Sunday 9 May 2010

Zimebaki Siku 2 Capello kuitangaza England
Gumzo, mijadala na minong’ono ipo kila kona Wadau wakimsubiri Fabio Capello, Meneja wa England, kutangaza Kikosi cha awali cha England cha Wachezaji 30 ili hatimaye kipunguzwe na kuwakilishwa FIFA hapo Juni 1.
Capello anategemewa kuwatangaza Wachezaji hao 30 siku ya Jumanne na Kikosi hicho kitaruka kwenda Austria Jumamosi ijayo ili kupiga kambi ya mazoezi.
England itacheza mechi za kirafiki na Mexico Mei 25, Uwanjani Wembley, na Japan, huko Austria, Mei 30
Fergie: ‘Bado nipo labda afya igome!’
Sir Alex Ferguson amedai ni afya yake tu ndio itaamua kama atang’oka au la kama Meneja wa Manchester United.
Ferguson, miaka 68, yupo Old Trafford kwa miaka 24 na na bado ana njaa ya ushindi.
Mwenyewe anasema: “Sidhani nitabadilika kadri nnavyozeeka. Mie ni mtu yule yule. Ninachoomba ni afya yangu iendelee kuwa nzuri.”
Ferguson aliingia Man United Novemba 1986 na ilimchukua hadi 1990 ili kushinda Kombe lake la kwanza aliponyakua FA Cup lakini amekiri kuwa sasa ni vigumu Mameneja kupewa muda mrefu kama huo ili kuonyesha mafanikio.
Ferguson amelalamika: “Klabu nyingi hutafuta Meneja mwenye mafanikio lakini wakimchukua akikaa muda mfupi bila mafanikio huonekana si Meneja mwenye mafanikio tena!”
Fergie akaongeza: “Ni mchezo mbaya kabisa, utamaduni wa fani hii sasa ni mafanikio tu! Kama alivyosema Roberto Mancini, ukipoteza gemu tatu tu huko Italia, basi kazi huna!”
Ferguson akamalizia kwa kukumbusha jinsi walivyotimuliwa Peter Reid, Ruud Gullit na Bobby Robson wakati Msimu mpya umeanza tu na hata hawajapata muda wa kujenga Timu zao na kuponda hatua hii kwa kudai: “Ukifika hatua ya kufukuza Mameneja siku chache baada ya Msimu kuanza basi wewe hujui kabisa namna ya kuiendesha Klabu ya Soka!”

No comments:

Powered By Blogger