Friday, 23 April 2010

Wenger amlinda Adebayor
Bosi wa Arsenal Arsene Wenger ametoa wito kwa Mashabiki wa Arsenal kumheshimu Emmanuel Adebayor wakati Arsenal na Manchester City zitakapocheza kesho Jumamosi Uwanjani Emirates kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Wito wa Wenger unafuatia vitendo alivyofanya Adebayor, aliekuwa Mchezaji wa Arsenal kabla kuhamia Man City, katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu iliyochezwa Septemba na Man City kuifunga Arsenal 4-2 na Adebayor kwenda kushangilia kwa kejeli mbele ya Mashabiki wa Arsenal.
Kitendo hicho kilimpatia onyo kali toka kwa FA lakini pia katika mechi hiyo hiyo Adebayor alimtimba Robin van Persie na FA ikamfungia mechi 3.
Wenger ametamka: “Bila kujali kilichotokea mechi iliyopita ni muhimu kila mtu awe na nidhamu. Mtu hufanya makosa ambayo hujutia. Si kwa Adebayor tu hata kwa Viera na Toure- wote tunawakaribisha na tunaheshimu mchango wao kwa Arsenal.”
Kolo Toure, ambae ni Mchezaji mwenzake Adebayor Klabuni Man City na wote wametokea Arsenal, amemtaka Adebayor awe mtulivu na kutumia akili kwenye mechi na Arsenal.
Fergie azicheka kauli za kustaafu kwake
Sir Alex Ferguson ameziita kauli za kwamba atastaafu kuwa Meneja wa Manchester United mwishoni mwa Msimu wa 2010/11 kuwa ni za kipuuzi na kuzicheka.
Ferguson amesema: “Ni upuuzi mtupu! Hamna ukweli! Sina nia ya kustaafu na hata nikitaka kustaafu Watu ntakaowajulisha ni David Gill [Mkurugenzi Mtendaji wa Man United] na Familia ya Glazer.”
Ferguson amesisitiza kitu pekee kitakachoamua atabaki Manchester United au la ni afya yake na kwa sasa bado ni nzuri tu.
Huu ni mwaka wa 23 kwa Sir Alex Ferguson, mwenye umri wa miaka 68, kuwa Bosi wa Manchester United na ndie Meneja anaesifika wa kuwa na mafanikio makubwa mno katika historia ya kandanda ya huko Uingereza.
Msimu huu, Manchester United inawania kutwaa Ubingwa wa England kwa mara ya 4 mfululizo ikiwa ni kutaka kuweka historia kwa kuwa Klabu ya kwanza kuweza kufanya hivyo.
Hata hivyo, Man United wapo nafasi ya pili pointi moja nyuma ya Chelsea huku mechi zimebaki 3.

No comments:

Powered By Blogger