Karata ya mwisho kwa Liverpool leo!!
Liverpool leo watasali kila namna ili kuomba Uwanja wao wa Anfield uwape matokeo mema pale watakapojaribu kugeuza kipigo cha 2-1 walichopewa na Benfica wiki iliyokwisha katika Robo Fainali ya EUROPA LIGI huku wakijua fika hii ndio nafasi pekee kwao kuweza kutwaa Kombe Msimu huu.
Wiki iliyopita huko Ureno, Daniel Agger aliwapa Liverpool bao la kuongoza lakini bao mbili za penalti za kipindi cha pili zilizopigwa na Oscar Cardozo ziliwapa Benfica ushindi wa 2-1.
Meneja wa Liverpool Rafa Benitez ametamba kuwa wana uwezo wa kuichapa Benfica hapo Anfield na katika kuhakikisha hilo, Benitez alimtoa Staa wake Fernando Torres katika mechi ya Ligi Kuu hapo Jumamosi Liverpool ilipotoka sare 1-1 na Birmingham ili apate kupumzika vizuri.
Katika mechi ya leo, Liverpool itamkosa Winga Ryan Babel ambae alipewa Kadi Nyekundu huko Ureno Benfica ilipoikaribisha Liverpool.
Wakati Liverpool wanataka kukipindua kipigo, wenzao Fulham pia leo wamo kwenye kinyang’anyiro cha EUROPA LIGI na wako Ujerumani kucheza na Wolfsburg na wao Fulham wanataka kulinda ushindi wao wa 2-1 walioupata katika mechi ya kwanza wiki iliyopita.
Meneja aliemwita Refa muongo kumkabili Pilato wa FA!!
Meneja wa Wigan Roberto Martinez anatakiwa na FA ajibu mashitaka ya kutokuwa na tabia nzuri kwa kosa la kudai Refa Stuart Attwell ni ‘muongo’ kauli aliyoitoa mara baada ya kipigo cha 3-0 toka kwa Manchester City na goli zote hizo ziliingia baada ya Beki wao Gary Caldweel kupewa Kadi Nyekundu na Refa huyo.
Caldwell alipewa Kadi hiyo dakika ya 56 huku mechi ikiwa 0-0 baada ya kumchezea rafu Carlos Tevez na baada ya hapo Tevez akafunga bao zote 3 ndani ya dakika 12.
Baada ya mechi, Martinez alimlaumu Refa na kusema hakuona wakati Caldwell anagongana na Tevez hivyo kutoa uamuzi kwa kitu ambacho hakikuona ni uongo.
FA ilimwandikia barua Martinez kutaka maelezo yake na sasa imeamua kufungua mashitaka.
Martinez amepewa hadi Aprili 22 kuwasilisha utetezi wake.
No comments:
Post a Comment