Tuesday 6 April 2010

UEFA CHAMPIONS LIGI: Messi ailipua Ze Gunners!!
• Barca 4 Arsenal 1
Ndani ya Nou Camp, Arsenal walichokoza nyuki pale walipofunga bao dakika ya 18 kupitia Niklas Bendtner lakini ndani ya dakika mbili Mchezaji Bora Duniani Lionel Messi akaisawazishia Barcelona na akaongeza bao nyingine mbili kwenye dakika ya 37 na 42.
Hadi mapumziko Barcelona 3 Arsenal 1.
Kipindi cha pili, Barcelona walicheza kwa tahadhari na kupunguza kasi na kushambulia kwa nguvu wakiwaacha Arsenal wahangaike kupata bao.
Hata hivyo, Mchawi Lionel Messi hakuridhika na bao zake 3 na kwenye dakika ya 87 akafanya ndumba zake na kupachika bao lake la 4.
Hivyo Mabingwa Watetezi wa Ulaya, Barca, wametinga Nusu Fainali na watacheza na Inter Milan ambao katika mechi ya awali leo waliitoa CSKA Moscow walipowafunga 1-0.
Vikosi vilivyoanza:
Barcelona: Valdes, Dani Alves, Marquez, Milito, Abidal, Busquets, Xavi, Keita, Pedro, Bojan, Messi.
Akiba: Pinto, Iniesta, Henry, Maxwell, Toure Yaya, Fontas, Jeffren.
Arsenal: Almunia, Sagna, Vermaelen, Silvestre, Clichy, Denilson, Diaby, Walcott, Nasri, Rosicky, Bendtner.
Akiba: Fabianski, Eduardo, Eboue, Traore, Campbell, Merida, Eastmond.
Refa: Wolfgang Stark (Germany)
Ferguson ana imani Man United wataitwanga Bayern
Kwenye Uwanja wa nyumbani, Manchester United, kesho Jumatano wanarudiana na Bayern Munich kwenye Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI baada ya kufungwa 2-1 wiki iliyopita huko Ujerumani huku bao la pili likitinga dakika za majeruhi.
Manchester United wanahitaji bao moja tu kuibwaga Bayern Munich na Meneja wao Sir Alex Ferguson ana matumaini makubwa ya kupata ushindi.
Ferguson amesema: "Watu wengi wanaamini tuna nafasi nzuri. Na mimi nafikiria tuna nafasi nzuri sana!”
Ferguson ameongeza kuwa ana matumaini makubwa kwa mechi na Bayern kuliko alivyokuwa Jumamosi walipocheza na kufungwa 2-1 Chelsea kwenye Ligi Kuu.
Ferguson amedai kuingia Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI ni motisha kubwa kwa Wachezaji wake
Ingawa Manchester United wana goli la ugenini dhidi ya Bayern Munich na pia wanacheza nyumbani, wana pengo kubwa kwa kumkosa Mfungaji wao mkuu Wayne Rooney alieumia kwenye mechi ya kwanza na Bayern lakini kuna minong’ono huenda Rooney akawepo benchi na hilo limedokezwa hata na Ferguson mwenyewe.
Ferguson amesisitiza: “Goli la ugenini ni muhimu kwani soka la siku hizi magoli ni magumu kupata. Na tunacheza Old Trafford na tukiwa hapo magoli hutiririka kwani Washabiki wanatupa morali kubwa. Mara nyingi tumekuwa tukishinda dakika za mwisho na hilo si juu ya Wachezaji tu, ni Washabiki pia wanaoleta changamoto! Tunaombea Jumatano iwe hivyo!”
Alipoulizwa kama anategemea Chipukizi Macheda ambae ndie aliefunga bao la Man United Jumamosi na Chelsea ataanza hasa kwa vile Berbatov anapwaya, Ferguson alisema Macheda ataanza benchi lakini atapewa fursa ya kucheza.
Ferguson amesema: “Macheda ndio kwanza amepona musuli za miguu na bega vilivyokuwa vinamsumbua Msimu wote. Huyu ni kijana mwenye kipaji kikubwa!”

1 comment:

Anonymous said...

HATA CHELSEA WALIJUUWA HAPO HAPO NYUMBANI MBELE YA HAO WANOKUPA HAMASA. FAGIE ANASEMA SIASA YA SOKA LKN SI SOKA. SOKA DKK90

Powered By Blogger