Thursday 10 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Fergie: ‘Hamna mabadiliko makubwa Man United!”
Sir Alex Ferguson amerudia tena kauli yake kwamba hakutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye Kikosi chake kwa ajili ya Msimu ujao na amesisitiza kuwa Kikosi kilichopo ni kizuri na kina uwezo wa kugombea Vikombe vikubwa.
Tangu auzwe Cristiano Ronaldo kwa Pauni Milioni 80 Mwaka jana ni Antonio Valencia, Chris Smalling na Javier Hernandez aka Chicharito ndio Wachezaji wapya walionunuliwa kwa thamani ndogo mno ambayo pengine haifiki robo ya thamani ya Ronaldo.
Mkurugenzi Mtendaji David Gill amekuwa akisisitiza na kuwapoza Washabiki kila mara kuwa fedha za kununua Wachezaji zipo ila ni juu ya Ferguson kuamua ni nani anamtaka.
Lakini Ferguson amekuwa na msimamo na mtizamo tofauti na amesema: “Kwa miaka mingi tumefanya juhudi kubwa kuwakuza Wachezaji Vijana na kuwaendeleza. Inabidi tutathmini hilo na labda tutaongeza Wachezaji wawili au mmoja.”
Fergusona akaongeza: “Soko la Wachezaji siku hizi ni gumu na hata hivyo Kikosi chetu ni kizuri. Msimu ujao tutapigana kurudisha Ubingwa nyumbani kwake na mahala bora Duniani.Tutarudi tena mwakani, siku zote Manchester United hufanya hivyo!”
Man City wambakisha Vieira
Manchester City wametangaza Kiungo Patrick Vieira atabakia hapo baada ya kumuongezea Mkataba wa Mwaka mmoja.
Viera, Miaka 33, alijiunga kutoka Inter Milan Mwezi Januari kwa Mkataba wa Miezi 6 na sasa atabaki Man City hadi mwishoni mwa Msimu ujao wa Mwaka 2010/11.
Msimu uliopita aliichezea Man City mechi 14.
Viera alishawahi kucheza Ligi Kuu akiwa na Arsenal aliokaa nao Miaka 9 hadi alipohama Mwaka 2005 kwenda Juventus.
Wachezaji Afrika Kusini wakiri mchecheto!!
Wachezaji wa Timu ya Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia, Afrika Kusini, wamekiri kuwa wanapatwa na wasiwasi kadri Ijumaa inapozidi kukaribia kwa ajili ya mechi yao ya ufunguzi na Mexico itakayochezwa Uwanja wa Soccer City huko Kitongoji cha Soweto Jijini Johannesburg.
Mshambuliaji wa Bafana Bafana, Bernard Parker, amesema: “Kadri ijumaa inavyokaribia tunapatwa na mchecheto! Fikra zetu zote hatutaki kuwaangusha Watu wetu!”
Hali hiyo imeungwa mkono na Winga Siphiwe Tshabalala lakini amesema kwa vile Taifa lote liko nyuma yao wanapata moyo mkubwa.
Afrika Kusini haijafungwa katika mechi 12 za majaribio walizocheza wakiwa chini ya Kocha toka Brazil Carlos Alberto Pereira.
Nae Kipa wa Bafana Bafana, Itumeleng Khune, amesisitiza: “Tunajua umuhimu wa kushinda mechi ya kwanza! Tupo nyumbani mbele ya Mashabiki wetu na hilo litatupa nguvu zaidi!”
Mitaa ya Johannesburg imetapakaa uzalendo wa kila aina kiasi cha kumfanya Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kuielezea hali hiyo ni nzuri kwani inaunganisha Taifa na ni manufaa makubwa kwa kuleta mshikamano kwa Watu wa rangi na asili tofauti Nchini humo na ametabiri hilo litadumu na kutawala muda mrefu.
Wengi wanategemea mengi toka kwa Bafana Bafana na wengi hawatachoka kupuliza Vuvuzela.

No comments:

Powered By Blogger