FA CUP: Pompey wapo Wembley licha ya mabalaa kibao!!
Jumapili, Portsmouth wanaingia Uwanja wa Wembley kucheza Nusu Fainali ya Kombe la FA na Tottenham wakiwa Klabu tofauti kabisa na ile ya mwaka 2008 iliyoingia Wembley na kutwaa Kombe hilo kwa kuifunga Cardiff City bao 1-0, bao alilofunga Nwankwo Kanu huku Meneja wa Timu akiwa Harry Redknapp.
Portsmouth ya sasa ni Klabu iliyobomoka kwa madeni na katika miezi 9 iliyopita imekuwa ikibadili Wamiliki kila kukicha, ipo mkiani Ligi Kuu na huenda ikawa tayari imeshashuka Daraja hiyo Jumapili ikiwa Hull City na West Ham zinazocheza mechi za Ligi Kuu Jumamosi zikishinda mechi zake.
Portsmouth inakutana na Tottenham kwenye Nusu Fainali ya FA Cup ambayo inaongozwa na aliekuwa Meneja wao Harry Redknapp na mbali ya hilo Klabu hizi mbili zinajuana fika kwa vile Portsmouth inao Wachezaji wanne waliowahi kuichezea Tottenham na Tottenham pia inao Wachezaji wanne waliowahi kuichezea Portsmouth.
Lakini si Wachezaji wote hao wanane watacheza Jumapili.
Jamie O’Hara hawezi kuichezea Portsmouth kwani yupo hapo kwa mkopo akitokea Tottenham.
Younes Kaboul yupo Tottenham lakini ashacheza Portsmouth mechi za awali za Kombe hili Msimu huu na hivyo haruhusiwi kucheza.
Nwankwo Kanu aliefunga bao la ushindi na kuwapa Pompey Kombe la FA mwaka 2008 ni mmoja wa Wachezaji wanne waliocheza Fainali hiyo ambao bado wapo Portsmouth.
Wengine ni Kipa David James, Hermann Hreidarsson na John Utaka.
Kanu alizungumza na kusema itawabidi Wachezaji kujituma kwa zaidi ya asilimia mia moja ili kushinda Kombe la FA kwani ni kitu pekee cha kuwapa Mashabiki wao kwa uvumilivu wao na sapoti yao licha ya matatizo makubwa ndani ya Klabu.
Hata hivyo Kanu amekiri Tottenham, kwa mtazamo wa wengi, ndio wenye nafasi kubwa ya ushindi.
Wiki mbili zilizopita, Tottenham iliifunga Portsmouth 2-0 kwenye Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment