Harry Redknapp.
Portsmouth ya sasa ni Klabu iliyobomoka kwa madeni na katika miezi 9 iliyopita imekuwa ikibadili Wamiliki kila kukicha, ipo mkiani Ligi Kuu na huenda ikawa tayari imeshashuka Daraja hiyo Jumapili ikiwa Hull City na West Ham zinazocheza mechi za Ligi Kuu Jumamosi zikishinda mechi zake.
Portsmouth inakutana na Tottenham kwenye Nusu Fainali ya FA Cup ambayo inaongozwa na aliekuwa Meneja wao Harry Redknapp na mbali ya hilo Klabu hizi mbili zinajuana fika kwa vile Portsmouth inao Wachezaji wanne waliowahi kuichezea Tottenham na Tottenham pia inao Wachezaji wanne waliowahi kuichezea Portsmouth.
Lakini si Wachezaji wote hao wanane watacheza Jumapili.
Jamie O’Hara hawezi kuichezea Portsmouth kwani yupo hapo kwa mkopo akitokea Tottenham.
Younes Kaboul yupo Tottenham lakini ashacheza Portsmouth mechi za awali za Kombe hili Msimu huu na hivyo haruhusiwi kucheza.
Nwankwo Kanu aliefunga bao la ushindi na kuwapa Pompey Kombe la FA mwaka 2008 ni mmoja wa Wachezaji wanne waliocheza Fainali hiyo ambao bado wapo Portsmouth.
Wengine ni Kipa David James, Hermann Hreidarsson na John Utaka.
Kanu alizungumza na kusema itawabidi Wachezaji kujituma kwa zaidi ya asilimia mia moja ili kushinda Kombe la FA kwani ni kitu pekee cha kuwapa Mashabiki wao kwa uvumilivu wao na sapoti yao licha ya matatizo makubwa ndani ya Klabu.
Hata hivyo Kanu amekiri Tottenham, kwa mtazamo wa wengi, ndio wenye nafasi kubwa ya ushindi.
Wiki mbili zilizopita, Tottenham iliifunga Portsmouth 2-0 kwenye Ligi Kuu.
FA CUP: Aston Villa v Chelsea
Leo Chelsea inaivaa Aston Villa Uwanjani Wembley, Timu ambayo wiki mbili zilizopita waliiwasha bao 7-1 kwenye Ligi Kuu, kwenye Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la FA na Nusu Fainali nyingine itachezwa kesho hapo Wembley kati ya Portsmouth na Tottenham.
Fainali itakuwa pia Uwanjani Wembley Mei 15.
Wiki mbili zilizopita, Uwanjani Stamford Bridge, Chelseaa ilitwanga Aston Villa 7-1 na Frank Lampard alipiga bao 4 peke yake.
Lakini Nahodha wa Chelsea, John Terry, ametahadharisha: “Hii itakuwa mechi tofauti kabisa. Villa wamekasirika kufungwa 7 na safari hii watakuwa na Wachezaji wao ambao hawakucheza mechi ile.”
Na Meneja wa Aston Villa, Martin O’Neill, amesema Timu yake ina nia ya kufika Fainali yao ya pili Msimu huu na kufanikiwa baada ya kufungwa kwenye Fainali ya Kombe la Carling na Manchester United bao 2-1 mwezi Februari.
Aston Villa na Chelsea zimeshakutana mara 140 na Villa wameshinda mara 55 na Chelsea mara 52.
Vikosi vinavyotarajiwa kuanza:
Aston Villa (Fomesheni 4-4-2): Friedel; Cuéllar, Dunne, Collins, Warnock; A Young, Petrov, Downing, Milner; Carew, Agbonlahor.
Chelsea (Fomesheni 4-3-3): Cech; Ferreira, Alex, Terry, Zhirkov; J Cole, Ballack, Lampard; Anelka, Drogba, Malouda.
Refa: Howard Webb [amechezesha mechi 34, Kadi Nyekundu 4, Kadi za Njano 123]
Wasaidizi wa Refa: Mike Mullarkey na Darrren Cann
Refa wa Akiba: Mark Clattenburg
Ronaldo akata tamaa Brazil
Mkongwe na Supastaa Ronaldo, anaeongoza kwa ufungaji wa jumla ya mabao mengi katika Fainali za Kombe la Dunia akiwa na bao 15, amekiri kuwa hawezi kuchukuliwa na Brazil kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini.
Ronaldo, miaka 33, siku hizi anachezea Klabu ya Corinthians huko Brazil na mara ya mwisho kuichezea Brazil ni Robo Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2006 walipotolewa na Ufaransa na hiyo ilkuwa mechi yake ya 97 kuichezea Brazil na kufunga jumla ya bao 62 kwa Timu hiyo.
Ronaldo amesema: “Nimecheza mechi chache Msimu huu hivyo sistahili kuichezea Brazil, hilo ni wazi! Lakini nikiitwa ntaitika-Brazil ni Nchi yangu!”
Fergie atetea kuwabwatia Bayern
Sir Alex Ferguson amegoma kuufuta usemi wake ‘hii ni tabia halisi ya Wajerumani’ alioutoa baada ya Bayern Munich kuitoa Manchester United kwa mabao ya ugenini siku ya Jumatano na kauli hiyo inafuatia lawama zake kwa Wachezaji wa Bayern Munich kwa kumshinikiza Refa Nicola Rizzoli kutoka Italia ili ampe Chipukizi toka Brazil Rafael Kadi na Refa huyo kweli akamlamba Kadi ya pili ya Njano na kuifanya Manchester United icheze mtu 10 kwa dakika 40 za kipindi cha pili na kutoa mwanya kwa Bayern kupata bao muhimu la pili lililowapeleka Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Ferguson alibwata mara baada ya mechi: “Kulikuwa hamna kipingamizi sisi kushinda tukiwa 11, wao walikuwa wamezidiwa! Lakini Rafael alionyesha uchanga wake na wao wakalazimisha atolewe! Kila Mchezaji wao alimkimbilia Refa- hii ni tabia halisi ya Wajerumani!”
Kocha wa Bayern Munich, Louis van Gaal, na Rais wake, Uli Hoeness, walikerwa na kauli hiyo na sasa Ferguson ameamua kuweka mambo sawa bila ya kufuta kauli yake.
Ferguson amedai jazba ilimtawala kwani alitoa kauli hiyo mara tu baada ya mechi lakini amesema wa kulaumiwa zaidi ni Wajerumani wenyewe kwa kumshikiza Refa wakijua Rafael tayari ana Kadi ya Njano.
Allardyce agoma kumsaidia Rafikiye Fergie
Meneja wa Blackburn Rovers, Sam Allardyce, majuzi alikuwa pamoja na Rafiki yake Sir Alex Ferguson walipokwenda pamoja huko Aintree kuangalia Mbio za Farasi na akanufaika pale Ferguson alipombonyeza aweke dau kwa Farasi aitwae “What a Friend” anaemilikiwa na Ferguson na kweli Farasi huyo akashinda na Allardyce akaambua kitita ambacho hakikutajwa.
Jumapili, Backburn inaikaribisha Manchester United huko Ewood Park katika mechi ya Ligi Kuu mbayo ni muhimu sana kwa Manchester United walio pointi mbili nyuma ya vinara Chelsea kwani ushindi utawarusha juu ya Chelsea ambao wikiendi hii hawachezi Ligi na wako kwenye Nusu Fainali ya FA Cup.
Allardyce amesema: “Ilikuwa siku nzuri huko Aintree na Ferguson kutubonyeza kumenifanya mimi na Wafanyakazi wengine wa Blackburn tupate vijisenti mfukoni! Lakini hilo haliwasaidii Man United Jumapili! Hii ni dabi ya Timu za Kaskazini na sisi tukiwa Ewood Park tunaweza kucheza na Timu bora- kama tulivyowaonyesha Chelsea [sare 1-1]!”
LIGI KUU: TATHMINI MECHI ZA WIKIENDI
Ratiba ya Wikiendi
Jumamosi, 10 Aprili 2010
[saa 11 jioni]
Hull v Burnley
West Ham v Sunderland
Jumapili, 11 Aprili 2010
[saa 8 mchana]
Wolves v Stoke
[saa 9 na nusu mchana]
Blackburn v Man United
[saa 11 jioni]
Liverpool v Fulham
[saa 12 jioni]
Man City v Birmingham
------------------------------------------------------------
Wikiendi hii kuna mechi 6 tu na Jumamosi ni siku muhimu mno kwa Portsmouth wanaotegemewa kushushwa Daraja hasa baada ya kuporwa na Ligi Kuu pointi 9 na umuhimu huo kwa Portsmouth, ambao hawachezi mechi ya Ligi Kuu wikiendi hii na badala yake wapo Wembley Jumapili kucheza na Tottenham kwenye FA Cup, ni ule ukweli kwamba ikiwa Hull City wataifunga Burnley na West Ham kuifunga Sunderland, Portsmouth watajihakikishia kushuka Daraja na kucheza Ligi ya Coca Cola Championship Msimu ujao.
Hull City v Burnley
Timu zote hizi mbili zipo kwenye zile Timu 3 za mkiani zilizo hatarini kuporomoka Daraja huku Hull City wakiwa nafasi ya 18 pointi tatu juu ya Burnley na wana mechi moja mkononi.
Hull kidogo wanakuwa na nguvu wakiwa nyumbani na hilo linawapa matumaini makubwa ukichukulia pia katika mechi ya mwisho Burnley walidundwa bao 6-1 na Manchester City.
West Ham v Sunderland
West Ham walijitutumua mechi iliyopita na kutoka sare ugenini walipocheza na Everton na matokeo mazuri kwao katika mechii ni kitu cha lazima hasa kwa vile wako pointi moja tu juu ya zile Timu 3 zilizo hatarini kuporomoshwa Daraja.
Sunderland wako kwenye ari kubwa baada ya kuipiga Tottenham 3-1 mechi iliyopita na wapo pointi mbili tu kufikisha pointi 40 ambazo Meneja wao Steve Bruce anategemea wakizifikisha watapona kuwemo balaa la kushushwa Daraja.
Blackburn v Man United
Man United watakuwa Ewood Park huku wakitaka pointi 3 ili wakwae kilele kwa vile Chelsea hawachezi Ligi hadi Jumanne kwa vile wanacheza FA Cup na Aston Villa siku ya Jumamosi.
Lakini Blackburn ni wagumu kufungika kwao na wamefungwa mechi moja tu katika 15 zilizochezwa Uwanjani kwao Ewood Park.
Wolves v Stoke City
Wolves wako pointi 5 juu ya zile Timu 3 za mwisho na walipata bahati mbaya kukosa pointi katika mechi yao ya mwisho walipofungwa na Arsenal 1-0 dakika za mwishoni.
Stoke kidogo wako nafasi ahueni na wanatoka kwenye ushindi wa mechi mbili mfululizo.
Liverpool v Fulham
Liverpool wanawakaribisha Fulham Uwanjani Anfield huku Timu zote hizo zikiwa zinatoka kwenye mafanikio ya kuingia Nusu Fainali ya EUROPA LIGI waliposhinda mechi zao siku ya Alhamisi.
Ingawa Liverpool wanadai bado wanapigania kuitwaa nafasi ya 4 ya Ligi na hivyo kucheza UEFA Msimu ujao, ukweli ni kwamba wapo nafasi ya 6 pointi 4 nyuma ya Manchester City walio nafasi hiyo ya 4 na ambao pia wana mechi moja mkononi.
Ikiwa wanataka kuweka uhai matumaini yao ni lazima Liverpool waifunge Fulham.
Man City v Birmingham
Ni muhimu kwa Man City walio nafasi ya 4 washinde mechi hii ili waijengee zege nafasi hiyo ya 4 kwenye Ligi na kuweka pengo la pointi 4 kati yao na Tottenham walio nafasi ya 5.
Birmingham wako salama kwenye Ligi Kuu wakiwa nafasi ya 9 lakini hawajashinda katika mechi 5 sasa na katika mechi hii watamkosa Kipa wao nambari wani, Joe Hart, ambae haruhusiwi kucheza mechi hii kwa vile ni Mchezaji wa Man City na yupo Birmingham kwa mkopo.

Friday 9 April 2010

Van Persie aanza zoezi
Straika mahiri wa Arsenal Robin van Persie karibuni atarejea uwanjani baada ya kuwa nje kwa miezi minne akiuguza enka aliyoumia mwezi Novemba akiichezea Uholanzi kwenye mechi ya kirafiki na Italia.
Van Persie tayari ameshaanza mazoezi na sasa anaweza hata kucheza mpira na anategemewa kuingia mazoezini na Kikosi cha kwanza muda si mrefu.
Vile vile, Arsenal imesema majeruhi wengine, Johan Djouroa na Kieran Gibbs, wanakaribia kuanza mazoezi.
Djourou yuko nje tangu Septemba baada ya kuumia goti na Gibbs alivunjika mfupa wa kidole cha mguu kwenye mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI Arsenal walipocheza na Standard Liege mwezi Novemba.
Kesho EL CLASICO ndani ya EL SANTIAGO BERNABEAU: Real Madrid v Barcelona
Ni mechi inayongojewa kwa hamu kubwa, ni mechi ambayo itaamua nani anachukua uongozi wa La Liga ‘jumla’ kwa vile Timu zote zimefungana zikiwa na pointi 77 ingawa Real ndie yuko mbele kwa tofauti ya goli moja tu.
El Clasico itachezwa El Santiago Bernabeau nyumbani kwa Real Madrid ambako Msimu uliokwisha katika mechi kama hii Barcelona iliifumua Real bao 6-2.
Katika mechi 3 za mwisho, Barca imeifunga Real mechi zote hizo ikiwemo ile ya kwanza ya La Liga Msimu huu kwa bao 1-0 ambalo Zlatan Ibrahomivc alipachika lakini safari hii huenda Ibrahimovic asicheze kwa vile ni majeruhi.
Wengi wanaitangaza mechi hii kama ni Mashindano yanayowakutanisha Wachezaji Bora Duniani Cristiano Ronaldo wa Real na Lionel Messi wa Barca na hili limepamba moto hasa baada ya Messi kuiangamiza Arsenal kwa kufunga bao zote 4 katika mechi ya Jumanne iliyopita.
Baada ya kuikosa mechi ya Arsenal kwa kuwa kifungoni, Masentahafu wa Barca, Carles Puyol na Gerrard Pique, wote watakuwepo dimbani.
Real watamkosa Supastaa Kaka ambae anauguza musuli za pajani na pia huenda Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Xabi Alonso, asiichezee Real kwa vile ana tatizo la musuli.
KWA UFUPI TU:
-Reina asaini Mkataba mpya
Kipa wa Liverpool, Pepe Reina, amesaini Mkataba mpya na utamweka Anfield hadi 2016.
Reina, miaka 27, alijiunga na Liverpool mwaka 2005 akitokea Villareal na mpaka sasa ameshaichezea Liverpool mechi 250.
Reina alianza Soka lake akichezea Timu ya Vijana ya Barcelona na Ukipa ameurithi toka kwa Baba yake Mzazi ambae alikuwa Kipa wa Barcelona na Atletico Madrid.
-Fergie kimya kuhusu kumsajili Villa
Sir Alex Ferguson amegoma kuingizwa kwenye uvumi kuwa Manchester United imekubaliana na Straika wa Spain David Villa ajiunge nao Msimu ujao.
Man United tayari imeshasaini Wachezaji wawili kwa ajili ya Msimu ujao, nao ni Chris Smalling kutoka Fulham na Mchezaji toka Mexico Javier ‘Chicharita’ Hernandes.
Majina ambayo yamezagaa kuwa yatatua Old Trafford ni Frank Ribery, Karim Benzema na David Villa.
Ferguson ametamka: “Ni suala la kupata Mchezaji atakaetuboresha au kutufanya tusiporomoke tulipo. Huo ndio mwongozo wetu siku zote. Kila Msimu kunakuwepo uvumi. Msimu uliokwisha ni Ribery na Benzema ingawa kweli Benzema tulitoa ofa. Sasa ni David Villa! Nina hakika mpaka mwishoni mwa Msimu Majina yanayovumishwa yatafika hata nusu dazeni!”
-Sagna ataka Plani B Arsenal
Beki Bacary Sagna ameitaka Klabu yake Arsenal iwe na mkakati wa kuwa na staili ya pili pale wanaposhindwa kuzishinda Timu kwa kutmia staili yao ya ‘Soka Tamu’ ya kumiliki mpira na kupasiana hadi kwenye mstari wa golini.
Siku ya Jumanne, Arsenal walipelekwa darasani na kufundishwa jinsi ‘Soka Tamu’ linavyochezwa walipotua Uwanja wa Nou Camp na kukutana na Vigogo wa ‘Soka Tamu’ Barcelona walioongozwa na Mchawi Lionel Messi aliewafunga bao 4 mguuni mwake.
Sagna amesema: “ Nadhani kuna wakati tunamiliki na kuuchezea mpira kupindukia! Hatufikirii nini bora kwetu! Lazima tupunguze uchezaji huo na tufikirie nini kitatuletea ushindi!”
Arsenal, ambao wako pointi 3 nyuma ya vinara Chelsea kwenye Ligi Kuu, wanaitegemea Ligi wapate angalau Kikombe Msimu huu na Sagna anajipa moyo kuwa Chelsea na Man United zitapoteza pointi katika mechi 5 zilizobaki.
Baada ya kupondwa UEFA CHAMPIONS LIGI, England ina Timu 2 Nusu Fainali EUROPA LIGI!!!
• Ni Liverpool v Athletico Madrid na Fulham v Hamburg!!
Wolfsburg 0 Fulham 0
Ile mbiu ya kutaka Bobby Zamora achukuliwe Kikosi cha England cha Kombe la Dunia jana iliendelea kupata nguvu zaidi pale Straika huyo ambae sasa yupo kwenye fomu ya hali ya juu alipofunga bao la ushindi sekunde ya 21 tu ya mchezo na kuifikisha Timu iliyokuwa haitegemewi na wengi Nusu Fainali ya EUROPA LIGI ambako watacheza na Hamburg ambao jana waliwatupa nje Standard Lege walipowakung’uta bao 3-1.
Wakiwa ugenini Ujerumani,Bobby Zamora alimzunguka Beki Simunek na kwa utulivu na ufundi mkuu alipachika bao kwenye sekunde ya 21 tangu maechi ianze na kuifanya Fulham isonge mbele kwa jumla ya bao 3-1 baada ya kushinda nyumbani bao 2-1.
Vikosi vilivyoanza:
Wolfsburg: Benaglio, Pekarik, Simunek, Barzagli, Schafer, Riether, Josue, Gentner, Misimovic, Grafite, Dzeko.
Akiba: Lenz, Martins, Hasebe, Johnson, Dejagah, Schindzielorz, Rever.
Fulham: Schwarzer, Baird, Hughes, Hangeland, Konchesky, Murphy, Etuhu, Duff, Gera, Davies, Zamora.
Akiba: Zuberbuhler, Kelly, Nevland, Riise, Smalling, Greening, Dikgacoi.
Refa: Viktor Kassai (Hungary)
Liverpool 4 Benfica 1
Liverpool jana waliendelea kujipa matumaini ya angalau kubeba Kombe moja Msimu huu pale walipokipindua kipigo cha 2-1 katika mechi ya kwanza na kuiwasha Benfica bao 4-1 na hivyo kutinga Nusu Fainali ya EUROPA LIGI na watacheza na Atletico Madrid ambao jana waliwabwaga Wahispania wenzao Valencia.
Dirk Kuyt ndie aliefungua kitabu cha magoli pale alipofunga goli baada ya kona lakini Mshika Kibendera alilikataa bao hilo kwa kunyoosha kibendera na ndipo Refa Bjorn Kuipers alipompiku na kulikubali.
Lucas akaongeza bao la pili na Fernando Torres akapiga bao la3.
Benfica wakapata bao moja kufuatia frikiki ya Oscar Cardozo lakini ni Torres tena aliwakata maini na kufunga bao la 4.
Vikosi vilivyoanza:
Liverpool: Reina, Johnson, Carragher, Kyrgiakos, Agger, Mascherano, Lucas, Kuyt, Gerrard, Benayoun, Torres.
Akiba: Cavalieri, Aquilani, Ngog, Degen, El Zhar, Ayala, Pacheco.
Benfica: Julio Cesar, Ruben Amorim, Luisao, Sidnei, David Luiz, Javi Garcia, Carlos Martins, Ramires, Aimar, Di Maria, Cardozo.
Akiba: Moreira, Airton, Maxi Pereira, Fabio Coentrao, Felipe Menezes, Alan Kardec, Eder Luis.
Refa: Bjorn Kuipers (Holland)
MATOKEO KAMILI:
ROBO FAINALI:
Alhamisi, Aprili 8
Atletico Madrid 0 v Valencia 0 [Jumla 2-2, Athletico wanasonga kwa bao za ugenini]
Liverpool 4 v Benfica 1 [5-3]
Standard Liege 1 v Hamburg 3 [2-5]
Wolfsburg 0 v Fulham 1 [1-3]
NUSU FAINALI
Alhamisi, Aprili 22
Hamburg v Fulham
Atletico Madrid v Liverpool
Alhamisi, Aprili 29
Fulham v Hamburg
Liverpool v Atletico Madrid
FAINALI
Jumatano, Mei 12

Thursday 8 April 2010

Karata ya mwisho kwa Liverpool leo!!
Liverpool leo watasali kila namna ili kuomba Uwanja wao wa Anfield uwape matokeo mema pale watakapojaribu kugeuza kipigo cha 2-1 walichopewa na Benfica wiki iliyokwisha katika Robo Fainali ya EUROPA LIGI huku wakijua fika hii ndio nafasi pekee kwao kuweza kutwaa Kombe Msimu huu.
Wiki iliyopita huko Ureno, Daniel Agger aliwapa Liverpool bao la kuongoza lakini bao mbili za penalti za kipindi cha pili zilizopigwa na Oscar Cardozo ziliwapa Benfica ushindi wa 2-1.
Meneja wa Liverpool Rafa Benitez ametamba kuwa wana uwezo wa kuichapa Benfica hapo Anfield na katika kuhakikisha hilo, Benitez alimtoa Staa wake Fernando Torres katika mechi ya Ligi Kuu hapo Jumamosi Liverpool ilipotoka sare 1-1 na Birmingham ili apate kupumzika vizuri.
Katika mechi ya leo, Liverpool itamkosa Winga Ryan Babel ambae alipewa Kadi Nyekundu huko Ureno Benfica ilipoikaribisha Liverpool.
Wakati Liverpool wanataka kukipindua kipigo, wenzao Fulham pia leo wamo kwenye kinyang’anyiro cha EUROPA LIGI na wako Ujerumani kucheza na Wolfsburg na wao Fulham wanataka kulinda ushindi wao wa 2-1 walioupata katika mechi ya kwanza wiki iliyopita.
Meneja aliemwita Refa muongo kumkabili Pilato wa FA!!
Meneja wa Wigan Roberto Martinez anatakiwa na FA ajibu mashitaka ya kutokuwa na tabia nzuri kwa kosa la kudai Refa Stuart Attwell ni ‘muongo’ kauli aliyoitoa mara baada ya kipigo cha 3-0 toka kwa Manchester City na goli zote hizo ziliingia baada ya Beki wao Gary Caldweel kupewa Kadi Nyekundu na Refa huyo.
Caldwell alipewa Kadi hiyo dakika ya 56 huku mechi ikiwa 0-0 baada ya kumchezea rafu Carlos Tevez na baada ya hapo Tevez akafunga bao zote 3 ndani ya dakika 12.
Baada ya mechi, Martinez alimlaumu Refa na kusema hakuona wakati Caldwell anagongana na Tevez hivyo kutoa uamuzi kwa kitu ambacho hakikuona ni uongo.
FA ilimwandikia barua Martinez kutaka maelezo yake na sasa imeamua kufungua mashitaka.
Martinez amepewa hadi Aprili 22 kuwasilisha utetezi wake.
Man United wamsaini Chicharito!!!!
Manchester United imekamilisha usajili wa Straika kutoka Mexico, Javier Hernandez, miaka 21, ambae anatoka Klabu ya Mexico Chivas da Guadalajara ambae pia anachezea Timu ya Taifa ya Mexico.
Hernandez, aka Chicharito, atajiunga na Man United hapo Julai 1 na mkataba wake haukuanikwa ila kipengele kimoja ni Manchester United kwenda kucheza Mexico katika ufunguzi rasmi wa Uwanja mpya wa Chivas huko Guadalajara unaoweza kuchukua Watazamaji 45,000 mwishoni mwa Julai.
Bosi wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amemsifia Mchezaji huyo mpya na kusema ni Kijana mwenye kipaji.
Chicharito huenda akaonekana Uwanjani Wembley akiichezea Mexico hapo Mei 24 itakapocheza mechi ya kirafiki na England.
Huyu ni Mchezaji wa pili kwa Man United kumsajili kwa ajili ya Msimu ujao, wa kwanza akiwa ni Sentahafu chipukizi kutoka Fulham Chris Smalling.
Fergie awashambulia Wachezaji Bayern!!
Sir Alex Ferguson amewashambulia vikali Wachezaji wa Bayern Munich kwa kumshinikiza Refa Nicola Rizzoli kutoka Italia ili ampe Chipukizi toka Brazil Rafael Kadi na Refa huyo kweli akamlamba Kadi ya pili ya Njano na kuifanya Manchester United icheze mtu 10 kwa dakika 40 za kipindi cha pili na kutoa mwanya kwa Bayern kupata bao muhimu la pili lililowapeleka Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Ferguson alibwata mara baada ya mechi: “Kulikuwa hamna kipingamizi sisi kushinda tukiwa 11, wao walikuwa wamezidiwa! Lakini Rafael alionyesha uchanga wake na wao wakalazimisha atolewe! Kila Mchezaji wao alimkimbilia Refa- hii ni tabia halisi ya Wajerumani!”
Kuhusu kumwanzisha Wayne Rooney mechi hiyo ambayo alishindwa kuimaliza baada ya kujitonesha mguu wage na hivyo kutoka baada ya dakika 55, wakati huo huo ambapo Rafael alitolewa, Ferguson amesema hakuumia sana na atacheza mechi ijayo wikiendi hii.
UEFA CHAMPIONS LIGI: Man United & Bordeaux nje, Nusu Fainali ni Bayern v Lyon!!
Ingawa Manchester United na Bordeaux zote zilishinda mechi zao za marudiano lakini zimebwagwa nje ya UEFA CHAMPIONS LIGI kwa magoli.
Manchester United iliifunga Bayern Munich bao 3-2 na kufanya jumla ya magoli iwe 4-4 na Bayern kusonga mbele kwa idadi kubwa ya magoli ya ugenini.
Huko Ufaransa, katika mechi baina ya Klabu za Ufaransa, Bordeaux ilifanikiwa kuilaza Lyon bao 1-0 lakini ikajikuta ikitupwa nje kwa jumla ya bao 3-2.
Nusu Fainali zitakuwa ni kati ya Inter Milan v Barcelona na Bayern Munich v Lyon.

Wednesday 7 April 2010

Breking nyuziii: Rooney ndani ya Kikosi dhidi ya Bayern Munich!!
Habari kutoka Old Trafford ambako lile pambano la kukata na shoka litaanza muda si mrefu kuanzia sasa kati ya Manchester United na Bayern Munich zimethibitisha kuwa Wayne Rooney amepona enka na anaanza mechi hiyo.
Rooney aliumia katika mechi ya kwanza kati ya Timu hizo wiki iliyopita ambayo Bayern walishinda 2-1.
Kikosi kamili cha Man United kitakuwa:
Van der Sar, Evra, Ferdinand, Rooney, Vidic, Carrick, Nani, Rafael, Fletcher, Valencia, Gibson
El-Hadj Diouf kumsalimi Pilato Mei 10
Straika wa Blackburn, El-Hadji Diouf anaetoka Senegal, atafikishwa Mahakamani Mwezi ujao kwa makosa ya kuendesha gari bila leseni wala bima makosa yanayodaiwa kutendeka huko Manchester Septemba 14 mwaka jana.
Diouf alisimamishwa na Polisi wakati akiendesha gari aina ya Porsche Cayenne na atafikishwa Mahakamani Mei 10 Jijini Manchester.
EUROPA LIGI: Kesho Liverpool kazi ipo na Benfica!!
Kesho, Liverpool wana mtihani mkubwa wa kuifunga Benfica ili waweze kuingia Nusu Fainali ya EUROPA LIGI na kuweka hai matumaini yao ya angalau kuvuna Kikombe kimoja msimu huu.
Liverpool wanahitaji ushindi ili kuwapiku Benfica ambao wiki iliyokwisha waliichapa Liverpool bao 2-1.
Wakati Liverpool wanamenyana na Benfica, wenzao wa Ligi Kuu Fulham watakuwa Ujerumani kurudiana na Wolfsburg Timu ambayo waliifunga bao 2-1 wiki iliyopita.
RATIBA:
ROBO FAINALI: Marudiano
[Matokeo mechi za kwanza kwenye mabano]
Alhamisi, Aprili 8
Atletico Madrid v Valencia [2-2]
Liverpool v Benfica [1-2]
Standard Liege v Hamburg [1-2]
Wolfsburg v Fulham [1-2]
NUSU FAINALI
Alhamisi, Aprili 22
Hamburg/Standard Liege v Fulham/Wolfsburg
Valencia/Atletico Madrid v Benfica/Liverpool
Alhamisi, Aprili 29
Fulham/Wolfsburg v Hamburg/Standard Liege
Benfica/Liverpool v Valencia/Atletico Madrid
FAINALI
Jumatano, Mei 12
Vitu Vitano vinavyoikabili Man United katika mechi na Bayern Munich leo!
Katika wiki moja, Manchester United wamekumbana na vipigo vikubwa viwili mfululizo pale walipofungwa 2-1 na Bayern Munich huko Ujerumani Jumanne iliyopita kwenye mechi ya kwanza ya Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI na Jumamosi wakafungwa tena 2-1 na Chelsea na kupokonywa uongozi wa Ligi Kuu.
Leo, ndani ya Uwanja wao Old Trafford, wanarudiana na Bayern Munich na wanahitaji ushindi wa bao 1-0 ili wasonge Nusu Fainali.
Lakini kuna Mchambuzi ameweka mambo matano bayana ambayo inabidi Man United wayakabili na kuyarekebisha ikiwa watataka kuifunga Bayer Munich leo.
Mambo hayo ni:
1. Beki wa Kulia:
Udhaifu wa nafasi hii umeonekana katika vipigo vya mechi hizo na Bayern na ile na Chelsea pale Mkongwe Gary Neville, miaka 35, aliposhindwa kuwadhibiti ipasavyo Frank Ribery na Florent Malouda.
Waziwazi, Sir Alex Ferguson ameogopa kumpanga Chipukizi Mbrazil Rafael da Silva ambae hana uzoefu.
Wengine ambao wangeweza kumudu nafasi hii ni John O’Shea na Wes Brown na wote ni majeruhi.
2. Kiungo
Siku za Paul Scholes kama injini zimepita na Darren Fletcher ameonekana chini ya kiwango katika mechi na Bayern na ile na Chelsea na hali kadhalika Michael Carrick.
3. Viungo Mawinga
Ferguson mara nyingi humchezesha Ji-sung Park kwenye mechi kubwa zinazohitaji nguvu kazi lakini wiki iliyokwisha kwenye mechi na Bayern alionyesha udhaifu na kumruhusu mara nyingi Beki wa kulia wa Bayern Philip Lahm kupanda na kufanya mashambulizi.
Nani anaweza kuchukua nafasi hii ingawa yeye si muhangaikaji lakini ujanja, mbinu na wepesi wake unaweza kuleta kizaazaa golini.
Giggs tangu aanze kucheza tena baada ya kuvunjika mkono hajarudi kwenye fomu.
4. Straika
Man United wakiwa kwenye fomu huwaendesha puta Wapinzani kwa spidi yao ya mashambulizi lakini kukosekana kwa Wayne Rooney na kuwepo kwa Dimitar Berbatov tu kunaikosesha Man United hiyo spidi.
Ferguson hana mbadala wa Rooney kwani Michael Owen ni majeruhi na waliobaki Federico Macheda na Mame Biram Diouf bado wachanga.
5. Historia
Historia ya Man United kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI inaonyesha wamebwagwa nje mara 4 kati ya 5 pale wanapoanza kufungwa katika mechi ya kwanza ya Mashindano haya.
Lakini mara hiyo moja waliyoibadili historia ni pale Msimu wa mwaka 2006/7 walipofungwa 2-1 huko Roma, Italia na katika marudiano Old Trafford, Man United wakaichabanga AS Roma bao 7-1.
Refa Mike Dean alieibeba Chelsea aadhibiwa!
Refa wa Ligi Kuu Mike Dean amepigwa stopu kuchezesha Ligi Kuu na wikiendi hii inayokuja ametupwa kuchezesha Daraja la chini ikiwa ni adhabu yake kwa kuchezesha vibaya mechi ya Manchester United na Chelsea Jumamosi iliyopita.
Pia, Mshika Kibendera wake, Simon Beck, ambae hakuashiria ofsaidi pale Drogba alipoifungia goli la pili Chelsea nae ametupwa kuchezesha Daraja la chini kwa makosa hayo.
Baada ya mechi hiyo, Sir Alex Ferguson aliwaponda Waamuzi hao na kuwaita wabovu na hawakustahili kuchezesha mechi kubwa.
Kabla ya mechi ya Man United na Chelsea uteuzi wa Refa Mike Dean kuchezesha mechi hiyo uliitwa ‘wehu’ na Meneja wa Burnley Brian Laws baada ya Refa huyo kuwapa Blackburn penalti feki na hivyo Burnley kufungwa wiki moja kabla.
Baada ya mechi hiyo ya Chelsea, Ferguson alisema alipofahamu Refa ni Mike Dean alipatwa na wasiwasi mkubwa.
Wenger anyoosha mikono kwa Messi!!
• Amfananisha na Mchezaji kwenye Gemu ya Kompyuta “PlayStation”!
Baada ya Lionel Messi kuifungia Barcelona bao zote 4 walipowanyuka Arsenal 4-1 na kuwabwaga nje ya Mashindano ya UEFA CHAMPIONS LIGI hapo jana Uwanjani Nou Camp, Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amekubali Mess indie Mchezaji Bora Duniani.
Wenger aliungama: “Yeye ni kama PlayStation! Katika mechi kubwa, Wachezaji wenye vipaji ndio huleta tofauti. Messi ndie Mchezaji Bora Duniani! Nawapa hongera Barcelona, walikuwa wazuri kupita sisi!”
Wenger aliendelea kumpamba Messi kwa kusema hukuadhibu kwa kila kosa unalofanya na pia kukiri kuwa kwa vile Messi ndio kwanza ana miaka 22 ana nafasi kubwa ya kujijenga na kuwa Mchezaji Bora kupita wote katika historia ya Soka.
Wenger alikiri wamevunjika moya kwa kutolewa UEFA na sasa wamebakiwa na LIgi Kuu ikiwa ndio nafasi pekee ya kutwaa Kombe Msimu huu.
Mechi yao inayofuata ya Ligi Kuu ni ile dabi ya Timu za Kaskazini ya Jiji la London watakapoenda Uwanja wa White Hart Lane kuikwaa Tottenham Jumatano ijayo.

Tuesday 6 April 2010

UEFA CHAMPIONS LIGI: Messi ailipua Ze Gunners!!
• Barca 4 Arsenal 1
Ndani ya Nou Camp, Arsenal walichokoza nyuki pale walipofunga bao dakika ya 18 kupitia Niklas Bendtner lakini ndani ya dakika mbili Mchezaji Bora Duniani Lionel Messi akaisawazishia Barcelona na akaongeza bao nyingine mbili kwenye dakika ya 37 na 42.
Hadi mapumziko Barcelona 3 Arsenal 1.
Kipindi cha pili, Barcelona walicheza kwa tahadhari na kupunguza kasi na kushambulia kwa nguvu wakiwaacha Arsenal wahangaike kupata bao.
Hata hivyo, Mchawi Lionel Messi hakuridhika na bao zake 3 na kwenye dakika ya 87 akafanya ndumba zake na kupachika bao lake la 4.
Hivyo Mabingwa Watetezi wa Ulaya, Barca, wametinga Nusu Fainali na watacheza na Inter Milan ambao katika mechi ya awali leo waliitoa CSKA Moscow walipowafunga 1-0.
Vikosi vilivyoanza:
Barcelona: Valdes, Dani Alves, Marquez, Milito, Abidal, Busquets, Xavi, Keita, Pedro, Bojan, Messi.
Akiba: Pinto, Iniesta, Henry, Maxwell, Toure Yaya, Fontas, Jeffren.
Arsenal: Almunia, Sagna, Vermaelen, Silvestre, Clichy, Denilson, Diaby, Walcott, Nasri, Rosicky, Bendtner.
Akiba: Fabianski, Eduardo, Eboue, Traore, Campbell, Merida, Eastmond.
Refa: Wolfgang Stark (Germany)
Ferguson ana imani Man United wataitwanga Bayern
Kwenye Uwanja wa nyumbani, Manchester United, kesho Jumatano wanarudiana na Bayern Munich kwenye Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI baada ya kufungwa 2-1 wiki iliyopita huko Ujerumani huku bao la pili likitinga dakika za majeruhi.
Manchester United wanahitaji bao moja tu kuibwaga Bayern Munich na Meneja wao Sir Alex Ferguson ana matumaini makubwa ya kupata ushindi.
Ferguson amesema: "Watu wengi wanaamini tuna nafasi nzuri. Na mimi nafikiria tuna nafasi nzuri sana!”
Ferguson ameongeza kuwa ana matumaini makubwa kwa mechi na Bayern kuliko alivyokuwa Jumamosi walipocheza na kufungwa 2-1 Chelsea kwenye Ligi Kuu.
Ferguson amedai kuingia Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI ni motisha kubwa kwa Wachezaji wake
Ingawa Manchester United wana goli la ugenini dhidi ya Bayern Munich na pia wanacheza nyumbani, wana pengo kubwa kwa kumkosa Mfungaji wao mkuu Wayne Rooney alieumia kwenye mechi ya kwanza na Bayern lakini kuna minong’ono huenda Rooney akawepo benchi na hilo limedokezwa hata na Ferguson mwenyewe.
Ferguson amesisitiza: “Goli la ugenini ni muhimu kwani soka la siku hizi magoli ni magumu kupata. Na tunacheza Old Trafford na tukiwa hapo magoli hutiririka kwani Washabiki wanatupa morali kubwa. Mara nyingi tumekuwa tukishinda dakika za mwisho na hilo si juu ya Wachezaji tu, ni Washabiki pia wanaoleta changamoto! Tunaombea Jumatano iwe hivyo!”
Alipoulizwa kama anategemea Chipukizi Macheda ambae ndie aliefunga bao la Man United Jumamosi na Chelsea ataanza hasa kwa vile Berbatov anapwaya, Ferguson alisema Macheda ataanza benchi lakini atapewa fursa ya kucheza.
Ferguson amesema: “Macheda ndio kwanza amepona musuli za miguu na bega vilivyokuwa vinamsumbua Msimu wote. Huyu ni kijana mwenye kipaji kikubwa!”
UEFA CHAMPIONS LIGI: Inter yaingia Nusu Fainali
Leo, Wesley Sneijder ameifungia Timu yake Inter Milan bao la frikiki dakika ya 6 na kuwashinda CSKA Moscow kwa bao 1-0 na hivyo kuihakikishia Inter inatinga Nusu Fainali kucheza na Mshindi wa mechi kati ya Barcelona na Arsenal wanaocheza baadae leo huko Nou Camp.
Mechi hii ilianza mapema, saa 1 na nusu usiku saa za bongo, katika Uwanja wa Luzhniki Jijini Moscow, Urusi na ni ya marudiano ambapo Inter Milan waliishinda CSKA Moscow pia kwa bao 1-0 wiki iliyopita lakini Mfungaji wa leo Wesley Sneijder hakucheza mechi hiyo kwa vile alikuwa majeruhi.
Licha ya kuwa na wasiwasi wa nyasi za bandia za Uwanja wa Luzhniki, Inter walionekana kutulia na kumiliki mpira vizuri katika mechi yote hiyo na wangeweza kupata mabao mengi zaidi kama wangejitutumua zaidi.
CSKA Moscow walimaliza mechi wakiwa mtu 10 baada ya Odiah kulambwa Kadi Nyekundu alipopewa Kadi za Njano mbili.
Vikosi vilivyoanza (Wachezaji walioingia na dakika waliyoingia kwenye mabano):
CSKA Moscow: Akinfeev, Semberas, Ignashevich Berezutsky, Berezutsky (Odiah 14), Shchennikov, Dzagoev, Mamaev, Gonzalez, Honda (Rahimic 77, Necid (Guilherme 71)
Inter Milan: Julio Cesar, Zanetti, Lucio, Maicon, Samuel, Stankovic, Sneijder (Muntari 86), Cambiasso, Eto'o, Milito (Balotelli 74), Pandev (Chivu 63)
Timu za England hatarini kutocheza Nusu Fainali UEFA
Leo na kesho ndio hatima ya Timu za England kujua wanaingia Nusu Fainali za UEFA CHAMPIONS LIGI au la wakati leo Arsenal atakapojimwaga ugenini Nou Camp kuivaa Barcelona na kesho Manchester United yuko kwake Old Trafford atakaporudiana na Bayern Munich.
Wakati Arsenal anatafuta ushindi au sare ya zaidi ya bao 2-2 kwa vile mechi ya kwanza walitoka suluhu 2-2 na Barcelona, Manchester United ni lazima washinde kwa vile walifungwa 2-1 huko Ujerumani wiki iliyopita.
Arsenal na Manchester United zikitolewa itakuwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2003 kwa England kukosa Timu kwenye Nusu Fainali za UEFA CHAMPIONS LIGI.
Mourinho auita Uwanja wa Luzhniki wa kitoto!
Kocha wa Inter Milan, Jose Mourinho, ambae leo yuko Moscow na Timu yake kurudiana na CSKA Moscow katika mechi ya Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI kwenye Uwanja wa Luzhniki ambao nyasi zake ni za bandia, ameuita Uwanja huo ni wa kitoto.
Inter Milan, walioshinda mechi ya kwanza kwa bao 1-0, leo wanahitaji suluhu tu iliwatinge Nusu Fainali kucheza na Mshindi wa mechi nyingine ya leo kati ya Barcelona na Arsenal.
Mourinho amesema alitaniana na Wachezaji wake kwa kuwaambia walipokuwa Watoto walicheza mpira barabarani hivyo leo hawawezi kushindwa kucheza kwenye Uwanja wenye nyasi bandia kwani ni sawa na uwanja wa kitoto.
Timu nyingi zimekuwa zikiulalamikia Uwanja huo wa Luzhniki na wengi wanahisi CSKA Moscow wanafaidika sana kwa kucheza hapo.
Newcastle yarudi Ligi Kuu
Newacastle jana ilifanikiwa kuifunga Sheffield United bao 2-1 kwenye pambano la Ligi ya Coca Cola Championship na kufanikiwa kupanda Daraja kurudi Ligi Kuu ambako waliporomoka Msimu uliokwisha.
Katika mechi ya jana, Newcastle walihitaji sare tu ili wapande Daraja lakini wakajikuta wako nyuma kwa bao 1 baada ya Sheffield kupata bao dakika ya 22 kupitia Richard Creswell.
Newcastle walisawazisha kwa penalti ya Peter Lovenkrands na Kevin Nolan akapachika bao la pili na la ushindi dakika ya 73.
Meneja wa Newcastle, Chris Houghton, aliechukua wadhifa huo baada ya Kevin Keegan kubwaga manyanga, alisema ni furaha kubwa kufuzu kupanda Daraja mbele ya Mashabiki wao Uwanjani kwao St James Park lakini wanataka ushindi katika mechi zao 5 zilizobaki ili wawe Mabingwa wa Daraja hilo.
Barcelona v Arsenal
Arsenal wanaingia Nou Camp kurudiana na Barcelona baada ya kutoka sare 2-2 wiki iliyopita lakini Timu yao ina majeruhi kibao na Kiungo Alex Song ameongezeka kwenye lisi hiyo ambamo wamo Cesc Fabregas, Andrey Arshavin na William Gallas.
Barcelona nao pia watawakosa Wachezaji kadhaa wakiwemo Masentahafu wao wote wawili Carles Puyol na Gerard Pique kwa vile wana Kadi.
Vile vile Mfungaji wao mkubwa, Zlatan Ibrahimovic, yuko nje kwa kuumia lakini watamkaribisha tena Kiungo mahiri Andres Iniesta ambae amepona maumivu baada ya kuzikosa mechi kadhaa.
Katika mechi ya leo, Wenyeji Barcelona wanahitaji sare ya 0-0 au 1-1 ili wasonge Nusu Fainali wakati Arsenal wanahitaji ushindi au sare yoyote ya zaidi ya bao 2-2.
Fergie hawezi kumpanga Rooney kabla hajapona vizuri
Sir Alex Ferguson amesema hawawezi kumchezesha Wayne Rooney katika mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI ya Manchester United na Bayern Munich siku ya Jumatano huko OldTrafford ikiwa Mchezaji huyo hayuko fiti kwa asili mia moja.
Rooney aliumia wiki iliyopita katika mechi ya kwanza kati ya Bayern Munich na Manchester United ambayo Bayern walishinda 2-1 na Jumatano ni lazima Man United washinde ili wafuzu kuingia Nusu Fainali.
Kumekuwa na habari kadhaa katika Vyombo vya Habari kuwa Rooney atacheza mechi hiyo ya marudiano baada ya kupona haraka.
Ingawa Ferguson amegoma kumchezesha Rooney lakini alidokeza kuwa huenda akamweka benchi kwa vile Mchezaji huyo ni king’ang’anizi.

Monday 5 April 2010

KUNA NINI LIGI ZA ULAYA!
Bordeaux, Manchester United na Schalke zote zilipokonywa uongozi wa Ligi za Nchi zao kufuatia mechi za wikiendi wakati Lyon, Chelsea na Bayern Munich walipoibuka vinara wa Ligi hizo.
Huko Spain na Italy misimamo ya Ligi imebaki kama ilivyokuwa awali ingawa tumbo joto linazidi kupanda.
Ligi Kuu England: Chelsea washika hatamu
Ushindi wa Chelsea wa 2-1 dhidi ya Manchester United umewapa uongozi wa Ligi hii wakiwa pointi mbili mbele ya Man United huku mechi zimebaki 5.
Katika mechi hizo 5 zilizobaki, kimahesabu mechi ngumu kwa Chelsea ni zile dhidi ya Tottenham na Liverpool.
Timu nyingine iliyonufaika sana kwa mechi za wikiendi ni Manchester City ambayo iliichabanga Burnley bao 6-1 na kutwaa nafasi ya 4 ambayo inaliliwa na Timu kadhaa nyingine ili kucheza UEFA Msimu ujao.
Tatu Bora: Chelsea (pointi 74), Manchester Utd (72), Arsenal (71)
Tatu za mkiani: Hull City (pointi 27), Burnley (24), Portsmouth (14)
Wafungaji Bora: Wayne Rooney (26), Didier Drogba (25), Darren Bent (22)
Ligue 1: Bordeaux inaporomoka
Bordeaux walipigwa 2-1 na Nancy na kunyang’anywa uongozi na kuporomoka hadi nafasi ya 4.
Inaelekea msimu wa Bordeaux umeanza kuingia mkosi kwani ghafla umeanza kuharibika pale walipofungwa 3-1 na Marseille kwenye Fainali ya Kombe la Ligi la Ufaransa na mechi iliyofuata ni mkondo wa kwanza wa Mashindano ya UEFA wakapigwa 3-1 na Lyon kisha juzi kwenye Lique 1 wakapokonywa uongozi wa Ligi hiyo walipofungwa na Nancy bao 2-1.
Lyon ndio wametwaa uongozi baada ya kuifunga Rennes 2-1.
Lakini Ligi ni ngumu hasa kwa vile ni pointi 3 tu inazitenganisha Timu 6 za juu na ni pointi moja tu kwa Timu 5 za juu.
Tatu Bora: Lyon (pointi 57, magoli +19), Montpellier (57, +7), Auxerre (57, +6)
Tatu za mkiani: Boulogne (pointi 24), Le Mans (21), Grenoble (15)
Wafungaji Bora: Mamadou Niang (magoli 15), Kevin Gameiro, Lisandro Lopez, Nene and Asamoah Gyan (wote 13 kila mmoja), Gervinho and Mevlut Erdinc (both 12)
Bundesliga: Bayern kileleni
Wakiongozwa na Ribery, Bayern Munich walifunga bao mbili katika dakika mbili na kuichapa Schalke bao 2-1 na kuwapora uongozi.
Tangu rekodi yao ya kutofungwa mechi 24 kumalizwa na kipigo toka kwa Nuremberg, Bayer Leverkusen wamefifia na wamefungwa mechi yao ya 4 kati tano za mwisho walipotandikwa 3-2 na Eintracht Frankfurt na sasa wako nafasi ya 3.
Tatu Bora: Bayern Munich (pointi 59), Schalke (58), Leverkusen (53)
Tatu za mkiani: Freiburg (pointi 25), Hanover (24), Hertha Berlin (22)
Wafungaji bora: Stefan Kiessling, Kevin Kuranyi and Edin Dzeko (wote bao 18 kila mmoja), Lucas Barrios (15), Eren Derdiyok, Albert Bunjaku and Claudio Pizarro (wotel 12 kila mmoja)
La Liga: Macho yote Jumamosi
Kama ilivyotegemewa, Barcelona na Real Madrid zote zimeshinda mechi zao za wikiendi huku Barca wakiwapiga Athletic Bilbao 4-1 na Real kuichapa Racing Santander 2-0.
Matokeo hayo sasa yanaifanya, EL CLASICO, yaani ile mechi ya Jumamosi kati ya Real Madrid na Barcelona huko Bernabeau, ndio iamue nani mbabe kati ya vigogo hao na pia nani achukue uongozi wa Ligi.
Tatu Bora: Real Madrid (pointi 77, magoli +57), Barcelona (77, +56), Valencia (56)
Tatu za mkiani: Tenerife (pointi 25), Valladolid (24), Xerez (23)
Wafungaji Bora: Lionel Messi (magoli 26), Gonzalo Higuain (24), David Villa (20)
Serie A: Ngoma ngumu
Timu zote za juu zilishinda mechi zao na kufanya msimamo uwe kama ulivyokuwa kabla ya mechi za wikiendi.
Vinara Inter Milan waliichapa Bologna 3-0 kwa mabao mawili ya Thiago Motta na moja la Mario Baloteli.
AS Roma waliitungua Bari 1-0 kwa bao la Mirko Vucinic.
AC Milan walikuwa kwenye vuta ni kuvute na Cagliari na hatimae kuibuka washindi wa bao 3-2.
Tatu Bora: Inter Milan (pointi 66), Roma (65), AC Milan (63)
Tatu za mkiani: Atalanta (pointi 31), Siena (26), Livorno (26)
Wafungaji Bora: Antonio Di Natale (magoli 22), Diego Milito (18), Alberto Gilardino (15)
Newcastle leo pointi moja tu wamerudi Ligi Kuu!
Newcastle ambao walishushwa Daraja toka Ligi Kuu msimu uliokwisha leo wanacheza na Sheffield United Uwanjani St James Park kwenye mechi ya Ligi ya Coca Cola Championship na wanahitaji sare tu ili wapande Daraja kurudi tena Ligi Kuu.
Newcastle ndio wanaongoza Ligi hiyo wakiwa na pointi 86 kwa mechi 40 na wa pili ni West Bromwich Albion waliocheza mechi 42 na wana pointi 83.
Kila Timu inatakiwa icheze jumla ya mechi 46.
Timu mbili za juu za Ligi hii ndio hupanda Daraja moja kwa moja kwenda Ligi Kuu na Timu ya 3 mpaka ya 6 hupangiwa Mchujo maalum kuipata Timu moja itakayoungana na hizo Timu mbili za juu kwenda Ligi Kuu.
Mpaka sasa Timu zilizo nafasi ya 3 hadi ya 6 ni Nottingham Forest, Cardiff, Leicester City na Swansea huku Blackpool iko nafasi ya 7 na inanyemelea kwa dhati kuingia kundini.
UEFA CHAMPIONS LIGI: Nani kutinga Nusu Fainali?
Marudiano ya mechi za Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni hapo kesho Jumanne na Jumatano huku Wachezaji kadhaa wakubwa watazikosa mechi hizo kwa sababu mbalimbali wakiwemo Wayne Rooney, Carles Puyol, Gerard Pique, Zlatan Ibrahimovic, Cesc Fabregas, Andrei Arshavin, Lisandro Lopez na Milos Krasic.
RATIBA:
(Mabao ya mechi za kwanza kwenye mabango)
[saa 3 dak 45, bongo taimu]
Jumanne 6 Aprili
CSKA Moscow-Inter Milan (0-1)
Barcelona-Arsenal (2-2)
Jumatano 7 Aprili
Manchester United-Bayern Munich (1-2)
Bordeaux-Lyon (1-3)
TATHMINI:
CSKA Moscow v-Inter Milan:
Inter Milan wanasafiri hadi Moscow, Urusi kuulinda ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya CSKA Moscow kwenye Uwanja wa nyasi bandia ambao ni mgumu kuchezeka kama hukuuzoea.
CSKA Moscow watawakosa Wachezaji wao wawili hodari, Milos Krasic na Evgeni Aldoni na wenzao Inter Milan watawakaribisha tena Wachezaji wao Masentahafu walioikosa mechi ya kwanza, Lucio na Thiago Motta.
Barcelona v Arsenal:
Arsenal walijitutumua katika mechi ya kwanza ya Timu hizi na kulazimisha sare ya 2-2 lakini watawakosa Wachezaji wao bora Cesc Fabregas, William Gallas na Andrey Arshavin ambao wote waliumia katika mechi hiyo iliyochezwa Emirates.
Barcelona ingawa wako nyumbani na wanahitaji sare ya 0-0 au 1-1 ili wafuzu, wanakabiliwa na kuwakosa Wachezaji kadhaa wakiwemo Masentahafu wao wote wawili, Puyol na Pique, ambao wana Kadi.
Pia Barca watamkosa Mfungaji wao mkuu na ambae ndie alifunga bao zao mbili huko Emirates, Zlatan Ibrahimovic, alieumia. Lakini injini yao amabayo haikucheza Emirates, Andres Iniesta, amepona na ataonekana kilingeni.
Lengo la Barca katika mechi hii ni kupata ushindi wa haraka ili wacheze kilaini kwa vile wikiendi ijayo ni ‘EL CLASICO’ watakapowavaa Wapinza wao wakubwa Real Madrid Uwanja wa Bernabeau.
Manchester United v Bayern Munich
Kwa Manchester United, hii ni mechi kubwa mno na muhimu mno, ili kuokoa Msimu wao ambao umeingia dosari kubwa baada ya kufungwa mfululizo mechi mbili muhimu.
Balaa ilianza walipofungwa 2-1 na Bayern Munich katika mechi ya kwanza na mechi iliyofuata wakapigwa 2-1 na Chelsea waliowapokonya uongozi wa Ligi Kuu.
Bila shaka, marudiano na Bayern Munich ni mechi ya kufa na kupona na wanahitaji ushindi wa bao 1-0 tu ili watinge Nusu Fainali lakini huenda mambo yakawa magumu kwani Mfungaji wao mkuu, Wayne Rooney, aliumia katika mechi ya kwanza huko Ujerumani ingawa kuna tetesi Rooney huenda akawa fiti kucheza mechi hii ya marudiano siku ya Jumatano.
Bordeaux v Lyon:
Msimu wa Bordeaux ghafla umeanza kuharibika pale walipofungwa 3-1 na Marseille kwenye Fainali ya Kombe la Ligi la Ufaransa na mechi iliyofuata ni mkondo wa kwanza wa Mashindano haya ya UEFA walipopigwa 3-1 na Lyon kisha juzi kwenye Lique 1 wakapokonywa uongozi wa Ligi hiyo walipofungwa na Nancy bao 2-1.
Hata hivyo, kwa Bordeaux, habari za faraja kwao ni kule Lyon kumkosa Mfungaji wao bora Lisandro Lopez aliefungiwa na pia Veterani wa Lyon Govou kutokuwepo.

Sunday 4 April 2010

Everton 2 West Ham 2
Timu inayopigana kufa na kupona ili kukimbia kushuka Daraja, West Ham, leo wakiwa ugenini Goodison Park, wamejitutumua na kulazimisha sare ya bao 2-2 na Wenyeji Everton.
Sare hii imeiweka Everton nafasi ya 8 wakiwa na pointi 50 na West Ham wako nafasi ya 17 wakiwa wamecheza mechi 33 na wana pointi 28 ikiwa ni pointi moja tu juu ya zile Timu 3 zilizo nafasi 3 za mwisho za kuteremshwa Daraja.
Everton walitangulia kufunga dakika ya 24 kwa bao la Diniyar Bilyaletdinov na lilipatikana pale Beki wa West Ham Jonathan Spector alipojaribu kuokoa lakini mpira ukamfikia Tim Cahill aliepiga kichwa golini na Mfungaji akausindikiza wavuni.
Kwenye dakika ya 39 Refa Webb aliwapa penalti West Ham baada ya Sylvain Distin kumchezea rafu Carlton Cole lakini Mido alipiga kiki hafifu ambayo Kipa wa Everton Tim Howard aliokoa.
Kipindi cha pili, West Ham walisawazisha kwenye dakika ya 59 baada ya kona iliyopigwa na Noble kuleta patashika ndani ya boksi na mpira ukamfikia Beki wa West Ham Manuel Da Costa aliouvurumisha wavuni.
Katika dakika ya 84, krosi ya Beki wa kushoto Leighton Baines ilimaliziwa kwa kichwa na Yakubu na kufanya Everton wawe mbele kwa bao 2-1.
Lakini bao hilo la Everton lilidumu dakika moja tu pale krosi ya Julien Faubert kupigwa kichwa na Mchezaji alietokea benchi la akiba Araujo Ilan na kuisawazishia West Ham.
Vikosi vilivyoanza:
Everton: Howard, Neville, Jagielka, Distin, Baines, Pienaar, Osman, Heitinga, Cahill, Bilyaletdinov, Saha.
Akiba: Turner, Hibbert, Yakubu, Senderos, Rodwell, Duffy, Wallace.
West Ham: Green, Faubert, Da Costa, Upson, Spector, Noble, Parker, Kovac, Behrami, Mido, Cole.
Akiba: Kurucz, Gabbidon, Ilan, McCarthy, Daprela, Spence, Stanislas.
Refa: Howard Webb
Liverpool yakwaa kigingi!
Uwanja wa Mtakatifu Andrew umewashinda Liverpool kutoka na ushindi pale walipotoka droo na Wenyeji Birmingham kwa bao 1-1 katika moja ya mechi 3 za Ligi Kuu za leo.
Mabao yote ya mechi hii yalifungwa kipindi cha pili.
Liverpool ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Nahodha wao Steven Gerrard lakini Birmingham wakasawazisha kwa bao la Liam Ridgewell.
Sare ya leo imefanya Liverpool washike nafasi ya 6 wakiwa wamecheza mechi 33 na kuwa na pointi 55.
Juu ya Liverpool wapo Tottenham waliocheza mechi 32 na wana pointi 58.
Nafasi ile ya ‘dhahabu’ inayogombewa na Timu za Manchester City, Tottenham, Liverpool na Aston Villa, nafasi ya 4, imekamatwa na Man City waliocheza mechi 32 na wana pointi 59.
Vikosi vilivyoanza:
Birmingham: Hart, Carr, Johnson, Dann, Ridgewell, Gardner, Ferguson, Bowyer, Fahey, Jerome, McFadden.
Akiba: Taylor, Larsson, Phillips, Benitez, Michel, Parnaby, Vignal.
Liverpool: Reina, Johnson, Carragher, Kyrgiakos, Insua, Benayoun, Gerrard, Lucas, Maxi, Torres, Kuyt.
Akiba: Cavalieri, Aquilani, Agger, Babel, Mascherano, Ngog, Degen.
Refa: Martin Atkinson
Fulham 2 Wigan 1
Katika mechi nyingine ya Ligi Kuu leo Jumapili, Fulham wakiwa kwao Craven Cottage wamefaulu kutoka nyuma na kushinda bao 2-1 dhidi ya Wigan Timu ambayo inachechemea kujinasua toka hatarini.
Wigan ndio walitangulia kufunga bao dakika ya 32 Mfungaji akiwa Jason Scotland bao lililodumu hadi mapumziko.
Fulham wakasawazisha kipindi cha pili dakika ya 6 ya kipindi hicho Mfungaji akiwa Stefano Okaka.
Bao la ushindi la Fulham lilipatikana kupitia Beki wao Brede Hangeland kufuatia kona ya Damien Duff.
Ushindi huu umeiweka Fulham nafasi ya 12 wakiwa na pointi 41 na Wigan wako nafasi ya 16 wakiwa na pointi 31 zikiwa ni pointi 4 tu juu ya Timu zile zilizo eneo la hatari la kuporomoka Daraja.
Vikosi vilivyoanza:
Fulham: Schwarzer, Davies, Hughes, Hangeland, Konchesky, Duff, Murphy, Etuhu, Dempsey, Gera, Elm.
Akiba: Zuberbuhler, Baird, Shorey, Okaka, Nevland, Smalling, Greening.
Wigan: Kirkland, Melchiot, Bramble, Scharner, Figueroa, McCarthy, Moreno, Diame, N'Zogbia, Rodallega, Scotland.
Akiba: Stojkovic, Gohouri, Amaya, Watson, Moses, Gomez, Sinclair.
Refa: Mark Clattenburg
Ancelotti: "Kutolewa UEFA kumetusaidia!"
Carlo Ancelotti amekubali kuwa kutokucheza UEFA katikati ya wiki kumewasaidia kuifunga Manchester United tofauti na Manchester United waliocheza mechi huko ujerumani siku ya Jumanne na kurudi England kucheza na Chelsea Jumamosi.
Chelsea wao walicheza mechi yao ya mwisho Jumamosi iliyokwisha na kupumzika wiki nzima.
Man United walicheza na Bayern Munich na wakapata pigo la kuumiziwa Mfungaji wao bora Wayne Rooney.
Chelsea sasa ndio wanaoongoza Ligi kwa pointi mbili mbele ya Man United.
Ancelotti amekiri unafuu walioupata kwa kusema: "Pengine tulinufaika kutolewa UEFA! Tulipumzika na kufanya mazoezi vizuri tu!"
Wenger kujadili hatima yake Arsenal
Arsene Wenger ataketi na Maafisa wa Arsenal mwishoni mwa Msimu ili kufikia makubaliano ya yeye kuongeza Mkataba wake au nini kifanyike.
Mkataba wa Wenger unamalizika mwakani lakini mwenyewe amesema yuko tayari kwa majadiliano. Kumekuwa na tetesi za chini kwa chini ambazo hata yeye ashawahi kuzikanusha kuwa Real Madrid wanamwinda ili ambadili Pellegrini.
Wenger alijiunga na Arsenal mwaka 1996 wakati akiwa hana umaarufu wowote lakini katika miaka 14 aliyokuwa hapo amejizolea sifa kubwa kwa kujenga Timu inayocheza Soka Tamu na kuifanya iwe moja ya Vigogo wa Ulaya.
Hata hivyo, sasa ni miaka mitano tangu Arsenal watwae Kombe kwa mara ya mwisho.
Arsenal walibeba FA Cup mwaka 2005 na huo ukawa ndio mwisho.
Burnley 1 Man City 6
Jana katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa mwishoni, Man City wakiwa ugenini waliichabanga Burnley bao 6-1 na kuchukua nafasi ya 4 inayogombewa na Tottenham, Liverpool na Aston Villa.
Huku mvua kubwa ikinyesha na uwanja kujaa maji, Man City nao walikuwa wakiangusha mvua ya magoli na walikuwa mbele kwa bao 5 wakati wa mapumziko.
Bao za Man City zilifungwa na Adebayor, bao mbili dakika ya 4 na 45, Bellamy dakika ya 5, Tevez dakika ya 7, Vieira dakika ya 20 na Kompany dakika ya 58.
Fletcher ndie aliewafungia Burnley bao lao pekee.
Burnley wako nafasi ya 19 ikiwa ni nafasi moja tu toka mkiani walipo Portsmouth.
Juu ya Burnley wapo Hull City na hizo ndizo Timu 3 zilizo hatarini kuporomoka.
ULE ‘WEHU’ KUMPANGA REFA MIKE DEAN WATIMIA!!
Fergie amponda vibaya Dean na wenzake!!!
Sir Alex Ferguson amewaponda vibaya Waamuzi wa pambano la jana la Ligi Kuu kati ya Manchester United na Chelsea ambalo Chelsea walishinda 2-1 na kuukwaa uongozi wa Ligi.
Didier Drogba alifunga bao la pili huku akiwa waziwazi ofsaidi na Ferguson amelaumu kukubaliwa kwa bao hilo.
Katika mechi hiyo Refa Mike Dean, ambae uteuzi wake kuchezesha mechi hiyo uliitwa ‘wehu’ na Meneja wa Burnley Brian Laws baada ya Refa huyo kuwapa Blackburn penalty feki na hivyo Burnley kufungwa, jana alipeta penalti 3 za wazi, mbili za Man United na moja ya Chelsea, pengine akitaka kufuta makosa yake aliyofanya katika mechi kati ya Burnley na Blackburn.
Ferguson alilalamika: “Kitu ambacho sielewi ni Mshika Kibendera kuwa mbele ya Drogba na hakuna hata mtu aliemziba na haoni ofsaidi! Mechi kubwa kama ile unataka Marefa wenye ubora na hatukuwapata! Ni kazi mbovu kabisaa!”
Tangu wiki yote iliyopita Refa Mike Dean amekuwa akimulikwa sana na Vyombo vya Habari baada ya Straika wa Blackburn Martin Olsson kuungama alijidondosha kusudi kwa vile walijua Refa huyo hutoa penalti kirahisi na penalti hiyo ndio iliyowaua Burnley katika mechi ya Ligi wikiendi iliyopita.
Ushindi huo wa Chelsea umewafanya wawe pointi 2 mbele ya Man United huku mechi 5 zimebaki na Ferguson amesema: “Mechi 5 zimebaki, wako pointi 2 mbele na wana goli 4 bora kupita sisi! Hakika wapo nafasi nzuri! Lakini tutabadilika na tunao uwezo wa kushinda mechi zote 5 lakini pengine hata hilo lisitusaidie!”
Powered By Blogger