Habari kwa ufupi:
-Benitez aukataa mkataba mpya Liverpool
Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, ameukataa mkataba mpya ambao ungemweka Liverpool kwa miaka mitano zaidi kwa sababu haumpi uhuru na madaraka ya kuchukua Wachezaji anaowataka na badala yake madaraka na uamuzi wa mwisho unabaki kwa wamiliki wa Klabu hiyo ambao ni Wamarekani wawili waitwao Tom Hicks na George Gillette.
Benitez amekuwa Liverpool tangu Juni 2004.
-Manucho aenda Hull City kwa mkopo
Fowadi kutoka Angola Manucho ambae ni Mchezaji wa Manchester United ameenda Klabu ya Hull City kwa mkopo hadi msimu huu utakapoisha.
Msimu uliokwisha Manucho alikuwa Panathinaikos vilevile kwa mkopo na tangu arejee Manchester United amecheza mechi moja tu na uhamisho wake kwenda Hull City ni kumpa nafasi ya kupata uzoefu wa kucheza LIGI KUU kwani akibaki Man U ni vigumu kuwapiku akina Rooney, Berbatov na Tevez na kupata namba.
-Pennant njiani kuhamia Portsmouth
Winga Jermaine Pennant wa Liverpool ambae kwa sasa hana namba kwenye kikosi hicho yuko mbioni kuhamishiwa Portsmouth.
Pennant alijiunga na Liverpool Julai 2006 akitokea Arsenal na ameshaichezea Liverpool mechi 81 na sasa atajiunga na Timu inayoongozwa na Meneja Tony Adams ambae wanafahamiana tangu walipokuwa wote Arsenal wakati huo Tony Adams akiwa ndie Nahodha wa timu hiyo.
-Mukukula atua Bolton
Ariza Mukukula, mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwa sasa ni raia wa Ureno, amehamia Bolton Wanderers kwa mkopo akitokea Klabu ya Ureno Benfica.
Mukukula, umri miaka 27, amekuwa hana namba ya kudumu hapo Benfica msimu huu na ameshawahi kuichezea Timu ya Taifa ya Ureno mara 4. Vilevile amewahi kushinda Kombe la UEFA mwaka 2006 alipokuwa akichezea Sevilla ya Spain.
-Rais wa Real Madrid Ramon Calderon ajiuzulu baada ya kugundulika aliiba kura za uchaguzi wake!!!!
Rais wa Klabu ya Spain Real Maldrid, Ramon Calderon, amelazimika leo kujiuzulu baada ya kugundulika aliiba kura wakati wa uchaguzi wa kuthibitisha nafasi yake kama Rais wa klabu hiyo hapo Desemba pale alipowapenyeza watu kumpigia kura wakati walikuwa hawana sifa za kupiga kura kufuatana na kanuni za klabu hiyo.
Baada ya kuibuka kashfa hiyo siku chache zilizopita, Calderon alijitetea hawajui watu hawo na akachukua hatua ya kumfukuza kazi Mkurugenzi aitwae Luis Barcena aliesimamia na kuendesha uchaguzi huo lakini Gazeti la Spain lenye kuaminika huko liitwalo Marca lilitoa picha zinazoonyesha baadhi ya wapigaji kura hao wasio halali wakiwa na Kaka wa Calderon aitwae Ignaciao na mtoto wa Calderon, Jamie.
Calderon alishinda Urais huo wa Real Madrid kwa kuahidi kuwanunua Wachezaji nyota Cristiano Ronaldo wa Manchester United, Fabregas wa Arsenal na Arjen Robben.
Mpaka sasa ameweza kutimiza ahadi ya kumchukua Robben tu na kushindwa kuwapata hao wengine wawili.
Hivi majuzi tu wakati Rais huyo wa Real Madrid akimtambulisha Mchezaji mpya toka Holland, Klaas-Jan Huntelaar, mashabiki waliojazana hapo walimpigia kelele na kumzomea Ramon Calderon: 'Yuko wapi Ronaldo!!!!'.
No comments:
Post a Comment