Man City yampuuza Drogba
Manchester City imezipuuza taarifa za kutaka kumchukua Didier Drogba ambazo Wakala wa Mchezaji huyo wa Chelsea amezitangaza.
Wakala huyo, Thierno Seydi, alidokeza kwenye mahojiano na Kituo kimoja cha Radio kuwa Drogba anaweza kuhama kutoka Chelsea kabla dirisha la uhamisho halijafungwa kwa vile yapo mazungumzo baina yao.
Lakini Man City, ambao tayari wameshatumia Pauni Milioni 60 kuwanunua Jerome Boateng, David Silva na Yaya Toure kwa ajili ya Msimu mpya, wamekanusha madai hayo na kusema hayana ukweli.
Drogba, Miaka 32, ndie alikuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Msimu uliokwisha kwa kupachika mabao 29 na amekuwapo Chelsea kwa Miaka 6 tangu ahamie hapo kutoka Marseille ya Ufaransa.
Seydi, akiongea na Radio RMC ya Ufaransa, alitamka: “Leo yupo Chelsea. Pengine kutakuwa na maajabu kabla ya Agosti 31. Sijaongea na Mtu yeyote ila ni Man City tu! Sisi tunamsikiliza kila Mtu”
Skandali zaiandama Ufaransa!!!
Baada ya kubwagwa nje ya Kombe la Dunia huko Afrika Kusini Raundi ya Kwanza tu na kushika mkia Kundi lao, Ufaransa, iliyogubikwa na kashfa ya ugomvi uliomfanya Mchezaji Nicolas Anelka afukuzwe huko Afrika Kusini na Wachezaji kugomea mazoezi, imetumbukizwa tena kwenye kashfa nzito baada ya uchunguzi wa Polisi uliokuwa ukizizima chini kwa chini kuibuka ghafla na kusababisha leo Wachezaji Mastaa, Franck Ribery na Karim Benzema, kuitwa Polisi na kuhojiwa kuhusu madai ya kutoa malipo ili kufanya ngono na Kahaba alie na umri mdogo ambao kisheria ulikuwa ukimtambua kama mtoto.
Uchunguzi wa Polisi ulianza tangu Aprili baada ya kuivamia Baa ya usiku huko Paris, Ufaransa na madai ya Kahaba huyo, Zahia Dehar, kwamba alitembea na Wachezaji wawili wakati umri wake ukiwa mdogo.
Hata hivyo, kitu kizuri kwa Benzema na Ribery, ni kuwa Zahia, mwenye Miaka 16, akiwa Miaka miwili chini ya umri unaoruhusiwa kwa Wafanyakazi halali wa ngono huko Ufaransa, amedai hakuwaambia Wachezaji hao kuwa alikuwa chini ya umri halali kwa Wafanyakazi wa fani hiyo.
Kisheria huko Ufaransa, kauli ya Zahia itawanusuru Mastaa hao.
Wote, Ribery, anaecheza Bayern Munich, na Benzema wa Real Madrid, wamekanusha kufanya kosa lolote.
Wakati Benzema amesema hahusiki na Binti huyo, Ribery amekiri kutembea nae lakini amesisitiza hakujua kama alikuwa ni chini ya umri halali.
Wakili wa Ribery, Sophie Bottai, amezungumza kuwa Mteja wake hastahili kuwa Kituo cha Polisi bali Uwanja wa Mpira.
Bottai amedai: “Uhalifu huu anaotuhumiwa, kisheria, lazima uwe na kusudio: inabidi awe anajua umri wa huyo Binti, na hilo hakujua! Inabidi huyo Binti awe anaonekana kama ni mdogo, hilo halikuwepo! Na inabidi Binti huyo adai alimwambia kuwa yeye ni mtoto, na hilo, pia, halikuwepo!”
Huko Ufaransa, ukipatikana na hatia ya kudai au kufanya ngono na Kahaba alie chini ya umri halali adhabu yake ni kifungo cha mpaka Miaka mitatu na faini ya Pauni 38,000.
Lakini ni jukumu la Upande wa Mashitaka kuthibitisha kuwa Mtuhumiwa aliujua umri wa Kahaba.
No comments:
Post a Comment