Friday 14 May 2010

KWINGINEKO ULAYA: Kitimtim Italia, Spain wikiendi hii!!
Ligi za Ujerumani na England zilimalizika wikiendi iliyopita na wikiendi hii Ligi za Italia, Spain na Ufaransa zinafikia tamati.
Huko Ufaransa tayari Marseille wameutwaa Ubingwa wa Ligue 1 baada ya kuukosa tangu 1992 lakini huko Italia na Spain Bingwa bado hajapatikana na atajulikana baada ya mechi za mwisho wikiendi hii.
Ifuatayo ni hali halisi na jinsi kitimtim kilivyo:
LA LIGA: Nani Bingwa Barca au Real?
Ni Mabingwa Watetezi FC Barcelona au Real Madrid ndio watavikwa Ubingwa wikiendi hii ingawa Barcelona ndie mwenye nafasi kubwa kwa vile yuko pointi moja mbele ya Real Madrid na hata akifungwa mechi yake ya mwisho na Real kutoka sare, na hivyo Timu hizo kufungana pointi, bado Barca wana nafasi kwa sababu tu waliwafunga Real mechi zote mbili za La Liga Msimu huu.
Barca wako nyumbani Nou Camp kucheza na Valadolid ambao wako hatarini kuteremshwa Daraja na Real wako safarini nyumbani kwa Malaga ambao pia wako hatarini.
SWALI:
Je Barca watatwaa Ubingwa kwa mara ya 20 au Real ndio Bingwa kwa mara ya 32?
MSEMO:
“Nimefurahia Msimu huu! Ni kampeni bora lakini si lazima tuwe Mabingwa ingawa upo uwezekano!” Cristiano Ronaldo wa Real Madrid.
SERIE A: Inter mbioni kutwaa Mataji Matatu!!
Baada ya kunyakua Coppa Italia wiki iliyopita na kuwemo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI watakapoivaa Bayern Munich wiki ijayo, Jumapili Inter Milan, chini ya Kocha machachari na mwenye vituko, Jose Mourinho, wanaweza kutwaa Kombe lao la pili ikiwa wataifunga Siena, Timu ambayo tayari ishaporomoshwa toka Serie A,na kutwaa Ubingwa wa Serie A.
Lakini ikiwa Inter Milan watateleza na AS Roma kuifunga Chievo Verona basi AS Roma watatwaa Ubingwa wa Serie A.
MSEMO:
“Ni ngumu kuifikiria Siena wakati tuna Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI siku chache baadae! Nataka Wachezaji wangu wawe Mabingwa wa Ulaya!” Jose Mourinho, Meneja wa Inter Milan.

No comments:

Powered By Blogger