Wednesday 5 August 2009

Liverpool wamsaini Aquilani toka AS Roma!!
Baada ya kumuuza Xabi Alonso kwa Real Madrid, Liverpool haraka haraka wamejaribu kuziba pengo lake kwa kutangaza kuwa wamemchukua Kiungo wa AS Roma ya Italia, Alberto Aquilani, Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Italia.
Inaaminika dau la ununuzi wake ni Pauni Milioni 20 na inasadikiwa baadae wiki hii Aquilani ataenda Liverpool kukamilisha uhamisho ikiwa pamoja na kupimwa afya yake.
Ferguson: “Liverpool hawana nafasi Ubingwa!’
Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, amewakata maini Mahasimu wao wa Jadi Liverpool kwa kuwaambia hawana nafasi yeyote ya kuchukua Ubingwa wa Ligi Kuu England wakati wao wanawania kuuchukua kwa mara ya 4 mfululizo na kwa mara ya 19 kwa ujumla ili kuwapiku Liverpool ambao wamefungana nao kwa kuwa Timu zilizonyakua Ubingwa huo mara 18 kila mmoja zikiwa ni mara nyingi kupita Klabu nyingine yeyote.
Ferguson alitamka: “Pengine msimu uliokwisha kwa Liverpool ulikuwa bora kupita mwingine wowote kwa miaka 20 iliyopita! Waliumaliza wakiwa na pointi 86, pointi 4 nyuma yetu na itakuwa ngumu kufikia tena hapo na pengine hawataweza kuyapita mafanikio hayo! Timu nyingine sasa zimeshaisoma Liverpool na kuijua vizuri!”
Alipoulizwa ikiwa Liverpool itaathirika kwa kuuzwa Kiungo wao Xabi Alonso kwa Real Madrid, Ferguson alijibu kuwa Alonso hawezi kuleta pengo kwa Liverpool kwa kuwa tegemezi kubwa la Liverpool ni Nahodha wao Steven Gerrard na Mshambuliaji Fernando Torres.
Ferguson ameonyesha kuitilia wasiwasi Chelsea kuwa pengine ndie mshindani wao mkuu huku wakiwa na Meneja mpya Carlo Ancelotti ambae ni Mshindi wa Makombe mawili ya Ulaya na Ubingwa wa Serie A akiwa na AC Milan.
“Ni Chelsea! Ancelotti ataibadili Chelsea uchezaji wake na watapata magoli mengi kupitia Didier Drogba na Nicolas Anelka!” Ferguson aliongezea.
Hata hivyo Ferguson amekiri kuwa Man U itakuwa na pengo kwa kumkosa Ronaldo lakini ana uhakika Chipukizi wa Timu yake watasimama kidete. Ferguson amekiri pia kuwa hawawezi kumpata Mchezaji mwingine atakaekuwa kama Ronaldo.
Ferguson amesema: “Watu watasema mengi, kwangu mimi Ronaldo ni Mchezaji Bora Duniani! Ukiwa na Mchezaji Bora ni vigumu kumpata mwingine kama yeye! Na wakati ukijua huwezi kumpata mwingine wa kuziba pengo lake, kilichobaki ni kutazama njia mbadala! Watu wanakosea na kudharau uwezo wetu wa kukuza vipaji. Tuna matumaini makubwa kwa Chipukizi wetu Evans, Welbeck, Gibson, Macheda na Pacha Da Silva. Nani na Anderson wameshaonyesha vitu vizuri na watapanda chati msimu ujao!”
Van der Sar nje wiki 8!!!
Wakati huo huo, Kipa Veterani, Edwin van der Sar, atakosa wiki nane za mwanzo wa msimu ujao unaoanza Agosti 9 kwa mechi ya “fungua pazia” kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya Chelsea baada ya kufanyiwa opersheni kutibu kidole cha mkononi kilichovunjika pamoja na mfupa mkono wake wa kushoto.
Van der Sar, miaka 38, aliumia akiokoa penalti kwenye mechi na Bayern Munich wiki iliyokwisha.
Makipa wa akiba Ben Foster na Tomasz Kuszczak wanategemewa kuchukua nafasi yake kwenye hiyo ya Ngao ya Hisani dhidi ya Chelsea.
Wachezaji Portsmouth watwangana kambini Ureno, warudishwa England!!!
Klabu ya Portsmouth imewatwanga Wachezaji wake wawili, David Nugent na Marc Wilson, faini ya mishahara ya wiki mbili na kuwafungisha virago warudi jijini Portsmouth kutoka kwenye kambi ya mazoezi huko Ureno baada ya kupigana makonde.
Katika taarifa yake, Klabu ya Portsmouth imesema Wachezaji hao walifanya utovu wa Nidhamu na wameadhibiwa kufuatana na kanuni za Klabu hiyo.
UEFA CHAMPIONS LEAGUE MTOANO: MATOKEO MECHI ZA MARUDIANO JANA:
FC Twente 1 v Sporting 1, (Sporting Lisbon yasonga mbele)

Maccabi Haifa 4 v FC Aktobe 3, (Haifa imefuzu),
Panathinaikos 3 v Sparta Prague 0, (Panathinaikos yasonga),
Sivasspor 3 v Anderlecht 1, (Anderlecht imepita),
MECHI ZA LEO: [KWENYE MABANO MATOKEO MECHI YA AWALI]
BATE v FK Ventspils, (0-1),
Debrecen v FC Levadia Tallinn, (1-0),
Dinamo Moscow vCeltic, (1-0),
Levski Sofia v FK Baku, ( 0-0),
NK Maribor v FC Zurich, (3-2),
Olympiacos v Slovan Bratislava, ( 2-0),
Partizan Belgrade v Apoel Nicosia, ( 0-2),
Politehnica Timisoara v Shakhtar Donetsk, ( 2-2),
Slavia Prague v FC Sheriff Tiraspol, (0-0),
Stabaek v FC Copenhagen, (1-3),

No comments:

Powered By Blogger