FA CUP: Aston Villa v Chelsea
Leo Chelsea inaivaa Aston Villa Uwanjani Wembley, Timu ambayo wiki mbili zilizopita waliiwasha bao 7-1 kwenye Ligi Kuu, kwenye Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la FA na Nusu Fainali nyingine itachezwa kesho hapo Wembley kati ya Portsmouth na Tottenham.
Fainali itakuwa pia Uwanjani Wembley Mei 15.
Wiki mbili zilizopita, Uwanjani Stamford Bridge, Chelseaa ilitwanga Aston Villa 7-1 na Frank Lampard alipiga bao 4 peke yake.
Lakini Nahodha wa Chelsea, John Terry, ametahadharisha: “Hii itakuwa mechi tofauti kabisa. Villa wamekasirika kufungwa 7 na safari hii watakuwa na Wachezaji wao ambao hawakucheza mechi ile.”
Na Meneja wa Aston Villa, Martin O’Neill, amesema Timu yake ina nia ya kufika Fainali yao ya pili Msimu huu na kufanikiwa baada ya kufungwa kwenye Fainali ya Kombe la Carling na Manchester United bao 2-1 mwezi Februari.
Aston Villa na Chelsea zimeshakutana mara 140 na Villa wameshinda mara 55 na Chelsea mara 52.
Vikosi vinavyotarajiwa kuanza:
Aston Villa (Fomesheni 4-4-2): Friedel; Cuéllar, Dunne, Collins, Warnock; A Young, Petrov, Downing, Milner; Carew, Agbonlahor.
Chelsea (Fomesheni 4-3-3): Cech; Ferreira, Alex, Terry, Zhirkov; J Cole, Ballack, Lampard; Anelka, Drogba, Malouda.
Refa: Howard Webb [amechezesha mechi 34, Kadi Nyekundu 4, Kadi za Njano 123]
Wasaidizi wa Refa: Mike Mullarkey na Darrren Cann
Refa wa Akiba: Mark Clattenburg
Ronaldo akata tamaa Brazil
Mkongwe na Supastaa Ronaldo, anaeongoza kwa ufungaji wa jumla ya mabao mengi katika Fainali za Kombe la Dunia akiwa na bao 15, amekiri kuwa hawezi kuchukuliwa na Brazil kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini.
Ronaldo, miaka 33, siku hizi anachezea Klabu ya Corinthians huko Brazil na mara ya mwisho kuichezea Brazil ni Robo Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2006 walipotolewa na Ufaransa na hiyo ilkuwa mechi yake ya 97 kuichezea Brazil na kufunga jumla ya bao 62 kwa Timu hiyo.
Ronaldo amesema: “Nimecheza mechi chache Msimu huu hivyo sistahili kuichezea Brazil, hilo ni wazi! Lakini nikiitwa ntaitika-Brazil ni Nchi yangu!”
Fergie atetea kuwabwatia Bayern
Sir Alex Ferguson amegoma kuufuta usemi wake ‘hii ni tabia halisi ya Wajerumani’ alioutoa baada ya Bayern Munich kuitoa Manchester United kwa mabao ya ugenini siku ya Jumatano na kauli hiyo inafuatia lawama zake kwa Wachezaji wa Bayern Munich kwa kumshinikiza Refa Nicola Rizzoli kutoka Italia ili ampe Chipukizi toka Brazil Rafael Kadi na Refa huyo kweli akamlamba Kadi ya pili ya Njano na kuifanya Manchester United icheze mtu 10 kwa dakika 40 za kipindi cha pili na kutoa mwanya kwa Bayern kupata bao muhimu la pili lililowapeleka Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Ferguson alibwata mara baada ya mechi: “Kulikuwa hamna kipingamizi sisi kushinda tukiwa 11, wao walikuwa wamezidiwa! Lakini Rafael alionyesha uchanga wake na wao wakalazimisha atolewe! Kila Mchezaji wao alimkimbilia Refa- hii ni tabia halisi ya Wajerumani!”
Kocha wa Bayern Munich, Louis van Gaal, na Rais wake, Uli Hoeness, walikerwa na kauli hiyo na sasa Ferguson ameamua kuweka mambo sawa bila ya kufuta kauli yake.
Ferguson amedai jazba ilimtawala kwani alitoa kauli hiyo mara tu baada ya mechi lakini amesema wa kulaumiwa zaidi ni Wajerumani wenyewe kwa kumshikiza Refa wakijua Rafael tayari ana Kadi ya Njano.
Allardyce agoma kumsaidia Rafikiye Fergie
Meneja wa Blackburn Rovers, Sam Allardyce, majuzi alikuwa pamoja na Rafiki yake Sir Alex Ferguson walipokwenda pamoja huko Aintree kuangalia Mbio za Farasi na akanufaika pale Ferguson alipombonyeza aweke dau kwa Farasi aitwae “What a Friend” anaemilikiwa na Ferguson na kweli Farasi huyo akashinda na Allardyce akaambua kitita ambacho hakikutajwa.
Jumapili, Backburn inaikaribisha Manchester United huko Ewood Park katika mechi ya Ligi Kuu mbayo ni muhimu sana kwa Manchester United walio pointi mbili nyuma ya vinara Chelsea kwani ushindi utawarusha juu ya Chelsea ambao wikiendi hii hawachezi Ligi na wako kwenye Nusu Fainali ya FA Cup.
Allardyce amesema: “Ilikuwa siku nzuri huko Aintree na Ferguson kutubonyeza kumenifanya mimi na Wafanyakazi wengine wa Blackburn tupate vijisenti mfukoni! Lakini hilo haliwasaidii Man United Jumapili! Hii ni dabi ya Timu za Kaskazini na sisi tukiwa Ewood Park tunaweza kucheza na Timu bora- kama tulivyowaonyesha Chelsea [sare 1-1]!”
No comments:
Post a Comment