Thursday, 29 April 2010

Ni Usiku wa EUROPA!!!
Liverpool v Atletico Madrid
Liverpool wako nyumbani Anfield wakijaribu kuambulia kitu Msimu huu baada ya kupoteza mwelekeo katika Mashindano yote lakini inabidi waupindue ushindi wa bao 1-0 walioupata Atletico Madrid kwenye mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ili watinge Fainali.
Hii ni mara ya tatu kwa Liverpool kufungwa mechi za kwanza katika EUROPA LIGI na kisha kuibuka kidedea mechi za marudiano dhidi ya Lille na Benfica.
Hata hivyo Liverpool wana kazi kubwa kulifuta goli la Mchezaji wa zamani wa Manchester United Diego Forlan hasa kwa vile wana matatizo kwenye safu ya mashambulizi kwa kukosekana Fernando Torres ambae ni majeruhi na pia kuna hati hati kuhusu kucheza kwa Dirk Kuyt na David Ngog kwani nao pia wana maumivu.
Pia Maxi Rodriguez haruhusiwi kucheza leo baada ya kuwahi kuichezea Atletico awali kwenye Mashindano haya.
Atletico wataongezeka nguvu baada ya Straika wao kutoka Argentina Sergio Aguero kumaliza kifungo cha mechi moja na hivyo atashirikiana na Diego Forlan mbele na pembeni watakuwepo Mawinga Antonio Reyes, Mchezaji wa Arsenal zamani, na Simao Sabrosa.
Fulham v Hamburg
Baada ya sare 0-0 ugenini huko Ujerumani, Fulham watajihisi wana nafasi nzuri sana kuwashinda Hamburg leo na kuingia Fainali hasa ukizingatia Hamburg ni goigoi na wikiendi iliyopita waliwashwa bao 5-1 na Hoffenheim kwenye Bundesliga na ikabidi Kocha wao Bruno Labbadia atimuliwe kufuatia matokeo hayo pamoja na kushinda mechi 3 tu kati ya 14 za nyuma yake.
Hata hivyo motisha pekee kwa Hamburg ni kutambua kwao kuwa Fainali ya EUROPA LIGI Msimu huu itafanyika Uwanjani kwao Nordbank Arena hapo Mei 12.
Fulham wana wasiwasi mkubwa kuhusu Mfungaji wao mkuu Bobby Zamora ambae ana maumivu ya mguu.
Pia watamkosa Chris Baird ambae amefungiwa mechi hii lakini nafasi yake itazibwa kirahisi na Beki toka Ghana John Pantsil ambae amepona.

No comments:

Powered By Blogger