Wednesday 12 May 2010

FAINALI: Fulham v Atletico Madrid
HSH Nordbank Arena, Hamburg, Ujerumani
SAA 3 DAKIKA 45 USIKU [Bongo Taimu]
Ni hatua ya kushangaza kwa Fulham leo kutinga Fainali ya EUROPA LIGI kwa kucheza na Atletico Madrid Uwanjani HSH Nordbank Arena Mjini Hamburg, Ujerumani.
Ni hatua ya kushangaza kwa vile hakuna alietegemea Fulham watafika Fainali kwa kuwabwaga Vigogo wa Italia Juventus, Mabingwa Watetezi wa UEFA CUP ambalo Msimu huu ndio linachezwa kwa mara ya kwanza kama EUROPA LIGI, Shakhtar Donetsk, na pia kuwasimamisha Hamburg kwenye Nusu Fainali wakati ilikuwa wazi kabisa Fainali hii itachezwa nyumbani kwa Hamburg Uwanja wa HSH Nordbank Arena.
Kwa kuipa Fulham mafanikio haya, Meneja wao Roy Hodgson, amepewa Tuzo ya Meneja Bora wa Msimu na LMA, Chama cha Mameneja wa Ligi hasa wakitambua Hodgson alitua katikati ya Msimu wa 2007/8 huku Timu ikiwa mkiani lakini akainusuru kushushwa Daraja.
Leo Fulham wanapambana na Timu yenye uzoefu kupita wao, Atletico Madrid iliyo chini ya Meneja Quique Sanchez Flores, ambayo ina Wachezaji mahiri kina Diego Forlan, Sergio Aguero na Jose Antonio Reyes.
Atletico Madrid hawajapata Vikombe vikubwa tangu washinde Ligi pamoja na Kombe la Mfalme huko kwao mwaka 1996 na mara ya mwisho kufanikiwa Ulaya ni mwaka 1962 walipotwaa Kombe la Washindi.
Kila Timu inategemewa kuwakilishwa na Mastaa wao huku Fulham wanategemewa kumchezesha Mfungaji wao mahiri Bobby Zamora akiwa amedungwa sindano ya maumivu na anategemewa kufanyiwa upasuaji mguu baada ya mechi hii ya Fainali na operesheni hiyo imemfanya akose kuitwa kwenye Kikosi cha England cha Kombe la Dunia.

No comments:

Powered By Blogger