Monday 5 April 2010

Newcastle leo pointi moja tu wamerudi Ligi Kuu!
Newcastle ambao walishushwa Daraja toka Ligi Kuu msimu uliokwisha leo wanacheza na Sheffield United Uwanjani St James Park kwenye mechi ya Ligi ya Coca Cola Championship na wanahitaji sare tu ili wapande Daraja kurudi tena Ligi Kuu.
Newcastle ndio wanaongoza Ligi hiyo wakiwa na pointi 86 kwa mechi 40 na wa pili ni West Bromwich Albion waliocheza mechi 42 na wana pointi 83.
Kila Timu inatakiwa icheze jumla ya mechi 46.
Timu mbili za juu za Ligi hii ndio hupanda Daraja moja kwa moja kwenda Ligi Kuu na Timu ya 3 mpaka ya 6 hupangiwa Mchujo maalum kuipata Timu moja itakayoungana na hizo Timu mbili za juu kwenda Ligi Kuu.
Mpaka sasa Timu zilizo nafasi ya 3 hadi ya 6 ni Nottingham Forest, Cardiff, Leicester City na Swansea huku Blackpool iko nafasi ya 7 na inanyemelea kwa dhati kuingia kundini.
UEFA CHAMPIONS LIGI: Nani kutinga Nusu Fainali?
Marudiano ya mechi za Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni hapo kesho Jumanne na Jumatano huku Wachezaji kadhaa wakubwa watazikosa mechi hizo kwa sababu mbalimbali wakiwemo Wayne Rooney, Carles Puyol, Gerard Pique, Zlatan Ibrahimovic, Cesc Fabregas, Andrei Arshavin, Lisandro Lopez na Milos Krasic.
RATIBA:
(Mabao ya mechi za kwanza kwenye mabango)
[saa 3 dak 45, bongo taimu]
Jumanne 6 Aprili
CSKA Moscow-Inter Milan (0-1)
Barcelona-Arsenal (2-2)
Jumatano 7 Aprili
Manchester United-Bayern Munich (1-2)
Bordeaux-Lyon (1-3)
TATHMINI:
CSKA Moscow v-Inter Milan:
Inter Milan wanasafiri hadi Moscow, Urusi kuulinda ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya CSKA Moscow kwenye Uwanja wa nyasi bandia ambao ni mgumu kuchezeka kama hukuuzoea.
CSKA Moscow watawakosa Wachezaji wao wawili hodari, Milos Krasic na Evgeni Aldoni na wenzao Inter Milan watawakaribisha tena Wachezaji wao Masentahafu walioikosa mechi ya kwanza, Lucio na Thiago Motta.
Barcelona v Arsenal:
Arsenal walijitutumua katika mechi ya kwanza ya Timu hizi na kulazimisha sare ya 2-2 lakini watawakosa Wachezaji wao bora Cesc Fabregas, William Gallas na Andrey Arshavin ambao wote waliumia katika mechi hiyo iliyochezwa Emirates.
Barcelona ingawa wako nyumbani na wanahitaji sare ya 0-0 au 1-1 ili wafuzu, wanakabiliwa na kuwakosa Wachezaji kadhaa wakiwemo Masentahafu wao wote wawili, Puyol na Pique, ambao wana Kadi.
Pia Barca watamkosa Mfungaji wao mkuu na ambae ndie alifunga bao zao mbili huko Emirates, Zlatan Ibrahimovic, alieumia. Lakini injini yao amabayo haikucheza Emirates, Andres Iniesta, amepona na ataonekana kilingeni.
Lengo la Barca katika mechi hii ni kupata ushindi wa haraka ili wacheze kilaini kwa vile wikiendi ijayo ni ‘EL CLASICO’ watakapowavaa Wapinza wao wakubwa Real Madrid Uwanja wa Bernabeau.
Manchester United v Bayern Munich
Kwa Manchester United, hii ni mechi kubwa mno na muhimu mno, ili kuokoa Msimu wao ambao umeingia dosari kubwa baada ya kufungwa mfululizo mechi mbili muhimu.
Balaa ilianza walipofungwa 2-1 na Bayern Munich katika mechi ya kwanza na mechi iliyofuata wakapigwa 2-1 na Chelsea waliowapokonya uongozi wa Ligi Kuu.
Bila shaka, marudiano na Bayern Munich ni mechi ya kufa na kupona na wanahitaji ushindi wa bao 1-0 tu ili watinge Nusu Fainali lakini huenda mambo yakawa magumu kwani Mfungaji wao mkuu, Wayne Rooney, aliumia katika mechi ya kwanza huko Ujerumani ingawa kuna tetesi Rooney huenda akawa fiti kucheza mechi hii ya marudiano siku ya Jumatano.
Bordeaux v Lyon:
Msimu wa Bordeaux ghafla umeanza kuharibika pale walipofungwa 3-1 na Marseille kwenye Fainali ya Kombe la Ligi la Ufaransa na mechi iliyofuata ni mkondo wa kwanza wa Mashindano haya ya UEFA walipopigwa 3-1 na Lyon kisha juzi kwenye Lique 1 wakapokonywa uongozi wa Ligi hiyo walipofungwa na Nancy bao 2-1.
Hata hivyo, kwa Bordeaux, habari za faraja kwao ni kule Lyon kumkosa Mfungaji wao bora Lisandro Lopez aliefungiwa na pia Veterani wa Lyon Govou kutokuwepo.

No comments:

Powered By Blogger