Wednesday 7 April 2010

Vitu Vitano vinavyoikabili Man United katika mechi na Bayern Munich leo!
Katika wiki moja, Manchester United wamekumbana na vipigo vikubwa viwili mfululizo pale walipofungwa 2-1 na Bayern Munich huko Ujerumani Jumanne iliyopita kwenye mechi ya kwanza ya Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI na Jumamosi wakafungwa tena 2-1 na Chelsea na kupokonywa uongozi wa Ligi Kuu.
Leo, ndani ya Uwanja wao Old Trafford, wanarudiana na Bayern Munich na wanahitaji ushindi wa bao 1-0 ili wasonge Nusu Fainali.
Lakini kuna Mchambuzi ameweka mambo matano bayana ambayo inabidi Man United wayakabili na kuyarekebisha ikiwa watataka kuifunga Bayer Munich leo.
Mambo hayo ni:
1. Beki wa Kulia:
Udhaifu wa nafasi hii umeonekana katika vipigo vya mechi hizo na Bayern na ile na Chelsea pale Mkongwe Gary Neville, miaka 35, aliposhindwa kuwadhibiti ipasavyo Frank Ribery na Florent Malouda.
Waziwazi, Sir Alex Ferguson ameogopa kumpanga Chipukizi Mbrazil Rafael da Silva ambae hana uzoefu.
Wengine ambao wangeweza kumudu nafasi hii ni John O’Shea na Wes Brown na wote ni majeruhi.
2. Kiungo
Siku za Paul Scholes kama injini zimepita na Darren Fletcher ameonekana chini ya kiwango katika mechi na Bayern na ile na Chelsea na hali kadhalika Michael Carrick.
3. Viungo Mawinga
Ferguson mara nyingi humchezesha Ji-sung Park kwenye mechi kubwa zinazohitaji nguvu kazi lakini wiki iliyokwisha kwenye mechi na Bayern alionyesha udhaifu na kumruhusu mara nyingi Beki wa kulia wa Bayern Philip Lahm kupanda na kufanya mashambulizi.
Nani anaweza kuchukua nafasi hii ingawa yeye si muhangaikaji lakini ujanja, mbinu na wepesi wake unaweza kuleta kizaazaa golini.
Giggs tangu aanze kucheza tena baada ya kuvunjika mkono hajarudi kwenye fomu.
4. Straika
Man United wakiwa kwenye fomu huwaendesha puta Wapinzani kwa spidi yao ya mashambulizi lakini kukosekana kwa Wayne Rooney na kuwepo kwa Dimitar Berbatov tu kunaikosesha Man United hiyo spidi.
Ferguson hana mbadala wa Rooney kwani Michael Owen ni majeruhi na waliobaki Federico Macheda na Mame Biram Diouf bado wachanga.
5. Historia
Historia ya Man United kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI inaonyesha wamebwagwa nje mara 4 kati ya 5 pale wanapoanza kufungwa katika mechi ya kwanza ya Mashindano haya.
Lakini mara hiyo moja waliyoibadili historia ni pale Msimu wa mwaka 2006/7 walipofungwa 2-1 huko Roma, Italia na katika marudiano Old Trafford, Man United wakaichabanga AS Roma bao 7-1.
Refa Mike Dean alieibeba Chelsea aadhibiwa!
Refa wa Ligi Kuu Mike Dean amepigwa stopu kuchezesha Ligi Kuu na wikiendi hii inayokuja ametupwa kuchezesha Daraja la chini ikiwa ni adhabu yake kwa kuchezesha vibaya mechi ya Manchester United na Chelsea Jumamosi iliyopita.
Pia, Mshika Kibendera wake, Simon Beck, ambae hakuashiria ofsaidi pale Drogba alipoifungia goli la pili Chelsea nae ametupwa kuchezesha Daraja la chini kwa makosa hayo.
Baada ya mechi hiyo, Sir Alex Ferguson aliwaponda Waamuzi hao na kuwaita wabovu na hawakustahili kuchezesha mechi kubwa.
Kabla ya mechi ya Man United na Chelsea uteuzi wa Refa Mike Dean kuchezesha mechi hiyo uliitwa ‘wehu’ na Meneja wa Burnley Brian Laws baada ya Refa huyo kuwapa Blackburn penalti feki na hivyo Burnley kufungwa wiki moja kabla.
Baada ya mechi hiyo ya Chelsea, Ferguson alisema alipofahamu Refa ni Mike Dean alipatwa na wasiwasi mkubwa.
Wenger anyoosha mikono kwa Messi!!
• Amfananisha na Mchezaji kwenye Gemu ya Kompyuta “PlayStation”!
Baada ya Lionel Messi kuifungia Barcelona bao zote 4 walipowanyuka Arsenal 4-1 na kuwabwaga nje ya Mashindano ya UEFA CHAMPIONS LIGI hapo jana Uwanjani Nou Camp, Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amekubali Mess indie Mchezaji Bora Duniani.
Wenger aliungama: “Yeye ni kama PlayStation! Katika mechi kubwa, Wachezaji wenye vipaji ndio huleta tofauti. Messi ndie Mchezaji Bora Duniani! Nawapa hongera Barcelona, walikuwa wazuri kupita sisi!”
Wenger aliendelea kumpamba Messi kwa kusema hukuadhibu kwa kila kosa unalofanya na pia kukiri kuwa kwa vile Messi ndio kwanza ana miaka 22 ana nafasi kubwa ya kujijenga na kuwa Mchezaji Bora kupita wote katika historia ya Soka.
Wenger alikiri wamevunjika moya kwa kutolewa UEFA na sasa wamebakiwa na LIgi Kuu ikiwa ndio nafasi pekee ya kutwaa Kombe Msimu huu.
Mechi yao inayofuata ya Ligi Kuu ni ile dabi ya Timu za Kaskazini ya Jiji la London watakapoenda Uwanja wa White Hart Lane kuikwaa Tottenham Jumatano ijayo.

No comments:

Powered By Blogger