Tuesday 20 April 2010

Inter Milan v Barcelona
Leo saa 3 dakika 45 usiku, saa za bongo, Nusu Fainali ya kwanza ya UEFA CHAMPIONS LIGI itachezwa huko Uwanjani San Siro, nyumbani kwa Inter Milan, kwa Wenyeji hao kuwakaribisha Mabingwa Watetezi, Barcelona, waliolazimika kusafiri kutoka kwao Spain kwa njia ya barabara kufuatia kusimama kwa Usafiri wa Anga kufuatia kusambaa kwa Majivu kutoka Volcano iliyolipuka huko Iceland.
Msimu huu, Timu hizi mbili zimeshawahi kukutana mara mbili kwenye Michuano hii katika hatua za awali za Makundi na mechi ya kwanza Uwanjani San Siro ilikuwa 0-0 na marudiano huko Nou Camp Barca walishinda 2-0.
Katika mechi ya leo, Barca wataikosa Injini yao moja ya Kiungo, Andres Iniesta, ambae ni majeruhi.
Inter, safu yao ya mashambulizi, itaongozwa na Mchezaji wa zamani wa Barca, Samuel Eto’o,
Mechi ya marudiano itafanyika Nou Camp Aprili 28.
Kesho kutakuwa na mechi ya Nusu Fainali ya pili kati ya Bayern Munich na Lyon.
Newcastle Mabingwa
Newcastle United, ambao tayari wamefuzu kupanda Daraja pamoja na West Bromwich Albion na kurudi Ligi Kuu England, baada ya Msimu mmoja tu kwenye Coca Cola Championship, jana walifanikiwa kuutwaa Ubingwa wa Daraja lao la Coca Cola Championship walipowafunga Plymouth bao 2-0.
Mabao ya Newcastle yalifungwa na Andy Carroll na Routledge.
Liverpool 3 West Ham 0
Katika mechi ya Ligi Kuu hapo jana, Liverpool walimudu kuichapa West Ham bao 3-0 na kushika nafasi ya 6 wakiwa na pointi 59 kwa mechi 35 na juu yao kwenye nafasi ya 5 wako Man City wenye pointi 62 kwa mechi 34 na nafasi ya 4 ni Tottenham waliocheza mechi 34 na wana pointi 64.
Mabao ya Liverpool yalifungwa na Yossi Benayoun, David Ngog na Sotiros Kyrgiakos.
Mutu kifungo Miezi 9
Straika wa Romania, Adrian Mutu, ameendelea kukumbwa na mabalaa ya kufumaniwa akitumia madawa marufuku na hivyo kufungiwa kwa mara ya pili na safari hii amekikwaa kifungo cha Miezi 9 kilichotolewa na Kamati ya Olimpiki ya Italia alipogunduliwa kutumia dawa marufuku Mwezi Januari katika mechi kati za Timu yake Fiorentina dhidi ya Bari na nyingine na Lazio na atatumikia kifungo hicho hadi Oktoba 29.
Mwaka 2004, akiwa Chelsea, alikikwaa kifungo baada ya kugunduliwa akitumia kokeni.

No comments:

Powered By Blogger