Saturday 1 November 2008

MECHI ZA LEO!

Meneja mpya wa Tottenham, Harry Redknapp, ambae katika mechi zake mbili za kwanza amewafunga Bolton na kuwatia kiwewe Arsenal kwa kulazimisha sare, sasa anapambana na timu ambayo haijafungwa na ndiyo inayoongoza LIGI KUU, Liverpool, itakayotua White Hart Lane baada ya kuipachika timu yake ya zamani ya Portsmouth bao 1-0 kwenye mechi iliyokwisha.
Nao Portsmouth watawakaribisha Wigan kwao Fratton Park ikiwa ni mechi ya pili kwa Meneja mpya Tony Adams wakijaribu kukwepa kufungwa mechi ya 5 mfululizo kwenye ligi huku Wigan, baada ya kuanza vema msimu, wamejikuta wakipata vipigo mfululizo kutoka kwa Fulham, Aston Villa, Liverpool na Middlesbrough na kuwafanya wateremka na kuwa miongoni mwa timu 3 za mwisho kwenye msimamo wa ligi.
Bolton ni timu nyingine inayoporomoka kadri ligi ikiendelea baada ya kupata vipigo vinne katika mechi zao 6 za mwisho na sasa wako nafasi ya 19 yaani nafasi moja juu ya timu ya mwisho kwenye msimamo wa ligi. Sasa wanakutana na Manchester City timu nyingine kigeugeu kwenye ligi kwani haitabiriki.
Everton, mpaka sasa washashinda mechi 3 za ligi na zote wameshinda ugenini. Nyumbani, Uwanja wa Goodison Park, hawajashinda hata mechi moja katika mechi 5 za ligi walizocheza hapo msimu huu. Everton watawakaribisha Fulham ambao juzi waliwafunga Wigan.
Chelsea, waliopoteza rekodi yao ya kutofungwa katika mechi 86 za ligi nyumbani Stamford Bridge baada ya kupigwa 1-0 na Liverpool, wanawakaribisha Sunderland kwenye hiyo ngome iliyopenywa ya Stamford Bridge.
Nao Arsenal, baada ya kupokwa tonge mdomoni na Tottenham ambao walilazimisha sare ya 4-4 wakati Arsenal walikuwa wakiongoza kwa bao 4-2 hadi dakika ya 88, wanasafiri kwenda kukutana na timu iliyopanda daraja msimu huu Stoke City ambao silaha yao kubwa ni Mchezaji wao Rory Delap ambae ni spesho kwa mipira ya kurusha inayofanya kila mara Stoke City wapate bao.
Ukichukulia jinsi mechi ya Arsenal na Tottenham ilivyoisha, taarifa za ngumi kwenye chumba cha Arsenal baada ya mechi hiyo na jinsi defensi ya Arsenal inavyoyumba, basi bila shaka Arsenal lazima wagwaye mipira ya kurusha golini atakayorusha Rory Delap.
West Ham waliochabangwa bao 2 na Ronaldo wakati walipotembelea Old Trafford kukutana na Mabingwa Manchester United wanasafiri tena kwenda Riverside kukutana na Middlesbrough waliowakung'uta Manchester City juzi.,
Kwenye Uwanja wa Hawthorns, West Brom watawakarbisha Blackburn huku timu zote zikitoka kwenye vipigo. West Brom walifungwa 2-1 na Newcastle huku Blackburn walitandikwa 3-2 na Aston Villa.
Hull City, timu iliyopanda daraja msimu huu na iliyoleta msisimko sana msimu huu baada ya kuzifunga Arsenal, Tottenham na Newcastle, itatua Old Traford kupambana na Mabingwa wenyewe Manchester United baada ya juzi kupigwa 3-0 na Chelsea.
Kuna kila dalili Manchester United na hasa Cristiano Ronaldo sasa wanaanza kupamba moto. Ronaldo ndie aliewapa ushindi baada ya kufunga bao 2 dhidi ya West Ham.
Hull City inaongozwa na Meneja Phil Brown ambae mwenyewe amekiri Sir Alex Ferguson ndie aliemsaidia kupata kazi ya Umeneja huko Derby County miaka mitatu iliyopita.
Phil Brown anasema: 'Alimpigia simu Mwenyekiti wa Derby. Sidhani kama angempigia kama angeona sifai. Namshkuru ni mtu mwema sana!'

No comments:

Powered By Blogger