Saturday 10 April 2010

LIGI KUU: TATHMINI MECHI ZA WIKIENDI
Ratiba ya Wikiendi
Jumamosi, 10 Aprili 2010
[saa 11 jioni]
Hull v Burnley
West Ham v Sunderland
Jumapili, 11 Aprili 2010
[saa 8 mchana]
Wolves v Stoke
[saa 9 na nusu mchana]
Blackburn v Man United
[saa 11 jioni]
Liverpool v Fulham
[saa 12 jioni]
Man City v Birmingham
------------------------------------------------------------
Wikiendi hii kuna mechi 6 tu na Jumamosi ni siku muhimu mno kwa Portsmouth wanaotegemewa kushushwa Daraja hasa baada ya kuporwa na Ligi Kuu pointi 9 na umuhimu huo kwa Portsmouth, ambao hawachezi mechi ya Ligi Kuu wikiendi hii na badala yake wapo Wembley Jumapili kucheza na Tottenham kwenye FA Cup, ni ule ukweli kwamba ikiwa Hull City wataifunga Burnley na West Ham kuifunga Sunderland, Portsmouth watajihakikishia kushuka Daraja na kucheza Ligi ya Coca Cola Championship Msimu ujao.
Hull City v Burnley
Timu zote hizi mbili zipo kwenye zile Timu 3 za mkiani zilizo hatarini kuporomoka Daraja huku Hull City wakiwa nafasi ya 18 pointi tatu juu ya Burnley na wana mechi moja mkononi.
Hull kidogo wanakuwa na nguvu wakiwa nyumbani na hilo linawapa matumaini makubwa ukichukulia pia katika mechi ya mwisho Burnley walidundwa bao 6-1 na Manchester City.
West Ham v Sunderland
West Ham walijitutumua mechi iliyopita na kutoka sare ugenini walipocheza na Everton na matokeo mazuri kwao katika mechii ni kitu cha lazima hasa kwa vile wako pointi moja tu juu ya zile Timu 3 zilizo hatarini kuporomoshwa Daraja.
Sunderland wako kwenye ari kubwa baada ya kuipiga Tottenham 3-1 mechi iliyopita na wapo pointi mbili tu kufikisha pointi 40 ambazo Meneja wao Steve Bruce anategemea wakizifikisha watapona kuwemo balaa la kushushwa Daraja.
Blackburn v Man United
Man United watakuwa Ewood Park huku wakitaka pointi 3 ili wakwae kilele kwa vile Chelsea hawachezi Ligi hadi Jumanne kwa vile wanacheza FA Cup na Aston Villa siku ya Jumamosi.
Lakini Blackburn ni wagumu kufungika kwao na wamefungwa mechi moja tu katika 15 zilizochezwa Uwanjani kwao Ewood Park.
Wolves v Stoke City
Wolves wako pointi 5 juu ya zile Timu 3 za mwisho na walipata bahati mbaya kukosa pointi katika mechi yao ya mwisho walipofungwa na Arsenal 1-0 dakika za mwishoni.
Stoke kidogo wako nafasi ahueni na wanatoka kwenye ushindi wa mechi mbili mfululizo.
Liverpool v Fulham
Liverpool wanawakaribisha Fulham Uwanjani Anfield huku Timu zote hizo zikiwa zinatoka kwenye mafanikio ya kuingia Nusu Fainali ya EUROPA LIGI waliposhinda mechi zao siku ya Alhamisi.
Ingawa Liverpool wanadai bado wanapigania kuitwaa nafasi ya 4 ya Ligi na hivyo kucheza UEFA Msimu ujao, ukweli ni kwamba wapo nafasi ya 6 pointi 4 nyuma ya Manchester City walio nafasi hiyo ya 4 na ambao pia wana mechi moja mkononi.
Ikiwa wanataka kuweka uhai matumaini yao ni lazima Liverpool waifunge Fulham.
Man City v Birmingham
Ni muhimu kwa Man City walio nafasi ya 4 washinde mechi hii ili waijengee zege nafasi hiyo ya 4 kwenye Ligi na kuweka pengo la pointi 4 kati yao na Tottenham walio nafasi ya 5.
Birmingham wako salama kwenye Ligi Kuu wakiwa nafasi ya 9 lakini hawajashinda katika mechi 5 sasa na katika mechi hii watamkosa Kipa wao nambari wani, Joe Hart, ambae haruhusiwi kucheza mechi hii kwa vile ni Mchezaji wa Man City na yupo Birmingham kwa mkopo.

No comments:

Powered By Blogger