Sunday, 4 April 2010

Everton 2 West Ham 2
Timu inayopigana kufa na kupona ili kukimbia kushuka Daraja, West Ham, leo wakiwa ugenini Goodison Park, wamejitutumua na kulazimisha sare ya bao 2-2 na Wenyeji Everton.
Sare hii imeiweka Everton nafasi ya 8 wakiwa na pointi 50 na West Ham wako nafasi ya 17 wakiwa wamecheza mechi 33 na wana pointi 28 ikiwa ni pointi moja tu juu ya zile Timu 3 zilizo nafasi 3 za mwisho za kuteremshwa Daraja.
Everton walitangulia kufunga dakika ya 24 kwa bao la Diniyar Bilyaletdinov na lilipatikana pale Beki wa West Ham Jonathan Spector alipojaribu kuokoa lakini mpira ukamfikia Tim Cahill aliepiga kichwa golini na Mfungaji akausindikiza wavuni.
Kwenye dakika ya 39 Refa Webb aliwapa penalti West Ham baada ya Sylvain Distin kumchezea rafu Carlton Cole lakini Mido alipiga kiki hafifu ambayo Kipa wa Everton Tim Howard aliokoa.
Kipindi cha pili, West Ham walisawazisha kwenye dakika ya 59 baada ya kona iliyopigwa na Noble kuleta patashika ndani ya boksi na mpira ukamfikia Beki wa West Ham Manuel Da Costa aliouvurumisha wavuni.
Katika dakika ya 84, krosi ya Beki wa kushoto Leighton Baines ilimaliziwa kwa kichwa na Yakubu na kufanya Everton wawe mbele kwa bao 2-1.
Lakini bao hilo la Everton lilidumu dakika moja tu pale krosi ya Julien Faubert kupigwa kichwa na Mchezaji alietokea benchi la akiba Araujo Ilan na kuisawazishia West Ham.
Vikosi vilivyoanza:
Everton: Howard, Neville, Jagielka, Distin, Baines, Pienaar, Osman, Heitinga, Cahill, Bilyaletdinov, Saha.
Akiba: Turner, Hibbert, Yakubu, Senderos, Rodwell, Duffy, Wallace.
West Ham: Green, Faubert, Da Costa, Upson, Spector, Noble, Parker, Kovac, Behrami, Mido, Cole.
Akiba: Kurucz, Gabbidon, Ilan, McCarthy, Daprela, Spence, Stanislas.
Refa: Howard Webb

No comments:

Powered By Blogger