Saturday 24 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

MATOKEO Mechi za Kirafiki Julai 23:
Ajax Amsterdam 3 v Chelsea 1
Deportivo la Coruna 1 v FC Twente 1 [FC Twente yashinda penalti 5-4]
Freiburg 1 v Werder Bremen 2
Panathinaikos 0 v West Ham 1
Manchester City 0 v Sporting Lisbon 2
Kocha adai amepewa ofa kuifundisha Brazil
Meneja wa Fluminense, Muricy Ramalho, amedai kuwa amepewa ofa ya kuchukua nafasi ya Dunga, alietimuliwa, kuifundisha Brazil lakini bado hajaikubali ofa hiyo.
Ramalho aliweza kutwaa Ubingwa wa Brazil mara 3 mfululizo kati ya 2006 na 2008 akiwa na Fluminense.
Ramalho amedai bado hajaongea na Viongozi wa Fluminense ili kuamua hatma yake.
Brazil ndio watakuwa Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014.
Chelsea watwangwa
Jana huko Amsterdam Arena, Uholanzi, Chelsea walichapwa bao 3-1 na Ajax Amsterdam.
Chelsea wako kwenye ziara ya Uholanzi na Ujerumani kwa ajili ya matayarisho ya Msimu mpya.
Huku wakichezesha Wachezaji Vijana wengi, Chelsea walijikuta wako nyuma dakika ya 6 tu baada ya Beki wao Jeffrey Bruma kujifunga mwenyewe.
Lakini dakika ya 25 Straika Daniel Sturridge alisawazisha.
Dakika mbili baadae Kipa wa Chelsea Turnbull alifanya kosa kubwa mpira ulipomponyoka na kumfikia Siem de Jong aliefunga kirahisi.
Dakika za mwishoni, Mchezaji toka Korea, Suk Hyunpjun aliifungia Ajax bao la 3 baada ya pasi ya Daley Blind.
Fulham wamlenga Eriksson na Hitzfeld
Baada ya Ajax Amsterdam kuwawekea ngumu kumchukua Kocha Martin Jol ambae tayari walishakubaliana maslahi binafsi, taarifa za toka ndani ya Klabu zinasema Fulham sasa inawataka ama Sven-Goran Eriksson, aliekuwa Kocha wa Ivory Coast huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia, au Ottmar Hitzfeld, Kocha wa Uswisi.
Eriksson, ambae Mkataba wake na Ivory Coast ulikuwa wa muda mfupi na ulikwisha tu mara baada ya Kombe la Dunia,  mwenyewe anataka kuifundisha Fulham licha ya Ivory Coast kutaka aendelee nao.
Mkataba wa Hitzfeld kwa Timu ya Taifa ya Uswisi unamalizika 2012.
Kwa sasa Fulham iko chini ya usimamizi wa Kocha Msaidizi Ray Lewington.
Vidic aukubali Mkataba mpya
Mkurugenzi Mkuu wa Manchester United, David Gill, ametangaza kuwa wamefikia makubaliano na Nemanja Vidic kuhusu Mkataba mpya na hivyo kuufuta utata wa kubaki kwake Manchester United.
Kumekuwa na habari kuwa Vidic yuko njiani kwenda Real Madrid lakini Gill ameziua habari hizo kwa kutamka: “Mwishoni mwa Msimu uliokwisha tulikaa pamoja na Vidic lakini hatukumaliza na Vidic akaenda kwenye Kombe la Dunia. Lakini baada ya Serbia kumaliza Kombe la Dunia tuliendelea tena kujadiliana na tumeshakubaliana. Atasaini akirudi toka likizo.”
Vidic alijiunga Man United kutoka Spartak Moscow Mwaka 2006 kwa Pauni Milioni 7 na Mkataba wake wa sasa kwa Man United utakwisha 2012.
Inasadikiwa Mkataba mpya una nyongeza ya Miaka miwili na pia Mshahara kupanda toka Pauni 70,000 kwa Wiki hadi 90,000.

No comments:

Powered By Blogger